Jimbo Katoliki la Kigoma, tarehe 21 Novemba 2021 linatabaruku Kanisa kuu la Bikira Maria Mshindaji lililojengwa kuanzia mwaka 1932 na kukamilika mwaka 1950 lilipotabarukiwa kwa mara ya kwanza. Jimbo Katoliki la Kigoma, tarehe 21 Novemba 2021 linatabaruku Kanisa kuu la Bikira Maria Mshindaji lililojengwa kuanzia mwaka 1932 na kukamilika mwaka 1950 lilipotabarukiwa kwa mara ya kwanza. 

Kanisa Kuu la Bikira Mshindaji Jimbo Katoliki Kigoma Latabarukiwa

Jimbo Katoliki la Kigoma, nchini Tanzania, katika maadhimisho ya Sherehe ya Kristo Yesu Mfalme wa Ulimwengu, tarehe 21 Novemba 2021 linatabaruku Kanisa kuu la Bikira Maria Mshindaji. Kwa mara ya kwanza Kanisa hili lilitabarukiwa na Askofu David Mathew, Balozi wa Vatican kunako tarehe 15 Agosti 1950. Askofu Joseph Mlola alianza mchakato wa ukarabati mkubwa 6 Machi 2019.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Fumbo la Ekaristi Takatifu ni chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Ni ishara thabiti na sababu ya hali ya juu kabisa ya ushirika katika uzima wa kimungu na umoja wa Taifa la Mungu ambalo hulifanya Kanisa liwepo. Ekaristi Takatifu ni kilele cha tendo la Mungu la kuutakatifuza ulimwengu katika Kristo Yesu na kilele cha tendo la waamini kuliabudu Fumbo la Utatu Mtakatifu. Kanisa ni mahali patakatifu panapowawezesha waamini kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu, Kuabudu, Kusali na Kutafakari Matendo makuu ya Mungu katika maisha yao. Waamini wanapaswa kutambua kwamba, Liturujia ni chemchemi ya kwanza na ya lazima ambayo toka kwake waamini wanaweza kuchota roho ya kweli ya Kikristo. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kitume “Misericordia et misera” anawaalika waamini kuendelea kushuhudia na kumwilisha huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya Mafumbo ya Kanisa, hasa Liturujia na Sakramenti za Kanisa, Neno la Mungu, Matendo ya huruma kiroho na kimwili. Baba Mtakatifu anasema, Ekaristi Takatifu, Upatanisho na Mpako wa wagonjwa ni Sakramenti za huruma ya Mungu. Ni mahali pa kuonja upendo, toba, wongofu wa ndani na msamaha kwani huruma yake ni kuu na huvuka kila vikwazo na vizingiti katika maisha ya mwanadamu! Kwa njia ya huruma, waamini wataweza kumwilisha upendo huu katika uhalisia wa maisha yao!

Ni katika muktadha huu, Jimbo Katoliki la Kigoma, nchini Tanzania, katika maadhimisho ya Sherehe ya Kristo Yesu Mfalme wa Ulimwengu, tarehe 21 Novemba 2021 linatabaruku Kanisa kuu la Bikira Maria Mshindaji. Kwa mara ya kwanza Kanisa hili lilitabarukiwa na Askofu David Mathew, Balozi wa Vatican kunako tarehe 15 Agosti 1950, Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni Mwili na Roho! Kanisa lilianza kujengwa kunako mwaka 1932 na Askofu Joseph Birraux wakati huo akiwa ni Askofu wa Vikarieti ya Tanganyika na kutumaini kurejea tena kunako mwaka 1936 lakini hakurejea tena baada ya kuchaguliwa kuwa Mkuu wa Shirika la Wamisionari wa Afrika, WF. Ujenzi ulicheleweshwa sana kutokana na kufumuka kwa Vita Kuu ya Pili ya Dunia kati ya Mwaka 1939 hadi mwaka 1945. Watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Kigoma, wanamkumbuka sana Bruda Ubaldi aliyefariki dunia baada ya kuanguka kutoka darini, wakati akijitahidi kuokoa maisha ya mfanyakazi wake aliyekuwa ameteleza, lakini hakuanguka na badala yake akaanguka na kufariki hapo hapo!

Kumbukumbu zinaonesha kwamba, uzinduzi wa Kanisa hili, ulihudhuriwa na viongozi wa Kanisa pamoja na Bwana Edward Twining, Gavana wa Tanganyika wakati ule. Kwa mara nyingine tena, watu wa Mungu Kigoma, walishikwa na simanzi baada ya Padre Gerard Janseen, tarehe 16 Agosti 1950 alipofariki dunia kutokana na ajali ya gari. Hata hivyo, Kanisa kuu la Bikira Maria Mshindaji liliendelea kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuadhimishia Mafumbo ya Kanisa. Lilifanyiwa ukarabati mkubwa kunako mwaka 1970 kwa kuondoa vigae na kuweka mabati. Katika maadhimisho ya Jubilei kuu ya Miaka 2000 ya Ukristo, Kanisa kuu la Bikira Maria Mshindaji liliadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu lilipotabarukiwa kwa mara ya kwanza, likiwa limejengewa mnara wenye kofia “Lilasayangana”. Kanisa hili liliheshimiwa sana kwa kuwa ni Makao makuu ya Hayati Askofu Alphonce D. Nsabi, Askofu wa kwanza Mzalendo wa Jimbo Katoliki la Kigoma, Apumzike katika usingizi wa amani, Amina.

Mchakato wa ukarabati mkubwa wa Kanisa kuu la Bikira Maria Mshindaji Jimbo Katoliki Kigoma ni sehemu ya maono na mawazo ya Askofu Joseph Roman Mlola, ALCP/OSS, wa Jimbo Katoliki la Kigoma. Ukarabati ulianza rasmi tarehe 6 Machi 2019. Hatua ya kwanza kabisa ya maadhimisho haya ilikuwa ni tarehe 26 Oktoba 2018 kwa kuhamisha masalia ya Hayati Askofu Alphonce D. Nsabi, Askofu wa kwanza Mzalendo wa Jimbo Katoliki la Kigoma na kwenda kuhifadhiwa kwenye Makaburi yaliyoandaliwa rasmi kwa ajili ya maziko ya Maaskofu wa Jimbo Katoliki la Kigoma. Hili ni tukio la kihistoria linalohudhuriwa na Maaskofu Katoliki kutoka katika majimbo mbalimbali, ili kushukuru na kuendelea kustaajabia makuu ya Mwenyezi Mungu anayowatendea waja wake Jimboni Kigoma!

Jimbo Katoliki Kigoma
20 November 2021, 14:37