Vatican News
Siku ya Sala ya Kiekumene ya Umoja wa Wanawake Wakristo Duniani, 6 Machi 2020: Imeandaliwa na Umoja wa Wanawake Wakristo Zimbabwe. Siku ya Sala ya Kiekumene ya Umoja wa Wanawake Wakristo Duniani, 6 Machi 2020: Imeandaliwa na Umoja wa Wanawake Wakristo Zimbabwe. 

Siku ya Sala ya Kiekumene Umoja wa Wanawake Wakristo Duniani, 2020

Siku ya Sala ya Kiekumene ya Umoja wa Wanawake Wakristo Duniani imeadhimishwa hapo tarehe 6 Machi 2020 na Sala imeandaliwa na Umoja wa Wanawake Wakristo Zimbabwe. Kauli mbiu ya maadhimisho haya imekuwa “Yesu akamwambia, Simama, jitwike godoro lako, uende”. Yoh. 5:8. Wanawake Wakristo nchini Zimbabwe, wametumia fursa hii kutafakari yaliyopita kwa uchungu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Siku ya Sala ya Kiekumene ya Umoja wa Wanawake Wakristo Duniani ilianzishwa na Mary Ellen James kunako mwaka 1887. Hiki ni kielelezo makini cha mwendelezo wa mchakato wa majadiliano ya kiekumene miongoni mwa Wakristo. Ni jibu muafaka kwa changamoto ya Kristo Yesu, kwa wafuasi wake, yaani kujenga umoja katika usawa na utofauti wao, ili Injili ya Kristo iweze kuwa na nguvu zaidi, inaposhuhudiwa na Wakristo wote pasi na migawanyiko; kwa kuondokana na wasi wasi pamoja na mashaka, ambayo wakati mwingine yanagumisha majadiliano ya kiekumene. Ni wajibu kwa Wakristo wote kujikita katika majadiliano ya kiekumene yanayofumbatwa katika sala na maisha ya kiroho; katika ushuhuda wa damu na huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii!

Wakristo kwa pamoja wanatafuta amani ing’aayo Uso wa huruma ya Mungu; kwa kuwa wapatanishi; watangazaji na mashuhuda wa Injili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Umoja wa Wanawake Wakristo Duniani, tangu awali umejihusisha sana na huduma katika sekta ya elimu, afya, ustawi na maendeleo ya jamii kwa watu maskini zaidi katika jamii. Kwa mara ya kwanza kunako mwaka 1926, Umoja wa Wanawake Wakristo Duniani, ukaanzisha Siku ya Sala ya Kiekumene ambayo iliadhimishwa tarehe 4 Machi 1927. Wanawake wa kiekumene kutoka Amerika ndio walioratibu na kusimamia tukio hili la kihistoria. Katika mwanga wa maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, Shirikisho la Vyama vya Wanawake Wakatoliki Duniani, WUCWO, UMOFC likajiunga na Umoja huu ili kukuza na kudumisha uekumene wa sala, maisha ya kiroho na huduma.

Siku ya Sala ya Kiekumene ya Umoja wa Wanawake Wakristo Duniani imeadhimishwa hapo tarehe 6 Machi 2020 na Sala imeandaliwa na Umoja wa Wanawake Wakristo Zimbabwe. Kauli mbiu ya maadhimisho haya imekuwa “Yesu akamwambia, Simama, jitwike godoro lako, uende”. Yoh. 5:8. Wanawake Wakristo nchini Zimbabwe, wametumia fursa hii “kutafakari yaliyopita kwa moyo wa uchungu na shukrani, wanataka kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo na nguvu ya imani, matumaini na mapendo, ili waweze kutembea katika mwanga wa tunu msingi za maisha ya Kiinjili”. Wanawake wa Zimbabwe wanasema, walisimama kidete kupigania uhuru wa nchi yao hadi kikaeleweka. Kutokana na uchu wa mali na madaraka, Zimbabwe ikaingia katika machafuko ya kisiasa; umaskini wa hali na kipato vikawapekenya, umoja wa kitaifa ukatoweka.

