Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili 15 ya Mwaka A wa Kanisa: Ushuhuda wa Neno la Mungu: Mifano mbali mbali inayotolewa na Kristo Yesu kwa wanafunzi wake. Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili 15 ya Mwaka A wa Kanisa: Ushuhuda wa Neno la Mungu: Mifano mbali mbali inayotolewa na Kristo Yesu kwa wanafunzi wake.  

Tafakari Jumapili 15 ya Mwaka: Ushuhuda wa Neno la Mungu!

Mifano inatualika kuitafakari na kujichunguza na hapo tunaweza kweli kubadili maisha yetu. Leo tunahamasishwa kufungua macho na mioyo yetu ili kupata ujumbe kusudiwa na Yesu. Ni kwa njia ya kukubali kujifunua sisi wenyewe kwa kutafakari na kuwa sehemu ya mifano ya Yesu hapo tunaweza kupata maana na ujumbe kinyume chake mifano inabaki kuwa ni lugha ngumu na ya mafumbo.

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na Salama! Yesu alikuwa ni muhubiri mahiri na mwenye mvuto mkubwa hata kama mara kadhaa tunaona wasikilizaji wake wakimuacha na kumkimbia kwa kuwa hawakuwa tayari kuupokea ujumbe wake. Kwa mtindo na lugha yake iliyogusa na kuakisi mazingira yao, hivyo makutano waliweza kupata ujumbe kusudiwa kirahisi. Yesu ananena na kuongea nao lugha ya picha iliyokuwa rahisi kueleweka na wasikilizaji wake. Mwinjili Mathayo anatuonesha Yesu anaongea na makutano kwa lugha ya mifano.  Ni nia ya Yesu kuona kuwa ujumbe unawafikia wasikilizaji wake na hasa pale wanapokuwa tayari kufungua mioyo na akili zao kulipokea Neno lake. Siku ile alitoka nyumbani, alitoka nyumbani kwake, mahali ambapo tungetegemea angelieleweka na kukubalika kirahisi, ila kinyume chake ni watu wa nyumbani mwake wakamuona Yesu ni mtu aliyechanganyikiwa, hivyo kutaka hata kumkamata kwa nguvu. Yesu anatoka na kwenda kando ya bahari ya Galilaya, mahali walipokuwepo makutano, anapanda chomboni na kuanza kuwahubiria. Chombo kinaweza kuwa ni meli au mtumbwi au ngalawa, ila chombo kinasimama jumuiya ya waamini, yaani Kanisa.

Ni wajibu wa Mama Kanisa kufundisha Habari Njema ya wokovu. Chombo kinapokuwa majini kinakuwa pia katika hatari za kila aina, ila daima kinabaki salama tukitambua chombo hicho kinaongozwa na Kristo Mwenyewe. Ni Kristo anayedumu kuwa mwalimu wetu na sisi wengine wote ni vyombo vyake, kila mwanakanisa ni chombo cha Kristo katika kuwavuta makutano, watu wanaokuwa mbali naye ili waweze kuupokea ujumbe wake. Yesu anazungumza nao kwa mifano, labda hata nasi tunajiuliza kwa nini anatumia mtindo wa mifano kwa kufikisha ujumbe wake? Kwa nini asinene nao moja kwa moja bila kutumia lugha ya mifano, lugha tafakarishi? Marabi waliifananisha lugha ya mifano sawa na utambi wa koroboi, ambao ni mdogo ila ukiwaka unaondoa giza na hata kutuwezesha kuigundua hazina ya thamani kubwa iliyojificha. Ndio kusema mifano inatusaidia kutafakari kwa kina ili kuweza kugundua hazina ya thamani iliyojificha. Mifano inabeba ujumbe, mifano inamfanya msikilizaji naye kushiriki katika kuugundua ujumbe unaofumbatwa ndani yake.

