Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 24 ya Mwaka B wa Kanisa: Kiri ya Imani ya Mtakatifu Petro na Masharti ya Ufuasi wa Kristo: Kujikana na kujitwika Msalaba! Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 24 ya Mwaka B wa Kanisa: Kiri ya Imani ya Mtakatifu Petro na Masharti ya Ufuasi wa Kristo: Kujikana na kujitwika Msalaba! 

Tafakari Jumapili 24 Mwaka B: Masharti ya Ufuasi wa Kristo Yesu!

Dhamira ya masomo ya dominika ya 24 ya Mwaka B wa Kanisa: Ni kushinda, kukwepa vishwishi, kukwepa kukwaza wengine na namna nzuri ya kupokea misalaba inayotunagukia katika maisha yetu kwa sifa na utukufu wa Mungu na kwa kujitakatifuza sisi wenyewe ili tuweze kustahilishwa kuurithi uzima wa milele. Imani haina budi kumwilishwa katika matendo ya huruma kwa wote!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 24 ya Mwaka B wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Dhamira ya masomo ya dominika hii ni kukwepa vishwishi, kukwepa kukwaza wengine na namna nzuri ya kupokea misalaba inayotunagukia katika maisha yetu kwa sifa na utukufu wa Mungu na kwa kujitakatifuza sisi wenyewe ili tuweze kustahilishwa kuurithi uzima wa milele. Somo la kwanza la kitabu cha Nabii Isaya (50:5-9); ni utabiri wa wasifu wa mtumishi wa Mungu. Mtumishi huyu ni mwema aliye tayari kutega sikio lake ili asikie na kufahamu vema mapenzi ya Mungu ili aweze kumtumikia vyema. Lakini huko kumtumikia Mungu kunamletea mateso na madhulumu na mwisho kifo, tena kifo cha aibu kabisa. Katika mateso yake atabaki imara na mwaminifu kwa Mungu. Ndiyo maana aliwatolea wapigao mgongo wake, na wang’oao ndevu mashavu yake; hakuficha uso wake usipate fedheha na kutemewa mate akitumaini kuwa Mungu atamsaidia ndiyo maana anasema; “Maana Bwana Mungu atanisaidia,” hivyo ana uhakika kabisa kuwa Bwana atamsimamia kwa sababu hiyo hakutahayari, bali aliukaza uso wake kama gumegume, wala hakuona haya maana aliamini kuwa; Mungu yuko upande wake, na hakuna atakayeshindana naye?

Mtumishi huyu anayetabiriwa na Isaya ni ni Yesu Kristo Bwana na Mwokozi wa maisha yetu aliyekufa kwa ajili yetu sisi ili tupate kukombolewa kutoka utumwa wa dhambi na mauti. Tukumbuke kuwa daima tunapokuwa upande wa Mungu na kutimiza mapenzi yake kwa moyo wa dhati, pasipo hila yoyote, Mungu hatuachi kamwe. Daima atatupigania katika shida na atatubeba kwa mbawa zake ili atuepushe na mabaya ambayo yangeweza kutupata. Matumaini yetu daima tuyaweke kwa Mungu naye atatuokoa, atatutetea, atatulinda dhidi ya mitego, hila na hatari za shetani.  Kwa imani na matumaini daima tuwe na ujasiri kujikabidhi kwake tukisema; “Nitamtumaini Bwana siku zote za maisha yangu, wala sitaogopa mabaya.” Katika somo la pili la Waraka wa Yakobo kwa watu wote (2:14-18); Mtume Yakobo anatufundisha kuwa imani peke yake isipokalimishwa katika matendo ya huruma kwa jirani zetu walio katika shida haiwezi kutuletea wokovu. Anahoji na kutuuliza Yakobo; “Yafaa nini, mtu kusema ya kwamba anayo imani, lakini hana matendo? Je! Ile imani yaweza kumwokoa? Ikiwa ndugu mwanamume au ndugu mwanamke yu uchi na kupungukiwa na riziki, na mtu wa kwenu akawaambia; Enendea zako kwa amani, ukaote moto na kushiba, lakini asimpe mahitaji ya mwili, yafaa nini?”

Kumbe imani yetu tu bila matendo, imekufa nafsini mwake. Ili imani yetu iwe hai na ituokoe ni lazima matendo yetu yamtangaze Kristo na kumpeleka kwa watu. Sisi wenyewe tuwe vyombo vya kumtangaza Kristo kwa wenzetu. Matendo yetu yatutambulishe kwa watu kuwa tunamfuata Kristo ambaye alikuja kutangaza ufalme wa Mungu. Ambaye alikuja kutufundisha namna ya kusali, namna ya kuhurumia, namna ya kutoa msamaha, namna ya kuenenda katika njia za Bwana. Ndiyo maana anatuambia; “Nimewapeni mfano, nanyi mkatende vivyo hivyo.” Tunapaswa kujiuza kuwa, je, matendo yetu yanamuakisi Kristo, yanamtangaza Kristo kwa watu au yanamdhalilisha? Injili ilivyoandikwa na Marko (8:27-35); ni mafundisho ya Yesu kuhusu umasiha wake ni wa namna gani. Mitume walijua kuwa yeye ni Masiya wa kisiasa atakayetumia nguvu za Kimungu ili kuwakomboa na mkono wa mkoloni. Yesu anayabatilisha mawazo yao kwa kuonyesha kuwa Yeye ni Masiya atakayewakomboa watu kwa mateso na kifo. Na hivyo yeyote anayetaka kuwa mfuasi wake lazima awe tayari kuteswa pamoja naye.

