Vatican News
Virusi vya Corona, COVID-19: Baba Mtakatifu Francisko anawaalika wanasiasa na wanasayansi kutoka kipaumbele cha kwanza kwa ustawi, maendeeo na mafao ya wengi na wala si fedha! Virusi vya Corona, COVID-19: Baba Mtakatifu Francisko anawaalika wanasiasa na wanasayansi kutoka kipaumbele cha kwanza kwa ustawi, maendeeo na mafao ya wengi na wala si fedha! 

Mwaliko wa Papa Francisko: Kiteni sera zenu kwa maendeleo ya watu

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu ya Pasaka amewakumbuka na kuwaombea wanasiasa, viongozi wa serikali na wanasayansi kutafuta na hatimaye, kuambata njia muafaka itakayosaidia mchakato wa mapambano dhidi ya ya homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, - Vatican.

Maambukizi makubwa ya homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 yamezua athari kubwa katika medani mbali mbali za maisha ya watu! Nchi zimefunga mipaka yake, kumbe watu hawezi kutoka na kuingia. Shughuli za umma zimesimamishwa, biashara na shule zimefungwa ili kudhibiti maambukizi ya ugonjwa huu. Watu wanatakiwa kubaki wakiwa wamejifungia majumbani mwao. Mapambano dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19, yanahitaji: umoja na mshikamano wa kitaifa na kimataifa, sadaka na majitoleo kwa ajili ya ustawi,  maendeleo na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu ya Pasaka, 13 Aprili 2020, katika maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, amewakumbuka na kuwaombea wanasiasa, watunga sera, viongozi wa serikali na wanasayansi kutafuta na hatimaye, kuambata njia muafaka itakayosaidia mchakato wa mapambano dhidi ya homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu.

Baba Mtakatifu amefafanua kwa kina Liturujia ya Neno la Mungu: Injili ya Mtakatifu Mathayo: 28: 8-15 pamoja na Kitabu cha Matendo ya Mitume Sura 2: 14; 22-32. Siku ya kwanza ya Juma, Kristo Mfufuka alikutana na wanawake na kuwatuma kwenda kuwaambia ndugu zake watangulie Galilaya, ndiko watakakomuona. Mwinjili Mathayo anadokeza jinsi ambavyo askari walivyohabarisha yote yaliyojiri. “Wakakusanyika pamoja na wazee, wakafanya shauri, wakawapa askari fedha nyingi, wakisema, “Semeni, ya kwamba wanafunzi wake walikuja usiku, wakamwiba, sisi tulipokuwa tumelala”. Mt. 28: 12-13. Kiini cha Liturujia ya Neno la Mungu ni wito wa kuchagua kati furaha, matumaini yanayobubujika kutoka kwa Kristo Mfufuka au tabia ya kutaka kukumbatia kaburi! Wanawake wanaonesha dira na mwongozo wa kufuata kwa kutoka kwa haraka kwenda kutangaza na kushuhudia Fumbo la Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu! Ingawa katika Agano la Kale, ushuhuda wa wanawake haukuaminiwa sana, lakini, wanawake wamekuwa na dhamana na mchango mkubwa katika ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa hadi nyakati hizi.

Kaburi wazi lililokuwa na ulinzi mkali, ilikuwa ni changamoto kubwa ambayo baadaye, imezua: rushwa ili kuwanyamazisha watu kuhusu Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Askari katika Maandiko Matakatifu wanaoneshwa jinsi ambavyo wamekuwa waaminifu katika kazi na wajibu wao. Ijumaa kuu, Askari baada ya kuona jinsi ambavyo Kristo Yesu alivyokata roho akakiri na kuungama kwamba, kwa hakika mtu huyu alikuwa ni Mwana wa Mungu. Wazee, Makuhani, Mafarisayo na Waandishi “wakaamua kuchukua njia ya mkato” kwa kuwapatia rushwa askari, ili kupindisha ukweli juu ya Ufufuko wa Kristo Yesu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, hadi leo hii watu wengi hawamfahamu Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu kwa sababu, Wakristo hawajamtangaza sana kwa njia ya maneno, lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko, kielelezo cha imani tendaji, inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Rushwa na ufisadi ni njia inayotumiwa na Shetani, Ibilisi ili kuwalaghai watu wa Mungu. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, mapambano dhidi ya homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, siku moja yataweza kufikia ukomo wake!

Mwelekeo kwa wakati huo unapaswa kujikita zaidi katika ufufuko wa watu, kwa kukazia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo, vinginevyo, ikiwa kama “fedha” itapewa kipaumbele cha kwanza, watu wa Mungu watarejea tena kwenye makaburi ya: baa la njaa; mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo; vita, ghasia na kinzani. Huo utakuwa ni mwanzo wa kutengeneza, kulimbikiza pamoja na matumizi ya silaha. Matokeo yake, ni watoto kukosa fursa za kwenda shule kupata elimu na watu wengi kutumbukia katika ujinga na umaskini! Haya yote ni kielelezo cha makaburi mamboleo. Huu ni wakati wa kufanya maamuzi magumu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu badala ya kutanguliza fedha, ambalo ni kaburi la utu na heshima ya binadamu. Baada ya Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu na kutoa Baraka ya Sakramenti Kuu, Baba Mtakatifu Francisko amewaongoza watu wa Mungu kusali Sala ya Malkia wa Mbingu.

SALA YA MALKIA WA MBINGU

Malkia wa mbingu, furahi, Aleluya.

Kwani uliyestahili kumchukua, Aleluya.

Amefufuka alivyosema, Aleluya.

Utuombee kwa Mungu, Aleluya.

Furahi shangilia, ee Bikira Maria, Aleluya.

Kwani hakika Bwana amefufuka Aleluya.

TUOMBE. Ee Mungu, uliyependa kuifurahisha dunia kwa kufufuka kwake Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao: fanyiza, twakuomba, kwa ajili ya Bikira Maria, tupate nasi furaha za uzima wa milele. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.

Papa: Jumatatu ya Pasaka

 

 

 

13 April 2020, 13:38
Soma yote >