Vatican News
Ujumbe wa Sherehe ya Pentekoste kutoka kwa Mwenyekiti wa Halmashauri Walei Taifa nchini Tanzania unaongozwa na kauli: Njoo Roho Mtakatifu Utujaze Upendo! Ujumbe wa Sherehe ya Pentekoste kutoka kwa Mwenyekiti wa Halmashauri Walei Taifa nchini Tanzania unaongozwa na kauli: Njoo Roho Mtakatifu Utujaze Upendo! 

Halmashauri Walei Tanzania 2020: Ujumbe wa Pentekoste!

Ujumbe kutoka kwa Mwenyekiti Halmashauri Walei Tanzania kwa ajili ya Maadhimisho ya Sherehe ya Pentekoste kwa Mwaka 2020 unaongozwa na kauli mbiu: “Njoo Roho Mtakatifu Utujaze Upendo”. Upendo na Amani katika maisha yetu vidumu katika moyo mmoja na roho moja katika Kristo Yesu. Tambua kwaba upendo ni tunda la Roho Mtakatifu na chemchemi ya maisha adili.

Na Gasper M. Makiluli, Halmashauri Walei Taifa, - Dar es Salaam.

Ufuatao ni ujumbe kutoka kwa Mwenyekiti wa Halmashauri Walei Taifa katika maadhimisho ya Sherehe ya Pentekoste kwa Mwaka 2020. Ujumbe huu unaongozwa na kauli mbiu: “Njoo Roho Mtakatifu Utujaze Upendo”. Upendo na Amani katika maisha yetu vidumu katika moyo mmoja na roho moja katika Kristo Yesu. Ndugu zangu waamini wakristo, upendo ukiwepo katika nafsi zetu, familia na jamii zetu kwa ujumla, amani itadumu. Hii ni kwa sababu hakuna kinachozidi upendo katika maisha ya mwanadamu. (1Kor.13:1-14). Hata kama ukifanya anayofanya malaika, kama huna upendo, wewe wafanya kazi bure.  Neno la Mungu linasema hata ukijitoa wewe na mali zako na kujiumiza, bila upendo haikufai kitu. Upendo haukai katika udhalimu na kuhesabu mabaya, haulipi kisasi wala hautafuti mambo yake wenyewe (ubinafsi). Upendo huamini yote, na kustahimili yote. Vitu vyote vitapita na kuisha lakini upendo haupungui kitu, bali utasafiri na wewe hadi mwisho wala hauna ukomo. Imani na matumaini yatasitawi sana kama upendo wako umesimama.

Tambua Ukweli Kuwa Upendo Ni Tunda La Roho Mtakatifu. Upendo kila mara unazaa matunda mema, ndio maana upendo wa Mungu Baba na Mungu Mwana ulizaa tunda jema la kwanza nalo ni Mungu Roho Mtakatifu. Tunapoadhimisha Pentekoste, tunakumbushwa sikukuu ya upendo wa Mungu kwetu. Tazama jinsi upendo ulivyo mzuri katika maisha, Yesu anajitoa kwa ukombozi wetu. Yesu alipojawa na Roho Mtakatifu mara tu baada ya ubatizo, upendo wake ulifurika hata akaanza kazi ya ukombozi wa watu wake kwa mateso makuu. Upendo ulimwongoza kufunga siku arobaini usiku na mchana, na Roho Mtakatifu ambaye ni upendo wa kwanza, alimwongoza katika vita dhidi ya Shetani na akamshinda vyema. Upendo ulimfanya awe na nguvu ya kuvumilia na kunyenyekea hadi kupandishwa msalabani kusulubiwa. Daima Yesu alikuwa amejawa na Roho Mtakatifu. Yesu ni Mungu – mtu, lakini hakujivuna wala kujivunia Umungu wake (Efe. 2:6-8). Zaidi alimtegemea Baba yake kwa sala na maombi. Je wewe unamtegemea nani na kujivunia nini?  Je, ni elimu yako, fedha zako au utajiri wako, umaarufu wako, cheo chako, afya yako au uzuri wako? Yatupasa kumtegemea Mungu Baba yetu nyakati za maisha yetu hapa duniani. Maisha yetu hapa duniani si ya kudumu bali yanapita tena kwa haraka.

