Padre Stefano Kaombe: Siku ya Kristo Yesu Mchungaji Mwema: Siku ya 58 ya Kuombea Miito: Dhamana na Jukumu la Familia kulea, kukuza na kutegemeza miito mbalimbali hasa Daraja Takatifu na Utawa. Padre Stefano Kaombe: Siku ya Kristo Yesu Mchungaji Mwema: Siku ya 58 ya Kuombea Miito: Dhamana na Jukumu la Familia kulea, kukuza na kutegemeza miito mbalimbali hasa Daraja Takatifu na Utawa. 

Padre Stefano Kaombe: Mapadre na Watawa Si Vitega Uchumi!

Padre Stefano Kaombe ambaye Mwaka 2021 anaadhimisha Jubilei ya Miaka 25 tangu alipopewa Daraja Takatifu ya Upadre amesema, umefika wakati wa kubadili “dhana ya Padre kuwa ni kitega uchumi na mradi wa familia” na kujielekeza zaidi kuhusu Daraja Takatifu ya Upadre kama wito na zawadi kutoka kwa Mungu. Wazazi na walezi wawategemeze mapadre na watawa katika huduma.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Siku ya 58 ya Kuombea Miito Ulimwenguni, iliyoadhimishwa Jumapili, tarehe 25 Aprili 2021, umenogeshwa na kauli mbiu “Mtakatifu Yosefu Ndoto ya Wito”. Baba Mtakatifu katika ujumbe wake, amekazia umuhimu wa: Ndoto, huduma na uaminifu; mambo msingi katika kukuza na kudumisha miito mbalimbali ndani ya Kanisa. Maadhimisho ya Siku ya Kuombea Miito Ulimwenguni yamekwenda sanjari na Maadhimisho ya Mwaka wa Mtakatifu Yosefu uliozinduliwa rasmi hapo tarehe 8 Desemba 2020 na yanatarajiwa kufungwa kwa kudema hapo tarehe 8 Desemba 2021. Hii pia nii Jumapili ya Kristo Yesu Mchungaji mwema!

Kwa upande wake, Padre Stefano Kaombe, Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Francisko Xsaveri, Chang’ombe, Jimbo kuu la Dar es Salaam, Tanzania katika mahubiri yake, amekazia nafasi na dhamana ya familia katika mchakato wa kuchipua, kulea na kukuza miito mbalimbali ndani ya Kanisa. Ametoa mifano minne ya Familia kadiri ya Maandiko Matakatifu ilivyokabiliana na changamoto ya: kupata watoto, kuwalea na hatimaye, kuwatoa sadaka kwa ajili ya sifa na ukutukufu wa Mungu katika huduma. Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu ni mfano bora wa kuigwa. Ibrahimu Baba wa Imani na Sara mkewe; Kilio cha Mama yake Samuel ina sadaka safi ya mtoto wake katika huduma, Mjane wa Sarepta, wawe ni mifano bora ya kumtegemea Mungu kwa kujisadaka katika malezi na makuzi ya miito mbalimbali ndani ya Kanisa. Wazazi na walezi wasaidie kutafsiri ndoto za watoto na vijana, ili waweze kujitoa kikamilifu katika huduma kwa Mungu na jirani zao.

Padre Stefano Kaombe ambaye Mwaka 2021 anaadhimisha Jubilei ya Miaka 25 tangu alipopewa Daraja Takatifu ya Upadre amesema, umefika wakati wa kubadili “dhana ya Padre kuwa ni kitega uchumi na mradi wa familia” na kujielekeza zaidi kuhusu Daraja Takatifu ya Upadre kama wito na zawadi kutoka kwa Mungu. Wazazi na walezi watambue kwamba, watoto ni zawadi ya Mungu, wawe tayari pia kumtolea Mungu zawadi ya watoto wao kwa ajili ya huduma kwa Kanisa kama Mapadre na Watawa na kamwe wasiwe ni kikwazo kwa watoto wao. Mapadre pia wawasaidie wazazi, ndugu na jamaa kutambua kwamba, Upadre ni wito na zawadi wanayoiwekeza katika imani na kamwe si kitega uchumi. Vinginevyo watawachanganya Mapadre badala ya kudemka katika huduma, watadumaa na kusinyaa kwa msongo wa mawazo, mwanzo wa kukata tamaa na kuonja machungu ya Upadre na utawa!

Kaombe Miito

 

25 April 2021, 16:15