Fr.Mavula&Fr.Malo:Ujumbe wa Papa wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana ni shule kwa jamii
Na Angella Rwezaula- Vatican.
Dominika tarehe 18 Septemba 2022 mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwa waamini na mahujaji waliofika katika uwanja wa Mtakatifu Petro Vatican, Radio Vatican ilifanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Radio Maria Tanzania, Padre Dominick Mavula wa Shirika la Damu Azizi, pamoja na Padre Shadrack Malo, Radio Maria Kisumu nchini Kenya.
Baba Mtakatifu Francisko katika tafakari yake leo hii, imeangukia kwenye Injili ya Luka 16,1-13, ambayo amebainisha kuwa inaonesha ufisadi wa mwakili na tajiri. Ni kwa jinsi gani mada hii ni muhimu sana kusisitiza katika jamii yetu, ambayo kila upande ufisadi, au tuseme kwa neno rahisi ukosefu wa uaminifu unaathiri mazingira yote kuanzia ndani ya familia hadi kufikia taasisi kuu?
Ujumbe wa Baba Mtakatifu ni shule nzuri katika jamii ya sasa, ya dunia hii kwa sababu kusema neno lenyewe ufisadi ni neno dogo kulitamka lakini ni pana na ni baya sana katika jamii. Ufisadi ni mfumo unapoanza katika hatua moja na kwenda kula katika hatua kubwa zaidi. Kwa maana hiyo kama ni shina la mti, ni kama mchwa unaokula kuanzia kwenye mizizi mpaka kwenye majani. Kwa namna hiyo ni ngumu kwa yeyote aliyeko katika mfumo huo au mche kutokuwa nje ya ufisadi, ama kutopata madhara ya ufisadi. Kwa njia hiyo janga hilo lililozungumzwa na Baba Mtakatifu ni janga ambalo linatafuna sana jamii ya binadamu; na kweli inahitajika kujitathimini wajibu wetu kama wanadamu hapa duniani, kwa maslahi mapana ya wenzetu tunaoishi nao na wale ambao tumekabidhiwa wajibu wa kuweza kuwatunza. Na hii ni kwa sababu tukifanya ufisadi tunaathiri watu wengi zaidi hata wale ambao hawana hatia wanaathirika na mambo haya.
Kwa upande wa Padre Shadrack Malo akizungumzaia kuhusu mtazamo huo wa ufisadi amekuwa na la kuongeza kusema. Ni vema kuwajibika katika Malaka tuliopewa, kutoa habari kamili kulingana na uwezo tulio nao na hasa katika ofisi tulizonazo, kutoa habari kamili ili kuweza kupambana na ufisadi.
Papa leo katika tafakari amehimiza juu ya mwaliko wa Yesu, kuwa wabunifu na kutenda mema kwa hekima na busara ya Injili, kwa kutumia mali ya ulimwengu huu, si tu ya zana lakini hasa zawadi zote tulizopokea kutoka kwa Bwana. Na zaidi akasema si kujitajirisha binafsi lakini kwa ajili yetu na kwa ajili ya ndugu. Kuhusiana na ushauri huo padre Mavula alikuwa na haya ya kueleza.
Ni wito mzuri na unawagusa kwa namna ya pekee kundi la watenda kazi, wenye nguvu ya kufanya kazi kwa sababu tumekirimiwa vipawa na mazingira, hivyo tunakundi kubwa la watu wenye uwezo wa kufanya kazi, lakini hawapo katika kundi la uzalishaji katika nadharia ya kutokuwa na ajira, kwa sababu Baba Mtakatifru anavyotuambua leo hii ni kutukumbusha kwamba Mungu ametukirimia zawadi za pekee, uwezo wa kufikiri, wa kutenda na tukijumlisha hayo yote kwa hekima. Hekima yenyewe iliyo kuu kwa kumwomba Mwenyezi Mungu atuongoze kujua tufanye nini. Bilashaka inawezekana kutumia mazingira yetu rahisi kabisa na mashine rahisi kabisa, ama nyenzo rahisi kabisa tukabadilisha hali ya maisha yetu. Na ndio huko kutumia vipaji na karama tulizopewa na Mwenyezi Mungu, lakini pia kutenda kwa kwa hekima zaidi kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Tumeshuhudia vijana katika sehemu kadhaa, hawana elimu kubwa ya kutosha, lakini kwa kukaa chini na kufikiria, kwa msaada wa Mwenyezi Mungu wameweza kusogea mbele katika Maisha yao. Kwa njia hiyo tuna vipawa, tuna karama, tuna elimu na baadaye lakini wengine wanayo bahati ya kuweza kusonga mbele, na kwa kuthubutu kufanya kazi ili mambo yote yaweze kuwa na maana katika Maisha yetu.
Kwa upande wa Padre Shadrack Malo alitoa hisia yake katika kuunganika na umati kwenye uwanja wa Mtakatifu Petro kusali sala ya Malaika wa Bwana na Baba Mtakatifu Francisko.
Ni mara yangu ya kwanza kufika hapa na pia kusikiliza mahubiri ya Papa moja kwa moja na niliguswa sana kwa sababu watu kutoka nchi mbali mbali walivyo jaa kwenye uwanja wa Mtakatifu Petro kusikiliza Papa alivyoongea kwa watu na pia kusikiliza mahubiri yake, na sio tu mahubiri pekee lakini pia tendo la kupokea baraka kutoka kwa Baba Mtakatifu. Ningependa pia kusema tusilalie vipawa tulivyopewa na Mwenyezi Mungu. Ni lazima twende kutekeleza wajibu wetu.
Katika ziara yao jijini Roma na nchini Italia kwa ujumla, Mkurugenzi wa Radio Maria Tanzania alisisitizia umuhimu wa kile walichojifunza kujikita nacho katika matendo.
Katika ziara ambayo tumefanya kama mababa wa kiroho wa Radio Maria mbali mbali za Afrika, hasa kwa nchi zinazozoungumza kiingereza, tumepata mang’amuzi mengi ya kutosha, lakini hasa ni kutukumbusha umuhimu wetu sisi kama wanadamu. Kwanza katika jamii, lakini pili umuhimu wa uwajibu tuliopewa kuwa wainjilishaji kwa kutumia Radio Maria, kwa namna ya pekee; na wajibu huo kila mara tunapaswa kufuata roho ya kimaria, Mama yetu Bikira Maria alipofanya ziara yake kwa Elizabeth, Mungu aliongea naye kupitia kwa kinywa cha Elizabeth. Na baada ya kusikiliza yale yatokayo kwa Mungu hakwenda tena kulala usingizi, bali alizana kufanya kazi. Alianza kuhudumia na kumbe na sisi katika ziara tuliyoifanya tumesikia ujumbe wa Mungu kupitia vinywa vya watu mbali mbali, wajibu wetu sasa ni kwenda kuwajibika na kutenda wajibu ambao tunatamani kufanya na watu katika jamii.
Na kwa upande wa Padre Shadrack Mkurugenzi wa Radio Maria Kisumu, kuhusiana na ziara hiyo ya mafunzo alikuwa na machache ya kuongezea
Radio Maria Sauti ya Kikristo nyumbani mwetu na tumepokea sauti ya Kristo kutoka kwa walimu wetu, waliokuwa wakituelekeza katika mafundisho yetu kwa siku tatu na pia ziara yetu. Tunaporudi nyumbani kama alivyotangulia kusema mwenzangu, ni lazima sauti ya kikristo isikike katika nyumbani mwetu.