Baraza la Maaskofu Katoliki Ubelgiji katika Waraka wake wa Kichungaji kwa Watu wa Mungu nchini humo wanawataka kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya matumaini! Baraza la Maaskofu Katoliki Ubelgiji katika Waraka wake wa Kichungaji kwa Watu wa Mungu nchini humo wanawataka kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya matumaini! 

Waraka wa Kichungaji wa Baraza la Maaskofu Katoliki Ubelgiji 2020

Baraza la Maaskofu Katoliki Ubelgiji katika Waraka wake wa kichungaji kwa watu wa Mungu nchini humo, linawahimiza kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa upendo na mshikamano wa dhati; wa matumaini na furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Kipindi hiki kiwe ni fursa ya kujipatia mapumziko, Iwe ni nafasi ya kufanya tafakari kuhusu mapenzi ya Mungu kwao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, Mama Kanisa anatumia silaha zifuatazo: Kufunga na kusali ili kuomba huruma na neema ya Mungu. Anawahimiza waamini kushiriki kikamilifu katika Ibada ya Misa Takatifu kwa nia mbali mbali, kielelezo cha uwepo endelevu wa Mungu anayewafariji na kuwaokoa waja wake. Tafakari ya Neno la Mungu, inalenga kuwasaidia waamini kuendelea kusoma alama za nyakati kwa mwanga wa Injili. Matendo ya huruma: kiroho na kimwili ni kielelezo cha Injili ya huruma na upendo kwa Mungu unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu. Ibada ya Rozari Takatifu, inapania kuwajengea watu imani, matumaini na mapendo katika kipindi hiki kigumu cha historia ya mwanadamu sanjari na kukimbilia faraja kwa Mungu anayeokoa kwa kutambua kwamba, sala ni chemchemi ya imani, matumaini na mapendo. Katika mapambano dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19 watu wa Mungu wanapaswa kuendelea kufuata ushauri wa wataalam wa afya pamoja na kutekeleza itifaki dhidi ya maambukizi ya Virusi vya Corona, COVID-19, ili mafanikio yaliyokwisha kupatikana yaweze kuendelezwa zaidi badala ya kutumbukia tena kwenye taharuki na hofu ya maambukizi mapya ya Virusi vya Corona, COVID-19.

“Mmebatizwa na kutumwa”.  Kanisa linaendeleza wito na utume wake wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia, agizo kutoka kwa Kristo mwenyewe kwa wafuasi wake. Hiki ni kipindi maalum sana kwa maisha na utume wa Kanisa sehemu mbali mbali za dunia. Huu ni muda wa kutangaza furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa; Kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa kwa ari na ushiriki mkamilifu na hatimaye, Kushuhudia imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Mwezi Oktoba 2019 Kanisa limeadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu Papa Benedikto XV alipochapisha Waraka wa Kitume:"Maximum Illud" yaani “Kuhusu Shughuli za Kimisionari.” Umekuwa ni muda muafaka wa: sala, katekesi, tafakari na matendo ya huruma! Ni wakati ambao umewawezesha waamini walei kutambua haki, dhamana na wajibu wao katika maisha na utume kwa Kanisa. Hii imekuwa ni fursa ya kuwahimiza waamini kujiwekea sera na mikakati ya kuyategemeza Makanisa mahalia: kwa njia ya rasilimali watu, vitu na fedha, ili Kanisa liendelee kutangaza Injili ya huruma, upendo na matumaini hadi miisho ya dunia!

Ni katika muktadha huu, Baraza la Maaskofu Katoliki Ubelgiji katika Waraka wake wa kichungaji kwa watu wa Mungu nchini humo, linawahimiza kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa upendo na mshikamano wa dhati; wa matumaini na furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Kipindi hiki cha Likizo ya Kiangazi kwa mwaka 2020, kitumike kikamilifu kama fursa ya kujipatia mapumziko, kwa kuzingatia mambo muhimu katika maisha. Iwe ni nafasi ya kufanya tafakari ya kina ili kuangalia katika maisha ya kila mmoja wao, Mwenyezi Mungu anataka nini kutoka kwao. Je, Mungu analitaka Kanisa kufanya kitu gani kwa wakati huu na kwa walimwengu katika ujumla wao! Ikumbukwe kwamba, Kanisa la Kristo ni chemchemi ya matumaini kwa wale waliopondeka na kuvunjika moyo hasa katika kukabiliana na janga na homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Tangu kufumuka kwa gonjwa hili hatari, watu wengi wamewekwa chini ya karantini, wengi wao wamewapoteza ndugu, jamaa na marafiki kutokana na ugonjwa huu. Kuna watu wameguswa na kutikiswa na homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19.

Kuna familia nyingi ambazo zimepoteza fursa za ajira. Lakini wakati wa mapambano dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19, watu wengi wameonesha umoja, upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Watu wamejisadaka na kujitolea rasilimali fedha, vitu na muda wao kwa ajili ya wale waliokuwa wameathirika zaidi na gonjwa hili. Baraza la Maaskofu Katoliki Ubelgiji linakiri kwamba, watu wengi wameguswa na kuonja uwepo endelevu wa Mungu katika hija ya maisha yao, badala ya kutumbukia na kuzama katika ombwe la giza nene, badala yake, wameshuhudia mwanga angavu wa Pasaka ya Kristo Mfufuka! Maaskofu wanakiri kwamba, kwa hakika waamini kushindwa kuhudhuria na kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Sakramenti mbali mbali za Kanisa, lilikuwa ni jaribio kubwa sana katika maisha ya kiroho. Lakini hata katika shida na mahangaiko haya ya ukavu wa maisha ya kiroho, Kanisa limeweza kubuni mbini mbali mbali za kuweza kuwafikia waamini huko waliokuwa wanaoishi, ili kuhakikisha kwamba, walau hakuna mtu ambaye alikosa kabisa huduma ya kiroho na kichungaji wakati wa kipeo cha janga la Corona, COVID-19.

Huu ni wakati wa kuendelea kujikita katika kipaji cha ubunifu sanjari na kuendeleza yale mema na mazuri yaliyoibuliwa wakati wa kipeo cha ugonjwa wa Corona, COVID-19. Lengo ni kuhakikisha kwamba, Jumuiya za waamini zinaendelea kuboreka zaidi katika maisha ya kiroho na kimwili, kwa kuzama katika mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu, kwa kujaliana na kusaidiana kama sehemu ya kukamilishana. Waamini waendelee kusoma alama za nyakati kwa kusikiliza na kujibu kilio cha maskini, wagonjwa na wale wanaoteseka kutokana na sababu mbali mbali za maisha. Ni matumaini ya Baraza la Maaskofu Katoliki Ublegiji kwamba, sera za kisiasa, kiuchumi, kijamii, kitamaduni na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, zitapata mwelekeo mpya, kwa kujikita katika ujenzi wa umoja na udugu wa kibinadamu. Ni wakati muafaka kwa waamini kujichotea amana na utajiri unaobubujika kutoka katika misingi ya imani, matumaini na mapendo, ili kukabiliana na changamoto mamboleo. Tunu hizi za maisha ya kiroho ni amana na utajiri ambao waamini wanaweza kuwashirikisha pia ndugu, jamaa na marafiki zao, ili kweli dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi!

Maaskofu Ubelgiji 2020
08 July 2020, 13:01