Vatican News
Sala ya mama awe wa asili au kiroho ina nguvu zaidi.Mama Maria ni mfano wa kuigwa kwa mama wote! Sala ya mama awe wa asili au kiroho ina nguvu zaidi.Mama Maria ni mfano wa kuigwa kwa mama wote! 

Kwa nini sala ya mama awe wa asili au kiroho ina nguvu zaidi?

Katika mantiki ya janga la virusi vya corona ambalo bado linendelea kupoteza viumbe wengi na kusababisha uchungu,huzuni na mahangaiko, Sista Loreta wa Shirika la Upendo,ametoa tafakari ya kina kwa kutoa swali:kwa nini sala ya mama awe wa asili au kiroho ina nguvu zaidi namna hii? Na kwa kutumia maandiko matakatifu anafafanua Injili ya Luka,jinsi Yesu alivyoweza kutazama maandamano makubwa ya mazishi ya mtoto huko Naim.Mama Maria pia ni mfano wa kuigwa kama Papa Francisko anavyosisitiza kila mara.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican

Katika muktadha wa janga la Corona, Ccovid 19 limetufanya watu wengi kutafakari kwa kina, kuanzia hata wale ambao walikuwa wamejisahahu kuwa wameumbwa na Mungu na ni viumbe dhaifu, kufikia hata wale ambao kila siku wanamwilishwa na neno la Mungu, kuanzia familia, makuhani na watawa. Na zaidi watu wengi kuwa na wasi wasi, hofu mashaka na hisia nyingi za kutojua ni siku, saa, nukta inafikia kuambukizwa na virusi hivi.  Kila pembe ya dunia, kuna vilio na huzuni  vinavyo sikika hapa na pale, wengi wakiomboleza kwa ajili ya wapendwa wao. Aidha wapo wengi ambao wanateseka kwa njaa na hata magonjwa mengine kutokana na kwamba hawawezi kwenda vituo vya afya; na wengine hawana kazi na wala makazi ya kuweza kutulia na kujikinga na adui hasiye onekana kwa macho yetu hadi chombo maalum cha kisayansi. Hata hivyo maombolezo  yameweza kukumbusha matukio ya kihistoria kuanzia enzi za Yesu hadi kufikia nyakzi za vita kuu ya dunia, majanga ya asili na yale yasiyo ya asili, ambayo kiukweli yamepoteza mamilioni ya viumbe vya Mungu.

Tukiwa katika wiki ya tano,  na ambayo tunakwenda  ukingoni kukaribia Dominika ya Matawi ijayo  ambamo tunaingia rasmi katika siku muhimu Kuu za Mateso, kifo na ufufuko wa Bwana, kwa wakristo wote , dunia nzima tumejikuta katika hali ambayo tunapaswa kutafakari kwa dhati , haijalishi dini yoyote maana virusi hivi havichagui, muda mwingi tunao hasa tukiwa na familia zetu. Katika mantiki hiyo, Sisita mmoja  Loretta wa Shirika la Upendo, ametoa tafakari ya kina hasa akianza na kuuliza swali moja na ambalo analijibu kwa kutumia maandiko matakatifu. Swali hili linaulizwa “Ni kwa nini sala ya mama awe wa asili au kiroho ina nguvu zaidi namna hii? Ni swali kwa hakika linalotokana na vilio hivi vya dunia, wengi ambao wanakufa bila hata kuwa na msindikizaji wa kiroho, au hata ndugu aliye karibu. Familia ningi hazijuhi ndugu hao wako wapi. Ni vilio na uchungu wa kina kwa mama na familia nyingi.

Katika kujibu swali la sala ya mama kuwa muhimu, Sisita Loretta anasema katika Injili ya Luka, Yesu aliwaweza kutazama maandamano makubwa sana ya kwenda mazishi huko Naim.Kwa hakika mji mzima ulikuwa pale. Alitazama vijana wanaume na wanawake waliokuwa wanalia. Alitazama wachungaji na mitume walikuwa kuwa wakilia. Alitazama wazee walio kuwa wakilia. Yesu alitazama mababa waliokuwa wanalia. Aliwatazama watoto waliokuwa wanalia. Yesu alizitazama nyuso za watu zilizokuwa zimejazwa na huzuni kubwa katika kuomboleza. Hakuna chochote ambacho kilionesha dalili ya kuondolewa huzuni huo na amaombolezo hayo, hadi alipoweza kwa mbali kumwona mama wa mtoto aliyefariki akiwa na uchungu mkali.

