Burkina Faso:Kanisa la Afrika kupokea Masalia ya Mt.Andrea Kim Dae-geon
Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican.
Masalia ya Mtakatifu Andrea Kim Dae-geon, padre wa kwanza na mfiadini wa kikorea ambayo sasa yanakaribishwa katika ardhi ya Afrika, na ambayo yamehifadhiwa katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu huko Koupéla nchini Burkina Faso. Katika ishara hiyo ya kina ni kutaka kusisitiza uhusiano uliopo kati ya Wakatoliki wa Korea Kusini na wa Burkina Faso. Na hivi karibuni, Kanisa Kuu hilo limekarabatiwa shukrani kwa mchango uliokusanywa kutoka katika Parokia ya Yeouidokatika mji wa Seoul , Korea Kusini. Si hilo tu lakini hata mwezi Juni 2021 huko Seoul walitoa zawadi ya dola 200,000 kwa ajili ya kusaidia dharura katika Nchi za Afrika ya Kati.
Imani ya kuungana kwa upendo wa Mungu
Tarehe 23 Novemba 2021, Askofu Mkuu wa Seoul, Kardinali Andrew Yeom Soo-jung, alikabidhi masalia ya mfiadini huyo ikiwa ni fursa ya kumbu kumbu ya miaka 200 tangu kuzaliwa kwake, kwa Monsinyo Julien Kaboré, mwenye asili ya mji wa Koupéla na Mshauri wa Ubalozi wa kitume nchini Ufilipini lakini mwanzo aliwahi kuwa katika Nchi hiyo. Katika tukio hilo pia alishiriki hata Askofu msaidizi, Job Koo Yobi, wa Seoul aliyepewa utume wa kushughulikia masuala ya Nje. Katika fursa hiyo Kardinali Soon- jung alisema kuwa: “Ninayo furaha kupewa fursa ya kujenga mshikamano wa kidugu kati ya Kanisa Katoliki la Nchi ya Korea Kusini na Burkina Faso kwa njia ya Mtakatifu Andrea Kim Dae-geon. Kardinali anaamini kuwa hili litawaruhusu kuungana kwa kina katika upendo wa Mungu, kama ishara ya kudumu ya umoja na ushirikiano wa kimisionari. Na kwa mujibu wa Monsinyo Kaboré, ni heshima kuhifadhi masalia ya mtakatifu wa kwanza wa Korea katika Kanisa la Burkina Faso; ni ishara ya umoja na muungano wa watakatifu. Mshauri wa Ubalozi ameelezea alivyoshangazwa kwa kina na historia ya ufidiani katika Kanisa katoliki la Korea, kabla ya kufika Ufilipini katika mchakato wake wa huduma, akiwa katika ubalozi wa Kitume wa Vatcican nchini Korea.
Monsinyo Kaboré aliomba Askofu Mkuu Yeom Soo-jung masalia kwa Jumuiya yake
Monsinyo Kaboré alipata fursa ya kujua historia ya wafidini wa Korea. Na baadaye katika fursa ya Jubilei iliyoanzishwa na Kanisa la Korea Kusini kwa ajili ya maadhimisho ya miaka 200 ya kuzaliwa kwa Mtakatifu Andrea, iliyohitimishwa mnamo tarehe 27 Novemba 2021, Monsinyo Kaboré alimwomba Askofu Mkuu Yeom Soo-jung zawadi hiyo kwa ajili ya Jumuiya Katoliki ya Nchi yake. Kwa sasa masalia mengine ya mtakatifu wa Kikorea, aliyetangazwa na wengine wafiadini 102, mnamo tarehe 6 Mei 1984 na Mtakatifu Yohane Paulo II, yapo katika maeneo mengi, ya peninsula na nje, kwa mfano nchini Italia, Macao na Indonesia.
Mshikamano na ushirikiano katika mafunzo ya kikuhani, kiafya na tiba
Kuanzishwa kwa mazungumzo na mshikamano kati ya Korea Kusini na Burkina Faso yanafanyika katika muktadha wa mkataba uliofanyika wakati wa ziara mnamo 2018 ya Kardinali Yeom Soo-jung katika nchi ya Afrika. Huo ni mshikamano wa kuongeza nguvu za ushirikiano katika uinjilishaji na kwa ajili ya kuhamasisha maendeleo endelevu, ya sekta ya kifedha na mafunzo nchini Burkina Faso. Shukrani kwa mkataba huo, umeweza kuongezwa hadi 2024, Jimbo Kuu la Seoul katika miaka mitatu, wameweza kufadhili mafunzo ya mapadre na waseminari wa Ouagadougou, kwa kuwaalika wajifunze katika Seminari ya Kitaalimungu ya Seoul na katika mantiki ya kiafya, wameanzisha ushirikiano kati ya Hospitali ya Mtakatifu Maria na Hospitali ya Paulo VI, hata kwa ajili ya mafunzo ya udaktari.