Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC hivi karibuni limezindua ujenzi wa Seminari kuu mpya ya Nazareti inayojengwa kwenye kitongoji cha Mwandakulima, Jimbo Katoliki la Kahama. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC hivi karibuni limezindua ujenzi wa Seminari kuu mpya ya Nazareti inayojengwa kwenye kitongoji cha Mwandakulima, Jimbo Katoliki la Kahama. 

Maaskofu TEC Wazindua Ujenzi wa Seminari Kuu ya Nazareti, Kahama!

Kanisa Katoliki nchini Tanzania linazidi kupiga hatua kuelekea uanzishwaji wa Seminari Kuu Mpya ya Nazareti inayotarajia kujengwa huko Mwendakulima, Jimbo Katoliki la Kahama. Baada ya kukamilisha hatua za awali na za msingi, yaani, kuzaliwa na kupitishwa kwa wazo la kuanzishwa kwa Seminari mpya kupitia vikao rasmi vya Maaskofu, sasa ujenzi umezinduliwa rasmi! Shukrani!

Na Padre Alfred Stanslaus Kwene, Tume ya Uinjilishaji, TEC, -Kahama.

Utangulizi: Dhamana ya Kanisa ni kulea, kusindikiza na kupalilia miito mitakatifu, lakini kwa namna ya pekee wito wa Daraja Takatifu ya Upadre. Seminari na nyumba za malezi ni mahali pa kulea na kuwasindikiza vijana katika maisha na wito wa Daraja Takatifu ya Upadre. Hapa waseminari wanapaswa kupewa malezi ya tunu msingi za maisha ya Kikristo kwa kukazia majiundo ya kiakili, kiroho, kiutu na kimaadili. Seminari ni mahali pa kukuza ukomavu, umoja na mshikamano na Kristo Yesu kwa njia ya Sala, Neno la Mungu, Mashauri ya Kiinjili na Sakramenti za Kanisa. Walezi wanapaswa kuwa kweli ni mashuhuda wa Injili ya Kristo! Ni katika muktadha huu, kwa moyo wa shukrani kwa Mwenyezi Mungu, Kanisa Katoliki nchini Tanzania linazidi kupiga hatua kuelekea uanzishwaji wa Seminari Kuu Mpya ya Nazareti inayotarajiwa kujengwa huko Mwendakulima, Jimbo Katoliki la Kahama. Baada ya kukamilisha hatua za awali na za msingi, yaani, kuzaliwa na kupitishwa kwa wazo la kuanzishwa kwa Seminari mpya kupitia vikao rasmi vya Maaskofu, hatua nyingine imekuwa ikisubiriwa kwa hamu kubwa.

Maadhimisho haya imekuwa ni fursa adhimu ya kutafakari juu ya: ukuu, uzuri na utakatifu wa wito na maisha ya Kipadre, zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kama wawakilishi wa Kristo Yesu mchungaji mwema, kati ya watu wake. Waseminari watambue kwamba, wanaitwa ili kuandaliwa na baadaye kutumwa kwenda kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kati ya watu wa Mungu. Hawa ni watu wanaokabiliana na changamoto mbali mbali za maisha. Ni watu wanaosubiri kuimarishwa katika imani, matumaini na mapendo. Imani inajengwa na kuimarishwa katika sala ambayo ni chachu ya umoja na mshikamano wa mtu binafsi na Kristo Yesu. Kumbe, Seminari ni nyumba ya sala, ambamo Kristo Yesu anawaita na kuwaalika waja wake, kujitenga kidogo ili kuimarisha mkutano pamoja na kusikiliza kwa makini Neno lake. Waseminari watambue kwamba, wanaandaliwa ili kuwa ni walimu wa watu wa Mungu katika imani ili waweze kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa ushupavu na mamlaka. Tunamshukuru Mungu kuwa siku ya tarehe 05 Julai, 2020 ilikuwa ni siku ya pekee sana kwetu nchini Tanzania, kwani tulishuhudia hatua nyingine muhimu ya kuzinduliwa rasmi ujenzi wa seminari hiyo.

