Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili 22 ya Mwaka B wa Kanisa. Amri za Mungu ni dira na mwongozo wa maisha adili na matakatifu. Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili 22 ya Mwaka B wa Kanisa. Amri za Mungu ni dira na mwongozo wa maisha adili na matakatifu. 

Amri za Mungu ni Dira, Mwongozo wa Maisha Adili na Matakatifu!

Amri za Mungu zinalenga kuboresha mahusiano na mafungamano ya Agano kati ya Mungu na Taifa lake! Waisraeli walipewa Amri Kumi kama sehemu muhimu sana ya masharti ya Agano. Maneo haya ni: Sheria, Kanuni na Amri zinazopaswa kufuatwa na taifa la Mungu. Mkazo hapa ni Neno ambaye anaumba, yaani Mwanaye mpendwa Kristo Yesu, Neno aliyefanyika mwili.

Na Padre Andrew Mlele Mtaki, - Vatican.

UTANGULIZI: Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican karibu katika tafakari ya Neno la Mungu katika Dominika ya 22 ya mwaka B wa Kanisa. Liturujia ya Neno la Mungu katika Dominika hii inatutafakarisha juu ya ukweli kwamba sheria ya Mungu ni uzima wa mwanadamu. Amri za Mungu zinalenga kuboresha mahusiano na mafungamano ya Agano kati ya Mungu na Taifa lake! Mwenyezi Mungu aliwapatia Waisraeli Amri Kumi kama sehemu muhimu sana ya masharti ya Agano. Haya ni maneno ambayo yametamkwa na Mwenyezi Mungu mwenyewe ni: Sheria, Kanuni na Amri zinazopaswa kufuatwa na taifa la Mungu. Mkazo hapa ni Neno ambaye anaumba, yaani Mwanaye mpendwa Kristo Yesu, Neno aliyefanyika mwili. Upendo unarutubishwa kwa njia ya neno kama ilivyo pia kwa ushirikiano wa dhati ili kujenga na kudumisha mawasiliano. Pale mtu anapozungumza hadi kufikia hatua ya “kukuna sakafu ya moyo wa mtu, hapo kwa hakika upweke hutoweka! Mwenyezi Mungu kwa njia ya “Maneno Kumi” yaani Amri zake amependa kujenga mawasiliano na mafungamano na binadamu na sasa anasubiri majibu muafaka kutoka kwa waja wake.

Ni mawasiliano yanayofumbatwa katika mchakato wa majadiliano ambayo kimsingi, ni chemchemi ya ukweli, furaha, upendo na utajiri ambao, wahusika wanatajirishana katika undani wao! Mwenyezi Mungu amempatia mwanadamu changamoto kubwa katika Amri zake, ili kumlinda na kumwongoza aweze kuishi Agano kwa uaminifu zaidi. Mwenyezi Mungu hana “wivu wala kijicho”, bali anawataka watoto wake wawe na uhuru kamili, kwa kusikiliza kwa makini maneno yake, kielelezo cha upendo wake usiokuwa na mipaka. Katika mazingira ya kutatanisha ili kutambua Amri za Mungu kuwa ni: Sheria, Neno au majadiliano waamini watambue kwamba Mwenyezi Mungu ni Baba mwenye upendo usiokuwa na kifani Amri za Mungu ni dira na mwongozo wa maisha adili na matakatifu. Salama ya mwanadamu iko katika kutenda kadiri ya maagizo ya Mwenyezi Mungu. Aidha, uaminifu kwa sheria ya Mungu unajidhihirisha zaidi katika matendo mema na adili na si tu katika maneno ya sheria na wingi wa taratibu za kufuata. Kwa sababu hiyo sheria ya Mungu ni sheria ya upendo. Hivyo basi tukiishi kwa upendo, tukitenda haki na kuwatendea wengine kwa wema tunayo hakika ya kwamba tunatembea katika njia yake Mungu mwenyewe.

TAFAKARI: Katika somo la kwanza (Kumb 4:1-2, 6) Musa, akitambua wazi ya kwamba hataingia katika nchi ya ahadi, anatumia nafasi aliyo nayo kutoa hotuba ya kuwaaga watu wa taifa teule na kuwaasa jinsi iwapasavyo kuenenda watakapoingia katika nchi ya ahadi. Anawataka wazishike amri za Mungu na hukumu zake, nao watapata heri ikiwa watakuwa waaminifu katika hilo. Anawakumbusha ya kuwa ukuu wake Mungu utajidhihirisha kati ya watu wa mataifa kupitia wao na mafanikio yao katika nchi ya ahadi yatategemea uaminifu wao kwa amri yake Mungu. Lakini sheria haiko tu katika maneno bali katika matendo. Watu wa mataifa watatambua tofauti iliyopo na watu wa taifa teule kwa njia ya matendo mema na si kwa njia ya maneno matupu.  Katika Somo la pili, Waraka wa Yakobo Mtume kwa watu wote (Yak 1: 17-18, 21-22, 27) anakumbusha ya kwamba Mungu amepanda neno lake ndani ya mwanadamu na ni hilo ndilo neno liletalo uzima, ndilo nelo lenye kuweza kuziokoa roho.

