Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili IV ya Kipindi Cha Kwaresima: Kristo Yesu chemchemi ya wokovu wa mwanadamu alitundikwa juu ya Msalaba, ufunuo wa huruma, upendo na msamaha wa dhambi. Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili IV ya Kipindi Cha Kwaresima: Kristo Yesu chemchemi ya wokovu wa mwanadamu alitundikwa juu ya Msalaba, ufunuo wa huruma, upendo na msamaha wa dhambi. 

Tafakari Jumapili IV: Yesu Wokovu Umetundikwa Msalabani

Tutambue kuwa, sio nyoka wa shaba aliyewaponya Waisraeli bali ni utii na imani yao kwa Mungu. Nyoka wa shaba alikuwa ni ishara tu kwao (Hek 16:5). Nasi kila tumtazamapo Yesu Kristo aliyetundikwa Msalabani tunapata uzima wa milele kwani tunakuwa na utii na imani kwa Mungu Baba kwa njia ya Yesu Kristo aliye Msalabani. Ni Jumapili ya furaha kwa sababu ya Wokovu!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya nne ya Kwaresima mwaka B wa Kiliturujia, siku ya ishirini na sita ya kujitakatifuza. Ni Dominika ya furaha kama wimbo wa mwanzo kutoka kitabu cha Nabii Isaya (66:10-11) unavyoimba; “Furahi Yerusalemu, mshangilieni ninyi nyote mmpendao; furahini, ninyi nyote mliao kwa ajili yake, mpate kunyonya, na kushibishwa kwa maziwa ya faraja zake.” Kwanini tunaalikwa kufurahi? Ni kwa sababu Pasaka i karibu, ukombozi u karibu, upatanisho umekaribia. Ndiyo maana katika sala ya Koleta Padre kwa niaba ya jamii ya waamini anasali; “Ee Mungu, umeleta kwa namna ya ajabu upatanisho wa wanadamu kwa njia ya Neno wako. Tunakuomba utujalie bidii ya kujiweka tayari kwa ibada na imani kuadhimisha sikukuu ijayo.” Katika Dominika hii Altare inaweza kupambwa na rangi ya mavazi ya kiliturujia yaweza kuvaliwa ya rangi ya pinki badala ya zambarau na vyombo vya muziki vyaweza kutumika. Somo la kwanza latoka kitabu cha pili cha Mambo ya Nyakati, ambacho ni kama ufupisho wa historia ya wana waisraieli. Somo hili limegawanyika sehemu tatu.

Sehemu ya kwanza inatueleza juu ya misiba, balaa na majanga ambayo Mungu aliruhusu yawapate wana wa Israeli kwa sababu ya dhambi zao kama adhabu kwao, adhabu aitoayo Baba mwema kwa wanae. Tunasoma kuwa; “Wakuu wote wa makuhani, na watu, wakakosa mno sawasawa na machukizo yote ya mataifa; wakainajisi nyumba ya Bwana…Mungu kwa huruma yake aliwaonya na kuwasahihisha kwa njia ya manabii lakini hawakusikia, badala yake waliwadhihaki na kuyadharau maneno yake; na kuwacheka Manabii wake, hata kusiwe na kuponya.” Matokeo ya dhambi na machukizo haya ni; Kuvamiwa na kuharibiwa kwa mji wa Yerusalemu na mataifa ya kipagani, kubomolewa kwa Hekalu lake, watu wake kuteswa mateso mengi, wengine kuuawa na wengine kupelekwa utumwani kama wimbo wa katikati kutoka (Zab.137:1-6) unavyoimba: “Kando ya mito ya Babeli ndiko tulipoketi, tukalia tulipoikumbuka Sayuni. Katika miti iliyo katikati yake tulivitundika vinubi vyetu, maana huko waliotuchukua mateka.”

