Kuna uhusiano mkubwa kati ya Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Sakramenti ya Ndoa Takatifu. Kuna uhusiano mkubwa kati ya Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Sakramenti ya Ndoa Takatifu. 

Uhusiano Kati ya Ekaristi Takatifu na Sakramenti ya Ndoa! Sadaka

Ninaona ni vema tukachukua muda kidogo ili kutafakari Fumbo la Ekaristi Takatifu na kweli za maumbile yetu kama wanadamu. Mwanadamu ni kiumbe chenye roho na mwili. Hivyo, hatuna budi kila mara kumwona katika ukamilifu wake na kamwe tusikae na kumakinika na upande mmoja bila kuutazama upande mwingine. Mwanadamu ni muunganiko kamili wa mwili na roho! Sadaka!

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma

Amani na Salama! Zawadi ya mwili ina nafasi ya pekee na umuhimu wa hali ya juu sana katika imani yetu ya Kikristo. Lakini, leo ninaomba katika sherehe yetu hii ya Mwili na Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo, tutafakari kwa pamoja juu ya Mwili wa Kristo na miili yetu mintarafu maumbile ya uzazi na dhana nzima ya maumbile yetu ya kijinsia. Ninaelewa kuwa siyo mada rahisi na hasa inapoletwa mbele yetu na mmoja ambaye ni mseja na kasisi wa Kikatoliki kama mimi, kwani huenda mtakuwa na maswali juu ya uzoefu wangu katika eneo hilo. Na kwa kweli, lengo langu hapa siyo kujadili sana au kutafakari juu ya Fumbo la Ekaristi Takatifu bali zaidi sana ni kutaka tuone mahusiano ya Mwili wa Kristo na dhana nzima ya miili yetu ya kibinadamu mintarafu maumbile ya uzazi. Leo tunapoishi katika ulimwengu wa utawandazi, hatuwezi kusema kuna miiko ya kujua mambo kadha wa kadha yanayohusu eneo hilo la maumbile yetu ya kijinsia. Kwa mazingira hayo, ninathubutu kusema kile ambacho, hapo awali, kilionekana kuwa ni miiko na siri kubwa. Leo hii, hakuna tena siri wala miiko ile ya kabla ya kipindi cha ulimwengu wa utandawazi. Leo, ndoa nyingi zinavunjika na kuparaganyika, kisa tu, mitandao ya kijamii au teknolojia ya mawasiliano. Leo, simu na mitandao imekuwa ni kichocheo kikubwa na cha haraka cha kujenga au kumomonyoa mahusiano.; Hivyo, vifaa au mifumo ya mawasiliano ya kijamii, ama inajenga mahusiano au kuyabomoa na kuyaangamiza kabisa.

Ni katika muktadha huu, ninaona kuwa ni vema tukachukua muda kidogo ili kutafakari Fumbo la Ekaristi Takatifu na kweli za maumbile yetu kama wanadamu. Mwanadamu ni kiumbe chenye roho na mwili. Hivyo, hatuna budi kila mara kumwona katika ukamilifu wake na kamwe tusikae na kumakinika na upande mmoja bila kuutazama upande mwingine. Mwanadamu siyo mwili tu, wala roho peke yake, bali ni muunganiko kamili wa mwili na roho. Ninaona kwamba kuna haja ya Sherehe ya Mwili na Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo kutusaidia pia kutafakari juu ya uhalisia wetu kama wanadamu na hasa katika eneo hilo la maumbile ya kijinsia, ambalo mara nyingi limekuwa likionewa aibu kusemewa. Katika mazingira fulani, Kanisa linaonekana kupoteza hata mvuto katika ulimwengu huu wa leo wa teknolojia na utawandazi, hasa katika mafundisho yake kuhusu elimu ya jinsia ya kimaumbile. Katika mazingira haya ya kimtanziko, ulimwengu umekosa kutenda haki kwa Kanisa kwa kuliona kama taasisi ambayo kazi yake ni kuweka sheria na maagizo ya nini kinaruhusiwa na nini kinakatazwa. Pamoja na ukweli kuwa maisha ya mwanadamu, karibu katika kila eneo kuna sheria na makatazo yake, ila ili kuelewa vema juu ya maumbile yetu ya kijinsia, haitoshi kubaki katika sheria na makatazo tu, bali kuingia na kuona hasa ukweli na uzuri na umaana wa maumbile hayo ya kijinsia.

Mimi siyo mwanamichezo ila ninadhani kwamba akija mchezaji mmoja makini na mzuri wa mpira wa miguu kama kijana Miquisone wa timu ya Simba, na akaanza kutueleza uzuri wa mchezo wa soka kwa kutueleza sheria zake, sidhani kama tutaonja uzuri wa mchezo huo. Mtu hapendi kuucheza au kuuangalia mpira kwa kuwa anapenda sheria za mchezo huo. Ukweli unabaki kuwa ukweli, kwamba mpira wa miguu ni zaidi ya sheria zake. Uzuri wa mchezo wa mpira wa miguu haupo tu katika sheria na miiko yake. Tena, hata wachezaji wa mpira hawaanzi kucheza kwa kujua sheria zake. Vivyo hivyo, hata sisi mashabiki, tena wa ngazi kama yangu, ambao hata uelewa wa sheria ni finyu sana, hungependa kuuangalia na kuushabikia tena kwa furaha. Hivyo, ili kuthamini dhana nzima ya sheria asili za maumbile ya mwanadamu kamwe haifai kuanza kwa kuangalia sheria na makatazo bali kuona uzuri na umaana wake mintarafu leo zawadi ya mwili.

