Tafakari ya Neno la Mungu: Kristo Yesu ni kilele cha ufunuo wote wa Maandiko Matakatifu. Safari ya imani inapata kikomo chake kwa kumtambua Kristo Yesu katika kuumega Mkate! Tafakari ya Neno la Mungu: Kristo Yesu ni kilele cha ufunuo wote wa Maandiko Matakatifu. Safari ya imani inapata kikomo chake kwa kumtambua Kristo Yesu katika kuumega Mkate! 

Tafakari Neno la Mungu Jumapili III ya Pasaka: Fumbo la Ufufuko!

Kristo Yesu ni kilele cha ufunuo wote wa Maandiko Matakatifu tangu Agano la Kale, yanamuelekea Kristo Yesu na yote yanapata mwanga mpya katika ufunuo katika Yeye! Safari ya maisha ya mwamini anayoifanya kwa kuambatana na Kristo Mfufuka inafikia kilele chake katika kumtambua Kristo Mfufuka pale Neno linaposomwa na kutangazwa pamoja na Kuumega Mkate, Ekaristi!

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Utangulizi: Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News tungali katika Kipindi cha Sherehe ya Pasaka. Tunaendelea kuadhimisha kwa furaha ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo, ufufuko ambao ni ishara ya ukombozi wetu na mwanzo wa maisha mapya ndani ya Kristo. Leo tunayasoma na kuyatafakari masomo ya  dominika ya 3 ya PasakaSomo la kwanza (Mdo. 2:14, 22-33) ni kutoka Kitabu cha Matendo ya Mitume. Somo hili ni sehemu ya mahubiri ya ufufuko ambayo mtume Petro aliyatoa kwa hadhara Sikuku ya Pentekoste. Cha pekee anachokitoa Mtume Petro katika somo la leo ni kwamba ufufuko huo wa Kristo ni suala lililokuwa ndani ya mpango wa Mungu wa ukombozi na tayari lilikwisha tabiriwa katika Maandiko Matakatifu. Ndicho anachokimaanisha anaposema kuwa hata Daudi, yaani katika Zaburi, anatoa ushuhuda huo. Mtume Petro ananukuu Zaburi ya 16 hasa maneno yasemayo “nimemweka Bwana mbele yangu daima, kwa hiyo moyo wangu utafurahi na mwili wangu utakaa katika matumaini kwa maana hutaiacha nafsi yangu katika kuzimu wala hutamtoa mtakatifu wako aone uharibifu”.

Zaburi hii, Wayahudi waliitumia kama sala ya kujiaminisha kwa Mungu. Ilikuwa hasa ni sala ya Walawi. Hili ni kabila ambalo wakati ardhi ya Israeli ilipokuwa inagawiwa kwa makabila 12 wao hawakugawiwa kwa sababu walikuwa ni kabila la makuhani na hivyo walipaswa kujihusisha tu na mambo ya hekalu. Licha ya kutokuwa na ardhi, walawi walionesha matumaini kwa Mungu kuwa ndiye fungu la posho lao, hataiacha nafsi yao kuzimu, yaani katika taabu na mahangaiko. wamemweka Bwana mbele daima naye hataiacha nafsi ya mtumishi wake ione uharibifu. Na hayo ndiyo maneno ya Zaburi ya 16 ambayo Mtume Petro anayanukuu. Mtume Petro anapoinukuu Zaburi hii anaipa tafsiri mpya. Anaonesha kuwa japokuwa Zaburi hiyo ilitumiwa na walawi, ulikuwa hasa ni utabiri unaoashiria ufufuko wa Kristo. Kristo ndiye kuhani wa kweli na maisha yake ni mfano halisi wa yule anayeweka matumaini yake yote kwa Mungu na hivyo ndiye aliyeahidiwa kuwa mwili wake hautaharibika kaburini wala nafsi yake haitaachwa kuzimu. Zaburi hii inadhihirisha alicholenga kuonesha Mtume Petro, kuwa ufufuko wa Kristo sio kitu kilichoibuka ghafla wala sio kitu cha kutungwa. Ni ukweli ambao unashuhudiwa na Maandiko Matakatifu yenyewe na tena ni ukweli ambao Maandiko hayo yaliutabiri kama sehemu ya mpango wa Mungu wa wokovu kwa wanadamu.