Umoja wa Wanawake Wakristo Zimbabwe unasema, sasa ni wakati muafaka kwa Zimbabwe kujikita katika mchakato wa haki, amani na upatanisho wa kweli, ili kuganga na kutibu madonda na makovu ya utengano, tayari kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa! Kama ilivyokuwa kwa yule mgonjwa, aliyehurumiwa na Yesu, akamponya hata Siku ya Sabato wanataka hata wao, Kristo Yesu aweze kuwakirimia nguvu ya ufufuko, ili waweze kusimama tena na kuanza “kuchanja mbuga kama wanawake wa shoka”. Wametumia fursa hii, kuwawezesha wanawake kiuchumi na kuwahamasisha ili wasimame kidete katika kuzitegemeza familia zao: kiroho, kiutu, kiuchumi na kitamaduni. Wakati wa machafuko ya kisiasa, wanawake pamoja na wasichana wengi nchini Zimbabwe walilazimika kuikimbia nchi yao ili kutafuta, hifadhi, usalama na maisha bora zaidi ugenini! Wale waliobaki, “wakazamia mijini” ili kutafuta riziki kwa ajili ya watoto wao! Mambo hayakuwa shwari sana huko mijini! Kwa hakika, wahenga wanasema, uchungu wa mwana aujuaye ni mzazi.

Familia ya Mungu nchini Zimbabwe katika kipindi cha miaka kadhaa, imeguswa na kutikiswa sana na baa la njaa, magonjwa na umaskini; ukosefu wa fursa za ajira; dhuluma na nyanyaso mbali mbali dhidi ya wanawake na wasichana. Lakini mbaya zaidi ni kusua sua kwa umoja na mshikamano wa kitaifa, amani na utulivu wa ndani, chachu muhimu sana katika mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu. Umoja wa Wanawake Wakristo Zimbabwe unasema Siku ya Sala ya Kiekumene ya Umoja wa Wanawake Wakristo Duniani kwa mwaka 2020 imekuwa ni fursa ya kujikita zaidi na zaidi katika mchakato wa ujenzi wa: haki, amani, upendo; umoja na mshikamano wa kitaifa unaofumbatwa katika msingi wa upatanisho wa kitaifa. Ni wakati muafaka kwa familia ya Mungu nchini Zimbabwe kujipatanisha na hatimaye kujipatanisha hata na Mwenyezi Mungu, tayari kujikita katika hija ya ujenzi wa haki na amani nchini Zimbabwe.

Wakati huo huo, Shirikisho la Vyama vya Wanawake Wakatoliki Duniani, WUCWO, UMOFC kwa kushirikiana na wanawake kutoka katika dini na madhehebu mbali mbali duniani katika Tamko lao kuhusu Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kwa Mwaka 2020 linasema kwamba, wanawake wanapania kusimama kidete kupambana na uchoyo na ubinafsi, kwa kutangaza na kushuhudia imani yao kwa Mwenyezi Mungu anayewakirimia zawadi ya maisha inayopaswa kulindwa na kudumishwa; kwa kuwasaidia maskini, watu waliokata tamaa; watu wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii na wale wote wanaojisadaka katika ujenzi wa utamaduni wa kiutu! Wanawake hawa wanataka kusimama kidete kulinda na kudumisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; kwa kushirikiana kwa karibu zaidi na wanasiasa, vyombo vya mawasiliano ya jamii, wachumi, wadau wa elimu, sayansi na sanaa sanjari na vijana wa kizazi kipya ili kuhakikisha kwamba, dini zinakuwa ni chombo cha ujenzi wa amani duniani, na kamwe dini zisitumike kuchochea chuki, uhasama na vita; na badala yake, waamini wa dini mbali mbali waheshimiane na kuthaminiana.

Wanawake wanataka pamoja na mambo mengine kujielekeza zaidi katika kukuza fadhila ya upendo wenye huruma na ujasiri katika imani ili kujiimarisha pamoja na kukuza kipaji cha ubunifu, ili kupambana kufa na kupona kama sehemu ya harakati za kung’oa mifumo yote ya utumwa mamboleo inayodhalilisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Hawa ni watu wanaoathirika kutokana na umaskini na baa la njaa; kwa kutaka kilio cha watu hawa kiweze kusikika katika Jumuiya ya Kimataifa. Wanawake wamedhamiria kuboresha uwezo wao wa kulinda na kutetea uhai; kwa kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Wanawataka kuwa ni madaraja yanayowakutanisha watu kutoka katika tamaduni na staarabu mbali mbali za dunia, ili kila mtu aweze kutajirishwa na tamaduni za wengine, kwa kushirikishana na kujadiliana katika ukweli na uwazi.

Wanawake wa imani wanakubaliana kimsingi juu ya tofauti zao za kidini; wanataka kujielimisha zaidi kwa kushirikiana na wanawake wenzao ili kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu. Ni katika muktadha huu, wanawake wa imani wanawaalika watu wote wenye mapenzi mema na wale wanaotaka kuishi katika misingi ya haki na amani, kuwaunga mkono katika makubaliano haya, kama kielelezo cha urafiki wa kijamii unaofumbatwa katika misingi ya kuheshimiana!

Wanawake Wakristo: Sala 2020
09 March 2020, 08:39