Tafakari ya Neno la Mungu Sherehe ya Yesu Kristo Mfalme wa Ulimwengu. Tafakari ya Neno la Mungu Sherehe ya Yesu Kristo Mfalme wa Ulimwengu. 

Kristo Yesu Ni Mfalme, Mwokozi na Mkombozi wa Ulimwengu Wote!

Kristo Yesu ni Mfalme na Mchungaji mwema wa wanadamu wote kwa maisha ya sasa hapa duniani na maisha yajayo mbinguni baada ya kufa; kwani Yeye ndiye Mfalme, hakimu na Mwokozi wetu. Kumbe iwe tu hai au tumekufa, kama anavyotuambia Mt. Paulo tu mali yake Kristo. Kumbe tunapoadhimisha sherehe hii tunapaswa kujiuliza kama kweli maisha yetu yanaakisi utawala huu!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 34 ya mwaka B wa Kanisa kipindi cha kawaida. Hii ni Dominika ya mwisho wa mwaka wa kiliturjia na dominika ijayo tunaanza mwaka mpya wa Kiliturujia mwaka C kwa dominika ya kwanza ya majilio. Kadiri ya utaratibu wa Mama Kanisa, Jumapili hii tunaadhimisha Sherehe ya Yesu Kristo Mfalme. Sherehe hii iliidhinishwa na Baba Mtakatifu Pius wa XI mwaka 1925 akiuambia ulimwengu kwamba: “Dunia haiwezi kuuepa utawala wa Kristo kama inataka kubaki salama.” Kwa kuwa tangu mwanzo, wakristo waliogopa kumwita Kristo Yesu Mfalme, kwa kuhofia kumfananisha na wafalme wa dunia hii, Baba Mtakatifu Pius XI alisisitiza kuwa; “Wakristo tusiogope wala tusione aibu juu ya kumkiri Kristo kuwa Mfalme, Mwokozi na Mkombozi wetu kwani Pilato alipomwambia; Wewe u Mfalme basi? Yesu alijibu; Wewe wasema, kwa kuwa mimi ni mfalme” (Yn.18:37). Kwa mwaka mzima Kanisa limetukumbusha ya kwamba: Kristo Yesu ni Mfalme na Mchungaji mwema wa wanadamu wote kwa maisha ya sasa hapa duniani na maisha yajayo mbinguni baada ya kufa; kwani Yeye ndiye Mfalme, hakimu na Mwokozi wetu. Kumbe iwe tu hai au tumekufa, kama anavyotuambia Mtume Paulo tu mali yake Kristo.

Kumbe tunapoadhimisha sherehe hii tunapaswa kujiuliza kama kweli maisha yetu yanaakisi utawala wa Yesu Kristo ndani mwetu, kama kweli tunamtumikia, na tuko chini ya utawala wake au tuko chini ya falme na tawala zingine ambazo kwazo kwa maisha yajayo zitatuangamiza milele yote. Kumbe sherehe hii inatuhimizwa kumfuata Kristo Yesu mfalme wetu, kusudi mwishowe atukaribishe katika ufalme wa milele mbinguni. Katika somo la kwanza la kitabu cha Nabii Danieli (7:13-14); tunakutana na tangazo la utukufu wa Masiha anayekuja mwisho wa nyakati. Danieli anasimulia alichokiona katika ndoto akisema; “Niliona katika njozi za usiku, na tazama, mmoja aliye mfano wa mwanadamu akawa pamoja na mawingu ya mbingu akamkaribisha huyo mzee wa siku, wakamleta karibu naye. Naye akapewa mamlaka, na utukufu, na ufalme, ili watu wa kabila zote, na taifa zote, na lugha zote, wamtumikie, mamlaka yake ni mamlaka ya milele, ambayo haitapita kamwe, na ufalme wake ni ufalme usioweza kuangamizwa.” Kadiri ya somo hili mmoja aliye mfano wa mwanadamu akija katika mawingu ni mfano wa Taifa teule la Israeli ambalo linatukuzwa na kuchukuliwa na Mungu baada ya kuteswa sana. Katika Agano Jipya huo ni mfano wa Yesu Kristo ambaye, baada ya mateso yake ametukuzwa na kufanywa mfalme na hakimu haki milele yote.

