Vatican News
Tafakari ya Neno la Mungu, Kesha la Sherehe ya Noeli: Mwanzo wa maisha mapya: Kristo Yesu, ndiye Nuru ya Mataifa! Tafakari ya Neno la Mungu, Kesha la Sherehe ya Noeli: Mwanzo wa maisha mapya: Kristo Yesu, ndiye Nuru ya Mataifa!  (@Vatican Media)

Sherehe ya Noeli ya Bwana: Tafakari ya Kesha la Noeli

Katika kesha la Noeli tunaalikwa kuwa na masikio na macho kama ya wachungaji, kuwa wazi na tayari kupokea Nuru kutoka Mbinguni, ndio kuwa na sikio la kusikiliza Neno lake na kulitii kwa kuliweka katika maisha yetu ya siku kwa siku. Ni kuwa na moyo wa unyenyekevu unaotusaidia kupokea ujumbe wa Mungu katika maisha yetu. Ni kuruhusu Mtoto Yesu azaliwe katika maisha yetu!

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

MKESHA WA NOELI: Kadiri ya tamaduni za kimapokeo za Kiyahudi walikuwa wanatofautisha usiku nne katika historia yao. Usiku wa kwanza ni pale mwanzoni mwa uumbaji ambapo Mungu alipoumba mwanga na basi giza lile likatoweka lilikuwa limefunika uso wa nchi. Usiku wa pili ni siku ile ambapo Abrahamu alifanya Agano na Mungu. Mwanzo 15. Usiku wa tatu ni ule walipokombolewa kutoka utumwani Misri, ndio pia Usiku wa Pasaka na Ukombozi kwao. Na wa nne ni usiku ule wa Masiha, giza halitakuwa tena na nguvu baada ya ujio wa Masiya. Zakaria 14:7 Ndio Usiku huu tunaoudhamisha leo katika Kesha hili la Noeli, kesha la kuzaliwa kwake Masiha, mwanzo wa maisha mapya ya ushindi kwani kwa kuzaliwa kwake sisi sote tunapata maisha yenye uzima wa milele. Masomo ya Mkesha huu wa leo yote yanatualika na kutusaidia kutafakari juu ya Huyu aliyezaliwa kuwa ni MWANGA. Somo la kwanza kutoka Kitabu cha Nabii Isaya tumesikia juu ya wimbo ule wa kimasiha kuwa watu wale waliotembea katika giza, ndio katika maovu na ubaya wa kila aina, nuru kuu inawazukia na hapo anaonesha si tu nuru inawazukia bali pia inaambatana na ishara zile muhimu tatu.

Ishara ya kwanza ni furaha, ni furaha ya ndani na kweli, ni furaha kama ile ya mkulima wakati wa mavuno au maaskari baada ya ushindi wa vita. Ishara ya pili ni amani na uhuru. Amani na uhuru unaopatikana kwa ujio wa Nuru na Mwanga. Watu wale hawatatembea tena katika utumwa bali sasa wanakuwa huru na wenye amani ya kweli. Lakini ishara ya tatu na kubwa kuliko zote ndio ‘’Mtoto amezaliwa kwa ajili yetu’’. Mtoto huyu ni kielelezo cha maisha mapya, ndiye Masiha wa Bwana. Wimbo wa Kimasiha wa Nabii Isaya tunaweza kuusoma na kuutafakari vema ikiwa tutaitafakari sambamba na somo la Injili ya Luka tulilolisoma katika Mkesha huu. Mwinjili Luka anatuonesha wakati dunia ikiwa gizani Mtoto anazaliwa kuja kutupatia mwanga. Ni mwanzo wa furaha kuu na amani ulimwenguni. Ni katika Mtoto huyu tunaona tumaini letu linalojidhihirisha katika majina ya Mtoto huyu, ‘’Mkombozi, Kristo, Bwana’’. Jinsi ilivyompendeza Mungu, watu wa kwanza kupokea Habari ile Kuu ya Furaha na Amani ni wale walioonekana kuwa ni watu duni na wa mwisho ndio wachungaji.

Ni wao waliokuwa na masikio ya kusikia na macho ya kuona ambao Mungu anawajalia kuwa wajumbe wa kwanza kushuhudia Habari ile Kuu ya Wokovu. Wanakuwa wamisionari wa kwanza kutii ujumbe wa malaika na hivyo kwenda kumsujudu Mtoto Yesu. Na Mwinjili Luka anatuonesha jinsi wachungaji walivyokuwa wamisionari wa kwanza kwani kila aliyesikia habari za wachungaji alibaki na mshangao mkuu. Nasi katika mkesha wa leo tunaalikwa kuwa na masikio na macho kama ya wachungaji, kuwa wazi na tayari kupokea Nuru kutoka Mbinguni, ndio kuwa na sikio la kusikiliza Neno lake na kulitii kwa kuliweka katika maisha yetu ya siku kwa siku. Ni kuwa na moyo wa unyenyekevu unaotusaidia kupokea kila ujumbe wa Mungu katika maisha yetu. Ni kuruhusu Mtoto Yesu azaliwe katika maisha ya kila mmoja wetu, azaliwe katika jumuiya na familia zetu. Noeli ni sherehe za Neema ya Mungu kwa mwanadamu, kwani Mungu anafanyika mwanadamu na kukaa kati yetu, ni Mungu anayebaki kuwa zawadi ya kweli katika maisha yetu.

Wakati wa Noeli kwa baadhi kuna desturi za kupeana zawadi ila yafaa kila mara kukumbuka kuwa zawadi ni ishara ya Mungu anayekuwa zawadi kwa kila mmoja wetu, ni Mungu anayetaka kuishi na kuongoza maisha ya kila mmoja wetu. Katika Pango lile la kulishia wanyama, katika mazingira yake duni na fukara tunaona Mungu anapenda kujipambanua nao. Ni Mungu mwenye kila enzi na nguvu anajishusha na kukubali kuzaliwa katika mazingira yale duni, anajitambua pamoja na watu duni na maskini wa dunia yetu. Ni kuanzia katika holi la kulishia wanyama inaanza safari ya historia ya wokovu wetu inayofikia kilele chake pale Kalvario.  Na ndio maana Makanisa ya Mashariki wanaiita na kuitambua sherehe ya Noeli kama Pasaka ya Kuzaliwa Bwana. Mwanga wa usiku huu ni ishara ya mwanga ule wa alfajiri ya Pasaka, siku ya ukombozi wetu. Nawatakia tafakari na Noeli njema.

24 December 2019, 12:22