Askofu Joseph R. Mlola: Ushemasi ni Huduma Kwa Watu wa Mungu
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Daraja ya Ushemasi “Diakonia” huwapa wadarajiwa chapa isiyoweza kufutwa na hufananishwa na Kristo Yesu aliyejifanya Shemasi, yaani mtumishi wa watu, kama ilivyojionesha siku ile iliyotangulia kuteswa kwake, alipowaosha miguu Mitume wake kielelezo cha Injili ya upendo unaomwilishwa katika huduma makini kwa watu wa Mungu kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko. Utume na dhamana ya Mashemasi katika maisha ya Kanisa ni kwamba, wao ni wasaidizi wa karibu wa Maaskofu mahalia. Hawa ni wahudumu wa Neno la Mungu, Mafumbo ya Kanisa kadiri ya daraja lao na hasa zaidi wadau wakuu katika utekelezaji wa matendo ya huruma kwa maskini, na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Maskini ni watu ambao Kristo Yesu aliwapatia kipaumbele cha kwanza katika maisha na utume wake. Huu ni wito wa kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu, Kristo na Kanisa lake. Wito huu ni kwa ajili ya mafao ya Kanisa na wala si fursa ya mtu kujitafuta mwenyewe. Mashemasi wawe na huruma na wenye bidii wakienenda katika ukweli wa Bwana Yesu Kristo aliyejifanya mtumishi wa watu! LG 29. Mashemasi wanawekwa wakfu kwa ajili ya huduma ya upendo kwa watu wa Mungu; ni mashuhuda wa utakatifu wa watu wa Mungu unaopata chimbuko lake katika maisha ya Sala za Kanisa; tafakari ya Neno Mungu na nidhamu katika maisha ya utii, useja na ufukara.
Ni katika muktadha huu, Askofu Joseph Roman Mlola ALCP/OSS wa Jimbo Katoliki Kigoma, tarehe 20 Januari 2022 ametoa Daraja takatifu ya Ushemasi kwa Majandokasisi watano wa Jimbo Katoliki la Kigoma. Katika mahubiri yake, amedadavua historia ya huduma ya Kikuhani kwa watu wa Mungu tangu Agano la Kale na changamoto zilizojitokeza katika Agano Jipya kiasi cha Mitume wa Yesu kuamua kuwachagua watu wenye sifa kwa ajili ya huduma ya kimwili na Mitume wakaendelea kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Askofu Mlola kwa namna ya pekee kabisa, amewaalika watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Kigoma kusali kwa ajili ya kuombea miito mitakatifu ndani ya Kanisa, lakini zaidi wasali kwa ajili ya Mapadre, ili Kanisa liweze kuwapata Mapadre, wema, watakatifu na wachapakazi, wanaoweza kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu na jirani zao. Hao wanapewa dhamana ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Ni wajibu wa waamini kuwakumbuka na kuwaombea Mashemasi wapya, ili kile ambacho Mwenyezi Mungu ameanzisha ndani mwao, aweze kukikamilisha, yaani waweze kufikia Daraja Takatifu ya Upadre.
Ili kuweza kufikia huko, kuna haja ya kujikita katika kuziishi Amri za Mungu na kuendelea kukaa katika pendo lake. Kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake, Kristo Yesu, amewashirikisha waja wake: huruma, msamaha na upendo usiokuwa na kifani; unaobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Mashemasi wapya wanahamasishwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa watu wa nyakati hizi. Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuwahamasisha watu wa Mungu kutambua kwamba, wanayo dhamana na wajibu wa kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yenye mvuto na mashiko. Kwenye dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa, Baba Mtakatifu anakazia ukuhani wa waamini wote na umuhimu wa waamini kushiriki kikamilifu Sakramenti za Kanisa. Anahimiza majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni ili kujenga udugu wa kibinadamu. Anapenda kuhamasisha ari na mwamko wa kimisionari pamoja na umuhimu wa waamini walei kuwa ni chachu ya uinjilishaji mpya na utakatifu kwa njia ya ushuhuda wa maisha, kama kielelezo makini cha imani tendaji!
Askofu Joseph Roman Mlola ALCP/OSS wa Jimbo Katoliki Kigoma amehitimisha mahubiri yake kwa kusema, umoja, upendo na mshikamano wa dhati ni mambo msingi katika utangazaji na ushuhuda wa Injili ya upendo kwa watu wa Mataifa. Dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa inajikita katika: Ufahamu wa kina wa Neno la Mungu; umuhimu wa toba na wongofu wa ndani; ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Haya ni mambo msingi katika mchakato mzima wa uinjilishaji mpya katika ulimwengu mamboleo na kwa namna ya pekee Jimbo Katoliki la Kigoma. Waamini waendelee kujikita katika dhana ya: Umoja, Ushiriki na Utume wa Kanisa unaofumbatwa katika umisionari. Mashemasi wapya wa Jimbo Katoliki la Kigoma, wanaojiandaa sasa kwa ajili ya Daraja Takatifu ya Upadre ni: Shemasi Bernard Vyokuta kutoka Parokia ya Katubuka. Shemasi Christopher Kitandala kutoka Parokia ya Makere. Shemasi Noel Romwald kutoka Parokia ya Kumwerulo. Shemasi Eusebius Ntibinona kutoka Parokia ya Kabanga na mwishoni katika idadi hii ni Shemasi Joseph M. Wassira kutoka Parokia ya Kidahwe. Ibada ya Misa Takatifu imeadhimishwa kwenye viwanja vya Kanisa la Seminari Ndogo ya Mtakatifu Yosefu Iterambogo.
Ni katika kunogesha tu yajayo huko mbeleni: Itakumbukwa kwamba, Askofu Joseph Mlola alipewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 12 Julai 1997. Tarehe 10 Julai 2014 akateuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Kigoma. Kumbe, ikimpendeza Mwenyezi Mungu katika huruma na upendo wake mkuu, Mashemasi hawa wapya watawekwa wakfu kuwa Mapadre tarehe 12 Julai 2022 kama sehemu ya uzinduzi wa Jubilei ya Miaka 25 tangu Askofu Mlola apewe Daraja Takatifu ya Upadre. Lakini kwa vile hii ni sikukuu ya Mapadre wapya, Askofu Joseph Mlola ataadhimisha kilele cha Jubilei ya Miaka 25 ya Upadre hapo tarehe 14 Agosti 2022 kwa kujikabidhi chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria. Kama kawaida, wazamiaji hawakosekani, lakini ikumbukwe kwamba, Kigoma, ndo mwisho wa Reli! Yajayo yanatia imani, matumaini na mapendo!