Fundisho hili Yesu analitoa akiwa njiani kuelekea katika vijiji vya Kaisara Filipi baada ya kuwauliza swali Mitume wake jinsi watu wanavyomchukulia na kumfahamu akisema; “Watu huninena mimi kuwa ni nani?” Nao wakatoa majibu kadiri walivyosikia watu wakisema yaweza kuwa ni; Yohane Mbatizaji, Eliya au mmojawapo wa manabii. Baada ya majibu kutoka kwa watu swali sasa likawa gumu, kibao kikageuzwa kwao akiwauliza; “Na ninyi mnasema ya kuwa mimi ni nani?” Petro akamjibu kwa niaba; “Wewe ndiwe Kristo.” Akawaonya wasimwambie mtu habari zake. Baada ya hapo akaanza kuwafundisha kwamba imempasa Mwana wa Adamu kuteswa mateso mengi, na kukataliwa na wazee, na wakuu wa makuhani, na waandishi, na kuuawa, na baada ya siku tatu kufufuka.” Mitume hawakuelewa fundisho hilo. Hapa yakaanza makemeo kati ya Yesu na Petro. Petro alimtoa Yesu pembeni na kumkemea kuwa haiwezekeani hilo limtokee. Yesu naye akamkemea Petro mbele ya wanafunzi wengine akimwambia; “Nenda nyuma yangu, Shetani; maana huyawazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu.” Hapo akatoa masharti na mwongozo wa yeyote anayetaka kuwa mfuasi wake kuwa lazima; “Ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake, amfuate. Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake, ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu na kwa ajili ya Injili, huyu ataisalimisha.”

Swali na fundisho la Yesu ni la nyakati zote. Nasi kila mmoja katika nafsi yake tunapaswa kujiuliza: “Yesu ni nani kwangu?” Je, ni Kristo mwana wa Mungu, Bwana na mwokozi wa maisha yangu? Je, niko tayari kujikana, kujitwika msalaba wangu na kumfuata ili kuiponya nafsi yako. Petro alitambua kuwa Yesu ni Kristo mwana wa Mungu lakini hakuwa tayari kuyashika masharti ya kumfuata hata akaitwa shetani. Kwa kumwita Petro shetani, Yesu hana maana ya kusema kwamba anamwona Petro kuwa ibilisi bali ni “mshawishi” anayemshawishi Yesu asitimize kazi ya ukombozi. Kwa maana nyingine Yesu alimwambia Petro: “Niache nifuate njia yangu, usinishawishi niiache.” Ni fundisho kwetu tusifanye mzaha na vishawishi vinavyotufanya tumuache Mungu. Vikemee vishawishi kwa sauti ya ukali ili viweze kuondoka na ubaki umesimama imara katika njia ya Bwana. Daima shetani anakuja kwa sura na namna mbalimbali ambazo. Anaweza kuja kwa sura ya mwanamke, mwanaume, pombe, pesa, rushwa, madaraka, uchovu, mali au njaa. Lengo ni kukufanya usitimize mapenzi ya Mungu. Vikemee kwa ukali na umtegemee Mungu, naye atakuokoa.

Tukumbuke kuwa Msalaba waweza kuwa ni maumivu ya kuacha nia zetu mbaya, tamaa zetu mbaya, fikra zetu mbaya na maamuzi yetu mabaya na kujikita katika kuyaishi mashauri ya Injili kwa ajili ya uzima wa milele. Tunaalikwa kuachana na uroho wa kujilimbikizia chakula na mali wakati wengine wanakufa kwa njaa sababu ya umasikini. Kuachana na uroho na uchu wa madaraka, heshima na umaarufu unaowafanya wengine wateseke. Tusisahau kuwa tumekombolewa kwa fumbo la msalaba; mateso, kifo na ufufuko wa Yesu Kristo. Ndiyo maana masharti ya kunufaika na fumbo la msalaba ni kujikana mwenyewe, kujitwika msalaba wako, na kisha kumfuata Kristo. Hali yetu ya kibinadamu haipendi kusikia na kuuona msalaba ambao ni: matatizo na shida za kimaisha. Pengine twajisikia tunataka kufuata njia yetu wala siyo ya njia ya Mungu. Tunauonea aibu msalaba. Tumwombe Mungu Roho Mtakatifu atutolee aibu juu ya msalaba kwa sababu ya woga na unyonge wetu. Aijaze mioyo yetu nguvu na ujasiri ya kuitwaa misalaba yetu, kuichukua kwa ushujaa na kuibeba kwa hiari ikiwa katika umbo la ugonjwa, shida na taabu za kila namna, tupate nguvu za kuuchukua ili tuweze kuwa wafuasi wa kweli wa Yesu Kristo na mwisho tuurithi uzima wa milele.

J24 Mwaka B
08 September 2021, 15:00