Jumapili ya Yesu Kristo Mchungaji Mwema ni Siku ya Kuombea Miito Mitakatifu ndani ya Kanisa Jumapili ya Yesu Kristo Mchungaji Mwema ni Siku ya Kuombea Miito Mitakatifu ndani ya Kanisa 

Jumapili ya Kuombea Miito Mitakatifu: Mwaka wa Mt. Yosefu!

Ni Jumapili ya Miito Mitakatifu. Tunaalikwa kuiombea, kuienzi, kuitunza na kuidhamini miito mitakatifu ya Upadre na utawa inayopata chimbuko lake katika wito wa ndoa. Baba Mtakatifu katika ujumbe wake katika siku ya kuombea miito duniani kwa mwaka 2021, anasema kuwa Mtakatifu Yosefu, Baba mlishi na mlinzi wa Yesu na Kanisa, ni mlinzi pia wa miito mitakatifu katika Kanisa.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu dominika ya nne ya Pasaka mwaka B. Ni jumapili ya mchungaji mwema kama anavyosali Padre katika sala mwanzo akisema; “Ee Mungu Mwenyezi wa milele, utuelekeze kwenye furaha za mbinguni, kusudi sisi kondoo wako wanyonge tufike huko alikotoka mchungaji wetu shujaa.” Na katika sala baada ya komunio anahitimisha akisali; “Ee Mchungaji mwema, ututazame kwa mapendo sisi kundi lako. Upende kutuweka katika malisho ya milele sisi kondoo wako uliotukomboa kwa damu takatifu ya Mwanao.” Ni Jumapili ya Miito Mitakatifu. Tunaalikwa kuiombea, kuienzi, kuitunza na kuithamini miito mitakatifu ya Upadre na utawa inayopata chimbuko lake kutoka katika Ndoa Takatifu. Katika ujumbe wake katika siku ya kuombea miito alioutoa 19/03/2021 siku ya sherehe ya Mtakatifu Yosefu katika Kanisa la Mtakatifu Yohane Laterani wenye kichwa cha habari; “Mtakatifu Yosefu: ndoto ya wito”, Baba mtakatifu Francisko amesema kuwa Mtakatifu Yosefu, Baba mlishi na mlinzi wa Yesu na Kanisa, ni mlinzi pia wa miito katika Kanisa.

Somo la kwanza la Kitabu cha Matendo ya Mitume (Mdo. 4:8-12), linatueleza kuwa Petro pamoja na Yohana walipelekwa mbele ya baraza la wayahudi kwa sababu ya kumhubiri Kristo. Petro kwa ujasiri, akijaa Roho Mtakatifu anashuhudia mbele yao bila kuogopa kuwa Yesu waliyemkana na kumwua amefufuka, na kwa jina lake, mitume wanaponya wagonjwa, na kwa njia yake sote tutaokoka, wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo. Somo la pili la Waraka wa kwanza wa Mtume Yohane kwa watu wote (1Yoh. 3:1-2), linatufafanulia ukweli huu kuwa; Sababu ya mapendo yake, Mungu amemtuma Mwanae ili atufanye kuwa watoto wake. Kwa hiyo yatupasa kuishi kama watoto wa Mungu ili mwishowe tuweze kumwona Mungu mbinguni uso kwa uso. Ndivyo anavyotuandika Yohane akisema; “Tazameni, ni pendo la namna gani alilotupa Baba, kwamba tuitwe wana wa Mungu; na ndivyo tulivyo.” Yohane anasisitiza kuwa licha ya kuwa hakuna anayejua tutakavyokuwa hapo baadae baada ya kifo, lakini anatupa matumaini kuwa; “Atakapodhihirishwa Yesu, tutafanana naye; kwa maana tutamwona kama alivyo.” Na hili ndilo tumaini letu linalotufanya tuishi tukiwa tumeungana naye.

Injili ilivyoandikwa na Yohane (10:11-18) ndiyo imebeba dhamira na kiini cha ujumbe wa dominika hii ikitueleza uhusiano uliopo kati yetu sisi waamini tuliobatizwa na kumkubali Kristo kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yetu! Uhusiano huu ni kama wa Mchungaji na Kondoo. Yesu ndiye mchungaji mwema, anayeutoa uhai wake kwa ajili yatu sisi. Mfano huu Yesu aliutoa katika mazingira ya Palestina, nchi ya wafugaji. Nyakati hizo za Yesu, wafugaji wa kondoo walipeleka kondoo zao malishoni nje ya vijiji vyao. Usiku waliwakusanya kondoo wao pamoja katika boma kwa ulinzi dhidi ya wezi na wanyama wakali wa porini. Asubuhi boma lilifunguliwa, kila mchungaji alitangulia mbele na aliwaita kondoo wake, nao walimtambua na kumfuata. Yesu aliye mchungaji wetu mwema anatupenda na kutujali kama mchungaji anavyowapenda na kuwajali kondoo wake. Yesu anatujua vizuri tulio wake. Anamjua kila mmoja wetu kwa Jina lake, anajua mahitaji yetu binafsi, anajua madhaifu yetu, anajua magonjwa yetu, anajua tiba tunayohitaji kadiri ya majeraha yaliyosababishwa na dhambi.

