Vatican News
Hivi karibuni, Baba Mtakatifu Francisko alikutana na kuzungumza na watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi Hivi karibuni, Baba Mtakatifu Francisko alikutana na kuzungumza na watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi 

Watoto wanaoishi katika mazingira magumu wakutana na Papa na kumuuliza maswali magumu!

Fumbo la mateso na mahangaiko ya mwanadamu linaweza kuangaliwa kwa jicho la huruma, mapendo na udadisi. Kwa kusikiliza kilio na mahangaiko, mtu anaweza kubaki akiwa amepigwa butwaa! Mwanadamu anapoguswa na mateso pamoja na mahangaiko ya jirani zake, anaweza kuangua kilio na kuteseka pamoja nao, kama kielelezo cha ushuhuda wa upendo na mshikamano.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. - Vatican.

Kuna maswali mengi ambayo mwanadamu anajiuliza katika safari ya maisha yake hapa duniani, lakini, anashindwa kupata majibu muafaka kwani, majibu makini yanafumbatwa katika Fumbo la Mwenyezi Mungu! Mwanadamu katika unyonge wake, anaweza kuyaangalia yote haya kwa jicho la huruma, mapendo na udadisi mkubwa! Anaweza kusikiliza kilio na mahangaiko ya watu, akabaki akiwa amepigwa butwaa na kujiuliza kwanini haya yanatendeka? Mwanadamu anapoguswa na mateso pamoja na mahangaiko ya jirani zake, anaweza kuangua kilio na kuteseka pamoja nao, kama kielelezo cha ushuhuda wa upendo na mshikamano.

Huu ni muhtasari wa majibu makini yaliyotolewa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko alipokutana na kuzungumza na watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi kutoka Romania, wanaotunzwa na kulelewa mintarafu karama ya Padre Luigi Giussani, huko pembezoni mwa Jiji la Bucharest, nchini Romania. Watoto walimuuliza Baba Mtakatifu ikiwa kama kulikuwa kuna haja ya kwenda Kanisani kusali kwani mara kwa mara wanajikuta wakitumbukia katika dhambi na ubaya wa moyo!

Baba Mtakatifu anasema, hata wadhambi wanahimizwa kwenda Kanisa kusali na kukutana na Mwenyezi Mungu jinsi walivyo, katika ubora wao kama binadamu na udhaifu wao unaowabwaga dhambini, ili waweze kuwa tena na ujasiri wa kutubu na kumwongokea Mungu katika maisha yao! Waamini wajifunze kwenda Kanisani si kwa ajili ya kujionesha, bali iwe ni fursa ya kukutana tena na tena na Mwenyezi Mungu, ili kuomba huruma, neema, msamaha na upatanisho, tayari kuuvua utu wa kale na kuanza kujivika utu mpya unaofumbatwa katika maisha ya Kristo Mfufuka.

Watoto wanashindwa kuelewa ni kwanini wazazi wao wanawapenda sana wanapokuwa na afya, imara na wenye nguvu, lakini wanapokabiliana na magonjwa na ulemavu, wanataka kuwageuzia kisogo! Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, huu ni udhaifu wa binadamu na madhara ya dhambi; na hata wakati mwingine ni ushuhuda wa upendo na makuzi bora katika maisha, kiasi kwamba, mambo haya yanaacha ukakasi mkubwa kwa watoto wao! Ni makovu ya udhaifu wa binadamu ambayo hayakupata tiba kwa wakati muafaka, kiasi kwamba, wakashindwa kukua na kukomaa ili kukabiliana na changamoto katika maisha. Katika mazingira kama haya, watoto wajifunze kuwapenda na kuwaheshimu wazazi wao, ili hatimaye, kuvuka vikwazo vya udhaifu na ubinadamu wao, tayari kukumbatia huruma na upendo, amana kubwa kwa wazazi mbele ya watoto wao!

Watoto walimuuliza Baba Mtakatifu Francisko ni nani mwenye mamlaka ya kumhukumu mtu kwenda kuzimu kuteseka huko maisha yake yote, au kwenda mbinguni, kufurahi pamoja na Mwenyezi Mungu na malaika pamoja na watakatifu wake? Baba Mtakatifu anasema, Mwenyezi Mungu anataka kila mtu apate kuokoka na kupata maisha ya uzima wa milele! Kamwe hafurahii kifo cha mdhambi, bali anampatia nafasi ya kutubu na kumwongokea. Ijumaa kuu, Mama Kanisa anafanya kumbu kumbu ya mateso na kifo cha Kristo Yesu, ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Kwa njia ya ufufuko wake, aweze kuwakaribisha wote waliokombolewa kwa Damu yake azizi katika maisha ya uzima wa milele. Kristo Yesu, ni Mchungaji mwema aliyesadaka maisha yake kwa ajili ya ukombozi wa walimwengu! Daima Kristo anaendelea kuchakarika ili kuwatafuta kondoo waliopotea kama anavyojionesha katika Maandiko Matakatifu. Anawafahamu kondoo wake kwa majina pamoja na udhaifu wao wa kibinadamu, lakini anapofanikiwa kuwaokoa, anawabeba mabegani mwake, ili kuwaonjesha huruma na upendo wake usiokuwa na mipaka!