Kile kilichoonekana kuwa ndoto, taratibu kinaelekea kuwa uhalisia sasa. Japo bado safari ni ndefu, lakini yatupasa kumshukuru Mungu kwa hatua hii muhimu.Ushiriki: Tukio hili kubwa la uzinduzi rasmi wa ujenzi wa seminari lilishuhudiwa na watu mbalimbali, wakiwemo maaskofu saba, yaani, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Askofu Mkuu Gervase Nyaisonga; Makamu wa Rais wa Baraza la Maaskofu, Askofu Flavian Kassala; Mwenyekiti wa Bodi ya Kaskazini ya Seminari, Askofu Joseph Mlola, ALCP/OSS; Mwenyekiti wa Bodi ya Kusini ya Seminari, Askofu John Ndimbo; Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Tabora, Askofu Mkuu Paulo Ruzoka; Askofu Msimamizi wa Jimbo la Kahama, Askofu Ludovick Joseph Minde, ALCP/OSS; kadhalika na Askofu wa Jimbo la Kondoa, Askofu Bernardini Mfumbusa.  Wengine waliohudhuria tukio hilo ni Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu, Padre Charles Kitima, mapadre wawili watendaji katika Ofisi ya Taifa ya Mashirika ya Kipapa; mapadre wa Kahama; watawa wa kike na wa kiume pamoja na waamini walei toka ndani na nje ya Jimbo la Kahama.

Matukio Muhimu ya Siku hiyo: Tukio hili muhimu na la kihistoria lilipambwa na shughuli kuu tatu: Adhimisho la Misa Takatifu, Kutembelea eneo la ujenzi na Mikutano kadhaa ya muhimu. Adhimisho la Misa Takatifu. Ni tukio la pekee kabisa lililotambulisha uzinduzi rasmi wa ujenzi wa seminari hiyo ni Adhimisho la Misa Takatifu iliyoadhimishwa katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Karoli Lwanga, la Jimbo la Kahama. Misa hii iliongozwa na Askofu Mkuu Paulo Ruzoka wa Jimbo Kuu la Tabora (Metropolitani inayojumuisha pia jimbo la Kahama). Kati ya watu waliohudhuria adhimisho hilo ni pamoja na Maaskofu wote saba, Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, mapadre wawili wanaohudumu katika Idara ya PMS – Taifa, Padre Msimamizi wa Ujenzi wa Seminari ya Nazareth na Familia ya Mungu ya Jimbo la Kahama, yaani, mapadre, watawa na walei.

Ibada hiyo ya Misa Takatifu ilipambwa kwa mambo mengi mazuri ikiwemo mahubiri mazuri yaliyosheheni utajiri mwingi iliyotolewa na Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Askofu Mkuu Gervase Nyaisonga. Huku akihusianisha tukio hilo na Masomo ya Dominika hiyo, hasa Injili (Mt.11:25-30), Rais wa Baraza alikazia zaidi juu ya faraja itokayo kwa Mungu, kama ujumbe wake msingi. Kwa upande mmoja aliwaalika Wakristo wa Jimbo la Kahama – lililo wazi kwa sasa, kupokea ujumbe wa faraja kwani “mwokozi” wao, yaani Askofu Mpya wa Jimbo la Kahama yuko mbioni kupatikana. Kwa upande mwingine alikazia kuwa kwa Kanisa zima la Tanzania, siku hiyo ilikuwa ni siku ya faraja kutokana na habari njema ya kuelekea kuzaliwa Seminari kuu mpya ya Nazareti. Zaidi sana, alitumia fursa hii kuwashukuru waamini wa Jimbo la Kahama, kuwaomba waendelee kusali kwa ajili ya miito mingi zaidi ya upadre na utawa, aliwaalika kuwa tayari daima kuitegemeza seminari hii wakati huu wa ujenzi wake na hata baadaye, itakapoanza rasmi kufanya kazi, pasipo kujali ni kwa kiasi gani wamekwishajitolea hadi sasa.

Kutembelea rasmi eneo la ujenzi na kutathimini kazi za awali za ujenzi zinazoendelea. Kabla ya adhimisho la Misa Takatifu ya Uzinduzi Rasmi wa Ujenzi wa Seminari hii, kulifanyika tukio jingine la muhimu sana. Tukio hili ilikuwa ni kutembelea rasmi eneo la ujenzi wa seminari na kutathimini kazi za awali za ujenzi ambazo tayari zilikuwa zimefanyika na zile zinazoendelea. Walioshiriki katika tukio hili ni maaskofu watano kati ya saba waliokuwepo, Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) na mapadre wawili wanaofanya kazi katika Idara ya PMS – Taifa. Ziara hii ilifanyika mara tu baada ya wajumbe tajwa kuwa wamewasili Kahama siku ya tarehe 04 Julai, 2020. Hakika ziara hii ilikuwa yenye manufaa kwani ilitoa fursa ya kutathimini kazi iliyokuwa imefanyika, kuainisha vipaumbele vipya katika kazi ya ujenzi na kuweka kwa pamoja mikakati mbalimbali katika kuhakikisha kuwa ujenzi huu unakamilika kwa wakati na vizuri.

