Askofu Eusebius Nzigilwa wa Jimbo Katoliki la Mpanda anasimikwa rasmi tarehe 2 agosti 2020, tayari kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Mpanda! Hii ni Zawadi ya Mungu! Askofu Eusebius Nzigilwa wa Jimbo Katoliki la Mpanda anasimikwa rasmi tarehe 2 agosti 2020, tayari kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Mpanda! Hii ni Zawadi ya Mungu! 

Askofu Eusebius Nzigilwa, Jimbo la Mpanda: Unyenyekevu na Upendo

Makuu ya Mwenyezi Mungu: Miaka 15 ya Daraja Takatifu ya Upadre akateuliwa kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam. Katika Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 25 ya Daraja Takatifu ya Upadre, akateuliwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Mpanda. Hiki ni kielelezo cha ukomavu wa huduma ya: Kikuhani na Kichungaji kwa ajili ya familia ya watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Mpanda.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, Kristo Yesu aliye Mchungaji wa milele alijenga Kanisa Takatifu, akawatuma Mitume kama waandamizi wao, yaani Maaskofu, wawe wachungaji wa Kanisa lake hata ukamilifu wa nyakati. Kusudi Uaskofu wenyewe uwe mmoja na usiogawanyika, akamweka Mtakatifu Petro juu ya Mitume wengine, na katika yeye akatia chanzo na msingi udumuo na uonekanao wa umoja wa imani na wa ushirika. Ni katika muktadha huu, Maaskofu wanatambuliwa na Kanisa kama waandamizi wa Mitume kwani wanapaswa kutangaza na kushuhudia Injili kwa ajili ya Kanisa na asili ya maisha na utume wake siku zote. Maaskofu wamekabidhiwa huduma ya jumuiya pamoja na msaada wa Mapadre na Mashemasi, wakiliongoza kundi lake kwa niaba ya Mwenyezi Mungu, ambalo wao ni wachungaji wake, wakiwa kama walimu wa mafundisho, makuhani wa ibada takatifu, wahudumu wa uongozi. Kimsingi Maaskofu wanao wajibu wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Rej. LG, 20.

Basi, katika nafsi za Maaskofu, wanaosaidiwa na Mapadre, yupo kati kati ya waamini Kristo Yesu, aliye Kuhani Mkuu na kwa njia ya huduma yao mashuhuri huyashuhudia na kuyatangazia Mataifa yote Neno la Mungu na kuwapa waamini Sakramenti za imani bila kikomo. Tena kwa uangalifu wao wa kibaba, huviunganisha viungo vipya na Mwili wake kwa kuvizaa upya kutoka juu kwa Maji na Roho Mtakatifu. Kwa  hekima na busara yao hulielekeza na kuliongoza taifa la Mungu katika safari ya kuelekea kwenye heri ya milele. Kumbe, Maaskofu ni watumishi wa Kristo na mawakili wa siri za Mungu nao wamekabidhiwa huduma ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya neema ya Mungu, na huduma ya Roho na ya haki katika utukufu, daima wakijiweka chini ya maongozi ya Roho Mtakatifu, anayewajalia ukamilifu wa Daraja Takatifu. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanakaza kusema, Maaskofu, kwa namna bora na dhahiri, wanashika nafasi ya Kristo Yesu mwenyewe aliye: Mwalimu, Mchungaji na Kuhani Mkuu na hutenda katika nafsi yake “in Eius persona”. Kwa njia ya Sakramenti ya Daraja Takatifu, huwaingiza wateuliwa wapya katika umoja na Maaskofu. Hurika wa Maaskofu hauwezi kuwa na mamlaka usipounganika na Baba Mtakatifu, aliye Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Baba Mtakatifu Francisko anasema kwa ufupi sifa kuu za Askofu kuwa ni: unyenyekevu na huduma; mambo yanayofafanuliwa vyema na Mtakatifu Paulo, Mtume katika Waraka wake kwa Tito, akionesha mambo msingi yanayopaswa kufuatwa na kutekelezwa na Maaskofu, ili kukamilisha yale yanayopungua katika maisha na utume wa Kanisa; kwa kuwachagua na kuwasimika wazee wanaofaa kwa ajili ya uongozi wa Kanisa; watu wema na wenye kiasi, wapenda haki na watakatifu; watu wenye mifano bora ya kuigwa na jamii inayowazunguka. Askofu anayo dhamana ya kusali kwa ajili ya kuwaombea watu wote, kwa kutambua kwamba, kimsingi yeye ni mtu wa Mungu, aliyeteuliwa kati ya watu kwa ajili ya huduma, ili kuhakikisha kwamba, anakuza na kudumisha Ibada na Uchaji wa Mungu, mambo msingi katika kulinda na kudumisha utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Utume huu, umwezeshe Askofu kuwa kiongozi mkarimu, akitambua kwamba, Kristo Yesu ndiye anayewaita waja wake na kuwaweka wakfu ili kuendeleza kazi ya ukombozi!