Somo la pili la Kitabu cha Ufunuo (1:5-8); linahusu kufunuliwa kwa yale yaliyofichika. Kitabu hiki kilichoandikwa na Mtume Yohane mwishoni mwa maisha yake, miaka 60 baada ya kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo, lengo lake ni kutangaza ushindi wa mwisho wa Bwana wetu Yesu Kristo, na ushindi wa wafuasi wake. Somo hili linatuonyesha kuwa Kristo ni Mfalme mwenye nguvu na ukuu wake hauna mwisho. Ni “Mkuu wa Wafalme wa dunia” (Ufu 1:5), “Mfalme wa Wafalme na Bwana wa Mabwana” (Ufu 19:16). Yohani anapotumia cheo au jina hilo anawakumbuka Wakuu wa Warumi ambao kimsingi walikuwa wametawala ulimwengu wote uliojulikana kwa wakati ule kuwa Yesu ndiye Bwana na Mfalme wa maisha yote. Tukumbuke kuwa nyakati hizo sanamu ya mkuu wa Warumi iliwekwa kila mji na watu walilazimishwa kumwabudu. Cheo cha Bwana kilikuwa ni kwa ajili ya mfalme wa Kirumi tu. Wakristo wa kwanza walikataa kumwabudu mfalme wa Kirumi kadiri walivyoamriwa na sheria. Wengi walikubali kupoteza maisha yao kwa kufa mashahidi kuliko kuiabudu sanamu.

Kinyume chake walimwita Kristo kuwa “Bwana” wakikiri; “Wewe peke yako ndiye Bwana.” Kwa maneno haya waliikiri imani yao kwa Yesu bila kuogopa mateso na kuuawa. Wafalme wa dunia hii wanaweza kuwa na nguvu na uwezo lakini Yesu ndiye Uweza na Nguvu yenyewe kama alivyotabiri Danieli katika somo la kwanza akisema; “Naye akapewa mamlaka na utukufu na Ufalme ili watu wa kabila zote, na taifa zote na lugha zote wamtumikie, mamlaka yake ni mamlaka ya milele, ambayo haitapita kamwe, na ufalme wake ni ufalme usioweza kuangamizwa (Dan 7:14.) Ndiyo maana Yohani katika somo la pili anaandika; “Mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho asema Bwana Mungu, aliyeko, aliyekuwako, na atakayekuja, Mwenyezi” (Ufu 1:8). Alfa ni jina la herufi “A” ambayo ni kwanza katika alfabeti za Kigiriki na Omega ni jina la herufi “O” ambayo ni ya mwisho katika alfabeti za kigiriki. Kumbe Yesu ni mwanzo na mwisho wa kila kitu.

Injili ilivyoandikwa na Yohane (18:33-37); inatuonesha jinsi Yesu alivyojidhihirisha kama Mfalme wakati wa mateso yake na katika mahojiano yake na Pilato. Yesu Kristo ni kweli mfalme. Lakini utawala wake si wa siasa bali ni utawala wa mbinguni sababu Yeye alifika kubomoa uadui kati ya Mungu na binadamu. Alijenga utawala wa mbinguni kwa kuleta ukweli juu ya Mungu ili wale waliokuwa maadui wa Mungu waweze kumrudia. Kumbe tunaona kuwa masomo haya yanatupa ujumbe wa kutuimarisha sisi tuliowafuasi wake Yesu na kutuasa tuishi kijasiri na kwa furaha kwa kuwa: Mamlaka na uwezo wa Mfalme Kristo ni kuu kuliko mamlaka na uwezo wa wafalme wa dunia hii. Utangulii wa Sherehe ya Yesu Kristo mfalme inaupa Ufalme wake sifa zifuatazo; Ufalme wa kweli na maisha. Ufalme wa utakatifu na neema. Ufalme wa haki, upendo na amani. Basi na tumfanye Yesu Kristo awe mfalme wa maisha yetu ili tuweze kuwa na maisha ya neema, haki, upendo na amani.

Tafakari J34
17 November 2021, 14:44