Daima, Kanisa linafundisha na kuangalia juu ya dhana nzima ya maumbile ya kijinsia, likijikita katika sheria ya asili (Natural law). Hiyo ndiyo sheria ya kushiriki katika sheria ile ya milele ya Mungu mwenyewe. Ingawa sheria hiyo mama hutuongoza katika masuala ya sheria zihusuzo maumbile ya kijinsia, bado ninaona kama inatupa muono ambao ni finyu kwa kiasi fulani kwa sababu mara nyingi tunaishia kuyaona maumbile ya kijinsia kama yana lengo la kuzaana na kuujaza ulimwengu tu. Katika mkururo wa mawazo haya tafakarishi, unajikuta ukijiuliza mwenyewe kwamba vipi kuhusu watawa, walei wasiobahatika kuoa au kuolewa! Je, ni nia na lengo pekee ambalo tangu mwanzoni Muumba amependa kumjalia mwanadamu vipawa hivyo? Hivyo, katika sheria ya asili, tendo la ndoa linaonekana kuwepo kwa ajili ya nia kubwa ya kuzaliana na kuujaza ulimwengu. Kwa mtazamo huo wa asili, ambao mimi siupingi, badala ya kujikita na kuanzia katika sheria ya asili ya maumbile, tafakuri yangu itaanzia katika kiini cha imani yetu, yaani Karamu ile ya mwisho, Ekaristi Takatifu. Tena tafakuri yetu itajikita katika Ekaristi Takatifu ile ya kwanza ya Yesu pamoja na wanafunzi wake. Usiku ule, Yesu akiwa pamoja na wanafunzi wake, alitwaa mkate, akaubariki, na kuwapa wanafunzi wake, akisema, ‘’Huu ni Mwili wangu, unaotolewa kwa ajili yenu.’’

Kwa hiyo, kiini hasa cha imani yetu ni zawadi ya Mwili wake Bwana wetu Yesu Kristo (Corpus Domini au wengine wanaiita pia Corpus Christi yaani, Mwili wa Kristo). Katika zawadi hii ya Corpus Christi, labda swali linakuja mara moja kichwani kwamba Ekaristi Takatifu au Mlo ule wa Karamu ya Mwisho unaakisije maumbile yetu ya kijinsia? ‘’Huu ni Mwili wangu’’, ndiyo maneno anayotamka Yesu katika karamu ile ya mwisho au Adhimisho la kwanza la Ekaristi Takatifu kati ya Yesu na wanafunzi wake. Mara nyingi katika imani yetu, kuna hali fulani ya kusahau, na hata kuudharau mwili, na kukazia zaidi roho. Huwa wengi tunasahau kwamba mambo hayo mawili hutegemeana na kujengana. Kutokana na kujisahau, ndiyo maana unaweza kusikia hata misemo mbalimballi katika jamii ikishadidia na kusheheneza hali ya kiroho zaidi.  Utamsikia mtu akimsemea mwingine kuwa “huyu ni mtu wa kiroho.” Mwingine atakuambia kwamba “mwili unafaa nini mbele ya roho yangu?” Ipo misemo na kauli nyingi sana. Hiyo mifano miwili inawakilisha mingine mingi ambayo sijaitaja.

Mwanafalsafa wa Kifaransa wa karne ya 17 aliyejulikana kama Renè Descartes, katika kutumia njia yake ya mashaka ili kuwa na hakika juu ya uwepo wake, anaongozwa na maneno: ‘’Cogito ergo sum’’ ni maneno ya Kilatini yenye maana kwamba “kwa kuwa ninawaza au ninafikiri na nina hakika ninafanya kitendo hicho, basi nina hakika ya uwepo wangu.” Nipo kwa kuwa nina hakika kuwa ninafikiri. Uwepo wangu unahakikiwa na uwezo wangu wa kufikiri, wa kuwaza. Uwepo wangu unahakikiwa na uwezo wangu wa kiroho, yaani akili tambuzi! Kuna kishawishi cha kufikiri namna hiyo na hivyo kujikuta tukijiona kwamba kwetu mwili hauna umuhimu, kwani itoshe kuwa roho tu. Kwa kufikiri hivyo, hata mawasiliano yetu yanakuwa katika namna ya juu zaidi kuliko tunapokuwa katika uhalisia wa mwili na roho. Mawasiliano kati ya malaika, hakika ni ya juu zaidi kuliko yetu sisi wanadamu kwani wao ni roho tu. Hivyo, kati ya malaika mmoja na mwingine hakuna ukuta wa kuzuia mawazo ya mmoja. Hakuna jinsi wala namna ya kuficha kwa mwingine mawazo na fikra zake. Karamu ya mwisho leo inaturejesha katika kuwaza kwa namna nyingine. Ni kwa njia ya mwili, Yesu anatuonesha jinsi tunavyoweza kuingia katika mahusiano, iwe na Mungu au kati yetu binadamu.

