Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 15 Machi 2020 ametolea Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya wafanyakazi wote wanaoendelea kujisadaka wakati huu wa maambukizi ya Virusi vya Corona-COVID-19 Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 15 Machi 2020 ametolea Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya wafanyakazi wote wanaoendelea kujisadaka wakati huu wa maambukizi ya Virusi vya Corona-COVID-19  (Vatican Media)

Ibada ya Misa kwa wafanyakazi wanaojisadaka katika kipindi hiki cha Virusi vya Corona

Baba Mtakatifu amewashukuru wafanyakazi katika huduma ya afya, wafanyakazi katika maduka makubwa makubwa, madereva pamoja na vikosi vya ulinzi na usalama wanaowezesha walau kwa kiasi fulani maisha kusonga mbele. Baba Mtakatifu wakati wa mahubiri yake amefanya rejea katika Injili ya Jumapili ya tatu ya Kipindi cha Kwaresima, Mwaka A: Yesu chemchemi ya maji ya uzima!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko kama kielelezo makini cha mshikamano wa imani, matumaini na mapendo kwa watu wa Mungu wanaokabiliwa na tishio la Virusi vya Corona, COVID-19, Jumapili tarehe 15 Machi 2020, ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuwaombea wale wote wanaoendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma muhimu za kijamii. Baba Mtakatifu amewashukuru wafanyakazi katika huduma ya afya, wafanyakazi katika maduka makubwa makubwa, madereva pamoja na vikosi vya ulinzi na usalama wanaowezesha walau kwa kiasi fulani maisha kusonga mbele. Baba Mtakatifu wakati wa mahubiri yake amefanya rejea katika Injili ya Jumapili ya tatu ya Kipindi cha Kwaresima, Mwaka A wa Kanisa inayomwonesha Kristo Yesu akihojiana na Mwanamke Msamaria.

Baba Mtakatifu ameanza mahubiri yake kwa kusali Zaburi ya 24: 15-16: Sala katika taabu: “Uniangalie na kunifadhili, maana mimi ni mkiwa na mteswa, katika shida za moyo wangu unifanyie nafasi, na kunitoa katika dhiki yangu.” Mwinjili Yohane anasimulia kwa kina na mapana mahojiano ya kihistoria kati ya Kristo Yesu na Mwanamke Msamaria, tena mdhambi aliyeshindikana. Kwa mara ya kwanza katika Injili, Yesu anajitambulisha wazi wazi na kumsifia Mwanamke Msamaria kwa kuwa na ujasiri kiasi cha kumwambia ukweli kwamba, hakuwa na mume, bali katika maisha yake alibahatika kukutana na wanaume watano kwa nyakati mbali mbali. Na kwa ukweli huu, Mwanamke Msamaria anapata nafasi ya kumtambua Kristo Yesu kuwa ni Nabii na Masiha wa Mungu. Yesu anatumia fursa hii kumfafanulia kuhusu ukweli unaomtakasa na kumtakatifuza, ambacho ni kiini cha Injili.

Baba Mtakatifu anasema, kila mfuasi wa Yesu anao ukweli unaomtambulisha jinsi alivyo na wala si utaalamu wa kufafanua vifungu mbali mbali vya kitaalimungu, changamoto na mwaliko kwa wanafunzi wa Kristo kujenga na kudumisha utamaduni wa majadiliano. Mwanamke Msamaria alivutwa sana na hoja za Yesu kuhusu chemchemi ya maji, yanayobubujikia uzima wa milele, kwa sababu alitambua kwamba, kwa hakika alikuwa na kiu ya muda mrefu! Alikuwa na ujasiri kiasi cha kuthubutu kukiri na kuungama dhambi na udhaifu wake wa moyo unaomtambua Kristo Yesu kuwa Nabii wa Mungu. Yesu katika maisha na utume wake, alipenda zaidi kufanya majadiliano na watu katika ukweli na uwazi na kwa njia ya Roho Mtakatifu wanakirimiwa nguvu ya Roho Mtakatifu inayoyawezesha kumtambua Kristo Yesu kuwa kweli ni Mkombozi wa ulimwengu.

Baba Mtakatifu Francisko amehitimisha mahubiri yake kwa kusema kwamba, mahojiano kati ya Kristo Yesu na Mwanamke Msamaria yanahitimishwa kwa toba na wongofu wa ndani, si tu kwa Mwanamke Msamaria bali watu wa Samaria, kwa sababu walimsikia na kuamini kile alichokizungumza, kwa sababu hiki kilikuwa ni kipindi cha mavuno. Anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kumwomba Mwenyezi Mungu neema ya kusali daima katika ukweli na uwazi; kwa kumwendea jinsi walivyo na wala si kuwasilisha ukweli wa watu wengine, bali kuzungumza bila kumung’unya mung’unya maneno kwamba, kwa hakika, “nimekuwa na wanaume watano na huu ndio ukweli wangu”.

Papa: Mwanamke Msamaria

 

 

15 March 2020, 09:53
Soma yote >