Vatican News
Papa Francisko asema, Jumatano Kuu inajulikana pia kuwa ni Jumatano ya Usaliti unaooneshwa kwa namna ya pekee na Yuda Iskariote anaye saliti upendo wa Kristo Yesu. Papa Francisko asema, Jumatano Kuu inajulikana pia kuwa ni Jumatano ya Usaliti unaooneshwa kwa namna ya pekee na Yuda Iskariote anaye saliti upendo wa Kristo Yesu. 

Papa Francisko: Jumatano ya Usaliti: Uchu wa Mali na Fedha!

Ni watu wanaosingizia kutaka kumtumikia Mungu, lakini, ukweli wa mambo ni kwamba, wanataka kujitarisha kwa kujihusisha na biashara ya binadam. Yuda Iskariote alikuwa ni mfuasi mkubwa wa Shetani, Ibilisi kwa sababu ya kumezwa mno na uchu wa fedha, kiasi cha “kudokoa” kile kilichokuwa kinatiwa kwenye hazina yao. Haiwezekani kuwatumikia Mabwana wawili, yaani Mungu na fedha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, - Vatican.

Michezo ya upatu na kamari ni donda ndugu linaloendelea kusababisha maafa na majanga makubwa katika maisha ya watu sehemu mbali mbali za dunia. Mchezo wa kamari na upatu ni matokeo ya myumbo wa uchumi kitaifa na kimataifa pamoja na kutopea kwa kanuni maadili na utu wema. Upatu ni dhambi kubwa inayopukutisha maisha ya watu na kudhalilisha utu, heshima na haki msingi za binadamu na hivyo kuwa ni chachu ya rushwa, ufisadi na kizingiti katika ustawi, maendeleo fungamani na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu Francisko katika Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Jumatano tarehe 8 Aprili 2020, amewaombea akina Yuda Iskariote katika ulimwengu mamboleo, yaani watu wanaojihusisha na magenge ya kihalifu kitaifa na kimataifa; wachezesha upatu pamoja na kamari, wanaojinufaisha kwa matatizo na mahangaiko ya watu wengine, kutubu na kumwongokea Mungu, tayari kuanza mwelekeo wa maisha mapya.

Hata katika shida na mahangaiko ya watu wengi kutokana na maambukizi makubwa ya homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 kuna watu ambao wanaendelea kujifaisha wenyewe kwa michezo ya upatu na kamari! Hawa ndio akina Yuda Iskariote katika ulimwengu mamboleo, wanaojihusisha na biashara ya binadamu na viungo vyake. Ni watu wanaosingizia kutaka kumtumikia Mungu, lakini, ukweli wa mambo ni kwamba, hawa watu wanataka kujitarisha kwa kujihusisha na biashara ya binadamu pamoja na viungo vyake. Yuda Iskariote alikuwa ni mfuasi mkubwa wa Shetani, Ibilisi kwa sababu ya kumezwa mno na uchu wa fedha, kiasi cha “kudokoa” kile kilichokuwa kinatiwa kwenye hazina yao. Haiwezekani kuwatumikia Mabwana wawili, yaani Mungu na fedha. Injili kama ilivyoandikwa na Mtakatifu Mathayo: 26: 14-25 inaonesha usaliti wa Yuda Iskariote kwa sababu alipenda sana fedha na matokeo yake ni usaliti na hatimaye kuishia kujinyonga. Baba Mtakatifu anakaza kusema, hata katika ulimwengu mamboleo kuna watu kwenye taasisi ambao si waaminifu hata kidogo, wana uchu wa fedha, mali na utajiri wa haraka haraka, kiasi kwamba, inakuwa ni rahisi kutumbukia katika kishawishi cha kusaliti upendo kwa fedha au mambo ya kidunia!

Yuda Iskariote alijinyonga na kutoweka katika uso wa dunia, lakini hata leo hii kuna wafuasi wake wengi wanaoendeleza biashara ya binadamu kiasi hata cha kuthubutu kuwauza ndugu na jamaa zao. Yuda Iskariote, aliwaendea mwenyewe wakuu wa Makuhani na kufanya nao biashara ili aweze kumsaliti Kristo Yesu. Uchu wa fedha ulichafua ule upendo ambao Kristo Yesu alikuwa anawaonesha Mitume wake. Jambo la kushangaza ni kuona kwamba, Kristo Yesu, hamtambui Yuda Iskariote kama “Msaliti”, bali rafiki, lakini anamwonya kwa kumwambia hadharani “Ole wake mtu yule ambaye anamsaliti Mwana wa Adamu. Ingekuwa heri kwake mtu yule kama asingalizaliwa!” Baba Mtakatifu anawakumbusha waamini kwamba, Shetani, Ibilisi, kamwe hawezi kuaminika. Anatoa ahadi na kuonesha mambo mazuri, lakini hatima ya yote haya ni kumwacha mtu katika hali ya kuchanganyikiwa na hatimaye ni kujikatia tamaa na hivyo kutema zaidi ya maisha. Huu ni muda kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuchunguza vyema dhamiri zao na kuangalia ukweli wa mambo! Kila mtu ana uwezo wa: kusaliti, kuuza na kuchagua mambo kadiri ya vionjo vya mtu binafsi. Mtu anaweza kuvutwa na hatimaye, kutumbukizwa kwenye uchu wa mali na fedha kwa sababu ndani ya kila mtu kuna Yuda mdogo. Baba Mtakatifu Francisko amehitimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa kuwapatia waamini na watu wote wenye mapenzi mema, Baraka ya Sakramenti kuu ya Ekaristi.

Papa Francisko: Jumatano ya Usaliti
08 April 2020, 13:32
Soma yote >