Pokea nguvu ya Roho Mtakatifu: Basi, kipindi hiki cha Pentekoste kila mmoja wetu atamani tena kupokea Pentekoste Mpya yenye nguvu za kuutafuta Ufalme wa Mungu na kujibidisha kufanya mazoezi ya kiroho. Mpokee Roho Mtakatifu na umpe nafasi maishani mwako ili akujaze upendo wa kweli. Zoezi la kwanza kabisa ni kukubali kuwa wewe ni mnyonge na mdhambi, ugeuke na ufanye toba ya kweli na endelevu (yaani metanoia). Hapo uombe kwa dhati kumpokea Roho Mtakatifu ili akuongoze katika hiyo safari yako. Zoezi la pili ni kutoa upendo, msamaha na kufanya matendo ya huruma kwa wengine. Upendo na msamaha ni kama mito miwili itokayo mbinguni, ukiwa na upendo utasamehe; viwili hivi vinategemeana na kukamilishana. Mazoezi haya ni muhimu sana, ili yatuwezeshe kuishi vema hapa duniani na hatimaye, twende kwa Baba mbinguni, kwani wote tu wasafiri kuelekea kwake. Roho Mtakatifu ndiye mwezeshaji mkuu wa hii safari yetu. Ni vema kukumbuka daima ya kuwa, Ufalme wa Mbinguni utapatikana kwa wale wenye nguvu ya kufanya mazoezi haya ya kiroho, yaani, walio tayari daima kupiga mbio za kiroho (1Kor.4:24-27; 2Tim.4:7; Waebr.12:1-2). Lazima na sisi tujitahidi kuwa miongoni mwa wale ambao siku kwa siku wanadumu katika mbio hizi.

Tumwombe Mungu atupe nguvu na ari ya kuishi upendo na huruma kama watoto wachanga. Tena, atuwezeshe kuzingatia matakwa ya ufalme wake. Ufalme wa Mungu ukifika, amani itakuwepo, kwani hakutakuwepo tena na uchu wa madaraka, uchu wa mali, ubinafsi na kuwanyima wengine haki zao. Hivyo, upendo ule tuliouzungumzia hapo awali utazaa matunda, nayo ni amani na furaha katika jamii. Kukiwa na amani na furaha katika Kanisa na ulimwenguni kwa ujumla, uwepo wa Mungu utadhihirika wazi na Roho Mtakatifu atasema na watu wake. Wanaolijenga Kanisa na kuufanya ulimwengu kuwa mahali pazuri zaidi pa kuishi, ndiyo sisi, hivyo tuombe kuimarishwa na Roho Mtakatifu ili tutimize vema wajibu huu. Ndugu zangu waamini walei, tunapoungojea Ufalme wa Mungu katika utimilifu wake, tunahimizwa tusijihangaishe sana katika kujua ni lini utafika, bali tunaalikwa kumwomba Roho Mtakatifu atushukie na kutuwezesha kuwa Mashahidi wa kweli wa upendo wa Mungu duniani. Ndio maana, Yesu alipokuwa anakaribia kupaa mbinguni, alipoulizwa: “Je, Bwana wakati huu ndipo unapomrudishia Israeli UFALME?” Alijibu hivi: “Si juu yenu kujua nyakati wala majira.  Lakini mtapokea nguvu akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu na katika Uyahudi wote, na Samaria na hata mwisho wa nchi” (Mdo.1:6-8).

Ndugu zangu waamini walei, pamoja na mwaliko tajwa hapo juu, Yesu alitoa ahadi nyingine kwa Mitume wake, ambayo tunapaswa kuitazama kuwa ni ahadi yetu pia: “Hata alipokuwa amekutana nao aliwaagiza wasitoke Yerusalemu, bali waingoje ahadi ya Baba, ‘Ile ambayo mlisikia habari zake kwangu: ya kwamba Yohane alibatiza kwa maji, hali ninyi mtabatizwa katika Roho Mtakatifu baada ya siku hizi chache” (Mdo.1:4-5). Hakika ahadi hii imetimia kwetu katika Pentekoste hii. Hivyo, tunaalikwa kumpa nafasi Roho Mtakatifu katika roho zetu, ili tuweze kumtumikia Mungu na kushuhudia Imani yetu bila woga.  Tukimruhusu Roho Mtakatifu aongoze maisha yetu, hatutaenda tena kwa mazoea katika Sala, mahusiano yetu na wengine, kazini, kanisani n.k., bali Roho Mtakatifu atakuwa ndiye kiongozi wetu, atatufundisha na hata kutufariji katika safari yetu ya kwenda kwa Baba mbinguni.

Njoo Roho Mtakatifu utujaze upendo.

Gasper M. Makiluli

Mkiti H/Walei Taifa, Tanzania.

TEC: Pentekoste
27 May 2020, 14:16