Kumkiri Yesu kuwa ni Bwana ni neema ya Roho Mtakatifu
Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican
Watu wanasema mimi ni nini? Je ninyi mnasema mimi ni nani? Ni maswali yaliyomo katika Injili ya Liturujia ya siku ya Alhamisi 20 Februari 2020 ambayo Papa Francisko ameanza nayo katika tafakari yake kwenya Kanisa la Mtakatifu Marta, Vatican. Papa amesema Injili inatufundisha kunia zile nyayo ambazo mitume tayari walipitia ili kuweza kumtambua Yesu ni nani. Nazo ni tatu, kumjua, kumkiri na kukubali njia ambayo Mungu amechagua kwa ajili Yake.
Kukiri Yesu kwa neema ya Roho Mtakatifu
Kumjua Yesu ni tendo ambalo tunafanya sisi wakati tunaposhika Injili mikononi mwetu na kujaribu kumjua Yesu; tunapo wapeleka watoto katika katekisimu (…); tunapowaleka kuudhuria Misa, lakini hiyo ni hatua moja tu, anambainisha Papa, na hatua ya pili ni ile ya kuungama kwa Yesu. Lakini kufanya hivyo peke yetu hatuwezi. Katika Injili ya Matayo Yesu alimwambia Petro “hayo hayakutokana na wewe. Ni Baba yangu aliyekujalia” . Tunaweza kukiri Yesu tu kwa njia ya nguvu ya Mungu na kwa njia ya Roho Mtakatifu. Hakuna yeyote awezaye kusema Yesu ni Bwana bila kuwa na Roho. Kwa maana hiyo Jumuiya ya kikristo inatakiwa daima kutafuta nguvu ya Roho Mtakatifu ili kukiri Yesu na kusema kuwa Yeye ni Mungu na kwamba Yeye ni Mwana wa Mungu.
Kukubali njia ya Yesu hadi msalabani
Lengo la maisha ya Yesu nini? Kwa nini alikuja? Papa anatoa maswali haya na kujibu. Kujibu swali hili maana yake ni kutimiza hatua ya tatu ya kumtambua Yeye. Papa Francisko amekumbusha kuwa, Yesu alianza kufundisha mitume kwamba, ilitakiwa ateseke, auawe na baadaye afufuke. Kukiri Yesu ni kuthibitisha kifo na ufufuko wake; siyo kukiri kuwa wewe ni Mungu na kusimama hapo, hapana! “ ni kusema kuwa wewe umekuja kwa ajili yetu na umekufa kwa ajili yangu. Wewe umefufuka. Wewe unatupatia maisha, Wewe umetoa ahadi ya Roho Mtakatifu wa kutuongoza”.
Kukiri Yesu maana yake ni kukubali njia ambayo Baba amechagua kwa ajili yake yaani unyenyekevu. Barua ya Paulo kwa Wafilipi anasema: “ Mungu alimtuma Mwanae akajikana na akawa mtumishi, akanyenyekea hadi mauti, mauti ya msalaba”. Ikiwa hatukubali njia ya Yesu, njia ya unyenyekevu alioichangua Yeye kwa ajili ya wokovu, si kwamba si wakristo tu, bali tunastahili kile ambacho Yesu alimwambia Petro:“ Nenda nyuma yangu shetani!”
Asiyefuata njia ya unyenyekevu siyo mkristo
Papa Francisko katika ufafanuzi wake wa Injili ya Siku amebainisha pia suala la Shetani kuwa anajua vema kuwa Yesu ni Mwana wa Mungu, lakini Yesu anakataa kikiri kwake kama alivyo mwondoa hata Petro aliyekuwa anakataa njia aliyochagua Yesu. Kukiri Yesu ni kukubali njia ya unyenyekevu na kunyenyekeshwa. Ikiwa Kanisa halitembei katika njia hiyo ni kukokosea na kugeuka ya kidunia. Ikiwa tunaona wakristo wengi wema, wakiwa na mapenzi mema, lakini ambao wanachanganya dini na dhana ya wema wa kijamii, wa urafiki na wakati tukiona makleri wengine ambao wanasema wanafuata Yesu, lakini wanatafuta sifa, njia zenye mikato na sikikuu, njia za kidunia, jua wazi kwamba hawatafuti Yesu bali ni kujitafuta wao binafsi.
Uthabiti wa kikristo katika maisha na katika huduma
Siyo wakristo ambao wanasema ni wakristo lakini kwa jina tu, kwa sababu hawakubaliani na njia za Yesu, za unyenyekevu. Tunasoma hata katika historia ya Kanisa, Papa Francisko anasema kwamba maaskofu wengi waliishi namna hii na hata mapapa wa kidunia ambao hawakujua njia ya unyenyekevu; hawakukubaliana nayo, kwa maana hiyo Papa Francisko anahimiza kuwa “lazima kujifunza kuwa ile haikuwa ni njia”. Papa Francisko amehitimisha akiomba neema ya kuwa na uthabiti wa kikristo katika huduma za maisha na neema ya njia yake ya unyenyekevu na isije kuwa ile ya ukristo wa kubabaisha.