Sehemu ya pili inaeleza kuwa Waisraeli wakiwa utumwani, waliyatambua, wakayakiri na kuyajuta makosa yao na kuomba msamaha kwa Mungu. Majuto na masikitiko yao yanajidhihirisha walipoambiwa waimbe baadhi ya nyimbo za Sayuni wakiwa ugenini, nao wakasema: “Tuuimbeje wimbo wa Bwana katika nchi ya ugeni?” Basi wakamlilia Mungu kwa viapo vya maneno mazito wakisema; “Ee Yerusalemu, nikikusahau wewe, mkono wangu wa kuume na unyauke, ulimi wangu na ugandamane na kaakaa la kinywa changu, nisipokukumbuka.” Ni majuto ya hali ya juu kabisa yanayotoka ndani ya mtima wa mioyo yao. Sehemu ya tatu ya somo hili inaeleza ukuu wa huruma na upendo wa Mungu kwa anayekiri na kutubu makosa yake. Waisraeli walipotambua na kukiri dhambi zao, Mungu aliwahurumia, akawasamehe dhambi zao na kuwarejesha katika nchi yao kwa mkono wa Koreshi, mfalme wa Uajemi aliyemuinua naye akawatangazia uhuru akisema; “Basi kila mtu katika ninyi nyote mlio watu wake, Bwana Mungu wake, na awe pamoja naye, na akwee,” mkaujenge upya mji wake na hekalu lake Bwana Mungu.

Katika somo la pili la Waraka wa Mtume Paulo kwa Waefeso, Mtume Paulo anashuhudia kuwa sisi tumekombolewa kwa upendo na huruma ya Mungu. Paulo anasema kabla ya ubatizo tulikuwa wafu, ni kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo tumezaliwa upya na kuvalishwa uzima mpya na wa milele. Kwa ubatizo tunaishi pamoja na Kristo, tumefufuliwa na tumeokolewa naye. Mtume Paulo anatukumbusha kuwa sisi ni viumbe dhaifu hatuna tendo lolote la kujivunia mbele za Mungu. Mungu kwa kuwa ni mwingi wa rehema, kwa mapenzi yake makuu alitupenda, hata wakati tulipokuwa wafu kuhusu dhambi na kutotii kwetu, alituhuisha pamoja na Kristo. Tumeokolewa kwa Neema zake. Akatuketisha pamoja na Kristo katika ulimwengu wa Roho. Kumbe hatukuokolewa kwa sababu ya mastahili ya matendo yetu, bali wokovu wetu ni zawadi tu itokanayo na Neema ya Mungu. Mema tutendayo sisi viumbe dhaifu ni ishara kwamba, neema ya Mungu inafanya kazi ndani yetu, na kuzaa matunda ya utukufu ndani mwetu.

Injili ilivyoandikwa na Yohane nayo imegawanyika katika sehemu tatu. Sehemu ya kwanza (3:14-15); inatukumbusha kuinuliwa kwa nyoka wa shaba na Musa jangwani baada ya kutolewa utumwani Misri kama ishara ya kuinuliwa kwa Yesu Kristo msalabani “ili kila mtu amwaminiye awe na uzima wa milele katika yeye.”  Waisraeli walipokuwa wakisafiri jangwani kuelekea nchi ya ahadi walikosa imani kwa Mungu, wakamnung’unikia. Mungu aliwaadhibu kwa kuwatumia nyoka wa moto wakawauma na watu wengi wakafa. Nao kama kawaida yao walitambua kosa lao, wakamlilia Musa awaombee msamaha kwa Mungu. Mungu akasikia kilio chao, akawahurumia, akawasamehe kosa lao, akamwamuru Musa atengeneze nyoka wa shaba na amwinue juu katika mti, ili yeyote atakaye umwa na nyoka wa moto akimtazama nyoka wa shaba aweze kupona. Tutambue kuwa, sio nyoka wa shaba aliyewaponya, bali ni utii na imani yao kwa Mungu. Nyoka wa shaba alikuwa ni ishara tu kwao (Hek 16:5). Nasi kila tumtazamapo Yesu Kristo aliyetundikwa msalabani tunapata uzima wa milele kwani tunakuwa na utii na imani kwa Mungu Baba kwa njia ya Yesu Kristo aliye msalabani.