Somo la pili (1Pet 1:17-21) ni kutoka katika waraka wa kwanza wa Mtume Petro kwa watu wote. Katika somo hili pia, Mtume Petro anazungumzia ukombozi katika alama za ukombozi za Agano la Kale. Katika Agano la Kale, sadaka ya ukombozi ilitolewa kwa kumwaga damu ya mwanakondoo. Ndivyo alivonena Nabii Isaya kuhusu mtumishi wa Bwana aliyechukuliwa kama mwanakondoo anayepelekwa machinjiioni (Rej: Isa 52:3) na pia rejea ya mwanakondoo wa Pasaka ambaye wayahudi walimchinja walipotoka utumwani Misri.  Katika alama hiyo hiyo, Petro anafundisha kuwa nasi tumekombolewa sio kwa fedha wala dhahabu bali tumekombolewa kwa damu azizi ya Kristo. Na kwa jinsi ile ile ambayo katika Agano la Kale damu ilimaanisha maisha, ndivyo pia Petro anamaanisha kuwa kukombolewa kwa Damu Azizi ya Kristo maana yake tumekombolewa kwa maisha ambayo Kristo aliyatoa kwa kifo chake Msalabani.

Injili (Lk 24:13-35) Injili ya dominika hii ni kutoka kwa mwinjili Luka na inaelezea tukio la Yesu mfufuka na wafuasi wawili wa Emau. Mwinjili Luka anaeleza kuwa katika siku ile ya kwanza ya Juma taarifa zilipoanza kusambaa kuwa Kristo amefufuka, Yerusalemu nzima ilijaa taharuki na kile tunachoweza kukiita hali ya sintofahamu. Ni katika taharuki na sintofahamu hiyo, wafuasi hawa wawili wanafunga safari kwenda kijiji cha Emau. Inawezekana waliamua kutoka Yerusalemu ili kujiepusha na taharuki hiyo na kwamba waliamua kurudi Emau ni ushahidi tosha kabisa kuwa wao nao hawakuiamini habari hiyo kuwa Kristo amefufuka. Wakiwa njiani, Kristo mwenyewe anawatokea, anazungumza nao njia nzima lakini hawakumtambua. Walikuja kumtambua walipofika nyumbani wakiwa mezani pale alipotwaa mkate na kuumega na kuwapa. Hapo ndipo walipoamini, wakapata nguvu za kurudi Yerusalemu ili na wao washuhudie kuwa kweli Kristo amefufuka.

Katika mwendelezo wa masomo ya dominika ya leo, tunaona pia katika Injili hii ufufuko wa Yesu unaongelewa katika msingi wake wa Agano la Kale. Yesu mwenyewe alianza kuwaambia wale wafuasi “Enyi wenye mioyo mizito ya kuamini yote waliyoyasema manabii, Je, haikumpasa Kristo kupata mateso haya na kuingia katika utukufu wake? Akaanza kutoka Musa na manabii wote akawaeleza katika Maandiko yote mambo yaliyomhusu yeye mwenyewe. Alicholenga kuwaambia Yesu ni kuwa hawakupaswa kushtushwa wala kuogopeshwa na habari zilizoanza kusambaa kuwa Kristo amefufuka. Wao kama Wayahudi walipaswa kuyasoma vema Maandiko Matakatifu na kutambua kuwa ufufuko huo ulikwishatabiriwa tayari katika Maandiko ya Agano la Kale. Ni muhimu pia katika somo hili kuona jinsi ambavyo ufufuko wa Kristo unakuwa ni tendo linalounganisha alama za Agano la Kale, Agano Jipya na maisha ya ushuhuda ya wafuasi wa Kristo. Tunaona kuwa baada ya Yesu kuwafafanulia Maandiko Matakatifu, alijifunua kwao katika kuumega Mkate.