Neno hilo ndilo sheria yake Mungu mwenyewe na ndio mwongozo wa maisha ya mwanadamu. Hata hivyo, haitoshi tu kulisikia neno hilo; haitoshi tu kusema ya kwamba neno hilo limepandwa ndani ya mwanadamu. Neno hilo linadai wajibu kwa upande wake mwanadamu. Mwanadamu anadaiwa kuliweka neno hilo katika matendo mema na adili. Uwepo wa neno la Mungu katika nafsi ya mwanadamu unaonekana katika matendo safi na matendo mema kwa wengine na hasa wahitaji. Huu ndio ushuhuda wa Injili ya huduma na mapendo inayopewa kipaumbele cha pekee na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, kama kielelezo makini cha umoja, mshikamano na mafungamano ya kibinadamu. Rej. GS 88. Somo la Injili, Marko (7: 1-8, 14-15, 21-23) Injili inaendeleza dhamira hii ya neno la Mungu lenye kuleta uzima na kuokoa roho zetu. Yesu anawajibu Mafarisayo na waandishi ya kuwa haitoshi tu kulijua kwa ufasaha neno la Mungu na sheria zake bali ni bora zaidi na ni wajibu kuliweka katika matendo. Maneno mengi hayafai kitu ikiwa moyo uko mbali na Mungu. Ikiwa wanajivuna ya kuwa wao ni waaminifu katika kulishika neno la Mungu basi na wadhihirishe hilo katika mwenendo safi na katika matendo mema. Wingi wa sheria hautaleta wokovu bali uaminifu katika maagizo yake Mungu ndiyo huleta uhuru wa kweli wa wana wa Mungu.

KATIKA MAISHA: Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican katika siku hii ya Bwana, tujiulize jambo moja msingi: Je, ni kwanini tunahitaji sheria na taratibu katika maisha yetu? Je, vina msaada gani kwetu? Hakika sheria na taratibu vina lengo la kulinda tunu zetu. Sheria ipo ili itusaidie kuziweka salama tunu zetu mbalimbali. Kinyume na hapo patazuka ghasia, fujo na kila aina ya uharibifu na mwishowe tutapoteza tunu zetu ambazo ni za thamani kubwa sana. Kwa sababu hiyo lazima tuipende sheria iliyo njema na kuishika kwa ajili ya faida yetu sisi na faida ya jamii nzima. Ili tuweze kukua kama watu binafsi na kama jumuiya tunahitaji kuwa na sheria, taratibu na kanuni. Aidha, tunaweza kufikia malengo yetu ikiwa tutakuwa waaminifu kwa sheria na taratibu zinazotuongoza katika kuyafikia malengo husika. Aidha, tunapotafakari faida ya sheria katika kuishi kwetu tunakumbushwa ya kuwa haitoshi tu kuwa na sheria nyingi bali sheria lazima zituletee manufaa na kutusaidia.

Sheria ni lazima ilete mageuzi chanya katika maisha ya mwanadamu. Haitufai kitu sheria ambayo inatuangamiza. Je, sheria tunazoziweka zinalenga kulinda haki na kuwasaidia wengine. Tunatoa mchango gani katika kutengeneza sheria zinazowalinda na kuwajenga wengine? Na sisi wenyewe je tunazizingatia au ni wepesi wa kuwasukuma wengine kushika sheria wakati sisi tunazikwepa? Zaidi ya hayo, tunatafakarishwa pia uhusiano uliopo kati ya sheria na kukua katika imani na upendo kwa Mungu na kwa wenzetu. Kila dini inayo sheria, taratibu na kanuni  zake. Lengo la uwepo wa sheria na taratibu hizi ni kumsaidia mwanadamu kumjua na kumpenda Mungu na pia kumpenda jirani. Dini yenye wingi wa sheria ambazo zinamweka mwanadamu mbali na Mungu ni dini isiyookoa. Je, sisi tunaokiri imani katika Mungu aliye Baba wa utaratibu tunasaidiwa vipi na sheria na taratibu tulizo nazo? Ikiwa tuna nafasi katika jumuiya zetu za kikristo tunawasaidia vipi wengine katika kuiishi sheria ya Mungu na kukua katika imani, upendo na matumaini. Na mwisho kabisa tunapewa nyenzo ya kutusaidia kutembea katika njia ya Mungu. Yesu anatualika kufanya tafakari ya kina na kurudi ndani ya mioyo yetu na kujichunguza. Ni nini kimeijaza mioyo yetu? Je, ni mawazo mema, ya amani, haki na upendo? Au tumeijaza mioyo yetu mawazo maovu yaliyo kinyume na Mungu na yasiyowasaidia wengine? Matendo yetu yanadhihirisha hazina iliyoko ndani ya mioyo yetu. Tutafute kujaza mioyo yetu kwa matendo yaliyo mema na matakatifu.

Liturujia J22
28 August 2021, 08:45