Kardinali Polycarp Pengo anaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu apewe Daraja Takatifu ya Upadre 20 Juni 1971. Seminari kuu ya Segerea inafanya kumbukizi la miaka 43 tangu kuanzishwa kwake. Kardinali Polycarp Pengo anaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu apewe Daraja Takatifu ya Upadre 20 Juni 1971. Seminari kuu ya Segerea inafanya kumbukizi la miaka 43 tangu kuanzishwa kwake. 

Kardinali Polycarp Pengo: Seminari Kuu ya Segerea Miaka 43

Seminari kuu ya Segerea ambayo imetimiza miaka 43 tangu kuanzishwa, Gambera wake wa kwanza alikuwa ni Padre Polycarp Pengo, kwa sasa Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam. Tunasherehekea miaka 43 ya Seminari tukiichukulia kama uzinduzi wa Jubilei ya Miaka 50, miaka saba baadaye, ili kuendelea kumshukuru Mungu.

Na Rev. Dr. Fr. Richard Laurian Tiganya, C.PP.S. - Dar es Salaam.

Tarehe 14 Januari 2022 ilikuwa siku ya shangwe na vifijo, pongezi kwa Baba Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, Tanzania kwa kutimiza miaka 50 ya Upadre, sambamba na miaka 43 ya Seminari kuu ya Segerea. Kama ilivyo kawaida Sikukuu kama hizi huanza kwa Misa Takatifu, na hivi Misa Takatifu ilianza saa 3:00 kamili Asubuhi katika Kanisa la Seminari, ikitanguliwa na maandamano yaliyosheheni furaha, nyimbo, ngoma na nderemo kwa ajili ya Baba Mwadhama Polycarp Karidinali Pengo na kuanzishwa kwa Seminari kuu. Nyimbo maarufu zilizotawala maandamano, wimbo wa Tazama anakuja kuhani, kuhani mkuu ulikuwa mmojawapo! Misa Takatifu iliongozwa na Baba Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo akiwa na Mapadre 14, kati ya hao 12 walikuwa Walimu na Walezi na wawili waliobaki wakiwa ni Wageni waalikwa seminarini.

Mara tu baada ya kufika Altareni kwa kuanza adhimisho la Ibada ya Misa Takatifu, Baba Gambera wa Seminari, Padre Tobias Ndabhatinya akimwalika Baba Mwadhama kwa ajili ya kuongoza adhimisho hilo, alitoa utangulizi akisema, tunamshukuru Mungu kwa Miaka 50 ya Upadre wa Baba Mwadhama, lakini pia kwa ajili ya miaka 43 tangu kuanzishwa Seminari kuu ya Segerea. Utangulizi uliendelea kuweka mambo wazi ya kwamba Seminari hii ambayo imetimiza miaka 43 tangu kuanzishwa, Gambera wake wa kwanza akiwa ni Padre Polycarp Pengo, kwa sasa Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam. Tunasherehekea miaka 43 ya Seminari tukiichukulia kama uzinduzi wa Jubilei ya Miaka 50, miaka saba baadaye, Gambera alizidi kufafanua.

Katika mahubiri yake, Baba Mwadhama Polycarp Pengo alikazia mambo makuu matatu ambayo yalilenga kukazia wito wa kila mmoja wa Mafrateri lakini pia udumifu katika wito wa Upadre kwa maana ya wale waliokwisha pokea Daraja Takatifu. Jambo la kwanza lilikuwa ni juu ya Uvumilivu unaosimikwa katika Hekima na Usikivu wa watu wawili yaani Samweli na Eli. Jambo la pili lilikuwa ni lile la kumwachia Mwenyezi Mungu nafasi atufinyange na kutuongoza pasipo kumwekea masharti. Na Jambo la tatu lilikuwa juu ya kipaji cha Ukuhani, kwamba ni kwa kila mmoja wetu pasipo kutazama kabila au utamaduni wake. Jambo hili la tatu lilisimikwa katika msingi wa ukuhani wa Melkisedeki, alieleza Baba Mwadhama Polycarp Pengo. Akifafanua mambo matatu tajwa, Baba Mwadhama alianza kusema kila anayeitwa anapaswa siku zote kuwa mvumilivu na msikivu kwa wanaomwongoza wakiwakilishwa na Eli tunayemsikia daima katika Kitabu cha Samweli.

Kijana Samweli anapoitwa na Bwana, wakati huo ni usiku anafikiri anaitwa na Eli na hivi anamwendea Eli na kumwambia mimi hapa, maana umeniita. Samweli hakuonesha ukaidi kwa mwito ule kwa kuwa ni usiku, maana angeweza kusema, huyu Mzee ni msumbufu ananiita usiku, amepitwa na wakati! Na mbaya zaidi ni lile jibu la Eli “nenda kalale sijakuita.” Kijana Samweli anavumilia na anamwendea Eli mara kadhaa, mpaka alipate jibu la hakika ‘nenda ukiitwa, sema “Nena Bwana kwa kuwa mtumishi wako anasikia.” Kwa upande wa msindikizaji ambaye ni Eli, kuna alama ya uvumilivu wa hali ya juu, ya kwamba katika umri ule, muda ule ulikuwa ni muda wa mapumziko, ni usiku. Eli angeweza kumwona Samweli kama kijana msumbufu asiyejali afya ya wazee. Na labda angeweza kufikiri kwamba amekunywa mvinyo zaidi, uliombofusha akili. Kumbe anavumilia ili kijana Samweli afikie utimilifu wa mwito wake. Anagundua kuwa kijana Samweli alikuwa katika hatua ya kuhakiki wito wake. Ndiyo kusema wito wetu unakua kwa kupitia hatua zilizopangwa na Mwenyezi Mungu na kuratibishwa na Kanisa.

