Askofu Willybard Kitogho Lagho wa Jimbo Katoliki la Malindi, Kenya tarehe 22 Agosti 2021 ametabaruku Kanisa la Parokia ya Karoli Lwanga Muyeye na kutoa Kipaimara kwa vijana 50 na 14 kupokea Komunio ya kwanza. Askofu Willybard Kitogho Lagho wa Jimbo Katoliki la Malindi, Kenya tarehe 22 Agosti 2021 ametabaruku Kanisa la Parokia ya Karoli Lwanga Muyeye na kutoa Kipaimara kwa vijana 50 na 14 kupokea Komunio ya kwanza. 

Yaliyojiri Parokia ya Karoli Lwanga Jimbo Katoliki Malindi, Kenya!

Askofu Willybard K. Lagho wa Jimbo Katoliki Malindi, Kenya ametabaruku Kanisa la Parokia ya Karoli Lwanga, Muyeye. Ametoa Sakramenti ya Kipaimara kwa Wakristo 50 na 14 wamepokea kwa mara ya kwanza Ekaristi Takatifu. Ujenzi wa Kanisa la Parokia ulianza mwezi Februari 2017 na tarehe 22 Agosti 2021, Kanisa likatabarukiwa. Hii ni Parokia iliyoanzishwa tarehe 3 Juni 2018. Imani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Adhimisho la Fumbo la Ekaristi Takatifu chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa ni kiini cha Parokia. Kimsingi, Fumbo la Ekaristi Takatifu linaadhimishwa siku ya Bwana, yaani Dominika, Jumuiya ya waamini inapopata nafasi ya kukutanika ili kusikiliza, kutafakari Neno la Mungu na hatimaye, kutumwa kutangaza na kushuhudia matendo makuu ya Mungu katika uhalisia wa maisha yao, kama kielelezo cha imani tendaji! Neno Parokia, linapata asili yake kutoka katika lugha ya Kigiriki yaani “παρоικια” maana yake “Ujirani”. Kumbe, Parokia ni kitovu cha maisha na utume wa Kanisa, mahali pa kuinjilisha na kuinjilishwa. Hapa ni mahali muafaka pa kuwatakatifuza watu wa Mungu, tayari kutoka kifua mbele kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili; huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Inasikitisha kuona kwamba, kuna waamini wengi ambalo hawashiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa parokiani kutokana na vikwazo mbalimbali, ambavyo wanapaswa kuvivalia njuga kama sehemu ya mapambano ya maisha ya kiroho, hakuna kubweteka hadi kieleweke!

Parokia, ni mahali ambapo maisha ya Kisakramenti yanapewa uzito wa pekee sanjari na ushuhuda wa Injili ya upendo unaomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kama kielelezo cha imani tendaji. Parokia ni mahali ambapo, utamaduni wa watu kukutana unapaswa kujengwa na kudumishwa, ili kukoleza majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni tayari kujenga mshikamano wa udugu wa pamoja na kuendelea kuwa wazi kwa ajili ya watu wote. Jumuiya ya Kiparokia inapaswa kuwa ni wasanii wa utamaduni wa ujirani mwema, kama kielelezo na ushuhuda wa imani tendaji inayomwilishwa kwa namna ya pekee katika Injili ya huduma. Pamoja na ukweli huu, Mama Kanisa anatambua kwamba, kuna uhaba mkubwa wa miito ya Kipadre katika baadhi ya maeneo, kiasi kwamba, mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache katika shamba la Bwana. Kumbe, kuna haja ya kuwa na mwelekeo na utambuzi mpya wa “dhana ya Parokia”.

Ni katika muktadha huu, Jumapili tarehe 22 Agosti 2021, Askofu Willybard Kitogho Lagho wa Jimbo Katoliki Malindi, Kenya ametabaruku Kanisa la Parokia ya Karoli Lwanga, Muyeye Jimbo Katoliki la Malindi. Ametoa Sakramenti ya Kipaimara kwa Wakristo 50 na 14 wamepokea kwa mara ya kwanza Ekaristi Takatifu. Ujenzi wa Kanisa la Parokia ulianza mwezi Februari 2017 na tarehe 22 Agosti 2021, Kanisa likatabarukiwa. Hii ni Parokia iliyoanzishwa tarehe 3 Juni 2018. Ni Parokia ya 21 kuanzishwa Jimbo Katoliki la Malindi na ina waamini 604 wanaohudumiwa na Wayesuit chini uongozi wa Padre Sostenes Luyembe, SJ, Paroko akisaidiana na Padre Damas Missanga, SJ. pamoja na Padre Atakelt Tesfay, SJ.

