Vatican News
Sala ya Malaika wa Bwana tarehe 5 Agosti 2018. Sala ya Malaika wa Bwana tarehe 5 Agosti 2018.  (Vatican Media )

Papa Francisko: Mkijiaminisha kwa Kristo, mtatenda kazi ya Mungu!

Imani kwa Kristo Yesu, inawawezesha waamini kutenda kazi ya Mungu. Ikiwa kama waamini watajiaminisha kwa Mwenyezi Mungu na hivyo kujenga uhusiano na mafungamano ya imani na mapendo kwa Yesu, wataweza kutenda matendo makuu yanayorembwa kwa uzuri wa Injili, kwa ajili ya mafao, ustawi na mahitaji ya jirani zao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mwinjili Yohane katika sura ya sita, anaendelea kumwonesha Kristo Yesu, mwingi wa huruma na mapendo, anayewalisha watu kwanza kabisa kwa Neno la Mungu na pili kushibisha njaa ya mwili, kiasi cha kuleta mvuto kwa watu wengi kuanza kumtafuta, ili kukutana naye tena. Lakini, Yesu alitaka kuwasaidia watu hawa kupata chakula cha uzima wa milele na wala si kwa kuridhika kwa mambo mpito, kumbe, walipaswa kuwa na mwelekeo mpana zaidi, badala ya kuhangaikia: chakula cha kila siku, mavazi, fursa za ajira na mambo kama hayo! Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili, tarehe 5 Agosti 2018.

Yesu anawaambia watu waliokuwa wanamtafuta kwamba, si kwa sababu waliona miujiza aliyotenda, bali ni kwa vile tu, walikula wakashiba na hivyo, anawataka kupiga hatua mbele, ili kufahamu zaidi maana ya muujiza alioutenda, yaani, Kristo Yesu ni zawadi ya Baba wa milele, chakula cha uzima wa milele kilichoshuka kutoka mbinguni. Hiki ndicho chakula kinachoshibisha mwili na kuzima njaa ya maisha ya uzima wa milele! Kwa maneno mengine, Kristo Yesu ni chakula cha maisha ya kiroho, ambacho anawaalika wale wanaomtafuta kukihangaikia katika maisha yao.

Baba Mtakatifu anasema, kila siku Yesu anawapatia waja wake: Neno la Mungu, Mwili na Damu yake Azizi! Lakini kwa bahati mbaya, wale waliokuwa wanamfuata hawakuweza kuyafahamu mafundisho haya mazito na ya kina kutoka kwa Yesu, ndiyo maana wanamuuliza wafanye nini ili waweze kuitenda kazi ya Mungu? Wao walidhani kwamba, inatosha kutimiza Amri za Mungu, ili kutendewa tena muujiza kama ule wa kugeuza mikate mitano na samaki wawili, watu wakashiba na kufurahia maisha! Hiki ni kishawishi cha kutaka kuigeuza dini kuwa ni utimilifu wa Amri za Mungu na hivyo kujenga mahusiano na Mwenyezi Mungu kama Bwana na watwana, kiasi kwamba, watwana wanapaswa kutekeleza Amri za Bwana wao, ili kuonja wema na ukarimu wake.

Yesu anafafanua kwamba, kazi ya Mungu ni kumwamini Yeye aliyetumwa na Mungu. Ni maneno mazito ambayo Baba Mtakatifu anasema, Kristo Yesu anataka kuyaelekeza hata kwa waja wake leo hii. Kazi ya Mungu si kutenda tu, bali ni kumwamini Kristo Yesu aliyetumwa na Baba wa milele. Hii ina maana kwamba, imani kwa Kristo Yesu, inawawezesha waamini kutenda kazi ya Mungu. Ikiwa kama waamini watajiaminisha kwa Mwenyezi Mungu na hivyo kujenga uhusiano na mafungamano ya imani na mapendo kwa Yesu, wataweza kutenda matendo makuu yanayorembwa kwa uzuri wa Injili, kwa ajili ya mafao, ustawi na mahitaji ya jirani zao.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Kristo Yesu anawataka wafuasi wake kuhangaikia chakula cha kila siku, lakini zaidi, watoe kipaumbele cha kwanza kwake, ili kujenga mahusiano na hivyo, kuimarisha imani kwake ambaye kimsingi ni: mkate wa maisha ulioshuka kutoka mbinguni, ili kuzima njaa ya ukweli, haki na mapendo. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewaomba waamini kumwelekea Bikira Maria, ambaye, Jumapili tarehe 5 Agosti, Kanisa limefanya kumbu kumbu ya kutabarukiwa kwa Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu lililoko Jimbo kuu la Roma, ili kweli Bikira Maria afya ya Warumi aweze kuwaenzi katika hija ya imani kwa kujisadaka kabisa katika mpango wa Mungu unaofumbatwa katika maisha yao.

Sikiliza kwa raha zako mwenyewe!

 

05 August 2018, 08:17