Kongamano la IV la Ekaristi Takatifu Kitaifa Nchini Tanzania 9-12 Septemba 2021 Kauli mbiu "Ekaristi Takatifu Chemchemi ya Uzima Wetu". Uzinduzi wa maadhimisho haya Jimbo kuu la Tabora. Kongamano la IV la Ekaristi Takatifu Kitaifa Nchini Tanzania 9-12 Septemba 2021 Kauli mbiu "Ekaristi Takatifu Chemchemi ya Uzima Wetu". Uzinduzi wa maadhimisho haya Jimbo kuu la Tabora. 

Kongamano IV la Ekaristi Takatifu Kitaifa, Tabora: Ufunguzi Rasmi

Askofu Flavian Matindi Kassala katika uzinduzi wa Kongamano la IV la Ekaristi Takatifu Kitaifa Jimbo kuu la Tabora amekaza kusema, Mtakatifu Yosefu ni Mlinzi wa Kanisa ambalo ni Mwili wa Kristo, lililojengwa juu ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Hili ndillo jibu muafaka ambalo Mwenyezi Mungu analitoa kwa Mfalme Daudi. Imani thabiti!

Na Askofu Flavian Matindi Kassala, - Kongamano la IV la Ekaristi, Jimbo kuu la Tabora

Maadhimisho ya Kongamano la IV la Ekaristi Takatifu Kitaifa nchini Tanzania yananogeshwa na kauli mbiu “Ekaristi Takatifu chemchemi ya uzima wetu”. Sherehe zote hizi zinaadhimishiwa kwenye Kituo cha Hija ya Huruma ya Mungu Kitulizo cha Moyo, a.k.a “Pahija Ifuchang’holo” kuanzia tarehe 9 hadi 12 Septemba 2021, Jimbo kuu la Tabora. Ibada hii imeadhimishwa kwa heshima ya Mtakatifu Yosefu, kama sehemu pia ya Maadhimisho ya Mwaka wa Mtakatifu Yosefu na imeongozwa na Askofu Flavian Matindi Kassala wa Jimbo Katoliki la Geita ambaye pia ni Makamu wa Rais, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC. Ibada hii ya Misa Takatifu imehudhuriwa pia na Professa Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi, Waziri wa Katiba na Sheria kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katika mahubiri yake, Askofu Kassala amegusia kuhusu: Mahusiano na mafungamano ya Mfalme Daudi na Mwenyezi Mungu mintarafu uduni wa mazingira ambamo lilikaa Sanduku la Agano, kielelezo cha uwepo endelevu na angavu wa Mungu kati ya watu wa Taifa lake teule na hivyo kutia nia ya kutaka kumjengea Mwenyezi Mungu nyumba, na badala yake, Mwenyezi Mungu anaamua kumjengea Mfalme Daudi nyumba. Mtakatifu Yosefu ni dira ya tafakari ya mahusiano kati ya Mwenyezi Mungu na binadamu. Mwili wa Mtoto Yesu uliotunzwa kwenye Familia Takatifu, ndio mwili ambao Kristo Yesu anawagawia waja wake kila siku wakati wa kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu. Mtakatifu Yosefu, bado analilinda Kanisa la Yesu. Sasa unaweza kuendelea…!

Wapendwa katika Kristo. Tafakari yetu ya leo, katika uzinduzi rasmi wa Kongamano la Nne la Ekaristi la Kitaifa, linalotuleta Pamoja katika ardhi hii ya Jimbo Kuu la Tabora, ningependa tuongozwe na Habari tuliyoisikia katika Somo letu la Kwanza kutoka 2 Samuel 7:4-5; 16. Hata hivyo, pamoja na Somo letu hili kuongozwa na sehemu hii ya Maandiko Matakatifu, ujumbe wake halisi unaeleweka katika kuziangalia pia aya za 1-3 zilizotangulia. Katika aya hizo, Mfalme Daudi anaonja mapungufu katika mahusiano yake na Mungu, hususan makaazi ya Mfalme yaliyopatikana kama sehemu ya ushindi wa adui za taifa teule, ushindi ambao anautambua kuwa ni kwa msaada wa Mungu. Mapungufu yanayomsumbua Mfalme Daudi ni kuona Sanduku la Agano, lililo uwakilishi wa Mungu kati ya watu wake, linakaa katika mazingira duni. Anachotaka kutenda Daudi ni kama hisani kwa wema wa Mungu. Lakini kuna pia dalili za hisani ambayo ingefunga ukurasa wa mahusiano yao ya awali na Mungu na kufungua ukurasa mpya, kwani anaona kama Makazi ya kifahari kama yake yatamweka Mungu katika hadhi kama yake pia. Anaonja uduni kwa Mungu kutokana tu na mazingira ya Sanduku la Agano. Anasahau kuwa mengi bado yanahitajika katika kuliweka taifa teule katika hadhi iliyotakiwa na Mungu na si Mungu anayetakiwa na Mfalme. Anasahau kuwa mafanikio yaliyopatikana hayakutokana na hadhi ya makazi ya Sanduku la Agano, kama uwakilishi wa uwepo wa Mungu, bali upendo wa Mungu kwa watu wake katika hali zao zote.

