Vatican News
Papa Francisko awakumbuka na kuwaombea wanasiasa ili watambue kwamba, upendo ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha huduma ya upendo! Papa Francisko awakumbuka na kuwaombea wanasiasa ili watambue kwamba, upendo ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha huduma ya upendo!  (ANSA)

Papa Francisko: Siasa ni kielelezo cha hali ya juu cha upendo!

Siasa ni wito wa huduma miongoni mwa waamini walei ili kudumisha urafiki wa kijamii, ustawi, mafao na maendeleo ya wengi. Ni kwa njia hii, siasa inawawezesha watu kuwa ni wadau katika mchakato wa maendeleo yao wenyewe. Siasa inafumbata mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi, ili kukabiliana na changamoto zinazoendelea kuibuka katika ulimwengu mamboleo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, inalipa kwa vijana kujisadaka katika masuala ya kisiasa, huku wakiwa wamebeba amana na utajiri unaobubujika kutoka katika Injili ya Kristo na kwamba, siasa si sanaa inayomwezesha mtu kuratibu mamlaka, rasilimali na changamoto za maisha. Siasa ni wito wa huduma miongoni mwa waamini walei ili kudumisha urafiki wa kijamii, ustawi, mafao na maendeleo ya wengi. Ni kwa njia hii, siasa inawawezesha watu kuwa ni wadau katika mchakato wa maendeleo yao wenyewe, bila kuwahusisha watu mahalia, hapo hakuna siasa ya kweli! Siasa inafumbata mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi, ili kukabiliana na changamoto zinazoendelea kuibuka katika ulimwengu mamboleo! Fumbo la Umwilisho lililomwezesha Mwenyezi Mungu kuwa karibu zaidi na watu wake, liwe ni kigezo kwa wanasiasa kuwa karibu na wananchi wao ili kuweza kuwahudumia kwa upendo na majitoleo makuu! Kuhusiana na Siasa, Baba Mtakatifu anahimiza umoja na mshikamano katika utekelezaji wa mpango mkakati katika masuala ya kisiasa kadiri ya mwanga wa tunu msingi za Kikristo.

Maisha ya kijamii yanapaswa kurutubishwa na sheria ya upendo kwa Mungu na jirani; Kanuni maadili pamoja na ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo! Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican, Jumatatu, tarehe 20 Aprili 2020 amewakumbuka na kuwaombea wanasiasa kutoka sehemu mbali mbali za dunia, ili waweze kutambua dhamana na wito wao kuwa ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo. Haitoshi kwa mwamini kutekeleza Amri za Mungu, lakini pia anapaswa kujiaminisha chini ya maongozi ya Roho Mtakatifu anayewaongoza waja wake. Hii ni changamoto ya kujiaminisha katika uhuru wa Roho Mtakatifu. Kipindi hiki cha janga la homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, iwe ni fursa kwa wanasiasa kujikita zaidi katika kutafuta na kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi badala ya kuhangaikia masilahi ya vyama vyao vya kisiasa.

Katika mahubiri yake, Baba Mtakatifu alifanya rejea kwenye mazungumzo kati ya Kristo Yesu na Nikodemo, mmoja wa Mafarisayo aliyemwendea Kristo Yesu usiku ili kutaka kufahamu siri ya kuweza kuingia kwenye Ufalme wa Mungu! Siri kuu ni kuzaliwa mara ya pili katika maji na Roho Mtakatifu; na kumwachia nafasi Roho Mtakatifu ili kuratibu na kuongoza maisha ya waja wake. Hii ndiyo hali yake kila mtu aliyezaliwa kwa Roho Mtakatifu. Baba Mtakatifu amesema kwamba, si Mafarisayo wote walikuwa ni wabaya. Nikodemo ni kati ya Mafarisayo waliokuwa na shauku ya kutaka kuonana na Kristo Yesu! Baba Mtakatifu akifanya rejea kwenye Somo la Kwanza kutoka Kitabu cha Matendo ya Mitume Sura 4: 23-31 amesema, Jumuiya ya Wakristo ilikuwa imekusanyika katika sala, waliposhukiwa na Roho Mtakatifu, akawajaza nguvu ya kuweza kushuhudia na kutangaza Neno la Mungu kwa ujasiri.  Mitume walikuwa wamesimulia yale yaliyojiri wakati walipokamatwa, wakafungwa na hatimaye kufunguliwa na Wakuu wa Makuhani na wazee. Jumuiya ya Wakristo wa kwanza, ikatumia fursa hii kwa ajili ya kusali, ili kumwomba Mwenyezi Mungu aweze kuwalinda na kuwaongoza katika kipindi hiki kigumu, kwa kumwachia nafasi Roho Mtakatifu ili aweze kutenda kadiri anavyotaka.

Waamini walisali ili waweze kusimama kidete, kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa ujasiri mkuu, kwa kunyoosha mkono wake ili kuweza kuwaponya watu; ishara na maajabu vifanyike kwa njia ya Kristo Yesu. Hata walipokwisha kumwomba Roho Mtakatifu, wote wakajaa Roho Mtakatifu, wakanena Neno la Mungu kwa ujasiri. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, hii ilikuwa ni Pentekoste ya pili. Katika hali na mahangaiko yao ya ndani, kwa hofu ya Wayahudi, Jumuiya ya Wakristo wa kwanza ilimfungulia Roho Mtakatifu masikio ya nyoyo zao, ili kumsikiliza! Ili mwamini aweze kuzaliwa mara ya pili, kuna haja ya kujiandaa kwa njia ya sala, ili kumpatia nafasi Roho Mtakatifu aweze kutenda kwa uhuru katika maisha ya mja wake. Ujasiri wa kutangaza na kushuhudia Injili ni matunda ya mwamini anayejikabidhi chini ya maongozi ya Roho Mtakatifu. Mwishoni mwa mahubiri yake, amewaombea waamini ili Mwenyezi Mungu awasaidie kuwa wazi kwa Roho Mtakatifu, ili aweze kuwaongoza katika maisha na huduma yao kwa Mwenyezi Mungu. Baada ya Ibada ya Misa Takatifu, Baba Mtakatifu amewaongoza waamini na watu wenye mapenzi mema waliokuwa wakifuatilia Ibada hii ya Misa Takatifu kwa njia ya vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii, Kuabudu Ekaristi Takatifu na baadaye kusali Sala ya Malkia wa Mbingu inayotumika katika Kipindi hiki cha Sherehe za Pasaka.

Sala hii kwa lugha ya Kilatini:

Regína caeli laetáre, allelúia.

Quia quem merúisti portáre, allelúia.

Resurréxit, sicut dixit, allelúia.

Ora pro nobis Deum, allelúia.

Papa: Siasa: Mahubiri

 

20 April 2020, 14:13
Soma yote >