Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 27 ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa: Toba na wongofu wa ndani ni mwaliko kwa watu wote wa Mungu. Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 27 ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa: Toba na wongofu wa ndani ni mwaliko kwa watu wote wa Mungu. 

Tafakari Jumapili 27: Wongofu wa Ndani Ni Mwaliko Kwa Wote!

Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya 27 ya Mwaka A wa Kanisa inawakumbusha waamini kwamba, mwaliko wa toba na wongofu sio tu kwa wale wasiomwamini Kristo Yesu. Huu ni mwaliko wetu sote kwa sababu njia ya imani ya maisha ya mkristo ni njia ya wongofu usiokoma. Yaani ni njia ya maisha ambayo kila siku tunaalikwa kujifananisha zaidi na Kristo Yesu aliyejisadaka!

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Utangulizi: Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika kipindi hiki cha Tafakari ya Neno la Mungu. Leo tunayapatia ufafanuzi na kuyatafakari masomo ya dominika ya 27 ya mwaka A wa Kanisa. Hii ni dominika ya kwanza ya mwezi Oktoba, mwezi wa Rosari Takatifu na pia mwezi wa kuhamasisha ari na mwamko wa kimisionari. Ni mwezi ambao Kanisa limeutenga kwa ajili ya kuombea, kutegemeza na kualika mwitikio kwa kazi za kimisionari. Baba Mtakatifu Francisko tarehe 3 Oktoba 2020 majira ya jioni baada ya kuadhimisha Ibada ya Misa takatifu kwenye Kanisa lililoko chini ya Kanisa kuu la Mtakatifu Francisko wa Assisi, mjini Assisi, nchini Italia, atatia mkwaju kwenye Waraka wake wa Kitume ambao umepewa kichwa cha habari "Fratelli Tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii”. Waraka huu utatolewa hadharani, tarehe 4 Oktoba 2020 katika maadhimisho ya Sikukuu ya Mtakatifu Francisko wa Assisi aliyekazia: amani, utunzaji bora wa mazingira pamoja na huduma makini kwa maskini, aliyeteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa ni somo wake katika maisha na utume kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Somo la kwanza (Is 5:1-7) ni kutoka Kitabu cha Nabii Isaya. Kwa kinywa cha Nabii Isaya, Mwenyezi Mungu anatangaza hukumu kwa watu wake Israeli. Anawatangazia hukumu kwa maana wamemwangusha. Amewateua kama taifa lake, akawajalia zawadi nyingi sana, akawakinga na maadui zao wote na kuwaneemesha kwa kila namna lakini pamoja na hayo yote, watu wake hao wamemgeuka na kwenda kinyume kabisa naye. Nabii Isaya anafikisha ujumbe huu kwa kutumia lugha ya picha. Hii ni namna iliyokuwa inapendwa sana na manabii. Katika somo la leo, analitaja taifa la Israeli kama shamba la mizabibu la Bwana. Shamba ambalo halikukosa chochote kutoka kwa bwana wake lakini badala ya kuzaa zabibu nzuri na zenye afya, lenyewe likazaa zabibu mwitu. Afanye nini sasa kwa shamba lake hili? Anaapa kuliondolea vyote na kulirudisha kuwa ukiwa. Ujumbe huu wa Nabii Isaya siyo ujumbe unaoelea angani. Ni ujumbe uliotolewa katika kipindi halisi cha kihistoria ambapo Israeli alipoanza kupata misukosuko ya kisiasa na kiuchumi kutoka katika  mataifa jirani, alisita kumtumainia Mwenyezi Mungu katika changamoto hizo. Akasahau kote ambako Mungu amemtoa na badala yake akazitumainia nguvu za mataifa makubwa kwa ajili ya usalama wake. Shamba la mizabibu ndilo nyumba ya Israeli. Ndio sisi ambao Mungu ametulinda na kutuongoza katika maisha yetu. Ujumbe huu wa leo ni mwaliko kwetu kuonesha shukrani kwa wema huo wa Mungu. Ni mwaliko wa kutokumuasi na kutokutafuta kimbilio lingine tunaposongwa na changamoto za kimaisha.