Watoto wanashindwa kuona huruma na upendo wa Mungu, kwani kuna baadhi yao wamezaliwa na ulemavu katika maisha, wanajikuta wakiteseka na kuhangaika katika mazingira magumu na hatarishi. Baba Mtakatifu Francisko anasema, haya ni baadhi ya maswali yasiyokuwa na majibu ya haraka haraka katika maisha kwani yote haya yanafumbatwa katika Mpango wa Mungu anayependa kuganga na kuokoa, ili kudhihirisha utukufu wake kama ilivyokuwa kwa yule kipofu aliyebahatika kuona tena baada ya kutendewa muujiza na Kristo Yesu. Mwenyezi Mungu ni chemchemi ya maisha, imani na matumaini hata pale mwanadamu anapokabiliana na fumbo la mateso, ugonjwa na kifo! Mwenyezi Mungu ana mpango na kila mtu katika maisha yake! Wakati mwingine si rahisi sana kugundua mpango wa Mungu katika mateso na mahangaiko ya binadamu, jambo la msingi ni kuwa na imani na matumaini kwa Mwenyezi Mungu, asili ya wema, huruma na upendo kwa binadamu wote! Katika mateso, mahangaiko na hata mbele ya Fumbo la Kifo, Mwenyezi Mungu aendelee kuwa ni kimbilio na usalama wa binadamu!

Baadhi ya wazazi wanajisikia upweke kiasi cha kukata tamaa katika maisha kuona kwamba, wanashindwa kutekeleza dhamana na wajibu wao katika malezi, makuzi, ustawi na maendeleo ya watoto wao wenyewe kiasi kwamba, wanalazimika kutunzwa kwenye nyumba za watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi. Baba Mtakatifu anapenda kuwakumbusha wazazi na walezi wanaojikuta wakiteseka kutoka katika undani wa dhamiri zao, kuzingatia kwamba, uamuzi walioufanya, wameufanya kwa upendo na kwa ajili ya mafao ya watoto wao kutokana na sababu mbali mbali!

Kumbe, huko waliko wanaunda na kujenga familia mpya ya ndugu na jamaa zake Kristo Yesu, kama ilivyokuwa kwa Yesu alipomkabidhi Bikira Maria, kuwa ni Mama wa Kanisa. Watoto wanaoteseka kwa madonda na makovu ya kukoswa upendo, wanaweza tena kuonja upendo huu kwa njia ya ushuhuda wa Kanisa. Anawataka wazazi na watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi, kuaminiana, kuthaminiana na kusaidiana katika safari ya maisha yao ya kila siku!

Watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi, hata na wale wanaoishi katika nyumba za watoto yatima, wanasema, wanakosa huruma na upendo kutoka kwa wazazi wao, kiasi cha kujisikia kwamba, hawana tena thamani mbele ya wazazi wao! Baba Mtakatifu anasema, aliposoma swali hili, alijisikia uchungu mkubwa sana moyoni mwake, kiasi cha kuona machozi yakibubujika machoni mwake, kana kwamba, bomba la maji limepasuka. Baba Mtakatifu anakaza kusema, alipenda kuonesha ukaribu na uwepo wake wa faraja kwa watoto wanaoteseka kwa kukosa huruma na upendo wa wazazi na walezi wao kwa njia ya machozi yake. Haya si makosa ya watoto wanaozaliwa na hatimaye kulelewa katika mazingira magumu na hatarishi! Kuna sababu mbali mbali zinazopelekea watoto kujikuta wakiwa katika hali na mazingira kama haya!

Sababu kubwa ni umaskini wa hali na kipato; udhaifu wa binadamu; ukosefu wa haki msingi na hali ngumu ya maisha inayowapelekea baadhi ya wazazi na walezi kushindwa kutekeleza dhamana na wajibu wao barabara! Haya pia ni matunda ya utandawazi usiojali wala kuguswa na utu na heshima ya binadamu. Lakini, wakati mwingine, wazazi wanawapenda sana watoto wao, lakini wanashindwa kumwilisha upendo huu katika uhalisia wa maisha ya watoto wao na matokeo yake, watoto wanajenga chuki dhidi ya wazazi wao na hapo familia inakuwa ni mahali pa chungu kwa watoto wengi, kiasi cha kutafuta faraja nje ya familia zao!

Kwa upande wake Simona Carobene, Mratibu wa Kituo cha watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi kutoka Romania anasema, inakuwa ni vigumu sana kwake, kufanya mang’amuzi na uamuzi wa busara kukumbatia maisha ya kuwekwa wakfu kwa kuhofia ya mbeleni! Baba Mtakatifu anakaza kusema, maisha ya Mkristo daima ni safari ya kumfuasa Kristo kwa uaminifu na uvumilivu mkubwa, ili kukua na kukomaa kadiri ya mpango wake pasi na haraka, kwani mambo mazuri hayana haraka hata kidogo! Mwenyezi Mungu anaendelea kuwashangaza waja wake kwa kuwataka kuvunjilia mbali kuta za mipango ya maisha yao!

Hamu ya kuwa mtawa ili kufuasa Kristo Yesu kwa ukaribu zaidi kwa njia ya mashauri ya Kiinjili, ni kazi inayoweza kutekelezwa kwa ufanisi mkubwa kwa kujiachilia mikononi mwa Roho Mtakatifu, anayetumia watu mbali mbali ili kutekeleza lengo na madhumini yake. Hadi hapa, Baba Mtakatifu anasema, Simona Carobene amekuwa ni shuhuda na chombo cha huruma ya Mungu kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi! Anapenda kumshukuru na kumtakia ufanisi zaidi katika maisha yake ya mbeleni!

Sikiliza kwa raha zako mwenyewe!

 

31 July 2018, 07:40