Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC: Ni wakati muafaka wa kuwekeza katika utu, heshima na haki msingi za binadamu na utunzaji bora wa mazingira! Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC: Ni wakati muafaka wa kuwekeza katika utu, heshima na haki msingi za binadamu na utunzaji bora wa mazingira! 

Baraza la Makanisa Ulimwenguni: Miaka 50 ya Mama Dunia! 2020!

WCC: Kuna baadhi ya nchi, taasisi na makampuni ya Kimataifa yanataka kutumia Janga la Virusi vya Corona, kujitajirisha na kujinufaisha zaidi. Mchakato wa ufufuaji wa uchumi baada ya Janga la Corona ujielekeze zaidi katika mahitaji msingi ya binadamu sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Ni wakati muaka wa kuwekeza katika wongofu wa kiejolojia kwa mafao ya wengi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., - Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa katekesi yake, Jumatano, tarehe 22 Aprili 2020 ameungana na Jumuiya ya Kimataifa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mama Dunia. Hii ni fursa ya kupyaisha tena upendo katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa watu wanyonge ndani ya familia kubwa ya binadamu! Huu ni muda wa kujenga na kudumisha mshikamano wa upendo kama ambavyo inajidhihirisha katika mapambano dhidi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC, katika ujumbe wake kwa ajili ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Siku ya Kimataifa ya Mama Dunia, limegusia athari kubwa zinazoendelea kusababishwa na janga kubwa la homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Kuna watu wengi ambao wamepoteza maisha; kuna umati mkubwa sana wa wagonjwa walioambukizwa Virusi vya Corona, COVID.

Katika hali na mazingira kama haya, bado kuna baadhi ya nchi na taasisi ambazo zimejitumbukiza katika sera za ubaguzi, nyanyaso na uvunjaji wa haki msingi za binadamu; pamoja na kuendeleza chuki dhidi ya wageni “Xenofobia”. Kumekuwepo na vitendo vya vikosi vya ulinzi na usalama sehemu mbali mbali za dunia kutumia nguvu kubwa kudhibiti mwingiliano wa watu. Jambo la kusikitisha ni kuona idadi ya mauaji na nyanyaso za wanawake majumbani zikiongezeka kila kukicha! Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC., linasema, athari za Virusi vya Corona, COVID-19 ni kubwa sana, kiasi kwamba watu wamelazimika kubadili mitindo pamoja na vipaumbele katika maisha yao. Huu ni ugonjwa usiochagua wala kubagua! Changamoto kubwa kwa sasa katika Jumuiya ya Kimataifa ni kujizatiti katika ujenzi wa umoja, upendo na mshikamano; tayari watu wa Mataifa kuendelea kubadili misimamo na mitazamo ya maisha, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Ni muda muafaka wa kumwilisha Injili ya upendo inayosimikwa katika huduma makini kwa waathirika wote, lakini zaidi kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Katika muktadha huu, kuna umuhimu wa kusimama kidete kulinda na kudumisha mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote! Mama Dunia anategemewa na kila mtu kwa ajili ya maisha, ustawi na maendeleo yake. Huu ni wakati muafaka kwa Jumuiya ya Kimataifa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima, ustawi, maendeleo, mafao ya wengi na afya binadamu kama rasilimali tete inayohitaji kulindwa na wote! Kwa bahati mbaya kuna baadhi ya nchi, taasisi na makampuni ya Kimataifa yanataka kutumia Janga la Virusi vya Corona, COVID-19 kujitajirisha na kujinufaisha zaidi. Mchakato wa ufufuaji wa uchumi baada ya Janga la Corona ujielekeze zaidi katika mahitaji msingi ya binadamu sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.

Huu si wakati muafaka wa kuvuruga mikataba na itifaki za kimataifa juu ya utunzaji bora wa mazingira. Ni wakati wa kuendelea kujizatiti zaidi katika kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi ambazo zinaendelea kusababisha maafa na majanga makubwa kwa watu na mali zao sehemu mbali mbali za dunia. Ni muda muafaka wa kujizatiti katika kudumisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu; kwa kukazia ulinzi na usalama kwa watu wote bila ubaguzi wala maamuzi mbele yanayoweza kusababisha machafuko yasiyokuwa na mafao yoyote! Baraza la Makanisa Ulimwenguni linaitaka Jumuiya ya Kimataifa kuondokana na hofu na taharuki, kwa kuchukua hatua madhubuti za kujikinga dhidi ya maambukizi ya Virusi vya Corona, COVID-19 kwa kuzingatia kanuni maadili, utu wema na ujasiri. Ni wakati wa kuwekeza katika sera na mikakati ya afya bora na fungamani; kwa kujielekeza zaidi katika ujenzi wa jamii inayoheshimu haki msingi za binadamu pamoja na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, ili kulinda na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo!

Kwa upande wake, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Antonio Guterres katika kumbu kumbu ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mama Dunia anaitaka Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kulinda dunia dhidi ya homa kali inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 pamoja na vitendo vyote vinavyotishia maisha na usalama wa viumbe hai. Kwa wakati huu, kuna uharibifu mkubwa sana wa mazingira. Kuna majanga ya moto sehemu mbali mbali za dunia, lakini kwa namna ya pekee nchini Australia. Kuna ongezeko la kiwango kikubwa cha joto duniani kinachotishia usalama wa maisha ya watu na mali zao kutokana na ongezeko la kina cha maji baharini, ukame na mafuriko ya kutisha. Leo hii janga la homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 ni gonjwa ambalo linahusianishwa na ekolojia. Kuna uchafuzi mkubwa wa vyanzo vya maji na pamoja na hewa. Katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko anasema, changamoto zote hizi zinaweza kujibiwa kikamilifu kwa kujikita katika wongofu wa kiekolojia.

Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC.

 

24 April 2020, 06:47