Kanisa Katoliki Tanzania limekuwa ni mdau mkubwa wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi nchini Tanzania katika sekta ya elimu, afya na ustawi wa jamii. Kanisa Katoliki Tanzania limekuwa ni mdau mkubwa wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi nchini Tanzania katika sekta ya elimu, afya na ustawi wa jamii. 

Mchango wa Kanisa Katoliki Nchini Tanzania! Elimu, Afya na Ustawi wa Jamii

Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga amemhakikishia Rais Samia kuwa Baraza litatoa ushirikiano kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika masuala yote yenye ustawi, maendeleo na mafao ya watanzania, kuwa Kanisa linajishughulisha na ustawi wa mtu mmoja mmoja na ustawi wa jamii, Kanisa linajishughulisha kumstawisha mwanadamu kiroho na kimwili. Elimu na Afya!

Na Remigius Mmavele, - Dar Es Salaam.

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC, hivi karibuni, limempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kupokea majukumu ya urais wa nchi ya Tanzania, kuwa Mwanamke wa kwanza kuiongoza Tanzania, kuendesha kipindi cha mpito kwa serikali ya awamu ya tano kwenda awamu ya sita kwa utulivu na amani. Katika pongezi hizo zilizosomwa mbele ya Rais Samia na Askofu mkuu Gervas Nyaisonga, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania ambalo limempongeza pia Rais Samia kwa kuendeleza na kuongeza mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 pamoja na kuimarisha utetezi na ulinzi wa haki msingi za binadamu kwa njia mbalimbali. “Tunamshukuru Mungu kukubali wewe kuwa Kiongozi wa Taifa letu na tunakuombea Hekima, Afya na Mshikamano, Mungu akuwezeshe kutimiza majukumu yako vema na uweze kukidhi matarajio ya watanzania wote uliokabidhiwa” nukuu ya sehemu mojawapo ya salamu hizo za pongezi. Mkutano kati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ulifanyika katika Ukumbi wa Baraza la Maaskofu Katoliki uliopo Makao Makuu ya Baraza, Kurasini, Jimbo Kuu la Dar es Salaam.

Askofu Mkuu Nyaisonga amemhakikishia Rais Samia kuwa Baraza litatoa ushirikiano kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika masuala yote yenye ustawi, maendeleo na mafao ya watanzania, kuwa Kanisa Katoliki linajishughulisha na ustawi wa mtu mmoja mmoja na ustawi wa jamii, Kanisa linajishughulisha kumstawisha mwanadamu kiroho na kimwili. Kwa vile ni jukumu la Kanisa kumkomboa mwanadamu dhidi ya utumwa wa aina yoyote ile jambo ambalo ni msingi wa uwepo wa Kanisa Katoliki nchini Tanzania. Salamu za Baraza la Maaskofu Nchini Tanzania zimekwenda sanjari na ombi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kurejea nia yake ya awali ya kurekebisha sera mbalimbali katika sekta ya Elimu ili vyuo na taasisi za elimu ya juu zinazosimamiwa na Kanisa ili ziweze kutoa elimu kwa watu wenye hali duni ya maisha hususani vijijini liweze kufanikiwa. Kipindi cha kati ya Mwaka 1996 hadi 2016 kulikuwepo na mafanikio makubwa katika sekta ya elimu.

Mabadiliko ya sera mbalimbali za Sekta ya Elimu ya Juu yamelifanya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kupata hasara katika mikoa na wilaya zilizopo mipakani na vijijini katika maeneo ya Kagera, Songea mkoani Ruvuma, Mtwara na Ifakara. Katika sekta ya Afya pia Bazara la Maaskofu Katoliki Tanzania limetoa ombi kwa Rais kupitia upya sera ya ushirikiano baina ya mashirika ya dini na serikali ili kwa pamoja, ili lengo liwe kwa pamoja kutatua matatizo ya wananchi hasa katika maeneo ambayo yanauhitaji mkubwa na sio kuendeleza maeneo ambayo tayari yana uwekezaji mkubwa uliofanywa na taasisi na Kanisa katoliki. Ushindani katika sekta ya afya umesababisha Hospitali zinazomilikiwa na Kanisa kudhoofishwa hali ambayo inawakosesha wananchi wenye kipato cha chini kupata huduma iliyo bora na kwa gharama nafuu.

Awali akitoa utangulizi katika Mkutano huo Askofu Msaidizi Method Kilaini wa Jimbo Katoliki la Bukoba alieelezea kwa ufupi historia ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. Namna lilivyoanza hadi sasa linapoendelea kufanya shughuli zake nchini Tanzania. Askofu Msaidizi Kilaini ameeleza kuwa Baraza hilo lilianza pale wamisionari walipoingia nchini Tanzania na kuanza kuinjilisha ambapo ameeleza kuwa Wamisionari wa kwanza walifika Visiwani Zanzibar mwaka 1860 wakitokea nchi ya Reunion. Kundi hilo la kwanza ambalo ni la Shirika la Roho Mtakatifu liliingia Bagamoyo mwaka 1868 na baada ya kutoka Bagamoyo wamisionari hao walianza kuelekea kwenda hadi Kilimanjaro mwaka 1890 huko waliendelea kusambaa hadi Arusha, Tanga na kuingia Mombasa nchini Kenya.

Kundi la Pili lilikuwa la Wamisionari wa Afrika ambalo lilikuja mwaka 1878 ambalo baada ya kufika Bagamoyo lilielekea Tabora na kutoka Tabora likaelekea Mwanza na kuvuka kwenda mpaka nchini Uganda na kundi lingine lilishuka kwenda hadi Ziwa Tanganyika, Mbeya na sehemu nyingine za Magharibi ya Tanganyika. Kundi la tatu lilikuwa la Wabenediktini ambao waliingia Tanganyika mwaka 1887 ambao walifikia Pugu Jijini Dar es Salaam na kutoka hapo walisambaa kuelekea Bihawana Dodoma, Kwiro Mahenge, Tosamaganga wakashuka mpaka Songea na Mtwara. Askofu Msaidizi Kilaini aliendelea kumwelezea Rais Samia kuwa makundi hayo matatu yaliyofanya uinjilishaji yalikuwa na shughuli tatu muhimu ambazo ni kueneza dini, kuwatibu watu ambao walikuwa wakiwahubiria neno la Mungu pamoja na kuwapa Elimu, waliwafundisha kuandika, kuhesabu na vitu vingine.

Askofu Msaidizi Kilaini alieleza; “Mwaka 1912 Maaskofu Sita walikutana kwa mara ya kwanza jijini Dar es Salaam hapo ndipo mbegu ya kuanzishwa kwa Baraza la Maaskofu katoliki ilipoanza kupandwa, Maaskofu hao walikuwa kutoka Bagamoyo, Dar es salaam, Unyanyembe Tabora, Karema Ziwa Tanganyika pamoja na Nyanza Bukumbi. Mwaka 1912 Maaskofu hao walikutana kwa mara ya kwanza na kupanga namna ya kufanya kwa pamoja katika kuliongoza Kanisa Katoliki”. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania lilianza rasmi mwaka 1956 likiwa ni umoja wa Baraza la Maaskofu lilioundwa na Askofu mwafrika mmoja tu ambaye alikuwa Askofu Laurian Rugambwa wakati huo akiwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Rutabo.

Maaskofu Tanzania

 

12 July 2021, 16:03