Vatican News
Askofu Paul Hinder: Zawadi kubwa kutoka kwa Papa Francisko ni Ibada ya Misa Takatifu! Askofu Paul Hinder: Zawadi kubwa kutoka kwa Papa Francisko ni Ibada ya Misa Takatifu!  (AFP or licensors)

Papa Francisko Falme za Kiarabu: Zawadi kubwa ni Ibada ya Misa

Maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu itakayoendeshwa na Baba Mtakatifu Francisko ni kati ya zawadi kubwa zinazotarajiwa kwa ajili ya Wakristo huko Falme za Kiarabu. Hili ni Kanisa linaloundwa na wahamiaji pamoja na wakimbizi kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Amani, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi yanawezekana kwa kutambua kwamba, tofauti msingi ni amana na utajiri.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, udugu wa kweli unafumbatwa katika uwezo wa kushirikiana na kushikamana na wengine; kwa kutambua kwamba, tofauti zao msingi ni tunu inayowatajirisha wote, ili kutambuana na kuheshimiana, ili hatimaye, kuboresha mahusiano na mafungamano ya kijamii, kiroho na kiutu. Uhuru wa kidini ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayopaswa kulindwa, kukuzwa na kudumishwa na wote, kwani ni msingi wa haki zote za binadamu, utu na heshima yake.

Kumbe, umoja, udugu na mshikamano; amani na utulivu; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi ni muhimu sana katika mchakato wa ujenzi wa mafungamano ya kijamii! Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anasema, ili kukuza na kudumisha uhuru wa kidini kuna haja kwa waamini kuheshimiana, kuaminiana, kulindana na kusaidiana. Ili kuzingatia utawala wa sheria; waamini wa dini mbali mbali washirikiane na serikali zao; na kwamba, viongozi wa kidini watambue dhamana na wajibu wao pamoja na kuendeleza majadiliano yanayofumbatwa katika ukweli na uwazi, amani na utulivu!

Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake, anaendelea kukazia umuhimu wa waamini wa dini mbali mbali kujikita katika mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene. Kwa sasa Baba Mtakatifu anajiandaa kwa ajili ya hija 27 ya kitume huko Abu Dhabi, Falme za Kiarabu. Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu amewahi pia kutembelea nchi zenye idadi kubwa ya waamini wa dini ya Kiislam kama vile: Uturuki, Bosnia, Azerbaijan, Misri na huko Bangaladesh.

Askofu Paul Hinder, Msimamizi wa Kitume huko Falme za Kiarabu anasema, waamini wa Kanisa Katoliki wanakadiriwa kuwa ni milioni moja. Wengi wao ni wafanyakazi kutoka katika zaidi ya nchi 100 hasa zaidi: Ufilippini, India pamoja na nchi za Kiasia. Baba Mtakatifu amejipambanua kuwa ni mjumbe wa amani na majadiliano katika ukweli na uwazi. Kumbe, hija hii inaweza kusaidia kukoleza mchakato wa udugu wa ubinadamu. Hija hii ya kitume ni matunda ya diplomasia ya Vatican inayofumbatwa kwa namna ya pekee katika majadiliano kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Askofu Paul Hinder tangu mwaka 2003 amekuwepo Abu Dhabi na sasa tayari imegota miaka 15 ya uwepo na utume wake katika nchi za Yemen, Oman na Falme za Kiarabu. Katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, nchi ya Falme za Kiarabu imejipambanua sana katika huduma ya upendo na mshikamano katika Jumuiya ya Kimataifa. Maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu itakayoendeshwa na Baba Mtakatifu Francisko ni kati ya zawadi kubwa zinazotarajiwa kwa ajili ya Wakristo huko Falme za Kiarabu. Hili ni Kanisa linaloundwa na wahamiaji pamoja na wakimbizi kutoka sehemu mbali mbali za dunia.

Amani, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi yanawezekana pale waamini wa dini mbali mbali wanapotambua kwamba, tofauti zao msingi ni utajiri na amana inayopaswa kuendelezwa. Ubaguzi na nyanyaso za kila aina ni mambo ambayo yamepitwa na wakati. Wakristo kutoka katika Mapokeo na Madhehebu mbali mbali wanayo nafasi ya kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa kwa uhuru kamili.

Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake, ameshiriki kikamilifu katika majadiliano ya kidini kama ilivyokuwa nchini Misri. Lengo ni kukuza na kudumisha, amani, uhuru wa kidini na uhuru wa kuabudu; utu, heshima na haki msingi za binadamu; ustawi, maendeleo, mafao ya wengi pamoja na demokrasia shirikishi. Mateso na mahangaiko ya familia ya Mungu huko Yemen yameendelea kuacha chapa katika maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko.

Askofu Paul Hinder
31 January 2019, 17:48