Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili 20 ya Mwaka B wa Kanisa: Kristo Yesu ni mkate na kinywaji cha mbinguni. Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili 20 ya Mwaka B wa Kanisa: Kristo Yesu ni mkate na kinywaji cha mbinguni. 

Tafakari Jumapili 20 ya Mwaka B: Ekaristi Chakula & Kinywaji Cha Uzima

Ekaristi Takatifu ni chakula na kinywaji cha uzima wa milele. Somo la kwanza la katika kitabu cha Mithali (9:1-6); linaelezea sifa za Hekima. Katika Agano la Kale Hekima ni neno la Mungu, ni nafsi ya Mungu, na katika Agano Jipya Hekima ni Yesu Kristo kama anatueleza Mwinjili Yohane; “Hapo mwanzo, alikuwako Neno. Huyo Neno alikuwa pamoja na Mungu, naye Neno alikuwa Mungu.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 20 ya mwaka B wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya dominika 19B yalitualika na kutusisitiza kupokea Ekaristi Takatifu, chakula cha kiroho kinachotupa nguvu ya kuendelea na safari ya kuuelekea uzima wa milele mbinguni kwa mwaliko wa kuambiwa; “Amka, Inuka ule, maana safari hii ni ngumu kwako.” Masomo ya dominika hii ya 20 ya Mwaka B yanaendeleza msisitizo wa umuhimu wa Ekaristi Takatifu, chakula cha uzima wa milele. Somo la kwanza la katika kitabu cha Mithali (9:1-6); linaelezea sifa za Hekima. Katika Agano la Kale Hekima ni neno la Mungu, ni nafsi ya Mungu, na katika Agano Jipya Hekima ni Yesu Kristo kama anatueleza Mwinjili Yohane; “Hapo mwanzo, alikuwako Neno. Huyo Neno alikuwa pamoja na Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Tangu mwanzo huyo Neno alikuwa pamoja na Mungu. Vitu vyote viliumbwa kwa Yeye, wala pasipo Yeye hakuna cho chote kilichoumbwa ambacho kimeumbwa. Ndani Yake ndimo ulimokuwa uzima na huo uzima ulikuwa nuru ya watu. Nuru hung’aa gizani nalo giza halikuishinda” (Yn.1:1-5). Yohane anaweka wazi kuwa huyo Neno ndiye Yesu Kristo akisema; “Neno alifanyika mwili, akakaa miongoni mwetu, nasi tukauona utukufu Wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba, amejaa neema na kweli” (Yn.1:14). Yeye huyu Hekima anatualika kwenye karamu akimwambia kila mmoja wetu; “Njoo ule mkate wangu, ukanywe divai niliyoichangaya.” Ni mwaliko wa karamu ya Bwana ndiyo Ekaristi Takatifu, karamu aliyoiandaa Kristo mwenyewe.

Somo la pili la Waraka wa Mtume Paulo kwa Waefeso (5:15-20); ni mawaidha ya Mtume Paulo akiwashauri Wakristo wa Efeso waishi kadiri ya hekima ya Kikristo wakitafuta furaha yao katika Roho Mtakatifu siyo katika furaha za dunia akisema; “Angalieni sana jinsi mnavyoenenda; si kama watu wasio na hekima, bali kama watu wenye hekima. Hivyo msiwe wajinga, bali mfahamu ni nini yaliyo mapenzi ya Bwana. Tena msilewe kwa mvinyo, ambamo mna ufisadi; bali mjazwe Roho; mkisemezana kwa zaburi na tenzi na nyimbo za rohoni, huku mkiimba na kumsangilia Bwana mioyoni mwenu; na kumshukuru Mungu Baba siku zote kwa mambo yote, katika jina lake Bwana wetu Yesu Kristo”. Mtume Paulo anatukumbusha tutumieni vizuri muda tulionao (Ef. 5:16) kama vile sala ya Mzaburi isemayo; “Ee Bwana, unijulishe mwisho wangu, hesabu ya siku zangu ni ngapi, nijue jinsi nilivyo dhaifu” (Zab. 39:4). “Utufundishe kuzihesabu siku zetu vyema, tujipatie moyo wenye hekima” (Zaburi 90: 12). Paulo anatunaonya tusipoteze muda kwa mambo yasiyofaa akisema; “Wala msilewe mvinyo, kwani ulevi humwangamiza mtu, bali mjazwe Roho” (Ef. 5:18). Muda wa kuishi ni zawadi tunayopewa na Mungu hivyo hatuna budi kuutumia vizuri. Kuupoteza muda ni ukosefu wa shukrani kwa Mungu ndiyo maana Paulo anatuambia; “Daima mshukuruni Mungu Baba kwa jina la Bwana wetu Yesu Kristo kwa ajili ya yote” (Ef. 5:20). Siri ya mafanikio ni kufanya unalopaswa kufanya bila kukawia tukitambua kuwa namna ya kutumia vizuri muda ni kufanya lile unalofanya.

