Papa awakumbusha Ireland kuwaandalia vijana wakati endelevu!
Sr.Angela Rwezaula - Vatican
Rafiki wapendwa, nikiwa najiandaa kwa siku za hivi karibuni kutembelea Ireland, kwa ajili ya Mkutano wa Familia duniani, ninapenda kuwatumia salam za upendo watu wote wa Ireland: Ninafurahi ninapofikiria ninarudi Ireland!
Hayo ndiyo maneno ya mwanzo wa ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko alioutuma kwa njia ya Video Jumatatu 20 Agosti jioni kwa watu wote wa Ireland katika matazamio zira yake ya kitume kwenye Mkutano wa IX wa Familia Duniani, ziara ambayo ni ya siku mbili kuanzia tarehe 25-26 Agosti, na hivyo katika ujumbe huu anakumbusha umuhimu wa kuandalia vijana wakati endelevu.
Katika ujumbe wake anasema “Kama mnavyojua kuwa Mkutano wa dunia ni maadhimisho ya uzuri wa mpango wa Mungu kwa ajili ya familia; lakini pia ni fursa kwa ajili ya familia kutoka pande zote za dunia kukutana na kusaidiana kwa pamoja katika kuishi wito wao maalum. Famili leo hii inakabiliana na changamoto nyingi katika juhudi zao, ili kujikita katika upendo mwaminifu, kuwalea watoto katika thamani iliyo safi na ili wawe jumuiya kubwa, chachu ya wema, upendo na kutunzana kwa pamoja. Ninyi mnatambua hili.
Kadhalika Baba Mtakatifu anaendelea “ Ni matumaini ya kuwa fursa hiyo inaweza kuwa kisima cha upyaisho wa kutia moyo familia za kila pande ya dunia na hasa familia zile ambazo zitaweza kuwapo huko Dublin. Wanaweza kukumbuka nafasi msingi ya familia katika maisha ya jamii na katika ujenzi wa wakati endelevu ulio bora kwa vijana. Kwani vijana ni wakati endelevu! Ni muhimu sana kuwaandaa vijana kwa ajili ya wakati endelevu,kwa maana ya kuwaandalia leo hii, kwa wakati uliopo, lakini pia kwa njia ya mizizi ya wakati uliopita: ikiwa na maana ya vijana na babu zao: Ni muhimu”.
Kama ilivyo sababu maalumu ya ziara yangu kutembelea Ireland ni kuhusu Mkutano wa Familia duniani, lakini ninapendelea iwe kama fursa ya kuwakumbatia familia nzima ya Ireland. Ninasali kwa namna ya pekee ili mkutano uweze kusaidia kukua kwa umoja na mapatano kati ya waamini wote wa Kristo, kama ishala ya amani ya kudumu ambayo ni ndoto ya Mungu kwa ajili ya familia nzima ya binadamu.
Ninatambua jinsi gani kwa ari zote watu wanajitahidi kuandaa ziara yangu. Shukrani zangu za dhati kwa wote. Ninaomba kwa kila mmoja asali ili mkutano huo uweze kuwa kipindi cha furaha na hata cha utulivu, chenye kuwa na upendo mtulivu wa Yesu kwa familia zote na ukweli kwa ajili ya kila mtoto wa Mungu. Ninawakikishia ukaribu wangu, sala zangu na kuwaalika kusali kwa ajili yangu kwa maana ninahitaji. Na kwa moyo wote ninawabariki.
Mungu awabariki. Kwa jina la Baba, na la Mwana , na Roho Mtakatifu.