Ni kwa njia ya miili yetu, ndipo tunaweza kuingia katika mahusiano na mwanadamu mwingine. Tunaona, kusikia, kunusa na hata kugusa mwingine kwa kuwa tuna mwili. Hivyo, ni kwa njia ya miili yetu kunakuwa na mawasiliano yetu ya kibinadamu kati yetu. Miili yetu ndiyo chanzo na njia pekee ya mawasiliano kati yetu kama vile simu na vifaa vingine vya mawasiliano. Naomba ikumbukwe na kuzingatiwa kwa neno ‘’mwili’’ kwa wayahudi haikumaanisha tu nyama na misuli bali ni mtu mzima na kamili, ndio nafsi kamili yaani muunganiko kamili wa mwili na roho, basi tuongozwe na uelewa huo katika tafakari yetu ya leo. Mwili wa mwanadamu ndiyo mlango wa mawasiliano kati yetu. Kwa njia ya miili yetu, tunaweza kuhusiana kati yetu. Pamoja na kutumia lugha kwa mawasiliano, bado mawasiliano yetu yanachangiwa kwa nafasi kubwa kabisa na ile lugha ya mwili, ambapo tunaona uso ukiongea, macho yakiongea na mikono ikiongea. Hivyo, lugha hutusaidia na kutuingiza zaidi katika ukamilishano wa kimawasiliano zaidi, lakini inaonekana kabisa kwamba lugha ya kwanza inayomuunganisha mwanadamu na mwingine ni ile lugha ya mwili. Mtoto mchanga kabla ya kujifunza kuongea, anawasiliana na mama kwa lugha ya mwili. Hivyo, mara baada ya kuzaliwa, mtoto anawasiliana na mama na watu wanaomzunguka na kuanza hata kutabasamu! Hata kilio cha mtoto ni moja kati ya lugha za mwili za awali kabisa katika maisha ya kila mwanadamu, mtoto mara tu azaliwapo analia, ndio ishara ya uhai!

Chakula ni mojawapo ya kiunganishi muhimu sana cha mahusiano baina yetu. Familia inakaa na kushiriki pamoja meza ya chakula. Hali kadhalika, marafiki katika kuonesha na kuimarisha urafiki wao, kwa hakika, wanaalikana kushiriki chakula pamoja. Hivyo, chakula kinatuunganisha kwa namna ya pekee kabisa. Huwezi kusema kwamba mtu fulani ni rafiki yangu, wakati huwezi hata kutenga au kuona jinsi ya kushiriki naye chakula. Hakika, mara nyingi, tunawaalika marafiki zetu majumbani mwetu au kukaa nao mahali na kushiriki nao chakula kwa sababu kitendo hicho, kinatufanya tuimarishe urafiki wetu na kuonesha kujali. Nafasi ya kukaa na kula pamoja ni fursa inayoturudisha na kutukumbusha nyuma, lakini pia kushiriki hali zetu za sasa na huku tukiangalia kesho yetu kwa matumaini. Kwa kuzingatia umuhimu wa kula na marafiki, wakati anapoweka Agano Jipya kati ya Mungu na mwanadamu, Yesu anawakusanya na kuwaalika wanafunzi wake katika mlo ule wa jioni; karamu ile ya mwisho pamoja nao kabla ya mateso, kifo na ufufuko wake. Alitwaa mkate, akaubariki, kuumega na kuwapa wale. Hapa kula haikuwa tena kama vile mlo wa kawaida wa kibaiolojia bali sasa kuonesha muungano wa Agano Jipya unaojengeka katika Upendo kamili kabisa kati ya Mungu na mwanadamu. Na ndiyo hivyo hivyo, hata katika suala la maumbile yetu ya kijinsia.

Kwa kuwa sisi wanadamu tu viumbe tunaotumia lugha, mahusiano yetu ya kijinsia yanapewa maana ya kina zaidi. Ni kwa njia ya mahusiano hayo wawili, wanadamu wanaonesha muunganiko wa pekee kabisa. Ni kwa lugha ya miili, wawili wanaingia katika mahusiano ya mapendo. Miili inaongea hata kabla ya maneno ya lugha ya kawaida na hata kukubaliana kabla ya kauli za kutoka kinywani. Ni kwa njia ya miili basi mwanadamu anawasiliana kwa namna ya ndani na kina kabisa. Mwili umeumbwa kwa ajili ya mawasiliano, sura imeumbwa kwa kuwasiliana baina ya wanadamu. Sura ndiyo mlango wa nyumba ya mwili. Ni kwa njia ya sura, mtu anaingia katika mawasiliano na mahusiano na mwingine. Hivyo, kinywa na hata maneno au busu hukamilisha kile ambacho tayari sura ilishawasilisha. Hivyo, kwa msingi wa hoja za tafakuri hii, kama Kanisa huanza kuzungumzia juu ya dhana nzima ya maumbile ya kijinsia kwa kuanza kwanza kueleza nini kinaruhusiwa na nini kinakatazwa na Kanisa, ni kuanzia mahali pasipofaa sana. Maadili ya Kanisa siyo juu ya nini kinaruhusiwa na nini kinakatazwa na Kanisa, bali jinsi ya kuhusiana na wengine kwa namna ile ambayo Mungu katika uumbaji, ametaka tuhusiane na kuwasiliana.

