2022.05.17 Askofu Timothée Bodika Mansiyai wa Jimbo katoliki la Kikwit nchini DRC 2022.05.17 Askofu Timothée Bodika Mansiyai wa Jimbo katoliki la Kikwit nchini DRC 

Askofu wa Kikwit huko DRC:Ziara ya Papa ni tarajio la upatanisho

Askofu Timothée Bodika Mansiyai anasema yuko tayari kwa ajili ya kumpekea Papa katika ziara yake ya kitume ya katika nchi yake kuanzia tarehe 2 hadi 5 Julai 2022 na katika mahojiano na“Shirika la Kipapa la Kanisa Hitaji” anaeleza matarajio ya waamini.Kutoka kwa Papa Francisko, anasema,”tunatarajia ujumbe wa upatanisho kwa nchi iliyojeruhiwa.”

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Askofu  Timothée Bodika Mansiyai, wa Jimbo Katoliki la  Kikwit, katika eneo la kati -magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC ametoa maoni yake, katika mahojiano na  Shirika la Kipapa la Kanisa Hitaji kuhusiana na matarajio ya ziara ya Papa Francisko, ambaye atawasili katika nchi ya Afrika kuanzia tarehe 2 hadi 5 Julai 2022. Askofu Timothée Bodika Mansiyai amesema: “Habari za ziara ya Papa zilipotangazwa kwa umma, tulisisimka. Huyu ndiye Mtakatifu Petro anayekuja kwetu. Anakuja kama Mchungaji, ili kututhibitisha  imani, na tunahisi kubarikiwa sana na ziara yake” .  

Ni baada ya miaka 37,  Papa anarudi DRC:Wakatoliki wanasali

Miaka 37 baada ya ziara ya Mtakatifu Yohane Paulo II, Baba Mtakatifu Francisko atakutana na waamini wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na kwa Wakatoliki huu ni wakati wa furaha na shauku kubwa. Ili tujitayarisha vizuri  kwa ajili ya ujumbe ambao Papa atapeleka  katika nchi iliyojaa mivutano kutokana na vitendo vya makundi yenye silaha, ambayo yanawakabili watu, Askofu  Bodika, ameeleza kwamba wanasali  sala ya maandalizi ya ziara hiyo ya Baba Mtakatifu kila mwishoni mwa  kila adhimisho la Misa.

Papa ataweza kuona walei na vijana walio hai

Katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ni nchi kubwa na tajiri sana, lakini kuna mateso mengi katika jamii. Kwa maana hiyo askofu wa Kikwit amesema Papa anakwenda kwao  katika wakati wa taabu sana katika maisha ya nchi yao ambapo upatanisho bado uko mbali. Kwa kuendelea amesema: "Kwa mfano, itakuwa Goma, ambako kuna mvutano mkubwa, kuna makundi yenye silaha ambayo yanaeneza ugaidi kwa sababu za ubinafsi, hata ikiwa ni sehemu tajiri zaidi ya nchi". Mkutano na Papa Francisko  pia utakuwa fursa ya kujulisha baadhi ya sifa za Kanisa Katoliki mahalia nchini Congo DRC, kwa maana hiyo askofu amesisitiza kuwa Nchi yao  mara  baada ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatikani, walijitahidi sana kuimarisha walei katika Kanisa, na kwamba angependa kuwambia Baba Mtakatifu kwamba Yeye ni Rais wa Tume ya Maaskofu ya Walei, hivyo ataweza kuona walei hai na ataona vijana walio hai.

20 May 2022, 13:29