Papa Francisko tarehe 17 Desemba 2018 anaadhimisha Kumbu kumbu ya Miaka 82 tangu alipozaliwa. Papa Francisko tarehe 17 Desemba 2018 anaadhimisha Kumbu kumbu ya Miaka 82 tangu alipozaliwa. 

Papa Francisko: Kumbu kumbu ya miaka 82 ya kuzaliwa kwake!

Jorge Mario Bergoglio alizaliwa kunako tarehe 17 Desemba 1936 huko Flores, Bueno Aires, nchini Argentina. Akiwa na umri wa miaka 17 baada ya kujongea katika Mahakama ya huruma ya Mungu, alionja huruma na upendo wa pekee kutoka kwa Mwenyezi Mungu katika maisha yake. Baada ya masomo yake, akapewa Daraja Takatifu ya Upadrisho hapo tarehe 13 Desemba 1969.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kupokea salam na matashi mema kutoka sehemu mbali mbali za dunia anapoadhimisha miaka 82 tangu alipozaliwa! Itakumbukwa kwamba, Jorge Mario Bergoglio alizaliwa kunako tarehe 17 Desemba 1936 huko Flores, Bueno Aires, nchini Argentina. Akiwa na umri wa miaka 17 baada ya kujongea katika Mahakama ya huruma ya Mungu, alionja huruma na upendo wa pekee kutoka kwa Mwenyezi Mungu katika maisha yake. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi na Kitawa, akapewa Daraja Takatifu ya Upadri hapo tarehe 13 Desemba 1969.

Baada ya kufanya kazi na utume wake katika ngazi mbali mbali kama Padre na Mtawa, Mtakatifu Yohane Paulo II, kunako mwaka 1992 akamteuwa kuwa Askofu msaidizi wa Jimbo kuu la Buenos Aires, Argentina na kuwekwa wakfu tarehe 27 Mei 1992 na kuchagua maneno: Miserando atque eligendo” yaani “Akamwangalia kwa jicho la huruma na kumteua”. Kunako mwaka 2001, Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa na kumsimika kuwa Kardinali na tarehe 13 Machi 2013 akachaguliwa kuwa Khalifa wa Mtakatifu Petro na kuamua kuchagua jina la Mtakatifu Francisko wa Assisi, ili kukazia mambo makuu matatu: Amani, Maskini na Mazingira.

Katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro amekuwa ni mtetezi, chombo na mjumbe wa haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa. Ameendelea kujipambanua kama mtetezi wa maskini, wanyonge na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na hali mbali mbali za maisha yao, ili kulinda utu, heshima na haki zao msingi! Baba Mtakatifu Francisko amekuwa ni mtetezi mkuu wa mazingira nyumba ya wote, ili kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi kwani athari kubwa za mabadiliko ya nchi zinaendelea kuwatumbukiza watu wengi katika ombwe la umaskini wa hali na kipato pamoja na kusigina utu, heshima na haki zao msingi!

Vatican News inapenda kumtakia Baba Mtakatifu Francisko heri na baraka tele anapomwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa kuadhimisha kumbu kumbu ya miaka 82 tangu kuzaliwa kwake! Unaweza kuungana nasi kwa kumwombea Baba Mtakatifu kama anavyoomba daima akipata nafasi!

Papa: Miaka 82
15 December 2018, 16:36