Maadili siyo makatazo bali ni kuniwezesha kuishi na wengine kwa namna ile ambayo Mungu ametuumba kwa kuhusiana na kuwasiliana. Kitendo ni kibaya, siyo kwa sababu kinakatazwa, bali kwa kuwa kinakinzana na uhalisia na ukweli wa mahusiano baina yetu kama wanadamu. Hivyo, leo Yesu anabadili mtazamo mzima wa mitazamo yetu kuhusu maadili na maisha yetu wanadamu, kwani anaingia katika Agano na mwanadamu kwa njia ya zawadi ya Mwili wake (Corpus Domini). Ni kwa njia ya Mwili wake anatualika kuingia katika mahusiano ya pekee kabisa na Mungu. Huu Mwili unatolewa kwa ajili yetu, Mwili wake ni zawadi kwetu. Labda tutafakari nini maana yake kutupa Mwili wake kama zawadi kwetu. Hii inaweza kuwa ngumu kueleweka, hasa pale mwili tunapoushusha na kudhani kuwa unaweza kuwa mali ya mtu mwingine. Mitazamo kama ile ya mume kuwa ni mmiliki si tu wa mwili wake bali pia wa mke wake, inachochea ugumu zaidi. Hivyo, mwanaume angeweza kufanya lolote kwa mwili wa mke wake, lakini mke kamwe hawezi kuumiliki mwili wake kama vile mume awezavyo. Na ndio maana utaona hata katika jamii zetu mke akikutwa katika uzinzi au akikosa uaminifu, hapo linakuwa ni kosa kubwa sana na hata kusababisha ndoa nyingi leo kuvunjika. Kama ni mume anayekosa uaminifu, basi mke hana budi kusamehe kwani mume ana haki na mume wake, ila mke ni mali ya mume.

Leo Yesu anatoa Mwili wake kuwa zawadi yetu. Mwili wa Kristo ni zawadi kwa Kanisa lake, kwa ajili ya uzima wa milele. Anapotoa Mwili wake anatualika nasi kuwa na uelewa mpya juu ya miili yetu. Anatuambia kuwa ni mwili daima ambao unapaswa kunikumbusha kuwa mimi ni zawadi itokanayo na upendo wa wazazi wangu na hatimaye sote ni zawadi ya Mungu aliye Bwana na Muumbaji wetu sote. Sisi ni zawadi! Mwili kwa wayahudi si tu nyama na misuli bali mtu au mwanadamu katika ukamilifu wake, ndio muunganiko wa mwili na roho. Hivyo, hata mahusiano ya ndoa hayana budi kujengeka katika ukweli huo kuwa kila mmoja ni zawadi kwa mwenzake wa ndoa. Na pia, mwingine hana budi kumpokea mwenzake kama zawadi na kamwe si kama mali yake anayoimiliki au kuitawala. Ni mmoja anajitoa mzimamzima kama zawadi kwa mwenzake! Ni mahali ambapo wawili wale wanajifunza kujitoa zawadi kamili bila kujibakiza, huku wakijitoa kwa kuongozwa na imani na uaminifu kati yao. Ni mahali pa kujifunza kupokea zawadi, isiyo kama zawadi nyingine zozote tunazoweza kuzifikiria katika ulimwengu huu, kwani hapa zawadi inakuwa siyo kitu au mali bali ni mwili wa mwenzako, yaani mwenzako katika ukamilifu wake.

Hivyo, lazima kupokea zawadi hii ya juu kabisa kwa shukrani na kwa heshima kubwa. Mwingine kamwe si kitu bali ni mtu, hivyo huna budi kumpokea kwa heshima kubwa na shukrani ya pekee. Hivyo, maneno ya Kristo katika karamu ya mwisho yanatuongoza leo katika mahusiano ya kindoa kati ya mume na mke. Maisha ya ndoa ni maisha ya muunganiko. Kwa hiyo, hayana budi kuakisiwa na kitendo cha kujitoa baina ya hawa wawili. Wanandoa hawana budi, kama nilivyosema hapo juu, kujitoa na kupokeana kwa kila jambo kwa shukrani na heshima. Taasisi ya ndoa ni matunda ya kujitoa zawadi kwa wawili, yaani mtu mume na mtu mke, ndoa ni matokeo ya kujitoa zawadi kama vile Kristo anavyojitoa zawadi katika Adhimisho la Ekaristi Takatifu. Yesu anapotoa Mwili wake kuwa zawadi kwetu katika Karamu ya mwisho anakutana na hali kinzani isiyokuwa rafiki sana kwake. Yesu anashiriki mlo na karamu ile pamoja na Yuda Iskariote ambaye alimuuza kwa vipande vya fedha.

Anashiriki pia pamoja na Petro ambaye alimkana mara tatu na hata mitume wengine ambao kwa sehemu kubwa walikimbia na kujiweka mbali na Bwana na Mwalimu wao. Pamoja na hali hizi kinzani, bado Yesu hasiti kuutoa Mwili wake kwetu hata leo. Pamoja na ukweli kuwa mara nyingi tunakuwa mbali naye, bado Yesu anatoa Mwili na Damu yake kuwa chakula chetu kwa ajili ya uzima wa milele. Ni kwa kumwangalia Yesu katika mlo na karamu ile ya mwisho nasi pia na hasa wanaokuwa katika mahusiano ya kindoa kuiga na kujifunza kutoka kwake. Yesu anatoa Mwili wake katika mazingira yale ya kusalitiwa, kukanwa na hata kukimbiwa sio na watu wa mbali, bali wale aliowapa Mwili wake wale na Damu yake wanywe. Ni kwa kumwangalia Yesu tu katika karamu ile ya mwisho, ndipo kila mmoja anayeingia katika mahusiano ya kindoa anapata nguvu ya kusonga mbele pamoja na changamoto au magumu yanayoweza kutokea katika maisha ya muunganiko wa mume na mke.  Maumbile ya kijinsia hasa, ni kwa ajili ya kuwaunganisha mtu mume na mtu mke. Lugha ya mwili inawaunganisha wawili hawa. Inawaleta pamoja. Lakini, tumeona katika karamu ya mwisho mmegeko na kukosekana kwa muunganiko kamili baina ya Yesu na wanafunzi wake. Yuda anamsaliti Yesu, hamuoni tena Yesu kama Rafiki na Mwalimu wake, bali anamuona kama kitu au bidhaa ya kuwekwa na kunadiwa au kuuzwa sokoni kwa vipande 30 vya fedha.