Katika jambo la pili, Baba Mwadhama Polycarp Pengo aliwaalika Mafrateri na Mapadre wote, akisema tunapoitwa na Mungu mwenyezi, tusimwekee masharti, ndiyo kusema, tujiachilie, tujisalimishe katika mapendo yake ya kibaba, atufinyange na kutuunda kadiri ya mapenzi yake. Samweli hakuweka sharti lolote bali alijisalimisha kwa Mungu akisema ‘Nena Bwana kwa kuwa mtumishi wako anasikia’. Akiendelea kumega Neno la Mungu, Baba Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo alifafanua hoja yake ya tatu akisema, ukuhani tunaoupokea katika Kanisa ni kwa mfano wa Melkisedeki Kuhani Mkuu. Huyu Kuhani mkuu hajulikani anatokea wapi, hata wazazi wake hawajulikani! Ndiyo kusema wito wa ukuhani ni kipaji cha Mungu apewacho awaye yote anayestahili pasipo kutazama anatokea kabila gani wala ukoo gani. Kumbe, hakuna awaye yote mwenye uwezo wa kuweka masharti kulingana na kabila la mtu, bali kulingana na mapenzi ya Mungu.

Kisha tafakari hiyo alimshukuru Mungu kwa wito katika Kanisa na zaidi kwa mapaji aliyomjalia katika kipindi chote cha utumishi mpaka anapoadhimisha miaka hamsini ya Upadre na 38 ya Uaskofu. Baada ya shukrani hizo Liturujia ya Misa Takatifu iliendelea kama kawaida mpaka mwisho. Ili kutunza kumbukumbu, baada ya Misa Takatifu kulikuwa na tukio la kupiga picha, yaani Baba Mwadhama na Mapadre, Masista, Mafrateri na Waamini wengine walioshiriki adhimisho la Misa Takatifu. Wapiga picha walikuwa tayari kwa zoezi hilo muhimu kwa historia ya Seminari na maisha Baba Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo. Kwa tukio hili sehemu ya kwanza ya sherehe ilifikia mwisho wake kwa ufanishi kabisa.

Sehemu ya pili ya Maadhimisho ya Sherehe ya Miaka 50 ya Upadre wa Mwadhama na miaka 43 ya Seminari tangu kuanzishwa, ilipambwa na michezo, nyimbo, mashairi, maigizo yenye dhima ya kumpongeza Baba Mwadhama na viburudisho, lakini hasa chakula kilichoandaliwa na wapishi mahiri. Sehemu hii ya pili ilitanguliwa na mapumziko mafupi ambapo Baba Mwadhama, Gambera wa kwanza wa Seminari kuu ya Segerea, alipata nafasi ya kuzunguka na kujionea maendeleo ya Seminari kuu ya Segerea katika kipindi cha miaka 43 iliyopita. Jambo hili lilimpa faraja na furaha Baba Mwadhama kiasi cha kuamsha ari ya kusimulia yaliyojiri wakati Seminari inaanza. Mambo hayo yaligusa kazi nzito ya kujenga Seminari kimiundo mbinu, kimalezi na zaidi matukio magumu katika miaka hiyo ya mwanzo!

Kila penye sherehe hapakosi nderemo na vifijo na zaidi sana “Kinywaji Mlipuko (Champagne), keki furaha na mshikamano wa udugu wa kibinadamu, kumbe zilikuwepo chupa mlipuko za kutosha zikiambatana na keki mbili moja ikiwa kwa ajili ya Baba Mwadhama kutimiza miaka 50 na nyingine kwa ajili ya Seminari kuu kutimiza miaka 43. Kufunguliwa kwa kinywaji mlipuko na kukatwa kwa keki furaha, kuliipamba sherehe na kuongeza furaha upeo, vigelegele vikisikika ukumbi mzima! Hongera Baba Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo! Sherehe haikuishia hapo bali wakati Kinywaji mlipuko na Keki furaha vinaendelea kutumika historia ya maisha ya Mwadhama iliwekwa machoni pa washiriki wa sherehe, hakika iliamsha ari ya kusimama kidete katika miito yetu.

Ni katika muktadha wa kumbukizi hili la kihistoria waliokuwepo walipata fursa ya kufahamu kwa undani historia ya Seminari kuu ya Segerea, hakika Segerea kumekucha na Walatini wanasema, “Segerea kunogile.” Lililo na mwanzo lina mwisho, furaha ikafikia muda wa hairisho na hivi Baba Gambera Padre Tobias Ndabhatinya akiwashukuru wote walioandaa sherehe, akimshukuru Baba Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo kwa kukubali mwaliko wa Seminari, alimwalika Baba Mwadhama, mgeni rasmi aweze kutoa Neno na kufunga kwa Sala mnamo saa 8:45 hivi. Neno la Mwadhama lilibeba ujumbe wa shukrani kwa Mungu na kwa Seminari kwa ajili ya tukio lenyewe. Amina.

Segerea Miaka 43
18 January 2022, 16:00