Inakadiriwa kuwa, Jumuiya hii ilianza mnamo mwaka 1968 ikiwa inajulikana kama UMOJA WA WANAFUNZI WAKATOLIKI WATANZANIA ROMA. Inakadiriwa kuwa, Jumuiya hii ilianza mnamo mwaka 1968 ikiwa inajulikana kama UMOJA WA WANAFUNZI WAKATOLIKI WATANZANIA ROMA.  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Risala ya Watanzania Wakatoliki Italia Kwa Maaskofu Katoliki Tanzania

Madhumuni ya Jumuiya yetu: Kufahamiana, Kusaidiana katika nyanja mbalimbali za maisha ya Jumuiya yetu. Kumfanya kila Mtanzania kujisikia kuwa ni kiungo na sehemu ya lazima ya Jumuiya yetu. Kutambua, kudumisha, kuhifadhi na kutetea Utamaduni na hadhi ya Mtanzania. Kufurahi pamoja na kufarijiana pamoja na kumfanya mtanzania ajisikie nyumbani akiwa katika nchi ya ugenini. Kushirikiana na jumuiya nyingine za watanzania hapa Italia na nchi za A. Mashariki.

Na Padre Nicolaus Matungwa Gomano, Roma, Italia.

Mhashamu Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC, Wahashamu Maaskofu wakuu, Wahashamu Maaskofu, Mheshimiwa sana Padre Charles Kitima, Katibu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania pamoja na Msaidizi wako, mheshimiwa Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Balozi wa Tanzania nchini Italia) pamoja na ujumbe wako, wapendwa wanajumuiya wenzangu wa Jumuiya yetu ya Watanzania Wakatoliki Italia, wapendwa wageni wetu, TUMSIFU YESU KRISTO. Wahashamu Maaskofu, pamoja na wageni wetu, Jumuiya yetu ni Jumuiya ya Watanzania Wakatoliki Italia. Jumuiya hii inajumuisha Waklero (yaani Maaskofu, Mapadri na Mashemasi), pia Watawa (wa kike na wa kiume), Waseminari na Walelewa wa utawa. Hawa ni wanafunzi au wanaofanya kazi mbalimbali za kitume hapa nchini Italia. Jumuiya yetu kwa sasa ina wanajumuiya takribani 220 ambao wamejiandikisha. Inakadiriwa kuwa, Jumuiya hii ilianza mnamo mwaka 1968 ikiwa inajulikana kama UMOJA WA WANAFUNZI WAKATOLIKI WATANZANIA ROMA (Tanzanian Catholic Students in Rome/Italy). Kwenye kikao chetu cha tarehe 12.06.2021 tuliazimia kubadilisha jina la Jumuiya yetu na kuwa JUMUIYA YA WATANZANIA WAKATOLIKI ITALIA kwa sababu baadhi ya wenzetu waliokuwa hapa Roma kwa masomo na huduma mbalimbali wako katika miji mingine hapa Italia, hivyo wakaomba nao waendelee kuwepo katika Jumuiya hii ina hivyo kupelekea hata kubadili Katiba yetu mwaka 2022 ili iweze kuendana na uhalisia wa Jumuiya yenyewe kwa sasa.

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika Ibada ya Misa Takatifu
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika Ibada ya Misa Takatifu

MADHUMUNI ya Jumuiya yetu: Kufahamiana, Kusaidiana katika nyanja mbalimbali za maisha ya Jumuiya yetu. Kumfanya kila Mtanzania kujisikia kuwa ni kiungo na sehemu ya lazima ya Jumuiya yetu. Kutambua, kudumisha, kuhifadhi na kutetea Utamaduni na hadhi ya Mtanzania. Kufurahi pamoja na kufarijiana (mfano kushiriki katika Sherehe za wenzetu Watawa wanapoweka nadhiri zao, mwenzetu anapopata Sakramenti ya Daraja Takatifu na kutoa rambirambi pale mwenzetu anapoondokewa na wazazi, kaka na dada) na kumfanya Mtanzania ajisikie nyumbani akiwa katika nchi ya ugenini. Kushirikiana na Jumuiya nyingine za Watanzania hapa Italia na za nchi za Afrika Mashariki zilizoko hapa Italia. Kuadhimisha pamoja Ibada mbalimbali zilizopendekezwa na Katiba yetu katika kusherehekea sikukuu za Kitaifa za Taifa letu la Tanzania na za Kikanisa, pia kusherehekea kwa pamoja kwa sababu ya madhumuni fulani fulani pale inapoonekana inafaa kufanya hivyo.