Petro anamwahidi Yesu kuwa yupo tayari kutoa maisha yake kwa ajili ya Mwalimu na Rafiki yake, lakini wakati wa majaribu ulipofika, hakuweza kusimama na kuishi kiapo chake. Petro anamkana Yesu mara tatu kuwa hamjui na wala hana mahusiano na mtu huyu. Hata katika mazingira haya ya kusalitiwa na kukanwa Yesu anabaki kimya. Hana la kusema. Na hivyo hivyo, hata katika mahusiano ya ndoa, leo adui mkubwa ni usaliti na uongo, ni kukosa uaminifu wa dhati. Mfalme Daudi alipolala na Batsheba aliyekuwa mke wa Uria, dhambi au kosa lake, halipo katika kuzini tu bali katika uongo na hujuma. Na ndiyo maadili ya Ndoa katika Kanisa. Katika kusheheneza tunu ya zawadi ya mtu kwa mwenzake, linawaalika wanandoa kuwa wakweli na miili yao, ili kuepuka uongo na hujuma. Kushiriki tendo la ndoa na mwingine ni sawa na kusema ‘’ninajitoa mwili wangu kama zawadi kwako bila kujibakiza, sasa na daima, na pia ninakupokea nawe mwenzangu kama zawadi kwa heshima na shukrani kubwa.’’ Mwili naomba kukumbusha kila mara ni kujitoa mtu mzima kwa ajili ya mwingine na kwa daima.

Hata hivyo, bado maadili ya Ndoa yanawataka wanandoa kuwa na maneno ya kuponyana pale wanapoanguka katika uongo na hujuma. Ni kuwa na maneno yanayoweza kuponya madonda na machungu yaliyosababishwa na uongo na kukosa uaminifu. Hivyo, anayekosa uaminifu haitoshi tu ila kwa kutumia busara kubwa na hekima kuona pia kujipatanisha na mwenzake. Ninarudia kusisitiza hapa kwamba ni lazima kutumia hekima na busara ili kuepuka madhara zaidi. Pamoja na hayo, pale mwingine anapogundua, bila mashaka, kuwa mwenzake amekosa uaminifu, basi hapo aone jinsi ya kujipatanisha na Mungu na mwenzake wa ndoa pia. Katika Karamu ya mwisho Yesu anakuwa ni muhanga wa uongo na usaliti kama tulivyoona hapo juu. Ananunuliwa na wenye pesa na wenye nguvu na mamlaka. Anachukuliwa kwa nguvu na maaskari na kumuwamba pale juu msalabani. Yesu hakujibu dhuluma na usaliti kwa mabavu na nguvu bali aliyapokea yote kama mmoja aliye mnyonge na duni kabisa. Alijikabidhi katika mikono ya wanafunzi wake. Hali hiyo inaashiria kwamba alikataa kujitetea yeye mwenyewe. Hata kama walimsaliti na kumkana, yeye alibaki mwaminifu mpaka dakika ya mwisho. Yesu hakujibu uovu kwa uovu bali aliyapokea yote kwa utulivu na ukimya mkubwa!

Baadhi ya ndoa leo zinagubikwa na ubabe au mabavu na unyanyasi wa kila aina. Tunaweza kuona pia Mfalme Daudi kwa Uria ni ubabe na mabavu, alitumia madaraka yake katika kumdhulumu Uria. Hebu angalia jinsi wanawake leo wanavyonyanyasika kijinsia kwa kubakwa iwe majumbani, makazini, na kwa bahati mbaya, nikiri kwamba hata makanisani, matukio hayo ya aibu kubwa yanasikika. Si ajabu kabisa kusikia leo kuhusu wanawake wanaotumika kingono. Dhuluma za kingono leo dhidi ya watoto si tu zinasikika huko nje, bali hata kati yetu makasisi wa Kanisa Katoliki na madhehebu mengine. Tumetuhumiwa, na baadhi kuthibitika kwamba tunadhulumu watoto wengi ulimwenguni kote wa kike na kiume kwa kutumia nafasi zetu au madaraka yetu au nguvu na mabavu yetu. Nikiri pia kwamba hata baadhi yetu makasisi, mara ngapi tumetuhumiwa, na baadhi yetu kuthibitika kwamba tumetumia nafasi zetu kudhulumu ndoa za watu kwa kuingia katika mahusiano na wake zao. Hapo hakika, tunafanana na Mfalme Daudi alivyomdhulumu Uria. Hapo tunapotoka katika maana na uzuri wa tendo la ndoa, la hata juu ya maumbile yetu ya kijinsia kila linapotumika nje ya uzuri wake wa kujitoa zawadi na ya daima kwa mwingine.