Kibinadamu, hukumu na haja ya Daudi ni sahihi kabisa tena ya kustahili pongezi. Ni maono ya mbali kabisa na yanayostahili uhusiano ulio tunda la kufahamiana kati yao. Ufahamu huo unafikishwa kwa Nathani, si kama Nabii, bali mtu mwenye busara na uwezo wa kupima mambo. Nathani analipokwa wazo la Mfalme Daudi na katika busara yake anaonesha jinsi Daudi alivyo na uwezo wa kufikia maamuzi hayo kutokana na mahusiano aliyonayo na Mungu. Hata hivyo, katika Aya ya nne na ya tano, somo ambalo ndilo tulilolisikia, Mwenyezi Mungu, kupitia kwa Nathani yule yule, lakini sasa kama Nabii wake, anapeleka ujumbe kwa Daudi. Ujumbe wa Mungu unaelekea kukinzana na ule wa Daudi ambao Nathani aliisha ubariki. Lakini Nathani hafuatwi na Mungu kama mtu mwenye Busara, bali Nabii na lugha ya kinabii inasikika. “Nenda” ni sauti ya Mungu ambayo haihitaji ushauri wa kibinadamu. Ni ujumbe unaohitaji kufikia kwa mhusika mara moja. Na mwelekeo wa kwenda kwake unabeba ujumbe “kamwambie”. Hivyo mwelekeo na ujumbe vyote si tegemezi kwa nabii wala hali ya mpokea ujumbe. Ndiyo maana Nathani anapaswa kuupeleka, kuufikisha kwa mhusika hata kama yeye mwenyewe pia unamtia mazingira magumu kwani unapingana na busara yake ya awali kwa Daudi, aliyokuwa ameionesha muda mfupi tu uliopita. Lakini, kama nabii anatiwa nguvu na yule yule aliyemtuma, “Bwana Mungu asema …”.

Ni wazi kuwa Mfalme Daudi kama ataendelea na mtizamo wake wa awali kwa Nathani kama mtu wa busara tu, ataonja hali ya upinzani na usaliti wa Imani yake kwake. Kama Daudi angeng’ang’ania msimamo wake huo angefifisha na hata kuua nia nzuri iliyokuwa imebebwa na ujumbe wa Mungu lakini ikidai nafasi kwa wakati ujao. Hivyo, Daudi alipaswa kutizama wakati uliokuwepo katika muungano wa nyakati zilizopita na wakati ujao, ambao ulibeba bado wazo na nia yake ila kwa manufaa makubwa zaidi ya taifa la teule. Sifa hii ya Mungu ambayo mara nyingi inafunikwa hata katika nyakati zetu, inadhihirisha upendo wa Mungu kwa mwanadamu dhaifu, ambaye mara nyingi hufikishwa katika ukamilifu wake kwa kudhani anaingiliwa mipango yake. Ni mahusiano ambayo daima yanafungwa na ukweli wa maneno ya wahenga, ‘Subira Yavuta heri’. Maneno haya daima huvuta ya kale na kuyaunganisha na yajayo katika woga, mashaka na wasiwasi wa wakati uliopo.

Mtakatifu Yosefu ambaye Mama Kanisa katupatia mwaka huu kama dira ya tafakari ya mahusiano yetu na Mungu ni mfano hai wa subira yavuta heri. Maamuzi yake ya Maisha na Maria hapo awali hayakuwa ya kuigiza. Alimpenda kweli Maria, na aliamua kweli kumpa pendo lake. Lakini tunasikia kilichomtokea na maamuzi aliyokuwa kayachukua kama binadamu. Hata hivyo katika mahangaiko yake bado aliacha wazi nafasi ya Mungu katika maamuzi hayo. Ndiyo maana alikubali ushauri hata kwa njia ya ndoto tu.  Mafao ya Yosefu kukubali maelekezo ya Malaika wa Mungu hayakuwa ya papo kwa papo.  Alihitaji muda ili yeye asiwe mtendaji mkuu bali chombo cha Mungu katika kutekeleza mpango wa Mungu. Alimtunza mtoto Yesu na Maria Mama yake Kama baba mwaminifu na mpendelevu, kwa maelekezo ya Mungu mwenyewe. Uaminifu wake na upendo unamletea hadhi ya kuwa mtunza Ekaristi Takatifu. Baba Mtakatifu Francisko akizindua Mwaka wa Mtakatifu Yosefu anamtaja kuwa ‘mtu wa kawaida na mvumilivu, aliyebaki kuwa tumaini la kila siku la Familia Takatifu. Ni Yosefu aliyeutunza mwili wa Yesu na kuukuza katika nyumba yake kwa mapendo makubwa. NI MWILI HUU ULIOTUNZWA NA YOSEFU NDIYO ANAOTUGAWIA KRISTO KILA SIKU KATIKA EKARISTI TAKATIFU.