Vikao Mbalimbali vya muhimu vilivyofanyika: Vikao vitatu muhimu vilifanyika kama sehemu pia ya uzinduzi huu. Kikao cha kwanza kilifanyika siku ya Jumamosi Jioni na kukamilika siku ya Jumapili asubuhi na kilihudhuriwa na Maaskofu wote saba, Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu, mapadre wawili wanaofanya kazi katika Idara ya PMS Taifa, Padre Msimamizi wa Ujenzi wa Seminari ya Nazareth kwa sasa na mapadre wawili wanaosaidiana naye toka jimbo la Kahama.  Kati ya masuala yaliyojadiliwa katika kikao hiki ni kufanya mapitio ya jumla ya mikakati ya awali kuelekea uanzishwaji wa Seminari na kujadili matokeo ya ziara iliyofanyika ya kutembelea eneo itakapojengwa seminari hiyo. Kikao cha pili, japo kilikuwa kifupi sana, kilihudhuriwa na maaskofu wote saba, viongozi wa Halmashauri za Walei za kila parokia na viongozi wa jumuiya za kitawa zilizoko jimboni Kahama. Akiongea kwa niaba ya maaskofu wenzake saba waliokuwepo na kwa niaba ya Baraza zima la Maaskofu Katoliki Tanzania, Rais wa Baraza la Maaskofu alitumia fursa hiyo kutangaza rasmi kwa mara nyingine kuhusu uanzishwaji wa seminari hiyo; pia aliishukuru Familia ya Mungu ya Jimbo la Kahama kwa ukarimu wao katika kuanzishwa seminari hii mpya na mwishowe aliwaeleza juu ya wajibu wao katika kushiriki kazi ya malezi ya waseminari watakaokuwa wanasoma katika Seminari Kuu ya Nazareti.

Kikao cha tatu ilikuwa ni kati ya maaskofu wote saba na mapadre wote wanaofanya kazi jimboni Kahama. Ujumbe msingi katika kikao hiki ulikuwa ni kutangaza rasmi tena juu ya uanzishwaji wa seminari hii mpya katika jimbo lao; pia kuwashukuru mapadre wa Jimbo la Kahama kwa kuridhia kuwa seminari hii ianzishwe jimboni mwao na zaidi sana kwa kuwa tayari kutolea baadhi ya majengo ya jimbo kwa ajili ya kuanzisha seminari hii. Vile vile, katika Kikao hiki, Maaskofu waliomba ushirikiano wa mapadre katika kipindi hiki cha ujenzi wa seminari na baadaye itakapoanza rasmi. Kwa msingi huu, mapadre waliombwa kuungana na Baraza la Maaskofu Tanzania katika kuhakikisha kuwa sio tu kwamba seminari inaanzishwa bali inafanya kazi vizuri muda utakapowadia. Akiongea kwa niaba ya mapadre wenzake, Mwenyekiti wa Umoja wa Mapadre wa Jimbo Katoliki Kahama alithibitisha kuwa mapadre wemeridhia kwa moyo  mweupe kuanzishwa kwa seminari hiyo na kuwa wako tayari kuonesha ushirikiano wowote utakaohitajika katika kipindi hiki cha ujenzi na hata wakati seminari itakapoanza rasmi.

Hitimisho: Kama usemavyo msemo wa Kiswahili: “safari moja huanzisha nyingine”, ufunguzi huu rasmi wa ujenzi wa seminari ya Nazareti tunapaswa kuutazama kuwa sio mwisho bali ni hatua mojawapo muhimu katika safari ndefu iliyoko bado mbele yetu. Kwa kuzingatia hilo, mbinu mpya zilipendekezwa ili kuhakikisha kuwa ndoto hii inatimia. Kwa mfano, ilipendekezwa kuwa, kama itawezekana, kwa mwaka wa kwanza wa masomo unaotegemea kuanza mwezi Oktoba 2020, walau uanze na waseminaristi 80 hadi 100 hivi kwa masomo ya falsafa na taalimungu Hivyo, tumwombe Mungu ili atusaidie tuweze kutimiza ndoto hii ili kuandaa mazingira stahiki kwa ajili ya malezi ya mapadre wa kesho. Kwa Mungu hakuna lisilowezekana!

seminari ya Nazaret 2020
08 September 2020, 14:01