Baba Mtakatifu awataka Mapadre kuiga na kudumisha mfano bora wa maisha ya Mtakatifu Yohane Bosco katika utume wao! Baba Mtakatifu awataka Mapadre kuiga na kudumisha mfano bora wa maisha ya Mtakatifu Yohane Bosco katika utume wao! 

Papa Francisko awataka Mapadre kuiga mfano wa Mt. Yohane Bosco!

Mtakatifu Yohane Bosco aliwaona vijana maskini akatafuta mbinu mkakati wa kuweza kuwaendeleza, kwa kutembea pamoja na kuangaika nao katika hija ya maisha yao. Mapadre tangu siku ile wanapopewa Daraja Takatifu ya Upadre wakumbuke kwamba, wanaanza hija ya mateso ya watu wa Mungu. Ni wajibu wao kuwaangalia watu hawa kwa jicho la binadamu na jicho la Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mtakatifu Yohane Bosco, Padre, Baba na Mwalimu wa vijana wa kizazi kipya, anakumbukwa na kuadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 31 Januari. Katika maisha na utume wake miongoni mwa vijana, aliwataka vijana kuhakikisha kwamba, wanafuata kanuni ifuatayo kama sehemu ya mchakato wa utakatifu wa maisha! Aliwataka wawe ni vyombo na mashuhufa wa furaha ya Injili; wasome kwa bidii, juhudi na maarifa; wasali kwa Ibada na uchaji na mwishowe yote haya wayamilishe katika matendo mema!

Hii ndiyo changamoto ambayo imetolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 31 Januari 2019, wakati wa mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, kama sehemu ya kumbu kumbu ya Mtakatifu Yohane Bosco. Baba Mtakatifu anawataka mapadre kuwa na ujasiri wa kuangalia kwa kutumia jicho la binadamu na jicho la Mungu, ili kuguswa na mateso, mahangaiko na matumaini ya watu wa Mungu wanaokutana nao katika maisha na utume wao kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Yohane Bosco kwa vijana.

Mtakatifu Yohane Bosco aliwaona vijana maskini, waliokuwa wanataabika na kuishi katika mazingira magumu na hatarishi, akatafuta mbinu mkakati wa kuweza kuwaendeleza, kwa kutembea pamoja na kuangaika nao katika hija ya maisha yao. Mapadre tangu siku ile wanapopewa Daraja Takatifu ya Upadre wakumbuke kwamba, wanaanza hija ya mateso na mahangaiko na watu wa Mungu. Ni wajibu na dhamana yao kuwaangalia watu hawa kwa jicho la binadamu na jicho la Mungu. Ikumbukwe kwamba, mazingira na hali ya Mtakatifu Yohane Bosco yalikuwa ni magumu kweli kweli na kama mtu alitandikwa na umaskini, aliweza kuusikia kweli kweli bila utani. Kwa kuguswa na mahangaiko ya vijana hawa, akamua kuwekeza katika imani na matumaini kwa vijana.

Wakati ule Padre Giuseppe Cafasso alikuwa na utume maalum Jimbo kuu la Torino kwa sababu alikuwa anawahudumia wafungwa na mahabusu magerezani. Alikuwa na ujasiri wa kuwasindikiza wafungwa mpaka dakika ya mwisho wa maisha yao, wale waliokuwa wamehukumiwa adhabu ya kifo. Alikuwa ni rafiki mkubwa wa Mtakatifu Yohane Bosco. Ili kuweza kutekeleza dhamana na wajibu kama huu, Mapadre wanapaswa kuwa kweli ni watu wa sala, wanaotumia muda wao mwingi kwa ajili ya kutafakari Neno la Mungu na kulimwisha katika maisha na utume wao. Yohane Bosco hakuwa na Katekesimu ya Kanisa Katoliki, bali mikononi mwake alibeba Msalaba, kielelezo cha hekima, huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu. Akathubutu kuandamana nao katika Njia ya Msalaba wa maisha yao, kiasi kwamba, kwa vijana hawa akawa ni Baba, Mwalimu na Mlezi, sifa kuu za Padre mwema!

Baba Mtakatifu anawataka Mapadre kuacha kabisa kufikiri na kutenda kama watu wa mshahara, wanaoangalia muda wa kuingia na muda wa kutoka. Padre ni mtu anayepambana kwa kushikamana na Mwenyezi Mungu katika maisha, ili kuambata na hatimaye, kumwilisha upendo wa Mungu katika maisha ya watu wa Mungu. Baba Mtakatifu anamshukuru Mwenyezi Mungu aliyelizawadia Kanisa watakatifu kama Yohane Bosco! Mwishoni mwa mahubiri yake Baba Mtakatifu Francisko anasema, Mtakatifu Yohane Bosco katika ujana wake, alianza kufanya kazi ili mkono uweze kwenda kinywani! Alionja ugumu wa maisha, akajifunza Ibada na ukweli wa maisha, kiasi cha kukirimiwa na Mwenyezi Mungu moyo wa huruma na upendo, akawa kweli ni Baba na Mwalimu wa vijana. Ni Padre aliyebahatika kuwasaidia vijana kuwa ni mashuhuda wa furaha ya Injili, kwa sababu aliweza kuangalia changamoto za shughuli za kichungaji kwa jicho la Mungu na la binadamu!

Papa. Mt. Yohane Bosco

 

 

 

31 January 2019, 14:53
Soma yote >