Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC., linayaalika Makanisa wanachama kushiriki kikamilifu, tarehe 14 Mei 2020 kwa. Sala, Kufunga na Matendo ya Huruma, ili kuomba huruma ya Mungu dhidi ya Corona! Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC., linayaalika Makanisa wanachama kushiriki kikamilifu, tarehe 14 Mei 2020 kwa. Sala, Kufunga na Matendo ya Huruma, ili kuomba huruma ya Mungu dhidi ya Corona! 

WCC: Tarehe 14 Mei 2020: Sala, Kufunga na Matendo ya huruma!

Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC, linayaalika Makanisa wanachama wake wote, kuungana na watu wote wenye mapenzi mema ili kukimbilia huruma na upendo wa Mungu katika kipindi hiki kigumu cha historia ya maisha ya mwanadamu. Waamini wanamwomba Mwenyezi Mungu katika huruma yake, aweze kuwaokoa watu wake na janga la Virusi vya Corona, COVID-19., gonjwa hatari!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko amepokea na kuridhia Mapendekezo yaliyotolewa na Kamati Kuu ya Utekelezaji wa Hati ya Udugu wa Kibinadamu. Tarehe 14 Mei 2020 anawaalika waamini wa dini na madhehebu mbali mbali, kuunganika na kushikamana kwa njia ya sala, kufunga na kufanya matendo ya huruma: kiroho na kimwili ili kukimbilia huruma na upendo wa Mungu. Hii ni sehemu ya mapambano ya maisha ya kiroho dhidi ya janga kubwa la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Katika muktadha huu, Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC, linawaalika Makanisa wanachama wake wote, kuungana na watu wote wenye mapenzi mema ili kukimbilia huruma na upendo wa Mungu katika kipindi hiki kigumu cha historia ya maisha ya mwanadamu.

Waamini wanamwomba Mwenyezi Mungu katika huruma yake, aweze kuwaokoa watu wake na janga la Virusi vya Corona, COVID-19. Kwa mkono wake wenye nguvu, awaponye wagonjwa wote wanaomlilia usiku na mchana! Awajalie wanasayansi na watafiti waweze kupata chanjo na tiba ya gonjwa hili. Watu wamekata na kujikatia tamaa, wengi wao wamewekwa karantini; wanaonja machungu ya kifo kutoka ndani ya familia na Makanisa yao. Mshikamano wa sala, kufunga na matendo ya huruma, kiwe ni kielelezo cha umoja na udugu wa kibinadamu, ili kusaidiana na kutegemezana; kwani umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu! Kila mwamini wa dini na madhehebu mbali mbali, mahali popote pale alipo, asali na kumwomba Mwenyezi Mungu, kwa hakika, atawasikiliza na kujibu sala zao kwa wakati muafaka! Mwaliko huu umetolewa na Prof. Dr. Ioan Sauca, Katibu mkuu mtendaji wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC.

Kwa upande wake, Baraza la Maaskofu Katoliki Myanmar, linawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kufunga, kusali na kutenda matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama njia ya kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwaokoa na janga la Virusi vya Corona, COVID-19 sanjari na vita na kinzani zinazoendelea kusababisha majanga makubwa kwa watu na mali zao nchini Myanmar. Katika siku za hivi karibuni, kumekuwepo na mauaji ya watu wasiokuwa na hatia sehemu mbali mbali za Myanmar, hali inayotishia usalama wa maisha ya watu na mali zao. Kuna uhaba mkubwa wa chakula kwa asilimia 80% bado kitambo kidogo tu, watu wataanza kupoteza maisha kwa baa la njaa!

Biashara nyingi zimefungwa kutokana na ukosefu wa fedha na mtaji, hali ambayo itapelekea pia ukosefu wa fursa za kazi na ajira. Kuna watu zaidi ya 160, 000 wasiokuwa na makazi maalum, wanaoendelea kuteseka kwa kukosa huduma msingi! Hivi karibuni, Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Asia, FABC, liliungana na Baba Mtakatifu Francisko kuunga mkono jitihada za Umoja wa Mataifa za kutaka mataifa kusitisha vita sehemu mbali mbali za dunia, ili Jumuiya ya Kimataifa ijielekeze zaidi katika mapambano dhidi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19.