Tunaweza kukubaliana kuwa ili kuzungumzia maadili yanayohusu maumbile yetu ya kijinsia haitoshi kuzungumzia nini kinakatazwa na nini kinaruhusiwa na Kanisa.  Kama Mtakatifu Papa Yohane Paulo II alivyowahi kusema kuwa, hata mume anaweza kumbaka mke wake. Hii inashangaza tunaposikia kwa mara ya kwanza ila yafaa tukumbuke kila mara tendo la ndoa ni tendo la upendo. Hivyo, wawili wote kwa pamoja, lazima wajitoe kama zawadi na kamwe isiwe kwa ajili ya kutimiza matakwa ya mmoja tu. Hebu tufikirie watoto wangapi leo wanalazimishwa na hata kuuzwa katika soko la kitalii la ngono karibu duniani kote. Hebu fikiria watoto sio tu wa kule Tailandi na Ufilipino, bali hata katika miji yetu ya kitalii katika Afrika Mashariki na hata Afrika kiujumla. Hivyo, kila mara katika mahusiano ya kijinsia panapokuwa na mabavu na ukubwa wa aina yoyote ile, hapo mahusiano hayo yanapoteza maana na uhalisia wake kadiri ya mpango wa Mungu. Mahusiano ya kindoa hayapaswi kuwa bidhaa sokoni inayoweza kuuzwa, bali ni zawadi inayotolewa kwa msukumo wa upendo. Ndoa inaakisi Ekaristi Takatifu kwani ni zawadi na sio kitu au bidhaa, ni mtu anajitoa zawadi kwa yule anayempenda.

Karamu ya mwisho inatukumbusha kuwa kiini cha mahusiano ya kijinsia ni kukataa kila aina ya manyanyaso na badala yake ni maelewano na usawa. Mmoja anapotamani mwili wa mwingine, basi isiwe kwa namna ile ya kibinafsi kama vile ni mmiliki wa mwili wa mwingine, bali wanapaswa kuingia katika mahusiano ya upendo na kujitoa kwa heshima na shukrani na kamwe siyo kama simba atamanivyo nyama kwa kuirarua na kuisambaratisha. Tamaa ile haina budi kuamsha furaha kwa mwingine, na hivyo mwingine kujiona ni wa thamani na kamwe siyo kujisikia duni na mnyonge. Mtu anaposhirikishwa tendo bila msingi wa upendo wa Kimungu, anashiriki kwa lengo la kumfurahisha huyu mwenye nguvu, aidha kifedha au kimadaraka au hata nguvu za kimwili. Kitendo cha kushirikishana tendo la upendo wa mwili, kinapaswa kuamsha furaha na thamani kwa wote wawili na kamwe asiwepo mmoja anayetumia ukubwa au nafasi yake kwa kumtumia mwingine kama bidhaa. Mmoja asijisikie kamwe kuwa anatumika kwa ajili ya mwingine bali wote wawili wanajitoa kwa heshima na shukrani kubwa. Mtume Paulo anasema: ‘’Mke hana mamlaka juu ya mwili wake, bali mumewe anayo; hali kadhalika naye mume, hana mamlaka juu ya mwili wake, bali mkewe anayo’’ (1Wakorintho 7:4)

Tamaa ile haina budi kuwepo kwa wote wawili. Kila mmoja anatamani kutamaniwa, na hapo kuthamini pia tamaa ya mwingine. Daima kuna furaha kuona mwingine akikufurahia, na pia unaona fahari kuona mwingine naye akiona fahari juu yako.  Askofu Rowan Williams, Askofu mkuu wa Cantebury ambaye yeye ameoa na ana mke, anasema kwamba katika mahusiano ya kindoa, hapo sina dhamana juu ya mwili wangu mwenyewe. Kila mara ninapokuwa katika matamanio ninabaki na hali ifuatayo: Siwezi kujitimilizia tamaa na mahitaji yangu nikibaki mwenyewe. Tunakuwa katika hali ya kutoweza kujisaidia pale tunapobaki wenyewe bila mwingine. Ili mwili wangu uweze kuwa sababu ya furaha kwa mwingine, kumpokea mwingine kwangu hapo lazima awepo mwingine, ambaye ninamuona au kumgusa, kumpokea na kumthamini. Ndiyo kusema kuwa mimi ninakuwa zawadi na chanzo cha furaha kwa mwingine. Kutamani furaha yangu ni sawa na kutamani furaha ya yule anayenitamani. Furaha yangu ya kimwili, ni faraha ya kimwili ya mwingine.

