Sinodi-Afrika Bw.Annang:mchakato wa sinodi ni kama njia ya kidemokrasia
Sr. Jecinter Antoinette Okoth, FSSA
Sinodi ya bara iliyomalizika hivi karibuni mjini Addis Ababa, Ethiopia ilianza tarehe 1-6 Machi 2023, ambapo wajumbe wa Imani na dini nyingine walishukuru kuhusika kwao katika mchakato wa sinodi ya Kikatoliki huku wakibainisha kwamba Kanisa linarejea katikamizizi yake. Sinodi inayoendelea ya Maaskofu iliyoanza mnamo mwaka 2021 na inayotarajiwa kumalizika mnamo mwaka 2024, inaongozwa na kaulimbiu: “Kwa ajili ya Kanisa la Sinodi: Ushirika, ushiriki na utume,” kwa hiyo mkutano wa Juma moja wa Bara la Afrika ulileta pamoja washiriki 209 wanaojumuisha vijana, walei, wajumbe kutoka dini nyingine, wanaume na wanawake watawa, mapadre maaskofu na Makadinali.
Kwa upande wa Mwakilishi wa walei kutoka Mkutano Mkuu wa Kanisa la Kipresbyterian nchini Ghana akishirikisha maoni yake na AMECEA katika mahojiano Jumamosi tarehe 4 Machi 2023, ambapo Bwana Ludwig Annang Hesse alirejea maneno ya Bwana Bourial ambaye alikuwa ni Mjumbe kutoka nchini Tunisia na Mwandishi wa Habari wa Tunisia juu ya kuthamini ushirikishwaji na uwazi wa Kanisa Katoliki. “Mfumo wa sinodi ni wa kuvutia kwani tunajua Kanisa Katoliki kuwa la Maaskofu tofauti na Kanisa la Kipresbyterian ambalo tuna haki ya demokrasia juu ya jinsi tunavyofanya shughuli kwani maamuzi hufanywa na mkutano mkuu au baraza” alisema Bwana Annang.
Akiendelea na maelezo yake alithamini kujiunga na Kanisa Katoliki na kuwa sehemu ya mchakato wa sinodi ya kuzungumza juu ya yale ambayo huenda yakaonekana kuwa ya wasiwasi kwa Kanisa lakini ambayo alisema “Huduma ya Kikristo ni zaidi ya Wakatoliki pekee. Mfumo huu wa sinodi katika Kanisa Katoliki ulionekana kuwa mpya kwangu nilipousikia kwa mara ya kwanza, lakini nimeupenda mchakato hasa dhana ya mazungumzo ya kiroho ambayo nadhani ni sehemu ya demokrasia. Hiyo ndiyo dhana ya kupata mawazo na kuhusisha kila mtu kuwa na la kusema”. Bwana Annang ambaye amekuwa mwalimu wa huduma ya watoto katika Kanisa la Kipresbyterian nchini Ghana kwa miaka 45, alifichua kwamba uekumene una nguvu nchini humo kwa kuwa wale wa “Makanisa ya Kiprotestanti, Makanisa ya Kipentekoste, Makanisa ya Karismatiki na Kanisa Katoliki kwa kawaida hukutana ili kuzungumza masuala ya kawaida kama vile ya kujenga amani na suala la Wasagaji, Mashoga, Wapenda jinsia mbili, Wanaobadili jinsia na Queer ( LGBTQ).
Kiongozi huto aidha alikiri kwamba kabla ya kuhudhuria mkutano wa sinodi ya bara nchini Ethiopia,wajumbe waliotambuliwa walikuwa na mikutano miwili ya kuhamaisha sinodi ambapo walikuwa na nuru kuhusu mchakato wa sinodi na walitoa waraka wa kazi ili kusoma na kuelewa zaidi kuhusu sinodi. Bwana Annang alithamini mchakato wa sinodi ambao umechukua nafasi kwa wote kama kaka na dada na mbinu ambayo alisema “inaweza kutumika katika nafasi pana zaidi.” Kutokana na uzoefu wake Kanisa mahalia tayari linapitia mabadiliko na hata ingawa mtihani halisi utapatikana baada ya 2024, kwamba “Mtu hawezi kupitia mchakato wa miaka minne na kubaki vile vile.”