Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC: Ujumbe wa Sherehe ya Pentekoste kwa mwaka 2020: Karama za Roho Mtakatifu. Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC: Ujumbe wa Sherehe ya Pentekoste kwa mwaka 2020: Karama za Roho Mtakatifu. 

Baraza la Makanisa Ulimwenguni: Ujumbe wa Pentekoste: 2020

Pentekoste Sherehe ambayo Roho Mtakatifu aliwashukia Mitume, akawajaza mapaji yake, wakapata nguvu na mwamko mpya wa kutangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka, hii ni lugha ya upendo usiokuwa na mipaka kwa waathirika wa COVID-19.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Sherehe ya Pentekoste ina umuhimu wa pekee kabisa katika maisha na utume wa Kanisa. Hii ni Siku ambayo Roho Mtakatifu aliwashukia Mitume, akawajaza mapaji yake, wakapata nguvu na mwamko mpya wa kutangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka. Hii ni lugha ya upendo usiokuwa na mipaka. Hii ni sehemu ujumbe wa Sherehe ya Pentekoste kutoka kwa Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC. Sehemu ya kwanza ya Kitabu cha Matendo ya Mitume, kinaonesha jinsi ambavyo wafuasi wa Kristo Yesu, walivyokuwa wamejifungia ndani kwa woga na hofu ya Wayahudi. Lakini, Roho Mtakatifu alipowashukia, wakatambua uwepo wa Mungu kati yao, kiasi hata cha kuvunjilia mbali kuta za utengano zilizosababishwa na lugha, kiasi kwamba, kila mtu aliweza kusikia kwa lugha aliyozaliwa nayo. Utamaduni haukuwa tena kikwazo, bali mbeleko ya kubebea Habari Njema ya Wokovu. Kanisa lilianzishwa katika hali na mazingira magumu na hatarishi, lakini kwa nguvu ya Roho Mtakatifu, likafanikiwa kuibuka kidedea.

Tangu wakati huo, Kanisa limekuwa ni chachu ya mabadiliko katika maisha ya mwanadamu na Injili imekuwa ni kikolezo cha imani, matumaini na mapendo kwa watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia. Baraza la Makanisa Ulimwengu linasema kwamba, Wakristo sehemu mbali mbali za dunia, wanaadhimisha Sherehe ya Pentekoste kwa mwaka 2020 huku kukiwa na taharuki ya maambukizi makubwa ya homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Kuna mamilioni ya watu wameambukizwa na maelfu wamepoteza maisha. Kwa hakika Waswahili wanasema, “gonjwa hili hatari limepindua meza ya maisha ya kifamilia na jamii katika ujumla wake”. Gonjwa Limevuruga mwenendo mzima wa uchumi katika ngazi mbali mbali. Limewapigisha magoti wanasayansi; mataifa yenye nguvu za kiuchumi na kijeshi, hayakufua dafu mbele ya Virusi vya Corona, COVID-19. Huduma ya afya na miundombinu yake ikavurwa na kupepetwa sana. Gonjwa hili limekuwa ni kipimo cha utawala bora, ujasiri katika kuamua na kutenda; kusuka au kunyoa! Ni gonjwa ambalo kwa sasa linaendelea kusababisha baa la njaa kwa mamilioni ya watu, kiasi cha kutikisa misingi ya umoja na mafungamano ya kijamii, kitaifa na kimataifa.

Katika muktadha huu, wakati wa Sherehe ya Pentekoste kwa mwaka 2020, waamini na watu wote wenye mapenzi mema, wanahimizwa kushirikiana na kushikamana ili kutangaza na kushuhudia, ukuu na utakatifu wa Mungu, chemchemi ya uhai wa binadamu. Roho Mtakatifu anataka kuwainua na kuwaimarisha waamini katika misingi ya imani, matumaini na mapendo. Roho Mtakatifu anataka kuwajalia waamini ujasiri na nguvu ya kuweza kupambana na hali na mazingira yao; wawe tayari kupambana na mateso, magonjwa na kifo. Roho Mtakatifu anataka kuwasha moto wa upendo na mshikamano, ili kuwapenda na kuwahudumia wagonjwa, maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa mifumo na miundombinu ya kijamii. Waamini wamwombe Roho Mtakatifu ili awajalie wanasayansi na watafiti ulimwenguni mang’amuzi sahihi ili waweze kupata chanjo na tiba ya gonjwa hili la Corona, COVID-19.

Roho Mtakatifu awawezeshe waamini kuwa ni vyombo na mashuhuda wa faraja, umoja na upendo kwa waathirika wa gonjwa hili; kwa kuendelea kushikamana na wachungaji, madaktari, wauguzi na wafanyakazi katika sekta ya afya, ili kwa pamoja waweze kuwa ni mashuhuda wa upendo wa Mungu wenye huruma na faraja kwa watoto wake. Roho Mtakatifu ni chemchemi ya maisha mapya! Afyekelee mbali giza la kifo na mauti! Pentekoste ya Mwaka 2020, iwe ni nguvu ya kupyaisha maisha ya watu wa Mungu na ulimwengu katika ujumla wake! Roho Mtakatifu awe ni chanzo cha mabadiliko katika maisha ya watu!

WCC: Ujumbe wa Pentekoste

 

28 May 2020, 13:13