Yesu leo anatupa jibu la swali gumu linalotusumbua kila mara, swali ni kwa nini uovu ulimwenguni? Kwa nini Ufalme wa Mungu unakutana na upinzani mkali kila mara? Yesu anatumia njia ya mifano katika kutupa jibu la swali au maswali haya yanayomsumbua mwanadamu si tu nyakati zake bali hata leo.  Mfano wa Yesu katika somo la Injili ya leo, unatuacha na maswali pia mengi juu ya uhalisia wake, na hasa juu ya mtindo wa mpanzi wa kupanda mbegu zake. Kwa nini mpanzi anatoka na kutupa mbegu njiani, kwenye mawe na hata kwenye miiba? Kwa nini anatupa popote bila kujali kuwa ni upotezaji wa mbegu zake? Ni maswali ya haki kabisa kwetu leo kwani hatupati picha ya namna ya huyu mpanzi. Mwinjili anasisitiza sana juu ya namna ya upandaji wa mbegu anaoufanya mpanzi na msisitizo huo si wa bure bali ndio unaotuwezesha kuutafakari kwa kila ila kupata ujumbe kusudiwa.

Ni lengo la Yesu leo kutuonesha na kutupa majibu ya maswali yetu juu ya kwa nini kuna uovu ulimwenguni, kwa nini kama Mungu ni mwema hafanyi kitu katika kuujenga ufalme wake hapa duniani?  Somo letu la Injili ya leo ingawa ni refu, tunaweza kuligawa katika sehemu kuu tatu. Sehemu ya kwanza ndio ile ya aya 1-9 ambazo zinabeba mfano wa mpanzi, sehemu ya pili ni ile ya aya 10-17 ambapo tunakutana na misemo baadhi ya Yesu na sehemu ya tatu ni ya aya 18-23 ambapo tunakutana na maana ya mfano katika uhalisia wake. Ili kuelewa maana ya mfano wa mpanzi, yafaa tujue kwanza mazingira ya nyakati zile za Yesu. Nyakati zile mpanzi au mkulima hakuandaa shamba kwanza kabla ya kusiha mbegu. Maandalizi tunayoyajua ni kama ya kulima shamba, kung’oa miiba na visiki na hata kuondoa mawe na yale yote yasiyokuwa rafiki kwa ukuaji wa mazao yetu.

Kinyume chake mpanzi au mkulima alipanda mbegu au kusiha mbegu za kuzirusha shambani na ni baada ya kuota zile mbegu ndipo shamba lilisafishwa kwa kuondoa mawe na magugu na mengineyo ili kuruhusu mimea ile kukua vema. Hivyo tunaweza kuelewa kwa nini mbegu nyingine zilidondokea kwenye mawe, miiba na hata njiani. Kishawishi kwetu leo ni kuona kuwa mpanzi huyu anatumia nguvu na hata mbegu vibaya kwa kuzitupa si tu katika udongo mzuri bali hata njiani, juu ya mawe na kwenye miiba. Ni baada ya mbegu kuota hapo mkulima aliweza kutoa mawe, miiba, ili kusaidia mimea ile kukua na kustawi. Yesu anatumia mfano huo wa mpanzi, kuonesha hali yake ngumu aliyokuwa anaipitia. Yesu alifukuzwa kutoka kijiji chake cha Nazareti, Kafarnaumu walimuona kama amepagawa na kuchanganyikiwa, mafarisayo walitaka kumuua, na hata baadhi ya wafuasi wake walimuacha na kurudi nyuma.

Ni mazingira magumu na labda ya kukatisha tamaa, kuonesha kuwa misheni yake imeshindwa kuzaa matunda kwa ufanisi (Mathayo 11-12). Mfano huo umelengwa haswa kwa wale wafuasi wa Yesu, waenezaji wa Injili ambao wamekata tamaa baada ya kukataliwa au kukutana na upinzani wa Habari Njema. Pamoja na upinzani na magumu bado Yesu anaonesha kuwa Neno lake daima litazaa matunda kwani daima ni hai na lenye uzima.  Yesu anawaalika wafuasi na wasikilizaji wake katika mfano wake kwa kuwaalika ‘’kutazamana’’. Sio kutazama kwa macho ya nyama bali ili kuupokea ujumbe wake na kuuelewa daima hatuna budi kukubali kufungua macho ya mioyo yetu, ni kukubali sio tu kuwa wasikilizaji wa Neno bali wanaolipokea Neno na kuliruhusu kuwa na mizizi ndani mwetu. Ndio mwaliko wa kutushirikisha nasi katika kugundua siri za mbinguni, kuliishi Neno lake na hatimaye kuweza kuzaa matunda mema.

