Vatican News
Baraza la Maaskofu Katoliki Italia linawashukuru na kuwapongeza Mapadre na Watawa wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu nchini Italia. Baraza la Maaskofu Katoliki Italia linawashukuru na kuwapongeza Mapadre na Watawa wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu nchini Italia.   (Vatican Media)

Kanisa linawashukuru Mapadre na Watawa kwa Sadaka na huduma!

Kardinali Bassetti anawashukuru mapadre na watawa ambao wamekuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu kwa waamini katika parokia mbali mbali bila kuwasahau watu wenye mapenzi mema wanaoendelea kuonesha imani na matumaini yao kwa Kanisa. Mapadre wamekuwa ni mashuhuda wa Uso wa Kanisa ambalo ni rafiki kwa maskini na daima liko karibu kwa wote!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Gualtiero Bassetti, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI, katika waraka wake wa kichungaji kwa wakleri na watawa wote wanaotekeleza dhamana na utume wao nchini Italia, anapenda kuwapongeza kwa moyo wa dhati kabisa, kwa uwepo wao wa karibu kwa wagonjwa, familia na watu walioathirika kutokana na Virusi vya Corona, COVID-19. Kwa namna ya pekee, anawashukuru mapadre ambao wameendelea kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu kwa waamini katika parokia mbali mbali bila kuwasahau watu wenye mapenzi mema wanaoendelea kuonesha imani na matumaini yao kwa Kanisa. Mapadre wamekuwa ni mashuhuda wa Uso wa Kanisa ambalo ni rafiki kwa maskini na daima liko karibu kwa watu wanaoteseka kwa njia ya huduma makini.

Mapadre wamekuwa ni kielelezo makini cha ushuhuda wa: heshima, upendo na mshikamano, utambulisho wa huduma yao ya kichungaji hasa wakati huu ambapo watu wengi wameshikwa na hofu ya mashambulizi ya ugonjwa wa Virusi vya Corona, COVID-19. Wameendelea kusimama kidete kulinda na kudumisha afya ya umma kwa kutoa upendeleo wa pekee kwa maskini, wagonjwa na wazee. Hata katika hali ya faragha sana, wamekuwa ni vyombo vya matumaini na faraja kwa wagonjwa na wale waliofiwa na wapendwa wao. Wamesaidia kuwapatia baraka, wale wote waliotangulia mbele za haki, wakiwa na matumaini ya ufufuko, maisha na uzima wa milele.

Kardinali Gualtiero Bassetti anasema, kwa sadaka hii, Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, aweze kuwakirimia Makuhani wake, neema na baraka; amani na utulivu wa ndani katika utekelezaji wa dhamana yao ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Ni vigumu kuweza kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Parokia pasi na waamini. Lakini, katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, Mapadre wanatolea mateso, mahangaiko na matumaini ya watu wa Mungu na wala hakuna mtu awaye yote anayesahauliwa katika sala na maombi yao. Maadhimisho ya Ekaristi Takatifu kiwe ni kielelezo cha mshikamano wa maisha ya kiroho, hata ikiwa kama waamini hawapo Kanisani.

Hiki ni kipindi muafaka cha kufanya tafakari ya kina ya Neno la Mungu, tayari kuimwilisha katika uhalisia wa maisha na utume wao. Mapadre wawasaidie waamini kugundua umuhimu wa Neno la Mungu katika maisha yao; Kristo Yesu anayeendelea kuzungumza pamoja nao kwa njia ya watumishi wake. Ni muda wa kuzungumza na Mwenyezi Mungu kama rafiki kama ilivyokuwa kwa Musa, Mtumishi wa Mungu. Mapadre wawasaidie waamini kuchagua fungu bora kama ilivyokuwa kwa Maria. Mapadre waoneshe wema, uwepo wao wa karibu, ukarimu, upole na upendo kwa watu wanaotafuta msaada kutoka kwao kwa njia ya simu. Huu ni muda wa kutangaza na kushuhudia Injili kwa mfumo na mtazamo mpya zaidi. Upendo wa Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu unawawajibisha kuendelea kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu katika vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii, ili kuwahakikishia watu kwamba, hata katika shida na mahangaiko yao, lakini bado Mwenyezi Mungu anawapenda na kuwajali. Kipindi hiki ambacho watu wengi wako majumbani mwao pamoja na familia zao, ni muda muafaka wa kujenga na kudumisha utamaduni wa kusali pamoja kama familia.

Kardinali Gualtiero Bassetti katika waraka wake kichungaji, anawashukuru na kuwapongeza watu wanaojitolea kwa ajili ya huduma kwa maskini na wagonjwa; wanaosadaka muda wao kwa ajili ya kuwasikiliza na kuwahudumia wahitaji wa kiroho na kimwili. Anawashukuru wahudumu wa maisha ya kiroho magerezani, hospitalini na kwenye nyumba za kutunzia wazee. Huu ni mchakato wa kuwatangazia Watu wa Mataifa, Injili ya Huruma ya Mungu, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Kristo Yesu, ambaye ameonesha mshikamano wa dhati na binadamu katika Fumbo la Umwilisho, mateso na kifo na chake Msalabani ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Kristo Yesu ndiye Msamaria mwema, anayejishusha chini ili kuwaganga wale waliopondeka moyo kwa mafuta ya huruma ya Mungu na divai ya Sakramenti za Kanisa.

Kanisa limeagizwa kutangaza na kushuhudia huruma ya Mungu inayopaswa kupenya katika medani mbali mbali ya maisha ya mwanadamu. Huruma ni daraja inayomkutanisha Mungu na waja wake, kiasi cha kuonja upendo wake usiokuwa na mipaka. Kristo Yesu ni ufunuo wa huruma ya Mungu, changamoto na mwaliko kwa Kanisa kupyaisha sera na mikakati yake ya shughuli zake za kichungaji. Kanisa linapaswa kuwa ni chombo na shuhuda wa Injili ya matumaini, kwa njia ya mvuto wenye mashiko. Kardinali Gualtiero Bassetti anawashukuru kwa moyo wa dhati wakleri na watawa wote, kwa ushuhuda wa utume wao katika kipindi hiki tete cha historia na maisha ya watu wa Mungu nchini Italia. Anasema, Maaskofu wao wote, wanawashukuru na kuwapongeza.

Katika kipindi hiki, Maaskofu wameendelea kushirikishana mang’amuzi mbali mbali, kupeana habari na maamuzi yaliyofikiwa. Maaskofu waomeonesha wasi wasi na matumaini yao, kwani kwa pamoja wote wanajisikia kuwa ni sehemu ya Familia kubwa ya Mungu inayowajibika. Maadhimisho ya Fumbo la Pasaka kwa mwaka 2020 yatakuwa tofauti kabisa na jinsi ilivyozoeleka. Lakini, ikumbukwe kwamba, nguvu, ukuu na utukufu wa Kristo Mfufuka haufungamanishwi na mazingira au nyakati. Familia ya Mungu itaendelea kumwabudu na kumtukuza kwa sababu kwa njia ya Fumbo la Msalaba ameukomboa ulimwengu. Ugonjwa wa Virusi vya Corona, COVID-19 unawafanya watu wengi kuonja mateso ya Kristo katika maisha yao. Gualtiero Bassetti, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI, anahitimisha waraka wake wa kichungaji kwa wakleri na watawa wanaojisadaka kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu nchini Italia, akiwataka kukumbuka kwamba, “Ni neno la kuaminika, kwa maana: kama tukifa pamoja naye, tutaishi pamoja naye pia”. 2Tim. 2:11-12.

Kardinali Bassetti
17 March 2020, 15:17