Karamu ya mwisho ni mwaliko kwetu kushiriki uduni wa Kristo, kwa jinsi alivyojikabidhi mikononi mwa wanafunzi wake aliowaalika kuutwaa Mwili na Damu yake. Ni udhaifu wake wa daima kwani anabaki mpaka leo kujitoa kwetu tulio wanyonge na wadhambi. Kristo Mfufuka anawatokea wanafunzi wake na kuwaonesha makovu ya madonda yake. Ndiyo kusema kwamba anabaki daima hata katika utukufu wa milele akiwa na makovu ya madonda yale kama ishara ya unyonge na uduni wake, ishara ya Upendo wa Mungu kwetu. Ni kumbukumbu ya Upendo wa milele wa Mungu kwangu na kwako. Je, nasi mara ngapi tumekubali kubaki na makovu ya madonda yatokanayo na gharama ya upendo wetu kwa wengine? Kuamini katika ufufuko maana yake ni kuamini katika kupenda hata kwa kupata madonda na makovu kwani tunajua mwisho wetu siyo kifo bali kushiriki maisha ya utukufu wa milele pamoja na KRISTO mwenyewe. Usawa na upendo kamili kati ya wanandoa si tu ni Injili inayoishi bali ni kielelezo cha jamii zetu zinazokuwa na kishawishi cha tofauti na matumizi mabaya ya madaraka na mamlaka, iwe katika jamii za kiraia bali hata zile za kikanisa.

Mahusiano mazuri na yenye afya ya kindoa yanatoa changamoto kubwa hata katika taasisi za kisiasa katika ulimwengu wetu wa leo. Kama tangu nyumbani tayari watoto wanaonja usawa na hali ya kuheshimiana, basi hata wanapokuwa watu wazima na kuchukua wajibu mbalimbali hawatakuwa na kishawishi cha kugandamizana au kuona kuwa mmoja anabudi kuwa chini na kutawaliwa tu. Na ndio maana hata leo Mama Kanisa anajitathimi kuona kuwa anaweza kuwa na mapadre wanaothamini sadaka ya useja ikiwa tangu katika familia wamepokea malezi ya kuthamini maumbile na tofauti za kijinsia. Wasemari leo hawapaswi kulelewa tena kwa kukaa mbali na wanawake, badala yake kuwa msaada mkubwa katika kuwasadia kukomaa katika mahusiano na hivyo hivyo hata katika malezi ya watawa wa kike mintarafu mahusiano yao na watu wa jinsia ya kiume. Tofauti zetu za kimaumbile ya kijinsia ni uzuri wa uumbaji wa Mungu kwa mwanadamu. Pamoja na usaliti, tunaona Yesu anageuza usaliti ule kwa kujitoa Mwili na Damu yake kama zawadi kwa wanafunzi wake. Kila adhimisho la Ekaristi ni adhimisho la uaminifu, na ndiyo maana kila maadili ya Kanisa yanajengeka katika uaminifu. Tunajitoa wenyewe, miili yetu, maisha yetu, matumaini na hata hofu zetu, kwa mwingine bila kujibakiza sasa na daima. Na hili tunalishuhudia katika maagano ya wanandoa kuwa wanajitoa na kupokeana siku zote za maisha yao. Lakini, hii leo imeonekana kuwa changamoto kubwa katika jamii zetu.

Taasisi ya ndoa leo imekuwa ni moja ya taasisi inayokosa udumifu. Tunaishi katika ulimwengu wenye utamaduni wa kila kitu ni kwa mkataba tena wa muda mfupi, iwe kazini na hata majumbani. Na hii inazaa matatizo na sintofahamu nyingi katika jamii zetu na hasa kwa wanakanisa. Leo hata baadhi ya wakristo, wanaona labda Kanisa halina budi kubadili baadhi ya mafundisho yake mintarafu sakramenti ya ndoa. Na si tu kwenye maisha ya ndoa bali hata kwa sisi tulioingia katika maisha ya wakfu kama makasisi na watawa. Bado leo kuna wengi wanatoka katika maisha ya ukasisi na utawa kana kwamba siku ile ya kuwekwa wakfu tuliweka maagano au mkataba wa muda mfupi tu au basi ngoja kwanza niingie nione, nikiona kama mambo hayaendi basi nitarudi na kusema natoka! Ni utamaduni wetu wa leo, hakuna anayetaka kuingia katika mahusiano ya kudumu na ya kiaminifu bila kujali hali au nyakati kuwa ngumu au rahisi. Ni kama vile tunataka kupata wokovu kwa mteremko tu bila madhila yoyote. Uaminifu ni wa muhimu hata kati ya marafiki. Uaminifu usichukuliwe tu kuwa muhimu kwa watu wa maisha ya ndoa na hata wale wanaoitwa kuishi maisha ya wakfu kama makasisi na watawa.

Uaminifu hapa siyo tu ule wa kutopeana talaka na kuachana au kutengana. Badala yake ndiyo hali ya kujitoa mzimamzima kwa mwingine, kumuona mwingine ni kujiona wewe mwenyewe. Inachukua muda kuingia katika mahusiano. Inachukua muda kuwa huru na wazi mbele ya mwingine. Jinsi muda unavyosonga katika mahusiano, ndivyo mwingine anavyopata kukujua na hata kugundua si tu mema na mazuri yako, bali hata mabaya na udhaifu wako. Uaminifu daima ni hatarishi na una gharama zake zikiwamo kujali, kujinyima na kujitawala. Hivyo, ujasiri unahitajika ili kubaki katika mahusiano, hasa pale unapogundua udhaifu na mabaya ya mwingine. Ni kwa njia ya Ekaristi pekee tunapata nguvu kama ile ya Kristo mwenyewe hata baada ya kugundua kusalitiwa na kukanwa na hata kukimbiwa, bado anatoa Mwili na Damu yake kwangu na kwako. Yesu hata leo anaendelea kujitoa kwa ajili yetu sisi tunaomsaliti, kumkana na hata kumkimbia mara nyingi.  Kifo kinapobisha hodi, hapo mahusiano yetu yanakuwa matatani na hata tunakosa maneno ya kuongea, kwani sote tunagubikwa na machungu na hofu kuu. Katika karamu ya mwisho mbele ya Yesu ni kifo, kwani alishajua kuwa saa yake sasa imewasili na hana budi kutimiza mapenzi ya Mungu Baba. Ni katika muktadha huo hatuoni Yesu akiwasusa na kuwaacha wanafunzi wake ambao kwa kweli kila mmoja sasa hataki tena kutambulika kama mwanafunzi wake, bali anatoa Mwili na Damu yake kwa ajili yao na yetu mpaka leo.