Baraza la Maaskofu Katoliki  Tanzania Ad Limiba Visit 2023
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania Ad Limiba Visit 2023

MAFANIKIO: Tumefanikiwa kuwa pamoja sio tu kama wakatoliki, lakini kama watanzania kama katiba yetu inavyotutaka. Hii imejidhihirisha katika kupeana mkono wa pole pale mwenzetu anapofiwa na wazazi, au kaka au dada. Lakini pia katika furaha, kwenye matukio kama nadhiri kwa watawa au Daraja Takatifu. Kusali pamoja hasa tunapokutana kwenye mikutano yetu mbalimbali ambayo ni mara tatua u mara nne kwa mwaka, tukifuata mwaka wa masomo kwa sababu wengi ni wanafunzi. Kufanya mafungo ya mwezi kama katiba yetu inavyotutaka kwenye moja ya mikutano yetu, mmoja uwe mafungo ya mwezi au hija, angalau mara moja kwa mwaka. CHANGAMOTO. Ukosefu wa mahali pa kukutania na kufanya mikutano yetu. Imekuwa changamoto kubwa wakati fulani kupata sehemu ya kufanyia mikutano yetu. Hivyo, tulikuwa tunaleta ombi kwenu baba zetu Maaskofu kuwa kama itawapendeza tupate parokia hapa Roma, kama ilivyo kwa nchi nyingine mfano Nigeria wana parokia yao hapa Roma ambayo ni makubaliano baina ya Jimbo Kuu la Roma na Baraza la Maaskofu nchini Nigeria. Hii parokia itakuwa inahudumiwa na Mapadri watanzania walioteuliwa kutoka kwenye Baraza lenu na kwa namna hiyo kupata sehemu ya kufanyia mikutano yetu, lakini pia kusali pamoja. Pia itakuwa sehemu ya kufikia hata ninyi mnapokuja hapa Roma.

Watanzania wanaosoma na kuishi Italia
Watanzania wanaosoma na kuishi Italia

SHUKRANI: Kwako mpendwa sana Baba yetu, Askofu Mkuu Protase Rugambwa mmoja wa walezi wa Jumuiya yetu. Tunasikitika kwamba hatimaye tunakuaga ili ukatimize majukumu mapya uliokabidhiwa na Kanisa. Umekuwa nguzo kubwa katika Jumuiya yetu kwa kipindi chote ulichokuwa hapa Roma. Tunakutakia kila lililo jema na baraka za Kristo Mfufuka ziambatane nawe daima kwa wana wa Mungu Jimboni Tabora. Tunakuahidi sala zetu, nawe usiache daima kutukumbuka katika Altare ya Bwana. Tunakushukuru sana sana kwa malezi yako, majitoleo yako, nasaha zako na zaidi moyo wako wa kibaba katika Jumuiya yetu. Hakika ni hazina kwa Kanisa na kwa namna ya pekee kwa wana Tabora. Mungu azidi kukumiminia neema zake, ili matunda haya yakawe baraka kwa Taifa la Mungu Jimboni Tabora na kwa Kanisa zima. Tunakutakia safari njema utakapoondoka kurudi nyumbani. Baadaye tutakukabidhi zawadi yetu, kama ishara ya shukrani zetu kwa yale yote uliyotutendea. Tunatoa shukrani zetu kwenu ninyi Maaskofu wetu, mliokubali kushiriki nasi siku ya leo, na kuweza kukutana na Kanisa la Tanzania hapa Italia, kwa namna ya pekee wale mliotutuma kwa masomo na majukumu mbalimbali ya utume. Tumefarijika kwa ujio wenu huu. Tunazidi kuwaombea baraka za Kristo ziwaongoze daima katika kuchunga kundi alilowakabidhi. Tunawatakia safari njema mtakaporudi nyumbani. Tunatoa pia shukrani kwenu nyote wanajumuiya kwa ushirikiano mkubwa mnaotupatia sisi viongozi wenu hadi sasa katika kujenga na kudumisha umoja wetu na kufanikisha shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na matukio haya ya mkutano na sherehe zetu. Tunamshukuru pia kwa namna ya pekee Gambera wa “Collegio San Paolo” kwa kutupatia nafasi ya kufanyia mkutano wetu hapa. Mungu ibariki Afrika, Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Jumuiya yetu na mbariki kila mmoja wetu aliyepo hapa. Asanteni kwa kunisikiliza. RISALA HII IMEANDALIWA NA UONGOZI WA JUMUIYA YA WATANZANIA WAKATOLIKI ITALIA NA KUSOMWA KWENU NAMI MTUMISHI WENU PADRE NICOLAUS MATUNGWA GOMANO, (Katibu). Roma, 21.05.2023.

Wanafunzi Watanzania

 

 

27 May 2023, 14:05