Biblia Takatifu, inabainisha kuwa Yesu alishikwa na huruma  alipomwona mama huyo na mara moja alimfufua kijana aliyekuwa amekufa (Luca 7: 12-15).  Hiki kilikuwa ni kilio cha mama kilichogusa kwa kina moyo wa Mungu. Hii ni kweli kabisa kama methali ya kiswahili isemavyo "uchungu wa mwana aujuaye ni mzazi.... "Hata leo hii, ni Mama wengi wanalia mbele ya Bwana kwa ajili ya familia zao, kwa ajili ya ndoa zao, kwa ajili ya nyumba zao zote, ambazo zinagusa moyo wa Mungu!

Aidha amesema Sisita Loreta kuwa, ikiwa mama wanaacha kulia, na kuomba, basi familia zao (hasa watoto wao) wanapotea. Ibilisi anapata hata nafasi ya kuegemea na kuanza kuharibu nyumba, lakini  wakati wakirudi mama mahali pao pa haki, akawa kama nanga ya nyumba basi ngome za  mapepo yote hubomolewa! Hali kadhalika katika zaburi ya  17, 36, 57, 63 na 91 nafasi ya Mungu inafananishwa na ile ya Mama. Hii ni kutaka kuthibitisha kwamba kama vile mama anavyolinda na kutetea wanae, ndivyo hata Mungu anavyolinda watoto wake chini ya kivuli cha mabawa yake. Na tunapata kimbilio mahali pale; tunaweza kujificha humo hadi hatari itakapokuwa imekwisha.

Jukumu la mama ni hai ,  ambalo kwa baba hawezi kupata jibu kwa njia ya sala zake ikiwa anamkosea heshima au kumdharau. Anathibitisha hayo Mtatifu Petro katika barua yake kuwa: “Kadhalika ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa akili; na kumpa mke heshima, kama chombo kisicho na nguvu; na kama warithi pamoja wa neema ya uzima, kusudi kuomba kwenu kusizuiliwe”(1 Pietro 3: 7). Kwa kuwa  mama anapaswa kupewa heshima kama hiyo, mama hao  ni watu ambao wameshikilia sana na watunzaji wa nyumba. Kwa maana hii,  shetani huwaogopa akina mama maana ni nguvu msingi wa ndani ya nyumba na ambayo hutokana na kuomba kwao yaani sala ya kina! Ni Bwana ambaye ameweka ndani mwao ile  neema na uvimilivu ndani wa wakina mama ili waweze kushinda hali yoyote ile ambayo inaweza kutokea. ameandika sista Loretta.

Kwa kuhitimisha anasema leo hii kama wanawake wa nyumbani wanapaswa kujifikiria wenyewe ya kwamba wamebarikiwa , wafikirie wamejaliwa neema na kwa maana hiyo wao wanafikiriwa kuwa HATARI SANA HASA WANAPOSALI. Sista Loreta anawaalika wananawake wote, wawe asilia au kiroho wahabarishwe  juu ya tafakari lake ke na hasa katika kutambua nafasi msingi waliyo nayo mama  katika familia na jukumu kama nguzo yaa sala, kuwa ni ngome ya uvumilivu na upendo. Na wabarikiwe wote.

Papa Francisko anatukabidhi Mama wa Kanisa: Nikinukuu Sista Loreta  ambaye amesema kuwa “Ikiwa mama wanaacha kulia na kuomba, basi familia zao (hasa watoto wao) wanapotea. Ibilisi anapata nafasi ya kuegemea na kuanza kuharibu nyumba;lakini kama  akirudi mahali pake pa haki, kama nanga ya nyumba, ngome za mapepo hubomolewa”. Muktadha wa tafakari hii unaweza kuelekezwa pia katka mahubiri ya Papa Francisko na wito wake wa mara kwa mara ambao anawaalika waamini kutazama kwa namna ya pekee mfano wa  Mama Maria hasa wakati wa kipindi  cha shida na mateso.  Papa Francisko anasema maisha yetu yamekuwa na mafundo mengi na magumu kufunguliwa ya maisha, na katika hali hiyo pia ni vema kutazama mbinguni, kwa Mama Maria. Ni vizuri kutambua namna ya utazamwa kila mmoja na mama  Maria. Hali kadhalika ni mama wa kuigwa na mama wa wote,  kwa maana yeye anapotazama haoni dhambi,  bali anaona watoto wake. Mama Maria anatusimika katika mzizi wa Kanisa, mahali ambamo umoja unahesabiwa zaidi kuliko kuwa na migawanyiko na kutushauri tuweze kusaidiana mmoja na mwingine.(mahubiri ya Papa Francisko tarehe Mosi Januari 2019).

31 March 2020, 09:28