Ni katika muktadha huu, Askofu Flaviani Matindi Kassala, Makamu wa Rais, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika mahojiano maalum na Radio Vatican, Vatican News anapenda kuzungumzia kuhusu kusimikwa kwa Askofu mteule Eusebius Alfred Nzigilwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Mpanda, akigusia Jubilei ya Miaka 25 ya Daraja Takatifu ya Upadre na Miaka 10 ya Uaskofu Jimbo kuu la Dar es Salam. Askofu mteule Nzigilwa anasimikwa rasmi tarehe 2 Agosti 2020, Mama Kanisa anapoadhimisha Kumbukumbu ya Mtakatifu Eusebius wa Vercelli, Askofu na mfiadini (2 Machi 283 – 1 Agosti 371. Alikuwa ni Askofu wa Jimbo la Sardinia, Kaskazini mwa Italia. Katika maisha yake, akasimama kidete kutangaza na kushuhudia imani ya Kanisa juu ya Umungu wa Kristo. Aliteswa na kunyanyaswa, lakini hakuikana imani yake, kwani alitambua kwamba, tunu msingi za maisha ya binadamu zinabubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Askofu Flaviani Matindi Kassala anasema, Askofu Nzigilwa mwaka 2020 anasherehekea Jubilei ya Miaka 25 tangu alipopewa Daraja Takatifu ya Upadre. Hili ni tukio ambalo lina mwalika kuyatafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini, kama kielelezo cha moyo wa unyenyekevu unaofumbatwa katika huduma ya upendo kwa watu wa Mungu.

Ikumbukwe kwamba, Nembo yake ya Kiaskofu inapambwa na kauli mbiu “Unyenyekevu na Upendo”. Makuu ya Mwenyezi Mungu yameanza kujitokeza tangu alipokuwa anatimiza miaka 15 ya Daraja Takatifu ya Upadre, kwa kuteuliwa kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam. Katika Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 25 ya Daraja Takatifu ya Upadre, akateuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Mpanda. Miaka 25 inayo tafsiri mbali mbali Kibiblia, lakini katika muktadha huu wa Jimbo Katoliki la Mpanda, ni kielelezo cha ukomavu wa huduma ya: Kikuhani na Kichungaji kwa ajili ya familia ya watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Mpanda ambalo ni matunda ya Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2000 ya Ukristo. Huu ni mwaliko kwa watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Mpanda kuyapokea na kuyanafsisha mapenzi ya Mungu katika vipaumbele vya maisha yao. Mpanda wampokee Askofu Eusebius Nzigilwa kama zawadi ya Mungu, ambaye amejibu sala za watu wake. Katika hali ya unyenyekevu kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria, akamfungulia Mwenyezi Mungu “sakafu ya moyo wake” na kuyahifadhi yote aliyokuwa ameambiwa na Malaika. Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma, daima ana mipango yake ambayo pengine imefichika machoni pa mwanadamu.

