Vatican News
Papa Francisko asema, Panama ni nchi ya makutano ya watu mbali mbali duniani na mahali pa ndoto ya matumaini. Papa Francisko asema, Panama ni nchi ya makutano ya watu mbali mbali duniani na mahali pa ndoto ya matumaini. 

Panama 2019: Ni Nchi ya makutano ya watu na ndoto ya matumaini!

Baba Mtakatifu katika hotuba yake, amekazia mambo makuu mawili: Umuhimu wa nchi ya Panama katika Ukanda wa Amerika ya Kati na pili, Panama ni nchi ya ndoto ya matumaini kwa watu wengi! Papa anawashukuru wananchi wote wa Panama, kwa kujisadaka bila ya kujibakiza ili kuweza kuwapokea na kuwakirimia wajumbe wa maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, aliianza siku ya Alhamisi, tarehe 24 Januari 2019 kwa Ibada ya Misa Takatifu kwenye Ubalozi wa Vatican nchini Panama na baadaye akamtembelea Rais wa Panama ikulu na hatimaye, akazungumza na viongozi wa Serikali, wanadiplomasia pamoja na viongozi wa kiraia. Baba Mtakatifu katika hotuba yake, amekazia mambo makuu mawili: Umuhimu wa nchi ya Panama katika Ukanda wa Amerika ya Kati na pili, Panama ni nchi ya ndoto ya matumaini kwa watu wengi!

Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwashukuru wananchi wote wa Panama, kwa kujisadaka bila ya kujibakiza ili kuweza kuwapokea na kuwakirimia wajumbe wa maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani. Mkutano huu, unawawezesha viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kutambua nguvu na uwezo wa wananchi wao kuwa na ndoto ya ujenzi wa mji mkubwa unaoweza kuwapokea, kuwakirimia, kuwaheshimu na kukumbatia ili hatimaye kuwashirikisha amana na utajiri wa watu na tamaduni zao, kama alivyowahi kusema Bwana Simòn Boliva, Baba na muasisi wa nchi ya Panama.

Panama ni nchi ambayo imebarikiwa kuwa ni kitovu na daraja la Amerika ya Kati, mahali panapowakutanisha watu; alama ya maendeleo fungamani yanayobubujika kutokana na uwezo wa kuwaunganisha watu, sehemu muhimu sana ya utambulisho wa wananchi wa Panama, kila mtu akiwa na nafasi ya pekee katika kuchangia mchakato wa watu kukutana na hivyo kujisikia wamoja. Ni vigumu sana kufikiri ustawi na maendeleo ya nchi kwa siku za usoni bila ushiriki mkamilifu wa wananchi wote; sanjari na kutambua utu na heshima yao. Lengo hili linaweza kufikiwa kwa njia ya elimu na mazingira bora ya kazi; uhuru pamoja na kuwajali maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Baba Mtakatifu amewapongeza wazawa wa Panama, wanaoendelea kuchangia kuwa na mwelekeo sahihi kuhusu wazawa, kama ilivyojitokeza katika maadhimisho ya siku ya vijana wazawa kutoka Amerika ya Kusini kimataifa, hatua kubwa katika maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa mwaka 2019. Mkusanyiko huu una maana ya kusherehekea, kutambua na kusikiliza watu, ili kuwajengea matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi. Ni mwaliko wa kusimama kidete kulinda mafao ya wengi sanjari na kuhakikisha kwamba, rasilimali na utajiri wa nchi vinatumika katika misingi ya usawa na haki.

Vijana wa kizazi kipya katika furaha, ari, uhuru, utambuzi pamoja na uwezo wao wa kupembua na kuchambua mambo wanahitaji kuona viongozi wanaotekeleza dhamana na wajibu wao kadiri ya utu wa binadamu na dhamana yao kwa umma. Huu ni mwaliko wa kujikita katika misingi ya ukweli na uwazi; kwa kushuhudia kwamba, uongozi wa umma ni huduma inayofumbatwa katika uaminifu, haki pamoja na kupambana kufa na kupona na saratani ya rushwa na ufisadi wa mali ya umma, lengo ni kujenga siasa inayojikita katika utu, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu na mahitaji yake msingi, kama inavyofafanuliwa katika Wimbo wa Taifa la Panama.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, Panama ni nchi ya ndoto ya matumaini, mahali ambapo vijana kutoka pande mbali mbali za dunia, wanakutana, ili kuadhimisha na kusali kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa ulimwengu unaofumbatwa katika utu. Vijana wanatoa changamoto ya kuweza kuwa na mwono mpana zaidi dhidi ya hali ya kukata tamaa; chuki na uhasama; ushindani usiokuwa na tija wala mashiko unaofumbatwa kwenye falsafa ya mwenye nguvu mpishe! Vijana wanataka kuona mwelekeo mpya katika ubinadamu.

Kwa njia ya ukarimu, Panama imeonesha kuwa kweli ni nchi ya ndoto kwa vijana na changamoto ya kuwa na mwelekeo mpya, kwa kujikita katika upendo kwa jirani. Katika maadhimisho haya, vijana wanashuhudia njia mpya za mawasiliano, kufahamiana, mshikamano, kipaji cha ubunifu na uwezo wa kusaidiana kwa hali na mali dhidi ya upweke hasi, tayari kuandika historia mpya ya maisha yao!

Kuna uwezekano wa kuwa na ulimwengu mpya, unaowashirikisha vijana, ili kuleta mageuzi ya dhati kijamii na kwamba, ndoto ya kuwa fursa nzuri zaidi kwa leo na kesho iliyo bora ni haki ya kiutu! Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko amemshukuru na kumpongeza Rais wa Panama kwa kuhakikisha kwamba, mkutano huu unafanikiwa kwa kiasi kikubwa!

Papa: Diplomasia
25 January 2019, 12:35