2021.08.23:Ushuhuda wa kijana Despina Mdende mwimbaji (sauti ya Lirik),nyimbo Katoliki katika katika kwaya ya Parokia ya Segerea, Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam,Tanzania 2021.08.23:Ushuhuda wa kijana Despina Mdende mwimbaji (sauti ya Lirik),nyimbo Katoliki katika katika kwaya ya Parokia ya Segerea, Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam,Tanzania 

Tanzania:Despina,vijana tunapata changamoto za maisha tusikate tamaa!

Despina Mdende ni kijana aliyezaliwa kijiji cha Tanangozi,Iringa Tanzania.Akiwa mdogo alianza kuimba kwaya ya watoto baadaye watu wazima.Baada ya kufika Dar es Salaam ameendeleza kipaji hiki hadi kuimba kwa sauti nzuri sana(Lirik)katika kuinjilisha Neno la Bwana kupitia nyimbo."Kwa hakika vijana tunapata changamoto nyingi za maisha,lakini tusikate tamaa na kuacha kusikiliza sauti ya Mungu.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican.

Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, leo hii ninakuletea makala ya Uinjilishaji wa kina kupitia nyimbo za Kanisa Katoliki na ambazo kwa ujumla zinagusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.  Katika Waraka wa Baba Mtakatifu Benedikto XVI kwa bara la Afrika uitwao Africae Munus, yaani Dhamana ya Afrika unafafanua kwa kina juu ya mafundisho, maelekezo na changamoto ambapo  Baba Mtakatifu Benedikto XVI katika Waraka huo anajikita kwa mfano juu ya kulifanya upya Kanisa na Bara la Afrika kwa Uinjilishaji wa kina unaojengwa katika misingi ya msamaha, haki na amani. Katika Waraka huko Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI anatualika kuwa wahudumu wa kweli wa Neno la Mungu, ndani ya jumuiya zote za Kiafrika.  Kwa dhati Waraka huo unashiria hata bado leo hii mafundisho tangu Sinodi ya kwanza ya Maaskofu wa Afrika kuhsu utamadunisho wa mila na desturi za Kiafrika katika Imani ya Kristo inayojengwa katika Neno lake na Sakaramenti za Kanisa. Inatosha kuangalia ibada zinazoadhimishwa katika Kanisa la Afrika kila jumapili au siku kuu mbali mbali, jinsi zinazopambwa na nyimbo, ngoma, na vigelegele! Yote haya ndugu msikilizaji na msomaji wa Makala hii kwa hakika yaliweza kumgusa Baba Mtakatifu na akapenda nasi sote tuweze kutumia vizuri njia hizi za kumtangaza na kumshuhudia Kristo. Katika waraka huo alimtumia Mtakatifu Ireneo kwamba, utukufu wa Mungu unajidhihirisha katika viumbe wake, na wanadamu humtukuza Mungu kwa maisha yao. Kwa hiyo, Bara la Afrika, kwa uchangamfu na uhai wake linajiweka katika nafasi nzuri zaidi ya kumtukuza Mungu. Na kumbe kwa ujilishaji unaweza kupitia kwa njia nyingine kwa mfano kupitia nyimbo za kila siku ambazo zinaimbwa Kanisani au hata za tafakari na kumbe basi Waraka huu ni kivutio na hai katika bara la Afrika. Leo hii  ninapenda ninazungumza na kijana  ambaye anajulikana sana Tanzania kwa sauti yake nzuri (Lirik) kwa nyimba katoliki akihojiana na Idhaa ya Kiswahili ya  Radio Vatican.

Despina Mdende  akiwa katika kuimba
Despina Mdende akiwa katika kuimba

Wasikilizaji wanapenda wasikilize wewe ni nani

Ninaitwa Despina Elias Mdende. Ni mzaliwa wa kijiji cha Tanangozi, kati ya Mseke Wilaya ya Kilolo, Iringa Tanzania

Ndiyo kuimba ni kusali mara mbili kama asemavyo mtakatifu mmoja, watu wengi nchini Tanzania na kwingineko wameanza kutambua mwimbaji na mwenye sauti nzuri; je ulianzaje kuimba hadi kuboresha sauti yako?

Des: Nilipenda kuimba tangu mdogo sana, nikiwa kijijini ambapo nilishiriki katika kwaya ya watoto nikiwa darasa la tatu. Nilipofika darasa la saba, ndipo nikajiunga na kwaya ya watu wazima. Baada ya kuja Dar Ess Salaam nilianza kuimba na kwaya ya Mtakatifu Alois Gonzaga, Mabibo katika kigango cha Mtakatifu Petro Feba, Parokia ya Luhanga.

Umeimba nyimbo nyingi kwa kushirikiana na wanakwaye wengine lakini pia peke yako. Ni wimbo gani uliouimba kwa mara ya kwanza peke yako? Maana mimi nilikujua kwa wimbo wa ‘nitakushukuru’, labda kulikuwa na wimbo mwingine kabla ya huo?