Somo la pili (Waf. 4:6-9) ni kutoka katika Waraka wa Mtume Paulo kwa Wafilipi. Mtume Paulo anauandika Waraka huu akiwa kifungoni Roma ili kuwaimarisha kiimani ikiwa ni pamoja na kuwakumbusha dondoo muhimu za mafundisho yake alipokuwa kwao. Katika somo la leo, Mtume Paulo anaanza kuuhitimisha Waraka wake huu na hivyo anatoa majumuisho ya yale aliyowaandikia tangu mwanzo na kuwapa mausia ya mwisho. Anawasisitiza kudumu katika ile njia na nia njema waliyokuwa nayo tangu mwanzo. Anawaalika wasifadhaishwe na chochote. Wadumu katika sala, maombi na shukrani wakimuelekezea Mungu mahitaji yao yote. Mtume Paulo anatukumbusha nasi siku ya leo juu ya fadhila ya udumifu. Fadhila inayotusaidia kuendelea katika kuziishi nia na njia njema tulizojiwekea maishani kwa msaada wa Mungu. Anatukumbusha tuepuke kufa moyo, kukomea njiani katika juhudi na kukata tamaa hasa tunapokuwa tunasongwa na changamoto maishani. Tudumu katika bidii kama mwanzo, tusonge mbele kwa matumaini na Mungu wa amani atakuwa nasi daima.

Injili (Mt 21:33-43) Injili ya dominika ya ishirini na saba ya Mwaka A wa Kanisa ni kutoka kwa Mwinjili Mathayo. Ni mwendelezo wa dhana ya shamba la mizabibu ambayo imetolewa katika somo la kwanza katika dominika hii lakini pia ni dhana ambayo Kristo mwenyewe aliitoa kwa njia ya mfano katika Injili ya dominika iliyopita. Leo Kristo anatoa mfano mwingine. Katika mfano huu anaeleza kitendo cha watumishi katika shamba hilo la mizabibu kuwakataa wajumbe wote ambao mwenye shamba amekuwa anawatuma shambani kwake. Mmoja walimpiga, mwingine wakamuua na mwingine wakampiga mawe. Waliendelea kufanya hivyo hadi mwenye shamba alipoamua kumtuma mwanae wa pekee. Huyo ndio hawakumheshimu kabisa. Tena walipojua kuwa ndiye mrithi, walimuua ili wao ndio wawe warithi.

Shamba la mizabibu ndilo nyumba ya Israeli. Mfano huu anaoutoa Yesu unagusia kitendo cha taifa hilo kuwakataa manabii ambao kwa nyakati mbalimbali Mungu aliwainua ili kuziamsha dhamiri za watu wake. Watu wake hao wakaamua kuendelea kuziangamiza dhamiri zao kwa kuwakataa manabii na tena kuwaua ili wasiwakanye dhidi ya matendo yao yasiyofaa. Huyo mwana wa pekee ndiye Kristo mwenyewe ambaye naye walimkataa na kumuua. Kitendo hiki Yesu mwenyewe anakitafsiri kama kulitoa taifa teule la Mungu katika milki ya Mungu na kuliingiza katika milki ya watu. Yaani kumfanya Mungu asiwe tena mmiliki wa taifa lake bali taifa hilo limilikiwe na watu wenyewe. Mwisho wa mfano huu, Yesu anasema “Jiwe walilolikataa waashi limekuwa jiwe kuu la pembeni”. Anawakumbusha kuwa juhudi za kibinadamu na harakati zake ovu haziwezi kuuondoa msingi wa Kristo katika Kanisa lake na katika maisha ya watumishi wake waaminifu.

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, tupo katika dominika ya kwanza ya mwezi Oktoba. Huu ni mwezi wa Rosari Takatifu na pia ni mwezi wa kuhamasisha ari na mwamko wa kimisionari. Kwa njia ya sala ya Rosari Takatifu Kanisa linapenda kutukumbusha juu ya uchaji kwa Mama yetu Bikira Maria. Kwa namna ya pekee, ibada ya Rosari Takatifu inatukumbusha pia matokeo ya Bikira Maria wa Fatima aliyetuachia utume wa kusali Rosari Takatifu kwa ajili ya kuombea amani duniani na wongofu wa wakosefu. Sasa tunafahamu vizuri kuwa mwaliko wa wongofu sio tu kwa wale wasiomwamini Kristo. Huu ni mwaliko wetu sote kwa sababu njia ya imani ya maisha ya mkristo ni njia ya wongofu usiokoma. Yaani ni njia ya maisha ambayo kila siku tunaalikwa kujifananisha zaidi na Kristo. Ni mwezi pia wa kimisionari yaani mwezi wa kukuza uelewa wa kazi za kimisionari za kanisa kwa waamini wote. Kwa njia hii Kanisa linaalika kuombea kazi za kimisionari ikiwa ni pamoja na kutoa mwaliko wa kuzitegemeza na kuzishiriki kila mmoja kadiri ya nafasi na wito wake.  Shamba la mizabibu lililo nyumba ya Israeli, ndilo Kanisa linalohitaji kuhifadhiwa kwa ibada na majitoleo mbalimbali na pia linahitaji kuendelezwa kwa kazi za kimisionari. Tumwombe Mwenyezi Mungu atujalie neema ya kuyaishi haya katika mwezi huu maalumu, mwezi Oktoba.

Liturujia Wongofu

 

02 October 2020, 16:19