Ujio wa Yesu kama Masiha ni kinyume na matarajio ya wayahudi, kwani hakuja ulimwenguni kwa fahari na mbwembwe au maguvu ya kijeshi bali kwa kujinyenyekesha na kuzaliwa katika familia duni na maskini ya Nazareti. Yesu haonekani kuwa mwanamapinduzi iwe katika maisha ya kijamii au kisiasa, ni kinyume na matarajio ya watu wake, na hivyo kumkataa. Yesu badala yake alikuwa kama mbegu ndogo isiyoonekana wala kutambulika isipokuwa pale tu ilipoanza kuchipua na kumea na kukua na hata hatimaye kuwa mti mkubwa wenye kutoa matunda.  Na ndivyo pia Injili daima inamea na kukua ikianza kama mbegu ndogo isiyoonekana na wengi isipokuwa mara tu baada ya kuchipua na kukua. Labda hata nasi leo tulio wafuasi na rafiki zake Yesu tunajiuliza maswali kama bado kuna haja ya kuieneza Injili tunapoishi katika dunia yenye kila aina ya upinzani wa Habari Njema ya wokovu, kwenye ulimwengu wenye utamaduni wa kifo, ulimwengu wenye utamaduni wa giza na kila aina ya uovu. Je, leo tunaweza kutoka na kuwa mashahidi wa mashauri ya Injili yaani, ufukara, usafi wa moyo na utii? Je, leo tunaweza kuhubiri ufalme wa Mungu, yaani ufalme wa upendo, haki na amani?

Katika ulimwengu wa utamaduni wa soko huru, ulimwengu wa pesa na uchumi wa kibepari, nguvu na utu haupo tena kwa mtu bali katika vitu na pesa, ulimwengu ambapo mwanadamu amegeuzwa kuwa kitu ili kuzalisha lakini tunakwenda mbali zaidi hata kutumia mwili kufurahisha wengine. Ulimwengu ambapo kila mmoja ni mwamuzi wa ukweli, kila mmoja ni sahihi madamu tu hakuna anayemuingilia mwingine katika ulimwengu wake, kila mmoja anaamua kipi sahihi na kipi sio sahihi. Ni katika muktadha huo basi tunaona Yesu ananena na kila mmoja wetu leo tulio wafuasi na rafiki zake. Yesu ananena nasi leo kwa kutumia mfano wa mpanzi. Si tu Yesu ananena nasi kwa mfano bali zaidi sana anatualika nasi kuutafakari vema na kwa kina mfano huo ili kupata jibu kutoka kwake mwenyewe.  Mbegu kama ambavyo tumesikia kutoka Somo la Kwanza kutoka Kitabu cha Nabii Isaya, inawakilisha si tu chakula cha miili yetu bali pia ni nguvu ya ndani mwake inayowakilisha Nguvu ya Neno la Mungu kwa mwanadamu, na ndiye Neno aliyefanyika mwili na kukaa kati yetu, yaani Kristo mwenyewe. ‘’Kweli nawaambieni, punje ya ngano hubaki punje tu isipokuwa ikianguka katika udongo na kufa. Kama ikifa, basi huzaa matunda mengi’’. Yohane 12:24