Baada ya kumtambua katika kuumega Mkate, macho yao yalifumbuka wakapata nguvu na ujasiri wa kurudi Yerusalemu na huko wakamshuhudia kuwa kweli amefufuka. Safari yao ya kutoka Yerusalemu wakiwa wamejaa hofu na “sintofahamu” inageuka inakuwa safari ya kurudi Yerusalemu wakiwa na nguvu na uhakika wa kutoa ushuhuda. Upo uhusiano wa karibu sana wa somo hili na adhimisho la Misa Takatifu. Katika adhimisho la Misa huanza Liturujia ya Neno ambapo Maandiko Matakatifu husomwa na kufanyiwa tafakari, kisha hufuata Liturujia ya Ekaristi Takatifu ambapo Yesu mwenyewe hujifunua katika maumbo ya Mkate na Divai naye hujimega na kujitoa kama chakula kwa wafuasi wake. Baada ya adhimisho huwatuma waende kuwa mashahidi wa mafumbo hayo.  Katika uhusiano huu, injili ya leo inakuwa pia ni ushuhuda wa imani ya Kanisa la mwanzo juu ya adhimisho la Ekaristi Takatifu kama kumbukumbu ya Ufufuko wa Kristo na mwaliko wa kuwa mashuhuda wake.

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, masomo ya dominika hii ya 3 ya Pasaka, kati ya mafundisho yake mengi, yanatupatia mambo mawili ya kutafakari. La kwanza ni kuwa Kristo ndiye kilele cha ufunuo wote wa Maandiko Matakatifu. Yote tangu Agano la Kale yanamuelekea Kristo na yote yanapata mwanga mpya wa ufunuo katika Yeye. Tumeona katika somo la kwanza namna ambavyo Mtume Petro ameonesha utimilifu wa Zaburi ya 16 katika fumbo la ufufuko wa Kristo na hali kadhalika Kristo mwenyewe alivyowafunulia wafuasi wa Emau namna ambavyo Torati ya Musa na unabii wote unavyoashiria fumbo hilo hilo la Pasaka. Fundisho hili ni la msingi katika kuyaelewa Maandiko Matakatifu kama ufunuo mmoja ulio na kilele chake katika Kristo.

Jambo la pili katika tafakari yetu ni juu ya safari ya imani inayowakilishwa na safari ya wafuasi wa Emau. Safari ya wafuasi hawa ilianzia Yerusalemu kama safari ya watu waliokuwa wamekata tamaa. Njiani wanapokutana na Yesu, Yeye anawaanzishia safari nyingine ya kuwapitisha katika Maandiko Matakatifu. Safari hii mpya wanayoifanya na Yesu inafikia kilele chake katika kumtambua kuwa Kristo Mfufuka pale alipomega mkate kati yao. Hapo ndipo hofu na kukata tamaa kwao kunaisha, wanarudi palepale safari yao ya kwanza ilipoanzia na wanatoa ushuhuda wa ufufuko wa Kristo. Safari ya wafuasi hawa ndiyo safari ya imani ya kila mfuasi wa Kristo. Ni safari inayoanza katika mazingira halisi ya mfuasi, mazingira ambayo kwa kawaida huwa na changamoto nyingi za kimwili na za kiroho. Ni mazingira hayo pamoja na changamoto zake ambazo mfuasi anaalikwa kuzipitia katika mwanga wa Maandiko Matakatifu yakitiwa nguvu na Sakramenti za Kanisa ambazo kiini na kilele chake ni Ekaristi Takatifu. Na hapo safari hiyo ya imani hufikia ukamilifu wake katika maisha ya ushuhuda katika mazingira halisi. Kwa maadhimisho ya Ufufuko wa Kristo, Mwenyezi Mungu atujalie neema ya kuyasimika maisha yetu katika nguvu ya Neno  na Sakramenti zake ili tuwe mashuhuda wake katika maisha yetu ya kila siku. Amina.

Liturujia Jumapili III ya Pasaka

 

24 April 2020, 14:30