Padre Sostenes Luyembe, SJ, katika mahojiano maalum na Radio Vatican amesema kwamba, bado kuna changamoto kubwa mbele yao kama Parokia. Wanapaswa kujielekeza zaidi katika mchakato wa majadiliano ya kidini kwa kutambua kwamba, hili ni eneo lenye idadi kubwa ya waamini wa dini ya Kiislam. Parokia hii inakabiliwa na changamoto za uinjilishaji wa awali kabisa, ndiyo maana juhudi na nguvu kubwa zaidi inaelekezwa katika kujenga na kudumisha Jumuiya ya waamini, ili waweze kujitambua na hatimaye, kutekeleza dhamana na wajibu wao katika maisha na utume wa Kanisa. Ni wakati wa kuimarisha Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo. Mwaka 1976 katika Mkutano Mkuu uliofanyika mjini Nairobi, Kenya Maaskofu wa AMECEA walitangaza rasmi kwamba "Mfumo wa kuunda Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo, ndio mbinu mkakati rasmi wa uinjilishaji katika Kanisa la Afrika ya Mashariki na utapewa kipaumbele katika miaka ijayo.”

Tangu wakati huo Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristo zimekuwa agenda ya kudumu katika maisha na utume wa Kanisa Afrika Mashariki katika ujumla wake! Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristo ni Kanisa dogo mahalia la familia zinazopakana na ambalo kazi yake hasa ni kusali pamoja, kusikiliza na kutafakari pamoja Neno la Mungu na kulieneza kama kielelezo cha imani tendaji. Wanajumuiya wanahamasishana kuishi maisha ya Kikristo na kuwa mashuhuda wa imani yao. JNNK msingi wake ni Neno la Mungu na Ekaristi Takatifu ambavyo huwaimarisha katika Imani, Upendo na Matumaini katika Umoja (Koinonia - Umoja), wakimshuhudia Kristo Yesu aliyefufuka na kumtangaza kama Mungu na Mwokozi wao ndiyo imani ya Kanisa (Kerygma - Imani); na kushuhudia imani hiyo kwa huduma wanayotoa miongoni mwao wenyewe na kwa maskini (Diakonia - Utumishi).

Padre Sostenes Luyembe, SJ, anaendelea kusema kwamba, kama Parokia wanajielekeza zaidi katika maisha ya Kisakramenti. Kwa mfano Sakramenti ya Upatanisho ni muhimu sana katika safari ya maisha ya kiroho sanjari na mang’amuzi ya miito miongoni mwa vijana Wakristo. Ni katika Sakramenti ya Upatanisho, Mahakama ya huruma ya Mungu, mwamini anaonja huruma, upendo na msamaha kutoka kwa Mwenyezi Mungu; ni mahali ambapo mwamini kutoka katika undani wake, anaguswa na kupyaishwa, huku akitiwa shime ya kusonga mbele katika hija ya maisha ya toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha. Hii ni Sakramenti inayopania kujenga na kudumisha mahusiano ya ndani kabisa na Mwenyezi Mungu.

Maadhimisho ya Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia: “Famiglia Amoris Laetitia” unapania pamoja mambo mengine, kuwasaidia waamini kutambua umuhimu wa Injili ya familia katika maisha na utume wa Kanisa sanjari na ushiriki wao kiroho. Mang’amuzi ya upendo yanayopata chimbuko lake katika maisha ya familia yanakuwa ni wito wa kila mtoto anayezaliwa na hivyo kuwa ni dira na mwelekeo wa utakatifu wa maisha. Sala ni kiungo muhimu sana cha mahusiano na mafungamano ndani ya familia kila kukicha. Wito na Utakatifu wa maisha ni chemchemi ya upendo wa dhati katika maisha ya ndoa na familia, yanayowawezesha wanandoa kukabiliana na changamoto, matatizo na fursa mbalimbali zinazojkitokeza katika maisha yao. Sala ni kiungo muhimu sana kinachowawezesha wanandoa kuishi kikamilifu Sakramenti ya Ndoa katika maisha yao. Sala inawapatia wanandoa nafasi ya kupyaisha Neema waliyopokea ili hatimaye, kukabiliana na mapambano pamoja na majukumu yao ya kila siku. Changamoto ya utakatifu wa maisha inapata chimbuko lake kwanza kwa mtu binafsi, familia na hatimaye, wanandoa katika ujumla wao, kiasi hata cha utakatifu huu, kuwaambata majirani zao. Wito wa utakatifu wa maisha ni changamoto inayotolewa kwa watu wote wa Mungu.