Des: Kwa wastani nilipata changamoto nyingi sana kufikia nilipo kwakuwa nilikuwa bado mdogo, lakini nilikuwa ninapenda sana kuimba na nikaendelea na kwaya na wengine. Na baadaye nilianza kujaribu kuimba hata peke yangu tu. Na album ya kwanza inaitwa “ niongoze Bwana Mungu. Niliimba wimbo wa “Tupo huru”. Kwa bahati mbaya Album hiyo haikujulikana kwa sababu sikuwa na mtu kuniunga mkono. Baadaye niliendela taratibu lakini bila kukukosa changamoto lukuku, lakini chanamoto hizo zilinisaidia kukomaa hata kufikia kung’amua sifa kuu kwa Mungu kupitia nyimbo na ndiyo nikaimba wimbo wa “Nitaskushukuru kwa kuwa nimeumbwa kwa jinsi ya ajabu”. Na kumbe basi kabla ya wimbo huo, tayari nilikuwa nimeimba nyimbo nyingi tu! Vile vile baadaye niliendelea na utume huu katika kwaya ya Bikira Maria Mama wa Mungu katika Parokia ya Yohane wa Mungu, huko Yombo Vituka, Dar es Salaamu. Katika kwaya hiyo nikaendelea na ndipo nikaimba wimbo wa “Moyo wangu”. Kutokana na changamoto za maisha, niliondoka tena katika Parokia hiyo, mnamo 2019 nikahamia katika Parokia ya Roho Mtakatifu Segerea na kujiunga na kwaya ya Mtakatifu Malaika Gabrieli Mkuu, mahali ambapo nipo sasa ninaendelea na utume huu. Hapo nimeweza kuimba wimbo wa “ninakuabudu Mungu wangu”. Wimbo huo unajumuishwa kkatika Album nzima kabisa ambayo imebeba nyimbo tisa zilizoko kwenye audio: Nalifurahi, Ave Maria, Bwana Yesu furaha yangu, Ekaristi Takatifu, Ninakuabudu, Panis Angelicus, Twakusifu Mungu Mkuu, Nitakushukuru. Ndizo nyimbo ambazo nimeimba mimi binafsi na ninaendelea kuandaa nyingine kwa njia ya video nikiambatana na wengine.

Despina kwa kufuatilia nyimbo zako na wenzako zimejikita sana kutafakarisha na utulivu wa ndani kwa Bwana wetu, na hivi karibuni mmeimba wimbo wa “Niokoe” je jambo gani linakuvutia katika hili kwa ujumla katika nyimbo zenu ambapo unaweza kuwashirikisha wasikilizaji wetu wa idhaa ya kiswahili ya Radio Vatican, popote walipo?

Des: Bwana ni mwema zaidi katika maisha yetu ya kila siku, anazungumza kwa kila siku kwa kile kidogo na kikubwa, katika maisha yangu, nimepetia katika changomoto nyingi za maisha  na ambazo sidhani kama zimekwisha bali ni sehemu ya maisha yak ila mtu, lakini sijakata tamaa katu, kwa neema yake Mungu tu. Sitaacha kumwimbia Mungu na sitoacha kufuata mafundisho yake kila kuchapo! Lakini pamoja na hayo yote ninapenda waambia wasikilizaji, hasa vijana wenzangu wanao nisikiliza  kwamba kwa hakika vijana tunapata changamoto nyingi za maisha. Jambo muhimu ambalo ninawashauri na kuwasihi kama jinsi ambavyo ninajiambia mimi, ni kutokata tamaa, na kuacha kusikiliza sauti ya Mungu ambaye yeye anazungumza kupitia hata katika magumu au hata yaliyo rahisi katika maisha yetu ya kila siku. Bwana hakutuonesha njia nyingine rahisi zaidi ya Kalvario. Yeye alisema mwenyewe kuwa “Anayetaka kunifuata abebe msalaba wake na kunifuata”, (Mt16:24, Marko 8:34, Luka 9:23). Ndiyo njia pekee hata ya uinjilishii wetu kwa njia ya nyimbo zetu.

Mpendwa Despina tunapofikia mwisho wa mazungumzo yetu haya, je unalo la kuongeza?

Des: Ndiyo kitu msingi ambacho ninapenda kuwaomba kila mmoja, watu wazima na vijana ambao kwa hakika wanaweza kujiunga na kwaya kuimba, kwani kumwimbia Mungu ni kusali na kuomba. Ninasema hivyo kwa sababu kuimba kumenisaidia   sana kiroho hata ninapokuwa ninawaandaa watu kutafakari neno la Mungu la kila siku ya Dominika. Jambo jingine ninaomba mshikamano kwa hali na mali katika kusikiliza na kuniombea ili niweze kuendelea zaidi kutangaza Injili kwa njia hii ya uimbaji wa neno la Mungu.

Asante Despina Mdede kwa ushuhuda huo

Des: Asante

Despina Mdende  na sauti yake nzuri
Despina Mdende na sauti yake nzuri

Ndugu mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican, hayo yalikuwa ni mahojiano na Despina Mdende mwimbaji mzuri wa nyimbo katoliki katika Parokia ya Segerea, Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam, Tanzania, tuzidi kumwombea kila baraka katika utume huo mzuri. Na Neno la Mungu na liangaze maisha yetu na kukoleza umoja na mshikamano wa Wanafamilia ya Mungu kama Kristo anavyotuelekeza: Iweni wamoja kama mimi na Baba tulivyo wamoja alisema Mtakatifu Petro. Ninawaaga kwa kuwaachia kusikiliza pia na baadhi nyimbo zake:

USHUHUDA WA KUIMBA WA DESPINA
23 August 2021, 16:20