Maandalizi ya Siku ya Kimisionari Mwezi Oktoba mwaka huu yameanza jimboni Zomba nchini Malawi. Maandalizi ya Siku ya Kimisionari Mwezi Oktoba mwaka huu yameanza jimboni Zomba nchini Malawi. 

Malawi:Maandalizi ya Siku ya Kimisionari jimboni Zomba

Jimbo katoliki la Zomba,Malawi limeanza maandalizi ya Siku ya Kimisionari Ulimwenguni,inayofanyika Oktoba,24 ijayo.Katika fursa hiyo,Padre Mwakhwawa,Mkurugenzi wa PMS,Malawi amesema wakristo wanapaswa kuandaliwa na kuelewa vema nini maana ya Mwezi wa Kimisionari na Siku ya Kimisionari Ulimwenguni ili kushiriki kikamilifu shughuli mbali mbali zinazotarajiwa kwa mwezi Oktoba.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican.

Kuwatia moyo wakristo ili waweze kusali ndani ya familia zao; kuwafanya wawe na utambuzi kwa kiasi kikubwa kuhusu Siku ya Kimisionari Ulimwenguni, uwajibu wa kimisionari kwa kila mbatizwa na kuomba waamini wachangie kiuchumi shughuli za umisionari wa Kanisa, ndiyo mambo msingi ambayo yanashughulikiwa katika maandalizi ya Mwezi wa Kimisionari nchini Malawi.

Mwongozo wa Kitaifa wa Shughuli za Kipapa za Kimisionari (PMS) nchini Malawi wameanza nao katika matazamio ya maandalizi ya Siku ya Kimisionari Ulimwenguni itakayo adhimishwa tarehe 24 Oktoba 2021. Imetolewa taarifa kwa Shirika la habari za kimisionari Fides na Padre Vincent Mwakhwawa, Mkurugenzi wa PMS nchini Malawi, akiwashauri wakatoliki wote nchini Malawi kuwa na utambuzi huo na kusali ili maandalizi ya Mwezi wa Kimisonari na Siku ya Kimisionari ulimwenguni mwaka huu iweze kuwa na ufanisi.

Mara baada ya kufanya Mkutano kwa ajili ya kuanza maandalizi ya Siku ya Kimisionari, katika Parokia ya Mtakatifu Vincent wa Pauli huko (Katamba), jimboni Zomba, Padre Mwakhwawa amesema kuwa, wakristo wanapaswa kuelewa vema nini maana ya Mwezi wa Kimisionari na Siku ya Kimisionari Ulimwenguni, ili kuweza kushiriki kikamilifu shughuli mbali mbali zinazotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Walei la Jimbo katoliki la Zomba Bwana, Vito Sandifolo, akizungumza katika mkutano huo alithibitisha wanapaswa kuomba vyama vyote katoliki vya kijimbo kushiriki maandalizi ya Siku ya Kimsionari Ulimwenguni. Kwa mujibu wake, ameongeza kusema kuwa majimbo yamesambaza kwenye maparokia yao zana za taarifa kuhusu Shughuli za Kipapa za Kimisionari (PMS) ili wakristo waweze kusaidiana pamoja kuelewa kwa dhati maana kamili ya mwezi wa kimisionari na Jumapili ya Kimisionari”. Jimbo katoliki la Zomba, Malawi litakuwa mwenyeji wa tukio hili kitaifa kwa mwaka huu, kwa kuongozwa na kauli mbiu “Hatuwezi kunyamaza kwa kile tulichokiona na kusikia.”

04 August 2021, 14:29