Vatican News
TAIWAN-WEATHER-TYPHOON TAIWAN-WEATHER-TYPHOON  (AFP or licensors)

Mabadiliko ya tabianchi kuathiri sana sekta ya uvuvi, 2050

Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO linasema kwamba, sekta ya uvuvi ifikapo mwaka 2050 itaathirika vibaya sana kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Kumbe, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kujizatiti zaidi katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. - Vatican.

Takwimu zilizotolewa na Shrika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO, Jumatano tarehe 11 Julai 2018 zinaonesha kwamba kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi, hadi kufikia mwaka 2050, shughuli za uvuvi baharini hasa katika nchi maskini zaidi duniani, utaathirika sana, sanjari na kupungua kwa kiwango cha maji baridi duniani. Hali hii itakuwa na madhara makubwa sana kwa mamilioni ya watu wanaotegemea kwa kiasi kikubwa kupata mahitaji yao msingi kutoka katika sekta ya uvuvi baharini. FAO inasema, waathirika wakuu wa athari za mabadiliko ya tabianchi daima wataendelea kuwa ni maskini na akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi!

Kutokana na changamoto hii, shughuli za uvuvi baharini zitapungua kwa kiasi cha asilimia 2.8% hadi kufikia mwaka 2050, kiwango hiki kitaongezeka hadi kufikia asilimia 5.3%. Sehemu zitakazoathirika zaidi ni zile zinazotegemea kwa kiasi kikubwa sekta ya uvuvi hasa Ukanda wa Tropikali pamoja na Ukanda wa Pacifik. Athari hizi ni kutokana na kuongezeka kwa kiwango cha joto la maji pamoja na acid. Wachunguzi wa athari za mabadiliko ya tabianchi wanasema, hata kiwango cha ujazo wa maji ya bahari kinatarajiwa kuongezeka maradufu, kiasi cha kutishia usalama wa maisha ya watu na mali zao kwenye fukwe za bahari. FAO imebainisha kwamba, kiwango cha mvua zinazonyeesha kinatarajiwa pia kuongezeka maradufu, hali ambayo itasababisha mafuriko na maporomoko ya ardhi.

Monsinyo Fernando Chica Arellano, Mwakilishi wa Kudumu wa Vatican kwenye Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO, Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo, IFAD pamoja na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, WFP akichangia mada kwenye mkutano huu amekazia kwa namna ya pekee: Umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika mchakato wa uvuvi endelevu; changamoto zinazojitokeza katika sekta ya uvuvi zifanyiwe kazi pamoja na mambo msingi yanayopaswa kuzingatiwa katika sekta ya uvuvi duniani. Kanisa katika maisha na utume wake, linapania kwa namna ya pekee kabisa kukuza na kudumisha uvuvi endelevu, dhamana inayotekelezwa na taasisi zake mbali mbali duniani.

Ujumbe wa Vatican unaipongeza Jumuiya ya Kimataifa kwa sera na mikakati inayopania kuboresha sekta ya uvuvi pamoja na wavuvi wenyewe. Hii ni sekta inayotoa ajira kwa mamilioni ya watu; ni chanzo cha mapato ya serikali na jamii katika ujumla wake na kwamba, sekta ya uvuvi ni chanzo cha chakula na kwamba, inachangia kwa ujumla katika ukuaji wa uchumi kitaifa na kimataifa. Hapa, jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba,  kunakuwepo na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.

Monsinyo Fernando Chica Arellano, Pili amekazia umuhimu wa kujikita katika mchakato wa uvuvi endelevu na unaowajibika. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” anasema, bahari zimebahatika kuwa na wingi wa maji na sehemu kubwa ni viumbe hai ambavyo wakati mwingine vinahatarishwa kwa shughuli za kibinadamu. Bahari ni chanzo cha chakula na lishe kwa watu wengi duniani. Lakini pia uvuvi haramu na shughuli mbali mbali za binadamu zimepekekea baadhi ya viumbe vya majini kuanza kutoweka. Hali hii ina athari kubwa sana katika mzunguko wa chakula kinachotumiwa na binadamu. Kanuni maadili ya uvuvi unaowajibika inaonesha kwamba, sekta ya uvuvi ni chanzo cha chakula, ajira, mapumziko, biashara na uchumi; mambo msingi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi kwa kizazi cha sasa na kile kijacho! Kutokana na changamoto zote hizi, uvuvi unapaswa kuwa ni endelevu.

Lakini ukweli wa mambo unaonesha kwamba, kumekuwepo na mafanikio makubwa katika sekta ya uvuvi, lakini pia kuna kiwango kikubwa sana cha uvuvi haramu na uharibifu wa mazalia ya samaki, changamoto inayopaswa kuvaliwa njuga kuanzia sasa kwa kutambua kwamba, sekta ya uvuvi ni muhimu sana katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kumbe inapaswa kupewa kipaumbele cha pekee, kwa kupewa mwelekeo wa kiutu; unaothamini wavuvi kama binadamu wenye utu, heshima na haki zao msingi. Kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kupambana na biashara haramu ya binadamu, dhamana inayoweza kutekelezwa vyema zaidi kwa njia ya ushirikiano kati ya Serikali, Mashirika ya Kimataifa na vyama vya kiraia.