Ugumu wa kulipokea Neno la Mungu tunaona leo Yesu anarejelea Maandiko ya Agano la Kale, Kitabu cha Nabii Isaya. ‘’…Kusikia mtasikia, wala hamtaelewa; Kutazama mtatazama, wala hamtaona, maana mioyo ya watu hawa imekuwa mizito…’’. Ni katika mazingira haya tunaona Yesu ananena nao na hata nasi leo kwa mifano. Ni kwa njia shirikishi yaani ya kutafakari mifano ya Yesu hapo nasi tunaweza kuupata ujumbe wa Mungu kwetu. Mifano inatualika kuitafakari, kuingia ndani mwetu na kujichunguza na hapo tunaweza kweli kubadili vichwa na hata maisha yetu. Mifano inatualika nasi leo kufungua macho na mioyo yetu ili kupata ujumbe kusudiwa na Yesu. Ni kwa njia ya kukubali kujifunua sisi wenyewe kwa kutafakari na kuwa sehemu ya mifano ya Yesu hapo tunaweza kupata maana na ujumbe kinyume chake mifano inabaki kuwa ni lugha ngumu na ya mafumbo. Yesu leo anazungumzia aina nne za ardhi ambapo mbegu inaangukia, ndio kusema anatualika nasi kujitafakari na kujitambua tu aina gani ya ardhi. Uhaba wa matunda hautokani na mbegu wala mpanzi bali aina ya ardhi inapoangukia hiyo mbegu. Mpanzi anapanda kwa ukarimu na anarusha mbegu zake sio kwa upendeleo bali kwa kila mmoja wetu. Mpanzi ni Mungu mwenyewe, na mbegu ndio Neno lake linaloshuka na kumjia kila mmoja wetu.

Ni Neno linalotolewa kwa ukarimu mkubwa kwa kila mmoja wetu, ila kuzaa matunda inategemea na mioyo ya kila mmoja, jinsi tunavyoruhusu Neno kuzaa matunda katika maisha yetu. Mioyo migumu inafananisha na njia, mahali au sehemu ngumu kutokana na ukweli wa kukanyagwa na wengi. Ni ugumu wa ndani wa kulipokea Neno la Mungu na kuliacha lizae matunda katika maisha yangu. Ni moyo mgumu kwa kukubali kweli za Injili kwani ni moyo unaoongozwa na kutawaliwa na mantiki za dunia hii, mitindo ya kidunia, unaotawaliwa na mali na vitu vya ulimwengu huu. Ndio moyo usiokuwa na nafasi wala utayari kwa Neno la Mungu. Moyo unaokosa udumifu, ndio ule unaopokea kwa shangwe kwa muda mfupi tu. Ndio moyo unaofananishwa na jiwe au mwamba, ambapo Neno linapokelewa kwa furaha na shauku ila unakosa kina na hivyo kunyauka mara moja. Ndio maisha ya mmoja anayekosa kina katika maisha ya imani, ni kubaki na kuishi kimazoea bila kuzama kwenye kweli za Injili na kuzifanya sehemu za maisha yetu. Injili inapaswa kutawala maisha yetu yote na kuiruhusu kuwa na mizizi katika maisha yetu, si tu kubaki wasomaji wa Injili na kuishia kuwa watazamaji bali tunaalikwa kuishi Injili.

Moyo usio na utulivu wala amani, ndio moyo unaosongwa na mengi ya dunia hii. Ni moyo unaotawaliwa na mengi ya hapa duniani, iwe mali au vitu au matatizo ya dunia hii. Ni kwa kutawaliwa na malimwengu hapo tunajikuta tunashindwa kukua katika mahusiano na Mungu na jirani, kwani kila mara nafasi ya kwanza sio Mungu au Neno lake bali ni mambo ya kidunia. Mwisho kuna wale wenye mioyo mizuri, inayofananishwa na ardhi yenye rutuba. Ndio wale wanaolipokea Neno na kuruhusu lizae matunda ndani mwao. Ndio wale wanaokubali maisha yao yote kuongozwa na kutawaliwa na Injili. Ni hakika anayeishi Injili huyo anazaa matunda mema na mengi. Kwa kweli kila mmoja akijitafakari anaweza kujiona akiwa na hali zote nne, moyo mgumu kama njia, moyo unaokosa utulivu na udumifu na nyakati za moyo wenye rutuba. Neno la Mungu daima ni hai na lenye uzima ila hutegemea na mioyo yetu sisi wenyewe katika kuzaa matunda, katika kuwa na kina. Niawatakie tafakari na Dominika njema.

10 July 2020, 09:02