Vijana wa ulimwengu huko Assisi ili kueneza uchumi wa Francisko
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Ni karibia vijana elfu moja wanauchumi kutoka katika mchi 120 ulimwenguni waliofika kwa ajili ya kushiriki Toleo la Tatu la Economy of Francesco, yaani “Uchumi wa Francisko, tukio lililozinduliwa na Papa kwa ajili ya kutaka kueneza uchumi unaostahili na wenye thamani ya udugu. 'Uchumi wa Francisko', harakati ya kimataifa ya wanauchumi vijana, wajasiriamali wanaojishughulisha na mchakato wa mazungumzo jumuishi, ulizaliwa baada ya barua ya Papa Francisko, iliyotumwa mnamo 2019 kwa wanauchumi vijana, wajasiriamali na ulimwenguni kote. Kutokana na wito huo umekuwa mchakato wa kufikiria kwa upya uchumi. Mikutano miwili ya kwanza ilifanyika kwa njia ya mtandaoni kutokana na janga la uviko-19.
Toleo la Tatu la Uchumi wa Francisko kufunguliwa 22 Septemba 2022
Hatimaye katika tukio la toleo la Tatu limefunguliwa asubuhi tarehe 22 Septemba 2022. Aliyekuwa akiwapokea vijana kati ya watu wa kujitolea na Staff ya Uchumi wa Francisko, mmojawapo alikuwa ni Sr. Francesca Violato wa Shirika la Wafranciskani wa Mtakatifu Elizabeth au (Bettine huko Padua Italia) ambaye ni mmisionari nchini Equador kwa miaka 20. Katika mahojiano na mwandishi wa habari wa Vatican News, walioko huko Assisi amesema: “Kuna ulimwengu ambao unamiminika Assisi. Ulimwengu wa vijana, wanaopenda uchumi. Na ilikuwa nzuri kuwaona wakifika: hakukuwa na shida ya lugha kwa sababu tabasamu, kumbatio havikukosekana. Udugu ulipumuliwa. Machoni mwangu nina sura ya vijana wanaofika kituoni: safu ndefu ya vijana wenye shauku”.
Samuel Lekato:Kukutana na Papa ni kitu ambacho sitosahau maisha yangu
Na kwa upande wa Kijana mmoja Mmsai, Samuel Lekato, kutoka nchini Kenya, katika mahojiano na Mwandishi wa Vatican News kuhusu tukio linaloendelea katika jiji la Assisi amesema alivyokuja “kujumuika na vijana wengine kutoka ulimwenguni kote ambao ni viongozi na kila mtu”. Samuel pia ameeleza kuhusu sifa ya utamaduni wao wa kimasai kwamba ni adabu, kwani “kama wamasai tunaamini kushikilia sana tamaduni zetu” na hivyo kwa kuongezea yeye amesema kuwa “tamaduni nyingine sio za kupoteza, lazima kuzizingatia maana ni fahari kwetu nchini Kenya”.
Katika suala la uzoefu ambao atauchota kutoka katika Toleo hilo la Tatu la “Uchumi wa Francisko”, Samuel amesema jinsi gani “Ninatarajia kupata uongozi kwani nimekuwa kiongozi wa muda mrefu na ninaona uongozi huko ndani mwangu hivyo ni imani yangu kwamba nitaimarika katika uongozi wangu zaidi”. Hatimaye akifafanua hisia yake ya kukutana na Baba Mtakatifu Francisko anayetarajia kuwa Assisi, Jumamosi tarehe 24 Septemba 2022, Samuel Lekato amebainisha kwamba "ni kama fursa nzuri ambayo si kila mtu anapata kumwona na kumsalimia, kitu mbacho sitakisahau katika maisha yangu”, amehimitimisha, Samuel.