Tarehe 21 Desemba 2018, Mwenyezi Mungu akaingilia mipango yao kwa Baba Mtakatifu Francisko kumteuwa Askofu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga wa Jimbo Katoliki la Mpanda wakati huo, kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Mbeya. Katika sala na ukimya, watu wa Mungu wakaendelea kusali wakimwomba Mwenyezi Mungu awapatie mchungaji mkuu. Kwa unyenyekevu na moyo wa upendo kama ilivyokuwa ile sala ya yule mkoma aliyemsujudia Kristo Yesu akisema, “Bwana, ukitaka, waweza kunitakasa.” Yesu akanyoosha mkono, akamgusa, akisema, “Nataka, takasika” Mt. 8:1-3. Jibu la sala yao ni ufunuo wa Askofu Nzigilwa kama zawadi ya Mungu kwa familia ya Mungu Jimbo Katoliki la Mpanda. Ni jambo la msingi kutambua zawadi hii kwa njia ya imani, ili hatimaye, kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano wa watu wa Mungu, wanaoimba utenzi wa shukrani, kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria katika utenzi wake wa “Magnificat.” Askofu Flaviani Matindi Kassala anasema, utukufu wa Mungu unaendelea kujifunua taratibu kwa uwezo na karama ambazo Askofu Nzigilwa amekirimiwa na Mwenyezi Mungu katika kipindi chake cha Miaka 25 kama Padre na Miaka 10 kama Askofu Msaidizi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam.

Hili ni Jimbo lenye mahitaji makubwa yanayosimikwa katika wongofu wa shughuli za kichungaji. Lina matatizo, changamoto na fursa zake zinazohitaji majibu ya haraka yanayo bubujika kutoka katika mwanga wa Injili. Jimbo kuu la Dar es Salaam ni mlango wa changamoto za Kiinjili, Kitamaduni, Kisiasa, Kijamii na hata katika shughuli za kichungaji! Yataka moyo mkuu na unyenyekevu wa hali ya juu, kuliongoza Jimbo kuu la Dar es Salaam, daima kwa kujiaminisha chini ya maongozi ya Roho Mtakatifu na kuendelea kusoma alama za nyakati. Kwa miaka 10 Askofu Nzigilwa amepepetwa “kama karanga”, akajaribiwa, lakini hatimaye, akasimama imara kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu Jimbo kuu la Dar es Salaam. Kama dhahabu, amepitishwa kwenye tanuru na sasa yuko tayari kujisadaka bila ya kujibakiza katika unyenyekevu na upendo kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Mpanda. Hii ndiyo zawadi waliyomwomba Mwenyezi Mungu na sasa amewakirimia!

Watu wa Mungu Jimbo Katoliki Mpanda wawe wepesi kutambua karama, uzoefu na mang’amuzi yake ya shughuli za kichungaji, ili kuweza kuuelewa upendo wa Mungu kwa watu wa Jimbo Katoliki la Mpanda! Anakuja kwao kama mtumishi asiye na faida, ili kutumika kama mshumaa wa Pasaka! Sifa kuu ya Askofu mahalia ni huduma kwa watu wa Mungu bila ya kujibakiza kwa kutambua kwamba, yeye ndiye mchungaji mkuu kwa mfano wa Kristo Kuhani Mkuu. Askofu Flaviani Matindi Kassala katika mahojiano maalum na Radio Vatican anaendelea “kupanga nondo” kwa kusema, Askofu mteule Nzigilwa anasimikwa rasmi tarehe 2 Agosti 2020, Mama Kanisa anapoadhimisha Kumbukumbu ya Mtakatifu Eusebius wa Vercelli, Askofu na mfiadini. Ni Askofu ambaye alitekeleza utume wake katika mazingira magumu na hatarishi sana ya maisha! Akapambana na shida na changamoto mbali mbali katika maisha na utume wake kama Askofu, lakini hakukata tamaa! Mama Kanisa akatambua msimamo wake thabiti kuhusu imani juu ya Umungu wa Kristo Yesu, aliyezaliwa bila kuumbwa, Mwenye Umungu mmoja na Baba, ambaye vitu vyote vimeumbwa naye. Ameshuka kutoka mbinguni kwa ajili yetu sisi wanadamu na kwa ajili ya wokovu wetu!

