2021.09.14:Jubile ya fedha ya Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga , Jimbo Kuu Katoliki la Mbeya na  mapadre wengine ,Tanzania. 2021.09.14:Jubile ya fedha ya Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga , Jimbo Kuu Katoliki la Mbeya na mapadre wengine ,Tanzania. 

Ujumbe wa AMECEA katika Jubilei ya fedha ya Askofu Mkuu Nyaisonga

Mwenyekiti wa AMECEA Askofu Kasonde ameelezea kuwa Askofu Mkuu Nyaisongo na rais wa baraza la Maaskofu Tanzania ni nanga ya mshikamano kichungaji,akiwa katika fursa ya kuadhimisha jubilei ya fedha na wengine kutoka majimbo mbali mbali ya Tanzania katika kilele hicho Dominika 12 Septemba.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican.

Mwenyekiti wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Wanachama wa Afrika Mashariki (AMECEA), Askofu Charles Kasonde alituma ujumbe wake wa pongezi kwa Askofu Mkuu Mkuu Gervas Nyaisonga wa Jimbo Kuu Katoliki la Mbeya Tanzania na Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC),  kabla ya sherehe ya Jubilei ya fedha (mika 25) ya kuwekwa wakfu wa kikuhani iliyofanyika Dominika tarehe 12 Septemba 2021, ambayo ilijumuisha hata mapadre wote ambao walikuwa wanaadhimisha miaka 25 ya ukuhani kutoka majimbo mbali mbali ya Tanzania. Kabla ya sherehe hizo, zilinogeshwa hata hivyo na mafungo ya kiroho kwa Mapadre hao kutoka sehemu mbalimbali, waliopewa Daraja Takatifu ya Upadre na Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga kunako mwaka 1996. Kutokana na tukio hilo maalum Mwenyekiti wa AMECEA amchukua fursa hiyo kutoa shukrani na kumfafanua Askofu Mkuu Nyaisonga kuwa ni nanga ya mshikamano wa kichungaji.

Askofu Mkuu G.Nyaisonga na Rais wa Baraza la maaskofu katoliki Tanzania
Askofu Mkuu G.Nyaisonga na Rais wa Baraza la maaskofu katoliki Tanzania

Katika ujumbe wake kiongozi mkuu Askofu Charles Sampa Kasonde alioushirikisha kwenye mtandao wa AMECEA, Alhamisi tarehe 9 Septemba 2021, alimfafanua Askofu Mkuu Nyaisonga ambaye ni jumbe wa AMECEA kwamba yeye amekuwa nanga inayotambulika ya mshikamano wa kichungaji katika kanda hiyo, hasa tangu awe Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania tangu Juni 2018. “Kushiriki kwako kikamilifu katika mkutano Mkuu wa 19 uliofanyika Addis Ababa, Ethiopia na utayari wako, kwa niaba ya Baraza lako, kukubali kuwa mwenyeji wa mkutano ujao ni ishara tosha ya jinsi unavyoendeleza roho ya umoja ”. Kulingana na roho yake ya mshikamano, Askofu Kasonde alibainisha kwa shukrani ya kukubali kwa Askofu Mkuu Nyaisonga kumpatia kuhani wake Padre Anthony Makunde kuhudumu katika Sekretarieti ya AMECEA kama Katibu Mkuu tangu 2018.

Mwenyekiti wa AMECEA ameweza kuthamini miaka 25 hii  ya huduma ya Askofu Mkuu Nyaisonga tangu kuwekwa wakfu wa ukuhani na maisha mengi ambayo ameyabadilisha na kuyaongoza kwake Kristo. "Wito wako wa ukuhani kwa miaka 25 iliyopita umetoa mavuno mengi katika majimbo yote Katoliki ambapo umepanda mbegu ya Ukristo bila kukoma na bila kuchoka na kukuza ukuaji wa kiroho wa maelfu ya watu, Wakatoliki na wasio Wakatoliki sawa”. Aidha Askofu Kasonde alisisitiza kwamba "miaka ya Jubilei ni maalum katika maisha ya wanadamu hasa kama watumishi katika shamba la mizabibu la Kristo".

Askofu Kasonde ameandika kuwa: "Katika fursa ya tukio hili maalum na unapoangalia nyuma kwa miaka 25 iliyopita ya ukuhani wako ni kutoa shukrani kwa Mungu ambaye anatuita, nakupongeza na kukuombea ili uendelee mbele na afya njema, nguvu zaidi na nguvu." Askofu Kasonde akimtakia pia  heri Askofu Mkuu Nyaisonga ambaye alichaguliwa tena kwa muhula wa pili kuwa Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) kwa miaka mitatu ijayo, hadi Juni 2024. Kwa kuhitimishamisha ujumbe wake Askofu Kasonde anamwombea "kwa maombezi ya Bikira Maria Mama Yetu wa Afrika ili Mungu afanye tukio hilo kukumbukwa kwake, Kanisa la Tanzania na eneo lote la AMECEA".

Ikumbukwe kuwa  Askofu Mkuu Gervas Mwasikwabhila Nyaisonga alizaliwa tarehe 3 Novemba 1966. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi tarehe 11 Julai 1996 akapewa Daraja takatifu ya Upadre. Tarehe 9 Januari 2011, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI akamteuwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Dodoma na tarehe 19 Machi 2011 akawekwa wakfu na Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam na hatimaye, kusimikwa kuwa ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Dodoma. Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Mpanda na kusimikwa tarehe 4 Mei 2014. Tarehe 21 Desemba 2018 akateuliwa kuwa Askofu mkuu wa kwanza wa Jimbo kuu la Mbeya na kusimikwa rasmi tarehe 28 Aprili 2019 katika maadhimisho ya Jumapili ya Huruma ya Mungu.

JUBILEI YA MIAKA 25 YA UKUHANI WA ASKOFU MKUU NYAISONGA
14 September 2021, 10:15