Monsinyo Fernando Chica Arellano, anaendelea kudadavua kwa kusema, sekta ya uvuvi inaendelea kukua na kupanuka kiasi kwamba, kwa sasa kuna kiasi kikubwa sana cha samaki wanaosindikwa viwandani. Hali hii imepelekea kuibuka kwa kazi za suluba, ajira zisizo rasmi, ukosefu wa usalama kazini, hali inayopelekea kuwapo kwa mazingira magumu na hatarishi katika sekta ya uvuvi! Vitendo hivi vinatia uchungu na simanzi kwa wapenda haki duniani.

Ujumbe wa Vatican unakaza kusema, baadhi ya wavuvi wamejikuta wakitumbukia katika biashara haramu ya binadamu na viungo vyake; hali inayohitaji sera na mikakati itakayolinda na kudumisha, utu, heshima na haki msingi za wavuvi duniani. Mikataba na itifaki za kimataifa hazina budi kuzingatiwa. Tunu msingi za maisha ya kijamii na kiutu kama vile: haki, amani na mshikamano pamoja na maskini ni mambo msingi katika kukuza na kudumisha utu na heshima ya binadamu, aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Wavuvi waheshimiwe na kuthaminiwa; walindwe na kupewa haki zao msingi.

Jitihada hizi hazina budi kwenda sanjari na utunzaji bora wa mazingira ya bahari, kwa kulinda viumbe hai pamoja na kuwa na uvuvi endelevu na fungamani kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya kizazi cha sasa na kile kijacho! Ukwapuaji wa rasilimali za dunia ni hatari sana na kwamba, madhara yake yanaweza pia kuathiri sekta ya uvuvi. Tunu msingi za maisha ya kiroho nazo ni muhimu sana katika kulinda na kudumisha kazi ya uumbaji ambayo Mwenyezi Mungu amemkabidhi binadamu. Umoja, upendo, mshikamano na udugu ni mambo msingi yanayopaswa kudumishwa na wote, ili kukuza uvuvi endelevu na fungamani kwa ajili ya mafao ya watu wengi zaidi. Vatican itaendelea kushirikiana na FAO, Shirika la Kazi Duniani, ILO, na Shirika la Kimataifa la Shughuli za Majini,  IMO, ili kukuza na kudumisha malengo ya Jumuiya ya Kimataifa na kama sehemu ya utekelezaji wa Mafundisho Jamii ya Kanisa, kuhusu utunzaji bora wa kazi ya uumbaji.

Itakumbukwa kwamba, hivi karibuni, Kardinali Peter Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya Binadamu katika ujumbe wake kwa Jumapili ya Utume wa Bahari kwa Mwaka 2018 amekazia: changamoto wanazokabiliana nazo mabaharia katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku; ghasia na uharamia baharini; vyombo na mabaharia kutelekezwa pamoja na uchafuzi wa mazingira baharini. Katika maadhimisho ya Jumapili ya Utume wa Bahari, Mama Kanisa amewakumbuka mabaharia zaidi milioni 1.2 kutoka katika mataifa na dini mbali mbali wanaolazimika kuishi maisha ya shida sana katika vyombo vya usafiri baharini kiasi hata cha kushindwa kusherehekea matukio muhimu katika maisha ya familia zao.

Mabaharia wanachangia usafirishaji wa bidhaa zinazotumika sehemu mbali mbali za dunia kwa asilimia 90%. Mama Kanisa kwa kuthamini huduma na mchango wao, ndio maana ametenga Jumapili ya Utume wa Bahari kwa ajili ya kuwakumbuka, kuwaombea na kuwashukuru kutokana na mchango wao katika ustawi na maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu! Pamoja na shukrani zote hizi, lakini mabaharia na wavuvi wanakabiliwa na changamoto nyingi katika maisha na utume wao.

Kwa namna ya pekee aligusia kuhusu uchafuzi wa mazingira baharini, changamoto ambayo imevaliwa njuga na Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Laudato si”, yaani  “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”,  anakazia sana utunzaji bora wa mazingira kuwa ni changamoto inayojikita katika misingi ya haki, amani na mshikamano, kwa sababu mazingira ni sehemu muhimu sana ya maisha ya mwanadamu. Baba Mtakatifu anasema kuna haja ya kutunga sheria na sera makini zitakazodhibiti uzalishaji wa hewa ya ukaa angani kwa kuwekeza katika teknolojia na nishati rafiki na mazingira. Kuwepo na udhibiti madhubuti wa uchafuzi wa mazingira na uzalishaji wa hewa ya ukaa.

 

12 July 2018, 15:31