Yesu Kristo kama mchungaji mwema anatuongoza kuelekea katika imani na Kanisa kwa Sakramenti ya ubatizo. Katika Kanisa sote tunalishwa kwa Neno lake, mwili na damu yake, sote tunaponywa kwa sakramenti ya Upatanisho, kwa nguvu ya Roho Mtakatifu tunafanywa kuwa askari hodari wanaoufahamu na kuulinda ukweli unaookoa. Naye anatuongoza kuelekea nchi ya ahadi, Yerusalemu Mpya, Mbinguni, tukawe warithi wa uzima wa milele pamoja naye. Ni wajibu wetu kumfahamu Kristo mchungaji wetu mwema, tuitambue sauti yake ili kila anapotuita tunapokuwa tumepote, tuitambue sauti yake, tuisikilize na kuifuata kwani ndiyo inayotupeleka katika uzima wa milele. Katika ujumbe wake katika dominika hii ya kuombea miito mitakatifu, Baba Mtakatifu Francisko anatuasa kuiga mfano wa Mtakatifu Yosefu, mtu wa haki aliyepokea ujumbe wa Mungu katika ndoto na kuufanyia kazi mara moja bila kusita. Baba Mtakatifu anasema; tusikubali mtu kuzima ndoto zetu.

Tutimize ndoto zetu kama Mtakatifu Yosefu ambaye alipokea ujumbe wa Mungu mara nne katika ndoto. Ndoto ya kwanza ilimfanya awe baba wa masiha, ndoto ya pili ilimfanya akimbilie Misri na kuokoa maisha ya masiha na ya familia yake, ndoto ya tatu ilimtaka kurudi katika nchi yake na ndoto ya nne ilimfanya abadili njia na mwelekeo wa safari yake na kuelekea Nazareti ndiko ambako Yesu alianza kazi yake ya kuhubiri habari njema ya ukombozi (Mt. 1:20; 2:13.19.22). Mtakatifu Yosefu alikuwa na ujasiri wa kufanya haya yote ili kutimiza mapenzi ya Mungu. Ndivyo inavyopaswa kuwa kwa kila wito. Mtakatifu Yosefu alikuwa mtumishi mwema, aliishi maisha yake kwa ajili ya wengine na sio kwa ajili yake. Alijisadaka kwelikweli, mtu wa haki, mwenye usafi wa moyo, aliyependa na kujitoa bila kujibakiza, alikuwa na upendo usiotaka maslahi binafsi. Kwa upendo wake wa kibaba sisi tumezaliwa upya na kufanya watoto wa Mungu, kwa uangalizi wake akawa mlinzi wa familia na Kanisa, kwa kujitoa kwake bila kujibakiza akawa mlinzi na msimamizi wa kifo chema. Utumishi wake uliotukuka na huduma yake ya kujitoa bila kujibakiza, vyote viliongozwa kwa upendo usiojitafuta wenyewe. Hizi ndizo sifa anazopaswa kuwa nazo kila mkristo mbatizwa zaidi sana kila anayeitika sauti ya Mungu na kuamua kuishi ya miito mitakatifu ya upadre na utawa.

Anaendelea kusisitiza Baba Mtakatifu Francisko kuwa; Mtakatifu Yosefu ndiye mlinzi na msimamizi wa miito yote. Bila kupoteza muda Mtakatifu Yosefu aliisikia sauti ya Mungu na kufanya yote aliyoagizwa kwa wakati. Ndivyo inavyopaswa kuwa kwa kila mmoja katika wito wake. Kutokupoteza muda bali kuwahudumia wengine kwa haraka iwezekanavyo bila kuwa na kigugumizi. Mtakatifu Yosefu alikuwa mtu mwaminifu. Uaminifu katika maisha ya wito ni wa muhimu sana kwani ndio unampa mtu sifa ya kuwa mtu wa haki kama alivyokuwa Mtakatifu Yosefu (Mt. 1:19). Mwisho, Baba Mtakatifu akiwafariji na kuwatia moyo watawa na mapadre anasema kuwa; Neno la kwanza alilolisikia Mtakatifu Yosefu katika ndoto ni usiogope (Mt.1:20). Hivyo wote waliochagua maisha ya miito mitakatifu wanapaswa kuwa na ujasiri, kutokuogopa kujitoa na kujisadaka kwani ni katika kujisadaka tunajipatia utakatifu. Tukumbuke kuwa uaminifu ndiyo siri ya furaha, faraja na ujasiri wetu. Miito mitakatifu inategemea sana maisha ya sala, maadili mema, na majitoleo thabiti. Basi waamini wote wanaalikwa kuwasaidia wanaoitikia miito mitakatifu ya upadre na utawa kwa hali na mali, kutowakwaza kwa maneno na matendo yao, kutowatia katika vishawishi na kutowazuia kumtangaza  Yesu Kristo. Ni kwa kupitia wao Kristo mchungaji mwema anajidhihirisha na kufanya kazi ndani mwao kwa ajili ya wokovu.

Jumapili 4 Pasaka
21 April 2021, 16:16