Ifuatayo ni Risala ya Kamati Tendaji ya Parokia. Tumsifuni Yesu Kristo! Mhashamu Baba Askofu Willybard Kitogho Lagho wa Jimbo Katoliki Malindi, Kenya! Tunakukaribisha sana Parokiani Muyeye! Aidha tunakupongeza sana kwa kusimikwa kwako kuwa mchungaji wa Jimbo letu la Malindi. Hongera sana! Parokia ya Muyeye iko chini ya usimamizi wa Mt. Karoli Lwanga! Ni parokia ya Ishirini na Moja kuanzishwa Jimboni Malindi. Uzinduzi rasmi wa parokia hii ulifanyika tarehe 3 Juni, 2018, Sikukuu ya Mt. Karoli Lwanga na Wenzake Mashahidi. Takribani miaka Ishirini iliyopita, Wakristo wa kwanza wa eneo la Muyeye walikutanika kwa sala na ibada chini ya Mbuyu uliopo mbele ya Kanisa jipya, idadi yao ikiwa ni Wakristo wapatao Kumi. Kadiri ya sensa ya Parokia ya mwaka 2020, parokia leo ina wanaparokia 604. Tunamshukuru Mungu kwa ukuaji na uendeleaji wa parokia yetu kwa sasa ikiwa chini ya ulezi wa kiroho wa Mapadre Wayesuit!

Safari ndefu ya kuanzishwa kwa parokia hii inaanza mwaka 2000, sanjari na mwaka wa kuzaliwa kwa Jimbo la Malindi. Chini ya uongozi wa Mhashamu Askofu Francis Baldacchino aliyekuwa mfadhili mkuu wa Kanisa la kwanza kujengwa. Uongozi wa Jimbo ulifanikisha ununuzi wa viwanja kupitia Kamati ya Fedha Jimbo. Zoezi la ununuzi wa viwanja hivi lilisimamiwa na Mwenyekiti wa Halmashauri, wakati huo ikiwa Parokia ya Kanisa kuu, Bw. John Kamande. Kwa vipindi mbalimbali tumeweza kukua mwaka hadi mwaka – kuanzia chini ya mbuyu, jengo la bati, Jengo la Kanisa la Kigango, na leo hii Kanisa lenye hadhi ya Parokia! Tunawashukuru mapadre wa Mill Hill Fathers na Franciscans Sisters of St. Joseph ambao wametulea tangu mwanzo hadi kutufikisha ngazi ya kuwa Parokia. Aidha, tunawashukuru mapadre Wayesuit walioitikia ombi la Marehemu Askofu Emmanuel Barbara, OFM, kuja kuunganika nasi katika utume wa ujenzi wa Kanisa la Kristo! Parokia kwa sasa ina Kigango kimoja tu cha Mayungu (Mt. Bhakita), chenye waamini takribani Ishirini na Sita.

Uongozi wa Parokia: Muundo wa Uongozi wa Parokia yetu unafuatia maelekezi ya Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya wa uendeshaji wa Utume wa Parokia! Kwa ngazi ya kwanza tuna: Familia, Jumuiya Ndogo Ndogo na Vyama vya Kitume, ambazo zina uongozi wake. Viongozi wa Jumuiya wameunganishwa pamoja kupitia Halmashauri ya Walei Parokia. Halmashauri Walei inafanya utume wake chini ya Kamati Tendaji ya Parokia! Parokia inazo Jumuiya kumi yaani Jumuiya ya: Mt. Cecilia, Mt. Veronika, Mt. Paulo, Mt. Padre Pio, Bikira Maria Mama wa Mungu, Mt. Mikaeli, Mt. Bhakanja, Mt. Karoli Lwanga, Mtakatifu Gabrieli na Mt. Bhakita (Mayungu). Licha ya changamoto nyingi zilizopo, Jumuiya zote hizi zimejitahidi kuwa hai! Mikutano na sala za kila juma kwa Jumuiya inafanyika na kila mwezi Jumuiya zinatembelewa na mapadre kwa ajili ya misa na ibada. Jumuiya pia zimekuwa zikishiriki vyema kwenye shughuli za maendeleo ya Parokia na Kijimbo! Kuna wanajumuiya wachache ambao ni wavivu, lakini wengi wanajituma kwenye utume na shughuli za Kikujumuuya