Uhusiano wa kifo na maisha yetu ya kijinsia ya maumbile, vina uhusiano mkubwa, hata kama tunabaki tukishangaa. Katika Agano la Kale, ni kwa njia ya uzao tu, mtu alikuwa na uhakika wa kuendelea kuishi hata baada ya kifo chake. Hali hii ipo sana pia katika tamaduni zetu za Kiafrika. Hata unapowashirikisha wazazi, ndugu na jamaa na marafiki wazo la kuwa kasisi au mtawa, utasikia “kwa hiyo, utakufa bila kutuachia mjukuu au bila kutuachia sura yako.” Hapa kila mmoja ajaribu kuingia katika mila na tamaduni zake. Tunakubaliana kuwa uzao ni faraja kubwa pale mtu anapouacha nyuma baada ya kifo chake. Wazawa wanabaki wakibeba jina na sura ya mzazi wao. Na hata leo pia, bado mtazamo huo upo. Kwa akina mama wanapojifungua, saa ile wanaona ni saa ya kupambana kati ya uzima na kifo. Na ndiyo utasikia mama leo anasema tumbo la uzazi linamuuma pale mtoto wake anapopatwa na mabaya au magumu. Hebu fikiria leo akina mama wazazi wanaojifungua wakiwa na shida mbalimbali za uzazi, tena katika mazingira duni ya nchi yetu na bara letu na hata ulimwenguni kote. Fikiria leo akina mama wenye maambukizi ya virusi vya UKIMWI na wanapaswa kujifungua watoto salama. Fikiria leo akina mama wajawazito wasiokuwa na uwezo au jinsi ya kupata huduma bora za uzazi na mengi ya namna hiyo.

Katika Kristo pekee, upendo unashinda kifo! Upendo wa Mungu Baba kwa Mwana tunaona unashinda nguvu ya mauti na kifo.  Hivyo, kama kweli tendo la ndoa ni kitendo cha upendo basi daima kifo hakiwezi kuwa na neno la ushindi au kauli ya mwisho. Mama pamoja na maumivu na hofu kubwa ya kuwa kati ya uzima na kifo, bado anaendelea kutaka mtoto wa pili na wa tatu na kadhalika na kadhalika, kwani anasukumwa na upendo kwa watoto. Hapa hatuna budi kuonja na kuthamini upendo wa mama zetu. Jamii zetu leo tunaona zinagubikwa sana na agenda ya mahusiano au maumbile ya kijinsia, lakini kila mara tunakosa ukina na upana wa maana yake. Ukristo hauna budi kuonesha uzuri na maana yake na hivyo katika kuzamisha zaidi tafakuri yangu, ninarudia kusema kwamba Kanisa halipaswi kuanza kwa kufundisha sheria na makatazo na nini linaruhusu bali kuweka mbele ya waamini uzuri na maana pana ya jinsia za maumbile. Tabia zetu za mahusiano ya kijinsia, hazina budi kuwajenga watu katika heshima na mapendo yanayoakisi pande zote mbili kwa usawa. Zinapaswa kuponya madonda na kuvunja ukimya. Yanapaswa kujengeka katika uaminifu na pia kutoa nafasi kwa watu kuyaingia huku wakijua pia magumu na changamoto zake na jinsi ya kuyakabiri.

Kanisa halina budi kutenga muda wa kuwaanda vema wale wote wanaopenda kuingia katika mahusiano ya mume na mke. Ndoa nyingi leo zinajikuta katika mitafaruku isiyoisha kwa kuwa wahusika waliingia bila kujua nini maana pana na ya kina ya ndoa. Ndoa haina budi kuakisi karamu ile ya mwisho. Ndoa ni Sakramenti ya upendo, upendo unaoakisiwa na ule wa Yesu. Upendo usioangalia hatari ya kusalitiwa, kukanwa wala kukimbiwa bali unaojikabidhi mzimamzima kwa mwingine bila kutanguliza mashaka na kukosa imani kwa mwingine. Sehemu kubwa ya tafakari hii imechotwa na kuhaririwa kutoka katika Kitabu cha Pd. Timothy Radcliffe, OP kiitwacho “Christians and Sexuality in the Time of AIDS.’’ 2008. Ninawatakia tafakuri njema na hasa kwa wanandoa, tunapoadhimisha Dominika hii ya Sherehe ya Mwili na Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo. Sakramenti ya Ndoa Takatifu ni Sakramenti ya zawadi ya mwili kwa wanandoa kama vile Kristo anavyotoa Mwili na Damu yake kuwa zawadi yetu kwa ajili ya uzima wa milele. Ndoa ni safari ya maisha ya sasa na hata kusindikizana katika umilele.

03 June 2021, 09:04