Sehemu ya pili (3:16-18) inaeleza upendo wa Mungu kwa mwanadamu uliomfanya amtoa Mwanawe wa pekee, ili kila amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Na sehemu ya tatu (3:19-21) inaeleza ukinzani uliopo kati ya maisha ya nuru na maisha ya giza. Ukinzani huu ndio unaotoa hukumu. Na hukumu yenyewe ndiyo hii; “Nuru imekuja ulimwenguni, na watu wakapenda giza kuliko nuru; kwa maana matendo yao yalikuwa maovu. Maana kila mtu atendaye mabaya huichukia nuru, wala haji kwenye nuru, matendo yake yasije yakakemewa. Bali yeye aitendaye kweli huja kwenye nuru, ili matendo yake yaonekane wazi ya kuwa yametendwa katika Mungu.” Sehemu hii ya Injili ni mazungumzo kati ya Yesu na Nikodemo, Farisayo, mmoja wa baraza mkuu la Wayahudi, yaani “Sanhedrin”, ndilo baraza la juu kabisa la utawala lililoundwa na wazee 70 pamoja na Kuhani Mkuu. Nikodemu alimwendea Yesu usiku kwa kujificha (3:1-13), kwa kuogopa asifahamike kuwa ni mfuasi wa Yesu. Aliogopa kufahamika kuwa yeye ni mtu wa nuru, mtu wa haki anayetenda mema, anayempendeza Mungu, anayeshika amri na maagizo yake. Hivyo anaamua kuenenda katika giza.

Naye Yesu akampa "zake za usoni" kwa kumweleza ukinzani uliopo kati ya maisha ya gizani na maisha ya nuru. Yawezakuwa nasi tunapenda kuishi gizani, tunaikataa na kuikimbia nuru, hatupendi kuonekana kuwa sisi ni wakristo. Katika harakati za kuikataa nuru na kulikimbilia giza, tunamkana Kristo naye anatuambia tumekwisha kuhukumiwa. Kwa uhakika ukipenda maisha ya giza, unakuwa mtumwa wa dhambi, unamilikiwa na Ibilisi, unakuwa mtumwa wake, naye akishakuchukua mateka anakutenda kadiri anavyotaka na anavyopenda, atahakikisha amekuchakaza mpaka mwisho, naye hatakuacha mpaka pale utakapotubu na kuirudia nuru ya kweli, Yesu Kristo, Bwana na mkombozi wa maisha yetu. Tujitahidi basi kuishi maisha ya Nuru ili tuwe watu wa amani na furaha. Nikodemu alimwendea Yesu kwa kificho kwa kuogopa kupoteza kazi, cheo, mali na heshima yake mbele ya watu. Yawezekana hata nasi kama wakristo walei, watawa, mapadre na viongozi wengine wa Kanisa tukafanana na Nikodemu, kwa kushindwa kuuishi ukristo wetu ipasavyo, hatuyakemei maovu, hatuko wazi katika mafundisho ya imani, tunauminya ukweli, tuko tayari kupindisha amri za Mungu na sheria za Kanisa na pengine kukufuru Sakramenti ilimradi tu tupendwe na watu, tuonekane wazuri na wema mbele zao.

Tunaalikwa na ujumbe wa Kwaresima wa Mababa Askofu; tusifanye migumu mioyo yetu tuisikilize sauti ya Mungu. Tukumbuke kuwa Mungu anajua yote hata mawazo yetu, Mungu anaona yote hafungwi wala kuzuiwa na chochote hadanganywi wala hadanganyiki. Tuuishi ukristo wetu, tuishuhudie kweli nasi tutakuwa huru. Nikodemu baada ya kuelewa maana ya fumbo la umwilisho na mateso ya Yesu alijaa ujasiri akawa na nguvu ya kumshuhudia Kristo hata kumtetea waziwazi mbele ya Baraza la wasiohaki (Yn. 7:50-53) na baada ya kifo chake alinunua manukato na manemane ratili mia kwa ajili ya maziko yake (Yn 19:39). Nasi tuwe na ujasiri wa kumshuhudia Kristo kwa maneno na matendo yetu. Tumtazame Yesu msalabani, tuinue mioyo yetu kwa kufanya toba ya kweli, na kumtumainia Yeye ili tupate uzima wa milele. Tuwe na imani thabiti, tuwe na msimamo dhabiti katika kuuishi ukristo wetu, tukikumbuka kuwa imani bila matendo, imekufa (Yak 2,17). Imani yetu na idhihirishwe katika maisha yetu ya kila siku kwa matendo yetu mema. Basi sala baada ya komunio anayosali Padre kwa niaba ya jamii ya waamini akisema; “Ee Mungu, unayemtia nuru kila ajaye ulimwenguni humu, tunakuomba uitie mioyo yetu nuru ya neema yako, tuweze kuwaza daima yakupendezayo wewe Mwenyezi na kukupenda kweli”, itupe nguvu na hamu ya kumwamini siku zote Bwana na Mwokozi wetu aliyeinuliwa juu msalabani ili tupate uzima wa milele.

Jumapili 4 Kwaresima
11 March 2021, 15:54