UHAI WA VYAMA VYA KITUME: Kadiri ya himizo wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatikani, Parokia yetu imejitahidi kuwa na utume wa Marika na Vyama vya Kitume. Tunawashukuru wote wanaoitikia na kujiunga na utume huu ambao ni chanchu bora ya mshikamano wa kiimani. Vyama vya kitume na Marika vilivyo hai hapa parokiani ni:CMA; CWA; PMC; VIJANA; MAGIS; YCW; MT. ANNA; MARRIAGE ENCOUNTER (WANANDOA MARAFIKI); KWAYA. Baadhi ya Vyama na Utume huu wa Marika wako hai, ingawa wengine bado hawajasimama imara. Kadiri tunavyoendelea kukua, ni matumaini yetu kuwa tutasimama imara na kushikamana katika utume mbalimbali ambao ni muhimu sana kwa makuzi yetu ya kiroho, kiutu na kiimani!

MALEZI YA KIROHO: Malezi ya Kiroho ya Parokia ya Muyeye yako chini ya uelekezi wa mapadre Wajezuiti. Kwa sasa tunalelewa na Mapadre watatu Wajezuiti. Nyakati za likizo tunawapokea vijana walio kwenye malezi, ambao husaidia kwenye Katekesi, Jumuiya na Vyama vya Kitume na Marika. Kwa kila Siku za Juma kuna misa moja Parokiani. Misa hii huadhimishwa Saa Kumi na Mbili Asubuhi (12.30). Mahudhurio bado ni hafifu. Tunawahimiza Wakristo kujumuika kwenye ibada hizi za kila siku. Aidha, siku ya Alhamisi kila Juma tuna ibada ya Misa na Kuabudu Ekaristi Takatifu! Ibada hizi hufanyika kuanzia saa Kumi Jioni. Katikati ya wiki pia mapadre hufanya mizunguko ya misa za Jumuiya. Siku ya Jumapili tuna misa tatu parokiani na misa moja Kigangoni Mayungu. Mwitikio wa misa kwa Jumapili ni mzuri sana! Ulegevu upo kwenye misa za kila siku na Jumuiya.

HALI YA MAISHA YA KISAKRAMENTI: Uwepo wa Parokia umesaidia ukuaji wa maisha ya kiroho na kisakramenti ndani ya parokia yetu. Tukitambua kuwa maisha bora ya kikanisa yanategemea maisha ya kiroho ya kifamilia na hasa ya wanandoa, jitihada zinaendelea kufanyika kuwaalika wale ambao hawajafunga ndoa waweze kufanya hivyo! Mwitikio bado ni mdogo, lakini matumaini yetu ni makubwa kuwa wengi watajitahidi kufunga ndoa ndani ya Kanisa. Ukosefu wa ndoa unawafanya wengi wetu washindwe kushiriki kikamilifu Fumbo la Ekaristi Takatifu. Tutaendelea kuhimizana kuutambua umuhimu wa Sakramenti ya Ndoa! Aidha, wengi wetu pia tunapswa kujikumbusha Katekesi kama msingi mkuu wa maisha yetu ya kiimani, kwani tumesahau mengi tuliyojifunza utotoni! Vijana na watoto wengi wanaendelea kujitokeza kwa ajli ya mafundisho ya katekesi, ili kujiandaa kwa ajili ya Sakramenti za Ubatizo, Ekaristi na Kipaimara. Tunawashukuru wazazi ambao wamekuwa msitari wa mbele kuwahimiza watoto kuja kwenye mafunzo ya Katekesi parokiani. Kwa mwaka huu tumekuwa na wanafunzi zaidi ya mia moja, ambao wamekuwa wakiandaliwa kwa ajili ya Sakramenti mbalimbli hapa parokiani! Baadhi yao leo wamepokea Ekaristi na Kipaimara! Tunawapongeza wote!