KUMBE, Yosefu Analilinda Kanisa, lililo Mwili wa Kristo, lililojengwa juu ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, ambacho ni kilele cha Maisha na utume wa Kanisa. Anatekeleza ndoto ya Mfalme Daudi ya kumjengea Mwenyezi Mungu nyumba. Anajibu swali la Mungu lililoulizwa tangu nyakati za Mfalme Daudi, “Je wewe utanijengea nyumba ya Kukaa?” Swali hili ndilo linalojirudia leo, na katika kipindi kizima cha Kongamano letu. Ni nafasi ya kujiuliza kila mmoja kwa hadhi na nafasi yake katika Kanisa, “Je wewe utanijengea nyumba ya Kukaa?” Jibu lake si jepesi. Kwani katika nyakati zetu hizi, jibu lake ni la binafsi au letu sote? Katika majibu yetu ya jumla pengine ni jepesi. Lakini ukweli ni kwamba si hivyo. Kwanza kongamano ni nafasi ya kujiuliza; ‘Je, Mimi nakaa katika nyumba gani?’, ‘Je, Kristo ataipenda nyumba ninayotaka kumjengea leo; kijamii, kisiasa, kidini, kibinafsi, ili hata katika kutostahili kwangu, ampe mzao wangu au jirani yangu au mfuasi wangu, nafasi ya kumjengea nyumba?’ ‘Je, niko tayari walau kuwa mlishi tu wa Mwana wa Mungu kwa kuahilisha mipango yangu, japo kwa saa kadhaa za siku, kwa nafasi niliyo nayo, katika jamii leo, kwa kuwa faraja kwa wengine, hata kama inaingilia mipango yangu?’ Haya tunayaweza katika hali ya uhai wetu. Na sisi tumeamua kusema wazi kwa ulimwengu kuwa “Ekaristi Takatifu Chemchemi ya uzima wetu”. Kama kweli tunamaanisha hilo, basi tuipe nafasi Ekaristi kutujenga ili uonje thamani ya uzima wetu. Mungu na atubariki kujua nafasi ya Ekaristi katika Maisha yetu hasa kwa tafakari hii ya siku za kongamano. EKARISTI TAKATIFU… CHEMCHEMI YA UZIMA WETU.

Kwa upande wake Askofu mkuu Paul Runangaza Ruzoka wa Jimbo kuu la Tabora, katika Salam zake za kuwakaribisha watu wa Mungu katika Maadhimisho ya Kongamano hili, anamshukuru Mungu kwa kuliwezesha Jimbo kuu la Tabora kuadhimisha kumbukizi la miaka 121 ya mchakato wa uinjilishaji Jimbo kuu la Tabora. Maadhimisho haya yanafanyika wakati kuna changamoto kubwa ya maambukizi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Maadhimisho haya yanakwenda sanjari na Maadhimisho ya Kongamano la 52 la Ekaristi Takatifu Kimataifa “52nd International Eucharistic Congress” (IEC) ambalo lilizunduliwa tarehe 5 Septemba 2021, huko Jimbo kuu la Esztergom-Budapest, nchini Hungaria kwa kuongozwa na kauli mbiu “Visima vyangu vyote vimo kwako” Zab. 87:7. Baba Mtakatifu Francisko anategemea kushiriki katika Ibada ya Misa Takatifu ya kufunga Kongamano la 52 la Ekaristi Takatifu Kimataifa hapo tarehe 12 Septemba 2021. Makongamano yote haya yanapata chumbuko na asili yake kutoka nchini Ufaransa kunako mwaka 1881. Maadhimisho ya Kongamano la IV la Ekaristi Takatifu Kitaifa nchini Tanzania ni sehemu ya mchakato wa kusimika na hatimaye, kuzamisha imani katika akili, nyoyo na zaidi katika maisha ya watu wa Mungu ndani na nje ya Jimbo kuu la Tabora. Kongamano hili ni mahali pa kujichotea amana, hazina na utajiri wa imani ya Kanisa Katoliki mintarafu imani katika Fumbo la Ekaristi Takatifu. Itakumbukwa kwamba, Kongamano la Kwanza la Ekaristi Takatifu nchini Tanzania liliadhimishwa Jimbo Kuu la Dodoma mwaka 2008. Kongamano la Pili Kitaifa likaadhimishwa Jimbo Katoliki la Iringa mwaka 2016. Kongamano la III Kitaifa liliadhimishwa kwenye Viwanja vya Bikira Maria Malkia wa Kuanzia tarehe 8 Juni mpaka 11 Juni 2016. Maadhimisho yote haya ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha sadaka na majitoleo ya watu wa Mungu katika Majimbo husika.

Kongamano Ekaristi
10 September 2021, 15:01