Tuwe na muda wa kufanya yaliyo mema na ya kumpendeza Mungu na jirani ambayo yanatusaidia pia kuishi kwa kufura na amani. Tusisingizie hatuna mda wa kutenda matendo ya huruma ya kimwili na kiroho ili tujichotee neema za uzima wa milele. Ni makosa kusema sina muda. Muda tunao, labda hatuna muda wa kufanya mambo fulani tusiyopenda. Tunachokipenda tutapata muda wa kukifanya na kukifurahia. Hatari ni kuwa vya bure huumiza. Tumepewa muda bure. Tungekuwa tunanunua muda labda tungebana matumizi ya muda na kuutumia vizuri kwa yaliyo na tija. Muda unakimbia lakini usisahau wewe ni dereva wa maisha yako. Inategemea unaelekea wapi? Muda ni mfupi kiasi si wa kupoteza. Kuwa na muda wa kufanya kazi ndiyo gharama ya mafanikio. Kuwa na muda wa kufikiria ndilo chimbuko la uvumbuzi na mipango. Kuwa na muda wa kucheza na kufanya mazoezi ni siri ya kubaki kijana. Kuwa na muda wa kupenda kwa vile upendo ni moyo wa maisha ya familia na urafiki. Moyo huo haupaswi kusimama. Uwe na muda wa kucheka; kicheko ni wimbo wa moyo. Uwe na muda wa kusali kwa vile utakuwa karibu na Mungu. Kuwa na muda wa kusaidia watu ni kisima cha furaha. “Msifanye chochote kwa moyo wa fitina” (Waf. 2: 3). Fitina imejaa kulipa kisasi. Kulipa kisasi ni kupoteza muda wa kukua kiutu na kimaadili. Kulipa kisasi ni kupoteza muda wa kusukuma gurudumu la maendeleo mbele. Tutumie muda tulio nao kutenda mema; “Basi, tusichoke kutenda mema; maana tusipolegea tutavuna mavuno kwa wakati wake. Kwa hiyo, tukiwa bado na wakati, tuwatendee watu wote mema” (Gal. 6: 9).

Injili kama ilivyoandikwa na Yohane (6:51-59); ni mwendelezo wa mafundisho ya Yesu juu ya Ekaristi Takatifu. Katika mafundisho yake Yesu anasisitiza juu ya umuhimu na ulazima wa kupokea Ekaristi Takatifu ambayo ni mwili na damu yake kwa ajili ya uzima wa milele akisema; “Mimi ndimi chakula chenye uzima kilichoshuka kutoka mbinguni; mtu akila chakula hiki, ataishi milele. Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa milele, nami nitamfufua siku ya mwisho kwa maana mwili wangu ni chakula cha kweli, na damu yangu ni kinywaji cha kweli. Aulaye mwili wangu ma kunywa damu yangu, nami hukaa ndani yake. Kama vile Baba aliye hai alivyonituma mimi, nami ni hai kwa Baba; kadhalika naye mwenye kunila atakuwa hai kwa mimi.” Dharau na matokeo ya kuidharau Ekaristi Takatifu na kutoipokea ni makubwa na mabaya mno; kuukosa uzima wa milele kama anavyosisitiza Yesu Mwenyewe akisema; “Amin, amin, nawaambieni, msipoula mwili wake Mwana wa Adamu na kuinywa damu yake, hamna uzima ndani yenu. Basi tufanye hima kuvunja kuta zote zinazotuzuia kupokea Ekaristi Takatifu, tufanye hima kuipokea kwani ndiyo amana ya uzima wa milele.

J 20 Mwaka B
12 August 2021, 14:35