Itakumbukwa kwamba, Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu ilitiwa saini kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko mjini Kairo, nchini Misri, tarehe 4 Februari 2019 huko Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu. Huu ni mwaliko na changamoto kwa waamini wa dini mbali mbali duniani, kuungana na kushikamana, ili kufanya kazi katika umoja na udugu wa kibinadamu, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Hati hii ni nguzo msingi ya haki, amani na upatanisho. Hati inakazia pamoja na mambo mengine kwamba: binadamu wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mwenyezi Mungu; wanatakiwa kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha: uhai wa binadamu, mazingira nyumba ya wote, sanjari na kushikamana na maskini pamoja na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Hati ya Udugu wa Kibinadamu inapata chimbuko lake katika mikutano elekezi iliyowasaidia waamini wa dini hizi mbili kushirikishana: furaha, majonzi, matamanio yao halali pamoja na changamoto mamboleo.

Ni katika muktadha huu, Kamati Kuu ya Utekelezaji wa Hati ya Udugu wa Kibinadamu, inawaalika waamini wa dini mbali mbali ulimwenguni, Alhamisi, tarehe 14 Mei 2020, kumwomba Mwenyezi Mungu aweze kuwalinda binadamu. Wanakimbilia huruma na upendo wake, ili kushinda Janga la Virusi vya Corona, COVID-19, ili hatimaye, kurejesha tena amani na utulivu, afya, ustawi na maendeleo. Baada ya Janga hili, ulimwengu uweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi, kwa njia ya mshikamano na mafungano ya udugu wa kibinadamu kuliko ilivyokuwa hapo awali! Wapendwa waamini wa dini mbali mbali, Tume inasema, leo hii ulimwengu umekumbwa na janga kubwa linalotishia maisha ya mamilioni ya watu kwa sababu ya kuenea kwa haraka maambukizi ya Virusi vya Corona, COVID-19.

Tume inapenda kusisitiza kuhusu umuhimu wa tiba na tafiti za kisayansi katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Corona, lakini haiwezi kushindwa kumwelekea Mwenyezi Mungu, Muumbaji katika janga hili kubwa. Hivyo basi, Tume inatoa wito kwa waamini wa dini mbali mbali, ulimwenguni kote kumwelekea Mwenyezi Mungu kwa: kufunga na kusali, kwa unyenyekevu mkuu na hatimaye, kumwilisha sala hii katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Kila mtu mahali pake alipo, kadiri ya dini, imani au dhehebu lake, kumwomba Mwenyezi Mungu aweze kuliondoa janga na kuwanusuru kwa athari zote zinazotokana na ugonjwa huu. Waamini wamwombe Mwenyezi Mungu, awajalie wanasayansi na watafiti ili waweze kugundua tiba ya ugonjwa huu, ili kuuokoa ulimwengu kutokana na madhara yake makubwa: kiafya, kiuchumi na kiutu kutokana na kuenea kwa janga hili la hatari.

Kwa kutambua umuhimu na uzito wa Hati ya Udugu wa Kibinadamu, kumeundwa Kamati Kuu ya Utekelezaji wa Hati hii na kati ya wajumbe wake ni pamoja na: Kardinali Miguel Angel Ayuso Guixot, Rais wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini, Professa Mohamed Hussein Mahrasawi, Mkuu wa Chuo cha Al Azhar na Monsinyo Yoannis Lahzi Gaidi, Katibu muhtasi wa Baba Mtakatifu Francisko. Wengine katika kamati hii ni Jaji Mohamed Mahmoud Abdel Salaam, mshauri mkuu wa Mufti mkuu. Wajumbe wengine ni wale walioteuliwa kutoka Serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu, Baraza la Wazee wa Kiislam Umoja wa Falme za Kiarabu pamoja na watu maarufu katika tasnia ya habari Umoja wa Falme za Kiarabu. Kwa upande wao, viongozi wa Serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu pamoja na Amiri Jeshi Msaidizi, watahakikisha kwamba, Hati ya Udugu wa Kibinadamu inatekelezwa kwa dhati kabisa na Kamati iliyoundwa, ili kumwilisha malengo yaliyobainishwa kwenye Hati hii.

Baraza la Makanisa Ulimwenguni: Kusali, Kufunga na Matendo ya Huruma
13 May 2020, 12:55