MIRADI YA KIPAROKIA: Ili kunyanyua pato na uwezo wa Parokia, tunaendelea kujitahidi kuwa na miradi mbalimbali ya kimaendeleo. Tunao mradi wa kuwafunza vijana kwenye nyanja ya kilimo na ufugaji – kilimo cha mboga, ufugaji sungura, ndege na kuku. Mwitikio wa vijana hata hivyo umekuwa si mzuri! Tunashukuru uongozi wa Jimbo kwa kutuwezesha kupata kiwanja ambapo mradi huu unafanyika kwa sasa! CMA wana mradi wa viti vya kukodisha ambao husaidia kuingiza kipato kidogo. Kadiri fursa zitakavyojitokeza, itakuwa vyema kuwa na mradi utakaoingiza pato kubwa zaidi. CWA wanakamilisha uanzishaji wa mradi wa ufugaji kuku. Tunataraji mradi huu utajiendesha na kuwapatia kipato kina mama ili kunyanyua vyanzo vyao vya mapato. Parokia imejitahidi kuweka vibanda (stalls) vichache vya kukodisha kwenye viwanja vya parokia ili kuboresha vyanzo vya mapato ya kiparokia. Parokia kwa sasa ina mpango mahsusi wa kuanzisha Kigango cha kudumu huko Mayungu. Mipango ya ununuzi wa eneo imekamilika, na pale hali ya kifedha itakaporuhusu ujenzi huo utaanza polepole. Kuna shule ya watoto wadogo ambayo imeendelea kuwa chini ya ufadhili wa St. Vincent De Paul, kupitia Ofisi ya Parokia ya Kisumu Ndogo. Watoto wote wamekuwa wakisoma kwa kupewa msaada. Tunawashkuru wafadhili wote ambao wamekuwa wakichangia malezi, makuzi na elimu ya watoto hawa.

CHANGAMOTO: Hakuna utume bila changamoto! Baadhi ya changamoto tulizo nazo ni kama ifuatavyo: Kutambua mipaka ya Parokia yetu. Tunatumaini uwepo wako utasaidia huko mbeleni kuweza kutuainishia mipaka ya kiparokia. Kipato kidogo cha wanaparokia na uhaba wa fedha! Parokia haijaweza kufanya mambo mengi kimaendeleo. Nia zetu ni njema na tunaendelea kujitahidi kufanikisha polepole mipango tuliyo nayo kiparokia. Uchache wa makatekista na waalimu wa dini ili kuwafundisha watoto wengi tulio nao na kuwaandaa kwa ajili ya Sakramenti mbalimbali. Uwoga wa Wakristo wengi kurasimisha ndoa zao na kuzifanya kuwa Sakramenti! Tunawahimiza wasio na Sakramenti ya Ndoa wafanye hivyo! Ulegevu wa kushiriki shughuli za Kijumuiya na kanisa kwa ujumla! Wengi wetu ni wazembe wa kuhudhuria jumuiya na kushirikiana shughuli za kiparokia, kama vile usafi na uongozaji wa Ibada Jumapili. Baadhi ya vikundi vya kitume hawana miongozi mizuri ya kitume! Bado havijaimarika! Malezi ya watoto: Ushirikiano wetu katika kuwalea na kuwakuza watoto kiimani bado ni haba sana. Tunaendelea kuhimizana katika kuwaimarisha watoto wetu kiimani!

HITIMISHO: Shukrani zetu za dhati kwa Mungu kwa kuweza kutufikisha hapa tulipo kama parokia. Aidha, tunawashukuru waasisi wa Parokia hii ya Muyeye, Kanisa la Mt. Karoli Lwanga- mapadre wa Mill Hill Fathers na watata wa Franciscan Missionaries of St. Joseph. Shukrani za pekee kwa Br. Franz Bishof kwa kusimamia ujenzi wa Kanisa letu. Shukrani nyingi pia kwa wasanifu wa jengo hili, wajenzi, wafadhili na wanaparokia wote kwa kushikama kufanikisha ujenzi wa Kanisa hili. Shukrani pia kwa Hayati Askofu Barbara, OFM Cap., kwa kuturuhusu kuwa Parokia kabla ya kifo chake. Yeye ndiye aliyeweza kutuletea familia ya Wayesuit hapa Malindi. Tunawashukuru Wayesuit na viongozi wao kwa kuja kusafiri nasi katika safari hii ya kiimani! Tunamwomba Mwenyezi Mungu azidi kutupa ushirikiano mzuri na familia ya Wayesuit ili sote tunyanyuke kiimani, maadili na utume! Mungu atubariki sote wana Muyeye, na Jimbo zima la Malindi! Asanteni sana! Kamati Tendaji.

Jimbo Katoliki la Malindi
23 August 2021, 14:21