Askofu Flaviani Matindi Kassala amehitimisha mahojiano na Radio Vatican kwa kuombea umoja, upendo na mshikamano miongoni mwa watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Mpanda. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania linapenda kumhakikishia Askofu Eusebius Alfred Nzigilwa kwamba, wako pamoja katika urika wao, ili kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu nchini Tanzania. Ratiba elekezi inaonesha kwamba, Askofu Nzigilwa tarehe 30 Julai 2020 akiwa ameandamana na baadhi ya Maaskofu Katoliki Tanzania amewasili Jimbo kuu la Mbeya. Tarehe 31 Julai 2020 amefika Jimbo Katoliki la Sumbawanga na tarehe 1 Agosti 2020 anawasili Jimbo Katoliki la Mpanda. Jumamosi tarehe 1 Agosti 2020 majira ya jioni, atakabidhiwa ufunguo wa Kanisa kuu, waamini watasali Masifu ya Jioni na Askofu Nzigilwa atakiri Kanuni ya Imani na Kula Viapo vya Utii. Jumapili tarehe 2 Agosti 2020 atasimikwa rasmi kuwa mchungaji mkuu wa Jimbo Katoliki la Mpanda, Tanzania.

Itakumbukwa kwamba, Askofu Eusebius Alfred Nzigilwa wa Jimbo Katoliki Mpanda, alizaliwa tarehe 14 Agosti, 1966, Jijini Mwanza nchini Tanzania. Alipata masomo yake ya sekondari kutoka Seminari Ndogo ya Mtakatifu Petro, Jimbo Katoliki la Morogoro. Mnamo mwaka 1988 alishiriki katika mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa kwa mujibu wa sheria na baadaye, alijiunga na Seminari Kuu ya Kibosho, Jimbo Katoliki la Moshi, kwa masomo ya Falsafa na yale ya Taalimungu katika Seminari kuu ya Kipalapala, Jimbo kuu la Tabora. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, akapewa Daraja takatifu ya Upadre tarehe 23 Juni, 1995 kama Padre wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam. Kwa hakika mwaka 2020 anatarajia kuadhimisha Jubilei ya Miaka 25 ya Upadre. Kuanzia mwaka 1995-1996 alikuwa ni Padre mlezi, nyumba ya malezi, Jimbo kuu la Dar es Salaam, iliyoko Parokia ya Mtongani, Kunduchi.

Aliwahi pia kuwa ni Mkurugenzi wa Shirika la Kipapa la Utoto Mtakatifu kuanzia Mwaka 1996 hadi Mwaka 1997. Baadaye Kardinali Polycarp Pengo alimteuwa kuwa Gambera wa Seminari Ndogo ya Visiga, Jimbo kuu la Dar es Salaam kuanzia mwaka 1997-1999. Baadaye akaendelea na masomo ya juu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alikojipatia shahada ya kwanza ya elimu. Baada ya masomo, aliteuliwa kwa mara nyingine tena na Kardinali Pengo kuwa Gambera wa Seminari Ndogo ya Visiga, kuanzia 2003 hadi 2008 alipolazimika kwa mara nyingine tena kurudi Chuo kikuu cha Dar es Salaam kumalizia masomo yake katika Sayansi ya Elimu na hivyo kujipatia Shahada ya uzamili. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI tarehe 28 Januari 2010 akamteuwa kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam na kuwekwa wakfu tarehe 19 Machi 2010 wakati wa Sherehe ya Mtakatifu Yosefu, Mume wake Bikira Maria na Msimamizi wa Jimbo Kuu la Dar Es Salaam. Askofu Nzigilwa amekwisha hudumia watu wa Mungu akiwafundisha, kuwaongoza na kuwatakatifuza kama Askofu kwa muda wa miaka 10, yaani hadi raha!

Jimbo Katoliki la Mpanda, Tanzania limekuwa wazi kuanzia tarehe 21 Desemba 2018 baada ya Baba Mtakatifu Francisko kuunda Jimbo kuu Jipya la Mbeya linalojumuisha: Jimbo Katoliki la Mbeya, Jimbo Katoliki la Iringa na Jimbo Katoliki la Sumbawanga. Wakati huo huo, Baba Mtakatifu akamteua Askofu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga kuwa Askofu mkuu wa kwanza wa Jimbo kuu la Mbeya nchini Tanzania. Kabla ya uteuzi huu, Askofu Nyaisonga ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC, alikuwa ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Mpanda. Mchakato wa uinjilishaji nchini Tanzania unasonga mbele!

Askofu Nzigilwa, Jimbo Katoliki Mpanda
31 July 2020, 14:04